Home KIMATAIFA Ajabu waandamanaji Sudan wakita kambi jeshini!

Ajabu waandamanaji Sudan wakita kambi jeshini!

1436
0
SHARE

NA MITANDAO

Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa waandamanaji nchini Sudan waliokuwa katika harakati za kuuondoa utawala wa Rais Omar al-Bashir  waliugeuza uwanja uliopo nje ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo kuwa kitovu cha kutafuta hali ya baadaye wanayoitaka.

Watu wengi walikuwa wanajiuliza – ilikuaje waandamanaji hao walikwenda sehemu hiyo nyeti ambayo ndiyo ilikuwa alama ya nguvu ya utawala huo kwa zaidi ya miaka 30?

Wachunguzi wa mambo wanasema kwa kawaida, wananchi wanapokuwa na harakati za maandamano ya kupinga utawala huwa kunakuwapo sehemu moja ya kukutania. Wanataja kwa mfano  Medani ya Tahrir (Tahrir Square) ya Misri, Medani ya Taksim (Taksim Square) ya Istanbul, Uturuki na Barabara Kuu ya Habib Bourguiba (Habib Bourguiba Avenue) ya mjini Tunis, nchini Tunisia.

Waandamanaji katika maeneo yote hayo walinasa fikra za watu mbali mbali duniani kwani ni sehemu ambazo zilionyesha kwamba nguvu ya umma haiwezi kupuuzwa.

Amira Omer Osman, raia wa Sudan na Profesa wa Usanifu majengo katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane (Tshwane University of Technology -TUT) nchini Afrika ya Kusini akiandika katika Mtandao wa African Arguments wiki iliyopita anasema wakati maandamano yalipoanza Desemba 2018 alikuwa anajiuliza wananchi wa Sudan wangechagua eneo lipi la kukutania katika harakati zao.

Anasema maeneo ya wazi mjini Khartoum yako kadha – kama vile uwanja wa Al Saha Al Ghadraa, ambao una mahusiano ya kihistoria na utawala wa Bashir, na hivyo usingekubalika na waandamanaji.

Maeneo mengine pia yalikataliwa kwa sababu yalikuwa yakionyesha mahusiano na vyama/makundi mengine ya kisiasa. Aidha majengo kama vile Jengo la Bunge katika kitongoji cha Omdurman hayana maeneo yenye uwezo wa kukuchukua watu wengi.

Hivyo jibu lilikuja Aprili 6 2019 pale mamia ya maelfu ya watu waliandamana hadi makao makuu ya jeshi la Sudan katika majengo ya Wizara ya Ulinzi. Hivyo maandamano hayo yaliishia watu kukaa hapo siku baada ya siku, wiki baada ya wiki na baada ya kung’olewa kwa Bashir, waandamanaji waliendelea kukaa hapo hadi leo.

Amira anasema chaguo hili la makao makuu ya jeshi lilikuwa chaguo gumu sana, lakini lilikuwa muafaka. Kikawaida makao makuu ya jeshi huwa ni maeneo ambayo huzuiliwa watu kuingia, au kupiga picha, hadi kwa vibali maalum.

Lakini hata hivyo jeshi hilo liliruhusu makundi ya watu kuingia kupitia vizuizi vyake. Na si hilo tu, jeshi pia lilichukua hatua ya kuwalinda waandamanaji dhidi ya mashambulizi kutoka vyombo vya usalama wa taifa (National Intelligence and Security forces). Hivyo eneo hilo lilitoa ulinzi na usalama kwa waandamanaji.

Aidha, Amira anaongezea, chaguo la kukusanyikia eneo hilo lilikuwa lina lengo lingine – kwamba waandamanaji walijua fika kwamba “ushirikiano” na jeshi ulikuwa muhimu katika kuhakikisha kupatikana kwa serikali ya mpito.

Anasema haya yote yanatokana na utafiti na historia imekuwa ikionyesha – kwamba maeneo ya umma katika miji yanaweza kuwa yalijengwa kuwakilisha mamlaka za serikali, lakini mara kadha hutwaliwa na wananchi na kuwa maeneo ya harakati dhidi ya serikali.