Home Makala AMA KWELI CHADEMA NI “WATAKATIFU”

AMA KWELI CHADEMA NI “WATAKATIFU”

790
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA


NIMEBUTWAISHWA na kitendo cha kubainika Diwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Julist Kisoma kuwa hajui kusoma wala kuandika. Taarifa hiyo iliripotiwa na gazeti la Mtanzania Jumapili desemba 18 mwaka huu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa, lilichukua uamuzi wa kumsimamisha diwani huyo na kumtaka kutohudhuria vikao vya baraza hilo kwa tuhuma za kuidanganya Tume ya Uchaguzi na wananchi wake kuwa anajua kusoma na kuandika.

Kugundulika kwa diwani huyo kulikuja baada ya kukacha kusoma taarifa ya kata yake mara tatu mfululizo hali iliyolilazimu baraza hilo kumchukulia hatua. Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Halmashauri, Charles Makonga, diwani huyo hatahudhuria vikao na shughuli zozote za kuwawakilisha wananchi hadi pale tume itakapotoa uamuzi juu yake.

Kulingana na taarifa hiyo tunaweza kupata mantiki kwakuwa diwani hajui kusoma wala kuandika; Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano imedanganywa. Kamati Kuu ya Chadema imedanganywa nayo ikadanganya.

Wapigakura wa Mafinga wamedanganywa nao wakatudanganya taifa zima kuwa diwani wao si Kihiyo. Kwa maana hiyo hii nayo ni kero tupu na aibu.

Kwa muda mrefu tumewashuhudia manazi na wafuasi wa Chadema wakijipambanua kama chama kisicho na makosa. Wanajitapa kuwa chama chao hakina makosa ya kipuuzi. Chadema wamejijengea dhana hiyo kwamba wao ni chama ambacho kina mwelekeo wa ‘utakatifu’.

Labda tuseme Chadema ni chama cha watakatifu na malaika ambao hawajapata kukosea. Niwaombe radhi ndugu zangu wakristo kwa matumizi ya neno “watakatifu”, lakini ndilo linalowafaa chadema.

Nakifahamu chadema kama chama ambacho kimejijenga hatua kwa hatua na kuibuka na makada wapya kinyume cha matarajio ya miaka mingi kuwaona makada wa CCM wakihamia upinzani. Pamoja na sifa za kuwa chama kikuu cha upinzani, ipo sifa ya ziada ambayo wafuasi na viongozi wanajijengea kuwa wao Ni “watakatifu”.

Nami nawakubalia ni chama cha watakatifu na wanaongozwa na mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye ni kama malaika wao. Mbowe hakosei. Mbowe hana doa. Mbowe hana sifa mbaya iwayo yoyote tangu kuumbwa kwake na kuanzishwa kwa Chadema.

Nami nasema Chadema tangu kianzishwe hakijawahi kukosea. Hivi chama cha watakatifu na malaika kitakoseaje? Ndiyo maana imekuwa rahisi kumleta diwani kihiyo. Kwanini Kihiyo? Sababu mwaka 1996 aliyekuwa mbunge wa Temeke kupitia CCM, Ramadhani Kihiyo aligundulika kudanganya kiwango cha elimu yake.

Ilibainika kuwa hakuwa na elimu ya chuo kikuu kama alivyojinasibu. Kwamba Ramadhani Kihiyo alikuwa na elimu ya darasa la Saba tu. Kugundulika udanganyifu huo kulisababisha kufutwa Matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi wa kiti wa cha ubunge.

Hivyo uchaguzi wa marudio ukampa ushindi Augustine Mrema kuwa mbunge wa Temeke kupitia NCCR-Mageuzi. Kumteua mtu aliyedanganya elimu kuliifedhehesha CCM.

Wapigakura wa Temeke walifedheheka pia. Tume ya uchaguzi ikadanganganywa nayo ikawadanganya watanzania. Ndiyo kusema CCM kilionekana kama chama chenye kubeba uchafu mwingi mno ikiwemo wadanganyifu.

Tafsiri nyingine ilikuwa ni udhaifu wa Kamati Kuu ya CCM kutofahamu vema makada wake na elimu zao. Lilikuwa tukio lililoichojoa nguo CCM hususani jimbo la Temeke ambalo lipo katika mji mkuu wa kimataifa na na kibiashara na kwamba ndiyo “mapokezi” ya Tanzania.

Kutenguliwa ubunge wa Kihiyo kulileta ahueni kwa upinzani. Hata hivyo, wakati tukidhani kuwa tukio la mwaka 1996 kumhusu Kihiyo, ambaye alishindwa kesi mahakamni kwa kukosa vielelezo (vyeti) vya kuthibitisha elimu yake, kwa upande wao Chadema “hawajakosea”.

Walimteua diwani “msomi” ambaye asingeweza kukacha kusoma taarifa za Kata yake. Chadema wamedhihirisha kuwa wao ni mabingwa wa kuishi “kitakatifu” kwani hawajawahi kuwa na diwani kilaza bin mbumbumbu isipokuwa chama chao ni “kitakatifu” mno kuwahi kutokea duniani.

Kamati kuu ya Chadema imejaa wasomi. Imamteua mwanachama huyo kuwa mgombea udiwani kwakuwa….ni msomi ambaye hakutenda kosa. Nasema hivyo kuwa ndugu zetu wa Chadema wamejinasibu na kujitapa kila jukwaa wanalopata kuzungumza kwamba chama chao ni cha kisomi na wagombea wake bila shaka walikuwa wasomi pia. Sijui diwani huyo amekutwa vipi kuwa hajui kusoma wala kuandika.

Twaweza kubaini sasa kuwa alijaziwa fomu za kuomba kugombea ndani ya Chadema na baadaye NEC. Na hivyo tunaweza kuamini kuwa Kamati Kuu ya Chadema “haikudanganywa” kwakuwa siku zote imejipambanua kuwa “haidanganyiki”. Ndiyo kusema chama cha watakatifu kinachoongozwa na malaika hakiwezi kukutwa na takataka zozote zile.

Ndiyo kusema suala la kuwa na mgombea kilaza limekuwa “likilelewa CCM” pekee na vyama vingine visivyo vya kitakatifu ambako inalekea kuna viongozi wachovu na wenye kila aina ya mchoko.

Ndiyo kusema chama tawala kimezidi kuwa jamvi la uchafu huku chadema kikiwa chama cha wenyeheri. Kwanini nimetumia neno “watakatifu”? Kwasababu Chadema wanaonekana kuamini kuwa makosa yameumbwa kwaajili ha CCM na vyama vingine.

Ndiyo maana ilikuwa rahisi kuvituhumu CUF, NCCR-Mageuzi na baadaye ACT-Wazalendo kama CCM-B. Kwamba vyama hivyo vilikuwa vikitumika kwa maslahi ya CCM. Sijawahi kuona wafuasi wa CCM wakipinga au kukubali hoja hiyo, na pengine tuseme wameshindwa kushughulika nayo au wameipuuza.

Bahati mbaya ikiwa wamepuuza basi wanatakiwa kukumbushwa kuwa walituletea Kihiyo na wao siyo watakatifu. Ila Chadema wametuletea Kisoma “mtakatifu” na msomi wa ngazi za juu.

Ndiyo kusema chadema wanatudhihirishia utakatifu na kwamba masuala ya elimu na figisu zake zipo kwa Chama cha Mapinduzi, na wale wote wasiokuwa wafuasi wa UKAWA. Kwaajili Hiyo tunajionea uzalendo na ukamanda wa diwani Julist Kisoma! Ama hakika ni utakatifu wa ngazi za juu. Kwaherini.