Home Michezo ALIYEMVURUGA BOLT MASHINDANO YA DUNIA ANACHUKIWA BALAA

ALIYEMVURUGA BOLT MASHINDANO YA DUNIA ANACHUKIWA BALAA

1219
0
SHARE

images (1)

MWANDISHI  WETU NA MITANDAO

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Mashindano ya Riadha ya Dunia inayosimamiwa na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo huo  (IAAF) yalianza rasmi jijini London, Uingereza.

Tofauti na matarajio ya wengi kwamba mwanariadha nyota kutoka Jamaica, Usain Bolt angeendeleza rekodi kwa kuibuka na medali ya dhahabu katika mbio za mita 100 matokeo yalikuwa kinyume chake na kuambulia nafasi ya tatu.

Idadi kubwa ya waliojitokeza kushuhudia mbio hizo uwajani walikuwa na matarajio ya kumuona Mjamaica huyo akibeba taji lake la 20 huku akiwa anakaribia kutimiza umri wa miaka 31.

Lakini, aliyekuwa mshindi wa mbio hizo alikuwa ni Justin Gatlin wa Marekani ambaye alitumia sekunde  9.92 kummaliza kabisa staa Bolt.`

Bolt raia wa Jamaica, ambaye  aliambulia medali ya shaba akiwa ametumia sekunde 9.95,  aliishuhudia pia nafasi ya pili ikienda kwa Mmarekani mwingine, Christian Coleman, aliyetumia muda wa sekunde 9.94.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Bolt kupoteza medali ya dhahabu katika mbio za dunia za mita 100 tangu alipoanza kushiriki mchezo huo na moja ya rekodi zake ni ile ya mwaka 2011.

Kabla ya kuibuka kidedea, Gatlin alikuwa kwenye wakati mgumu kwani alipokuwa anaingia uwanjani alikuwa anazomewa na mashabiki wengi.

Mmarekani huyo, mwenye umri wa miaka 35, amekuwa na maadui wengi katika  mchezo huo huku mashabiki wakiamini kuwa ni mtumiaji wa dawa za kuongeza nguvu.

Gatlin, ambaye ni bingwa wa michuano ya Olimpiki ya mwaka 2004, amewahi kufungiwa mara mbili kwa makosa ya kutumia dawa hizo.

Mwaka 2001, akiwa mwanafunzi wa chuo, alifungiwa kushiriki michuano ya riadha akitajwa kutumia dawa aina ya amphetamine ambazo zimepigwa marufuku michezoni.

Hata hivyo,  baada ya mwaka mmoja, alirejeshwa mzigoni baada ya utetezi wake kuwa alizitumia kwa lengo la kupunguza maumivu na si kuongeza nguvu.

Miaka mitano baadaye, akiwa ameshinda mbio za mita 100 na mita 200, mjini Helsinki, Finland, alibainika kutumia dawa nyingine aina ya testosterone.

Alifungiwa miaka nane baada ya kuepuka kifungo cha kutojihusisha na riadha kwa kipindi chote cha maisha yake.  Alipunguziwa adhabu kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa mamlaka zinazopambana na upigaji vita na uzuiaji wa dawa hizo.

Akizungumzia zomea zomea aliyokutana nayo katika mbio hizo mjini London, Gatlin alisema aliamua kuzipuuzia na kuelekeza akili yake kwenye shindano husika na kufanikiwa kuibuka mshindi wa kwanza.

Naye mwanariadha nyota wa Marekani, Michael Johnson, ameibuka na madai kuwa Gatlin alizomewa kwa kuwa alikuwa tishio kwa Bolt.

Johnson, mwenye umri wa miaka 49, ameongeza kuwa tatizo lililopo ni kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikimwangalia zaidi Mmarekani mwenzake huyo na kuwaacha wanamichezo wengine.

“Katika michuano ya mwaka 2012 mjini London, hakuna aliyekuwa akimzomea Gatlin. Alipoanza kumkaribia Bolt katika michuano ya dunia ya mwaka 2015, ndipo ilipoanza hiyo tabia,” alisema.

Kwa upande wake, baada ya Bolt kupotezwa na Galt, Waziri Mkuu wa Jamaica hiyo, Andrew Holness, ameshauri kufungiwa maisha kwa kila mwanamichezo atakayebainika kutumia dawa za kusisimua misuli.

“Hiyo ndiyo njia pekee ya kuwahakikisha watu kwamba hawatakiwi kudanganya katika michezo,” alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, licha ya kuangukia pua kwa Gatlin, bado nyota ya Bolt iliendelea kung’ara ambapo alilazimika kuwa wa mwisho kuondoka uwanjani kwa lengo la kusalimia mashabiki takribani 50,000 waliojitokeza kumpa sapoti.

Kwa mujibu wa ratiba, Bolt atamaliza maisha yake ya mchezo wa riadha Agosti 12 ambapo atashindana mbio za mita 400 na baada ya mashindano hayo atastaafu rasmi mchezo huo wa riadha.

 

Itakumbukwa kuwa hazitakuwa mbio za mchezaji mmoja mmoja bali kwa timu yake ya Taifa ambayo ndiyo inayolitetea taji hilo.

 

Endapo Jamaica itafanikiwa kuchukua tena,  basi Bolt atakuwa amefikisha medali 12 za dhahabu, akimwacha Mo Farah wa England anayeshika nafasi ya pili atakayewakilisha nchi yake pia.