Home Makala AJALI YA ARUSHA, TUTAZAME NA UPANDE WA PILI

AJALI YA ARUSHA, TUTAZAME NA UPANDE WA PILI

1714
0
SHARE
Basi ambalo lililopata ajali na kusababisha vifo vya wanafunzi 33

NA OVERCOMER DANIEL,

TAARIFA ya ajali iliyotokea wilayani Karatu, mkoani Arusha ilianza kusambaa mitandaoni. Kwa kasi iliyotumika kusambaza na vielelezo vya picha vilivyoambatanishwa kwenye taarifa za ajali hiyo niliamini kuwa ni taarifa ya kweli.

Taarifa ya ajali hiyo imenishtua, imeumiza na imeleta simanzi kwa wazazi, hivyo natoa pole kwa wazazi, walezi, wamiliki wa shule, serikali ya mkoa wa Arusha, Wizara ya elimu na taifa kwa ujumla.

Sambamba na hilo napenda kueleza kwa uwazi kabisa kwa natofautiana na Mkuu wa mkoa wa Arusha,  Mrisho Gambo aliyehitimisha taarifa yake ya ajali hiyo kwenye ukurasa wake kuwa “Bwana alitoa na bwana ametwaa”, kauli ya kukariri, kauli ya kimazoea. Yaani Mungu huyu alingoja watoto watoke shuleni, akawasubiri njiani pale, kwenye korongo lile ili awatwae? Hapana!

Ni kweli tumeumia, lakini tuache mazoea, kwamba watu watakufa, tupaokea taarifa, tutashtuka halafu tutaomboleza kwa kusema bwana alitoa na bwana ametwaa, kisha tuendelee na shughuli zetu tukisburi Bwana awatwae wengine?

Mwaka 1996 walikufa watu kwenye Mv Bukoba, wengine kwenye Mv Spice Islanders maeneo ya  Nungwi Zanzibar, zimetokea ajali nyingi zisizo na vichwa wala miguu, tunalia, tunasema Bwana alitoa kisha tunaendelea na maisha! Tuambiane ukweli; tutafakari pamoja haya.

  1. TUANZE NA HIYO COSTA YA WANAFUNZI ARUSHA:

Tunaambiwa walitumia basi dogo aina ya Costa. Hapa tunaweza tusijadili juu ya vifo bali idadi ya vifo. Tunaambiwa wamefariki takribani watu 32, ukimuondoa dereva tutazungumzia abiria 31 kama hiyo ndio idadi ya vifo. Je, hakukuwa na uwezekano wa kupungua vifo hivyo? Usinishangae kwa swali hilo, fuatana na mimi!

Je, vifo hivyo vimesababishwa na gari kuanguka tu au hata waliokuwa waliokuwa hai walikufa kwa sababu ya kubanana? Kwa nini kubanana? Angalia gari iliyopata ajali, ni Toyota Costa, kwa hesabu za haraka (ruksa kunirekebisha) ina uwezo wa kubeba abiria (labda) wasiozidi 25-28, akiwemo dereva wakiwa wamekaa kwenye viti. Idadi ni vifo 32, hao wengine 7 walikuwa wamekaa wapi?

Mwezi Februari na Machi nilipata kuandika makala fupi mtandaoni kuelezea hatari inayowakumba wanafunzi wanaobebwa kwenye magariu hayo. Kwa ufupi nilitoa tahadhari juu ya uwezo wa magari hayo kubeba wanafunzi wengi kuliko idadi ya viti.

Nilieleza namna ambavyo magari mengi ya kubeba wanafunzi yanavyobeba watoto wetu kwa kuwarundika kama mizigo humo, wengine walidhani najifurahisha kwa kuhoji jambo hilo.

Sikuishia mtandaoni pekee bali nilifunga safari mpaka shule moja kwenda kuwakemea (na niliwakemea kweli kweli), na kuwataka waache tamaa, sisemi hayo ndio yametokea Arusha, nimesema tutafakari upande wa pili wa ajali hii!

  1. TUSIMSINGIZIE MUNGU:

Tusikimbilie kujitetea au kujivua lawama kwa kusema Bwana ametwaa katika kila ajali, inawezekana (inawezekana) ni uzembe na upuuzi wetu kama jamii unatawala maisha ya watu kwa mambo mengi hapa nchini. Mpaka leo naamini kuna magonjwa kama kipindupindu ni ya kujitakia huku tukisema Bwana ametwaa.

Kwa nini nasema tusimsingingizie Mungu?

  1. MAGARI MABOVU: Naomba wataalamu waende barabarani wakafanye utafiti, waende kwenye mashule wakafanye utafiti, magari mengi sana ni mabovu, angalia magari (vi hiace) vinavyofanya safari ndani ya jiji la Mbeya, mengi mabovu, kutembea barabarani hakutoshi vipi kuhusu afya za wasafiri, viti wanavyokalia na kadhalika?
  2. BARABARA ZETU: Hili halina ubishi hata kidogo, tuna barabara nyembamba na zingine huwa za shida kipindi hiki cha mvua. Angalia mazingira ya eneo ambalo basi hilo la wanafunzi limepatia ajali.

Je, hakuna uwezekano wa kuwa na barabara zinazoweza kupitika wakati wa masika na kiangazi bila shida? Je, kwa hali ya nchi yetu tunahitaji zaidi ndege au treni kuliko barabara? Kamwe sikosoi maamuzi ya serikali kununua ndege, bali najaribu kuona what could be implemented first! Nina uhakika nchi hii inahitaji madaraja, barabara na upanuzi wa barabara kuliko usafiri mwingine.

  1. MADEREVA WETU: Sijatembea sana duniani, lakini nadhani nchi hii ina madereva wa ajabu kuliko kwingine kokote. Hivi karibuni nilikuwa nchini Sweden, huko niliambiwa kupata leseni ya udereva ni sawa na kutafuta PhD Chuo kikuu cha Dar es salaam, na kwamba ukija kunyang’anywa kisha kuipata tena utazamie sana kudra za Mungu. Nikajiuliza, hivi hali kwetu hali ikoje.

Angalia madereva wetu wa daladala, wengi ni wababe, jeuri, viburi na sifa zingine zisizo za kiungwana, nina mashaka sana ikiwa hawa ndio wangekuwa madereva wa mabasi ya mikoani. Naogopa.

Lakini hata hawa wa mabasi ya mikoani nao kwa nini wazingatie alama za usalama barabarani kwa kuogopa tochi za askari barabarani? Kila kitu kiko wazi kwa nini kama wako sawa hawataki kufuata alama hizo, kwa nini hawataki kufuata miiko ya kazi hiyo? Rejea ajali ya Basi la abiria la City Boy kule Nzega mkoani Tabora mwaka jana. Rejea ajali mbalimbali kisha uliza abiria yaliyotokea kabla ya ajali, watu wakifa tunasema Bwana ametwaa!

  1. ASKARI WETU: Sijasahu na sitasahau, nilikata tiketi mjini Bukoba ili niwahi ndege Mwanza kunileta Dar es salaam. Wakati huo kulikuwa kumetokea ajali mbaya sana ya basi la Mohamed Trans karibu au maeneo ya Katoro, nilishuhudia kwa macho yangu askari aliyekuwa anakagua magari pale alisimamisha basi letu, ndani lilikuwa chakavu sana, na wakati anapanda ngazi Utingo wa basi hilo alimpa rushwa bila kusema chochote, yule askari akarudia Mlangoni.

Kama gari ingekuja kuua watu huko mbele Watanzania wangesema Bwana ametwaa, kumbe askari mmoja kauza roho za watu. Njia ya kutoka Singida mpaka Babati nilikuwa nashuhudia kwa macho yangu wakiruhusu mabasi yapite wakati yalionyesha dhahiri ni mabovu ila wao waliachana na madereva waliovunja sheria za barabarani ikimwemo mwendo wa ‘kasi ya ndege’ ardhini.

  1. JAMII YETU: Hapa naweza kudiriki kusema kuwa pengine jamii yetu ina mchanganyiko wa unafiki na ubinafsi. Wakati wale madereva wa City Boys wanafanya ile mizaha ya kifo kuna abiria walikuwa wanashangilia wasijue wanaaga dunia kwa nderemo, huku tuliobaki tunasema Bwana ametwaa!

Niliwahi kupanda basi Ubungo jijini Dar es salaam kuelekea Tanga kikazi, nilitumwa na bosi wangu ambaye sasa anafanya kazi nchini Ujerumani.

Gari lilijaza abiria kiasi kwamba wengine walikalishwa kwenye korido ya basi. Kitendo cha mimi kuhoji nilishudiwa kwenye basi mbele ya askari wa usalama barabarani pale stendi ya Maili moja Kibaha. Na waliochangia zaidi ni abiria wenzangu ambao walisika wakisema kifo ni mipango ya MUNGU!

HITIMISHO: Nchi hii ina matukio mengi yanayogharimu uhai wa watu wake sio kwa sababu Mungu amependa au Mungu anatwaa, bali kwa kuwa tumejiandalia hivyo. Mfano hai ni ugonjwa wa kipindupindu. Hivi kweli suala la vifo vya kipindupindu ni Mungu anatwaa watu wake? Kweli?

Sijigambi, sijivuni wala sio kwamba naomba kazi, bali nashauri serikali kupitia Wizara ya Afya iunde tume hata ya miaka miwili, sio tume ya kukomesha tu kipundupindu bali pia ya kufanya kipindupindu kibaki historia nchi hii. Na nitaomba kuiongoza hiyo tume (sio kuwa mjumbe, bali kuwa kiongozi wa tume hiyo). Niko serious! Sisemi jitihada zilizopo hazifai, hapana!

Sasa kama kilivyo kipindupindu hata ajali kwa sehemu kubwa sio Mungu anatwaa, mengi yanayotokea yanaweza kudhibitiwa tukitaka. Tukipanga na kuweka mikakati na kuamua kutekeleza! Nimegusia upakiaji wa abiria, miundo mbinu yetu, askari wetu na kadhalika.

Mwandishi wa makala haya  Mchungaji Overcomer Daniel ni msomaji wa gazeti hili.