Home KIMATAIFA Aliyefungwa miaka 73 ajigeuza binti atoroke gerezani

Aliyefungwa miaka 73 ajigeuza binti atoroke gerezani

890
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

MFANYABIASHARA wa dawa za kulevya mwenye jina kubwa nchini Brazil, Clauvino da Silva, mwishoni mwa wiki iliyopita alikuwa gumzo kwa wafuatiliaji wa kila kinachoendelea katika mitandao ya kijamii.

Da Silva aliwashangaza wengi kwa mpango wake wa kutaka kutoroka gerezani anakotumikia kifungo cha miaka 73 baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na usafirishaji wa ‘unga’.

Lakini sasa, huenda kutoroka si ishu, bali kilichoonekana kuwa kituko katika tukio hilo ni uamuzi wake wa kubadili mwonekano wake ili awe kama binti yake, akiamini angeweza kuwapita maaskari bila wao kumshitukia.

Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa na mamlaka, Da Silva mwenye umri wa miaka 42 alipanga na mtoto wake huyo mwenye umri wa miaka 19 aliyekuwa tayari kuingia gerezani kumsaidia kutumikia kifungo.

Ili kuwa na mwonekano huo wa kike, bibiye alimpa Da Silva kinyago kinachofanana na sura yake, wigi na fulana. Aidha, mbaya ni kwamba wakati kila kitu kikiwa kimekamilika, polisi walishitukia baada ya kumwona jamaa akimwomba mwanaye kitambulisho ambacho angekitumia kupita mlangoni.

Katika video iliyosambazwa mitandaoni na mamlaka, Da Silva anaonekana akivua kinyago hicho kilichomfanya kutokuwa na tofauti ya kimwonekano na binti yake huyo.

Wakati huo huo, gazeti maarufu la New York Times, limeiendea mbali stori hiyo, likidai kuwa hii si mara ya kwanza kwa wafungwa kutaka kutoroka gerezani nchini Brazil kwa kutumia staili ya mshikaji.

Chanzo cha habari hicho, Times, kilimtaja Da Silva kuingia kwenye orodha ya wengine 30 waliowahi kufanya hivyo.  Kwa upande mwingine, inasemekena kuwa binti yake ni mtu wa nane katika wale waliowahi kutaka kuwasaidia wafungwa kufanya hivyo.

Huku Times wakieleza hayo, gazeti la Reuters, ambalo pia ni la Uingereza, limeibuka na mwendelezo wa tukio hilo, likiripoti kwamba Da Silva atahamishwa gereza na atakumbana na adhabu kwa kosa alilofanya.

Wengi wanamkumbuka Da Silva kwa jina lake kubwa huko Brazil, akiwa kiongozi wa ‘Red Command’, kundi lenye nguvu nchini humo katika biashara ya dawa za kulevya.