Home Makala ANAYEKUFA NI MTU, FIKRA ZA MTU HAZIFI

ANAYEKUFA NI MTU, FIKRA ZA MTU HAZIFI

1294
0
SHARE

Na Victor Makinda


Wapenzi wasomaji wa safu hii ya Ukweli Ulivyo hususani wale mliokuwa mkivutiwa na mfululizo wa makala, Wakati wenzetu wanakwenda sayari nyingine sisi twende vijijini,mtaniwia radhi. Wiki hii sitoendelea na mfululizo wa makala hizo ambapo kimsingi nilikuwa naingia sehemu ya sita.

Sababu ya kutofanya hivyo ipo na imekuwa nje  ya uwezo wangu. Mfululizo wa makala hizo utaendelea kwani yapo mengi  ya kuandikwa vijijini. Natoa shukrani kwa wasomaji wote ambao mnaonipigia simu na mnaonialika kwa ajili ya kuja vijijini kwenu kujionea hali halisi. Nitakuja na nitaendelea kuvitembelea vijiji nikiwa na lengo la kuibua changamoto zinazokabili vijiji vyetu. Panapo majaliwa wiki ijayo nitaendelea na mfululizo huo wa makala za vijijini.

Katika safu hii ya Ukweli ulivyo leo hii ninakualika msomaji wangu tujadili pamoja nguvu na uwezo wa kuishi kwa fikra ambazo kimsingi fikra hizo hazifi kamwe. Ndiyo, Fikra hazifi unaokufa ni mwili.

Mwanamapinduzi Ernesto Che  Guevara,  aliwahi kunukulia maneno makali aliyoyatamka kuhusu nguvu na uwezo wa fikra zake. Che Guevero alisema, “ Najua unataka kuniua, Siogopi maana atakayekufa ni mtu na wala sio mimi, kwani mimi ni fikra ambazo hazitakufa kamwe”.

Ulishawahi kujiuliza swali kuwa wewe ni nani? Unaijua tofauti kati yako na fikra zako? Umewahi kujiuliza kuwa ikiwa utakufa utaacha nini Duniani? Wewe ni mwili, utakaokufa, na ikiwa umekufa na kuoza wanaobaki duniani watakukumbuka kwa lipi?  Njia pekee ya wewe kukumbukwa ni ama fikra zako au matokeo ya uliyoyafanya kutokana na fikra zao.

Ndiyo, ipo tofauti kubwa sana kati ya kuua mwili na kuua fikra. Wengi waliouawa au kufa kwa sababu ya fikra zao, waliokuwa na fikra sahihi,  wanaendelea kuishi. Miili yao ilikufa na kuzikwa lakini fikra zao zimebaki zikiishi na kamwe  hazijafa, nazo zinaishi hata sasa.

Tunayo mifano mingi juu ya fikra na nguvu ya fikra kuishi. Yesu Kristu, aliuuawa kifo cha kuwambwa msalabani. Yesu kama mwanafalsafa  nguli aliyewahi kuishi ulimwenguni, alikuwa na maono na fikra juu ya namna iliyo njema iliyompasa mwanadamu kuishi.  Yesu alikuwa na fikra za kupinga uonevu, ukandamizwaji na kusisitiza usawa wa kiutu.

Mafundisho yake yaliyojawa na maelekezo na maonyo juu ya namna mwanadamu anavyopaswa kuishi maisha yenye ustawi wa kiroho na binadamu mwingine. Alifundisha na kuelekeza watawala jinsi ambavyo wanapaswa kutawala vyema na namna ambavyo watawaliwa wanapaswa kuishi katika kutii mamlaka za utawala. Lakini fikra hizo zilionekana kuwa zinatishia ustawi wa utawala wa Wafalme na Makuhani wakuu. Yesu aliundiwa zengwe na kuwambwa msalabani hatimae kufa.

Lakini kifo chake kamwe hakikuua fikra zake. Kinyume chake fikra zake zimekuwa hai na zimepata umaarufu maradufu baada ya yeye kufa kuliko wakati alipokuwa hai.

Ipo mifano mingi mno ya fikra zinazoishi, Nelson Mandela, rais wa kwanza wa Afrika kusini huru, Utawala dhalimu wa kikaburu ulioshehenezwa na ubaguzi wa rangi na ukandamizaji na mauaji, ulimfunga jela mika 25. Lengo lilikuwa ni kufifisha fikra zake za kudai usawa, umoja, mshikamano na utengamano wa kitaifa. Fikra hizo ambazo zilimsukuma Mandela na waafrika wengine kuungana pamoja kupambana na ubaguzi wa rangi na ukoloni wa kisiasa na kiuchumi, ziliwakasirisha makaburu wa Afrika Kusini, Walimfunga Mandela kwa kipindi kirefu, wakidhani kuwa baada ya kifungo hicho kirefu, huenda atabadili fikra na mtazamao wake, lakini Mandela alibaki kuamini anachokiamini na hata baada ya kutoka gerezani aliendelea na harakati zake za kudai uhuru na hatimae kuupata uhuru huo toka kwenye makucha ya Makaburu. Mandela aliendeleza fikra zake za kuiona Afrika ya Kusini inayojali utu na undugu. Kuiona Afrika Kusini isiyo na ubaguzi wa rangi, matabaka wala uchumi wenye kutoa fursa upande mwingine na kunyima fursa kwa wazawa. Mandela baada ya kupata Uhuru na kuwa rais wa Afrika ya Kusini,alisamehe yote, alipandikiza usawa, utu wema na hali ya kiuchumi isiyo na matabaka kwa baadhi ya tabaka. Fikra za Mandela zinaishi na amekuwa ni mfano wa kuigwa mahali pote ulimwenguni. Hata hao wazungu ambao walimtweza wanaziheshimu mno na kuzienzi fikra zake ijapokuwa amekwisha kufa.

Hapa kwetu nyumbani Tanzania, tunaye Shujaa wetu wa Fikra zinazoishi. Huyu si mwingine bali ni  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanganyika huru. Huyu ni nguli wa fikra za kiuanamapinduzi. Mwalimu Nyerere alikuwa na fikra za mbali, si Tanzania pekee bali bara la Afrika na Ulimwengu kwa ujumla.

Yeye pamoja na kuhakikisha nchi yake Tanganyika/Tanzania inapata Uhuru, haikutosha bali alihakikisha kuwa nchi nyingine ambazo bado zilikuwa zikitawaliwa zinapata uhuru.

Mwalimu Nyerere alikuwa  Mwanamapinduzi wa fikra. Hotuba zake zimesheheni hekima kubwa ambazo zimejielekeza katika umoja, mshikamano na usawa wa kiutu.  Aliamini katika umoja na utu wenye kujaliana. Aliamini katika muungano na usawa. Alihakikisha kuwa jamii ya kitanzania inakuwa moja. Alichukia rushwa, wizi, ukandamizaji, ukoloni mambo leo, lakini kubwa zaidi alichukia sana utawala wa kiimla. Mwalimu Nyerere aliwachukia watawala wote waliokuwa  hawaheshimu demokrasia na kugeuka kuwa madikteta. Fikra zake zingali zinaishi na kuzidi kuamsha ari ya kuungana kama jamii moja. Tanzania iliyotoka na fikra za Mwalimu Nyerere ni moja hata sasa.

Mwalimu Nyerere alikuwa na fikra na aliamini katika fikra za ujamaa, na kuhakikisha kuwa kama Taifa tunanufaika na rasilimali zetu. Aliamini kuwa kama Taifa tunapaswa kuhakikisha kuwa rasilimali zetu zinatunufaisha sisi sote kwa pamoja na sio zinufaishe kikundi fulani cha watu na kuiacha jamii pana ikitaabika kwa kukosa mahitaji muhimu. Mwalimu Nyerere, alikuwa na fikra na maono ya usawa, utu wema, umoja na mshikamano.  Katika kuamini katika fikra hizo, alijitengenezea maadui wengi wa ndani na nje. Wapo waliomtazama kama mtu hatari kabisa katika ustawi wao. Lakini wapo waliomtazama kama mwanamapinduzi mkombozi wa wanyonge. Hii ndiyo sababu, ijapokuwa amekufa, amekufa mwili, lakini fikra zake zingali zinaishi hata sasa. Ukisikiliza hotuba zake, alichokuwa akikizungumza miaka ya 60 ni kama vile anazungumza leo. Hakika huyu alikuwa mfano bora wa mwanafikra ambaye fikra zake zinaishi.

Leo hii mahali pengi duniani, hotuba za Mwalimu Nyerere zimebaki kuwa kielelezo kikubwa cha kuhubiri usawa wa kiutu, usawa wa kiuchumi na usawa wa kiutawala na kuheshimu mawazo ya wengine katika kukuza demokrasia pana. Hapa kwetu Tanzania, ni nadra sana kusikiliza hotuba iwe ni ya kiongozi wa siasa au wa kiserikali pasipo kiongozi huyo kunukuu maneno ya Mwalimu Nyerere. Huu ni mfano wa kuishi kwa fikra.

Ukweli Ulivyo, Watawala wengi wa kiafika hasa hasa wale ambao huamini kuwa wao ni bora zaidi kuliko wengine, wale wanaoamini katika mawazo yao, wale wasioamini katika fikra mbadala, wamekuwa ni wakandamizaji wakubwa na waonezi kwa watu, au makundi ya watu wenye fikra mbadala. Watawala hawa wanasahau kuwa fikra mbadala ni chanzo kikubwa cha ustawi wa  kijamii na kiuchumi. Wengi wao wanaamini kuwa na fikra mbadala ni kuasi. Jambo ambalo sio la kweli.

Katika maisha ya biniadamu, iwe ni kiongozi au mtu yoyote awaye, anahitaji mchango wa kifikra kutoka kwa watu wengine. Haijalishi fikra hizo zinaweza kukwaza kiasi gani bali ifahamike kuwa fikra mbadala zi muhimu mno katika ujenzi wa uchumi imara, umoja, mshikamano na utulivu.

Nimalizie tu kwa kutoa wito kwa viongozi wa Ulimwengu huu, iwe ni wa vyama vya siasa au wa serikali za kiafrika, kuacha kuwanyanyasa wale wote ambao wanaonesha kuwa na fikra mbadala. Wapo viongozi ulimwenguni waliodirika hata kuwaua wale wote walioonesha kuwa na fikra mbala dhidi ya tawala zao. Ifahamike kuwa kuwatweza au kuwaua watu wenye fikra mbadala sio suluhu. Kwani kuua au kutweza mwili sio kuua fikra. Fikra huishi daima dumu. Fikra huvuka kizazi hata kizazi. Fikra sahihi za mtu hazifi, unaokufa ni mwili.