Home Habari kuu ANGUKO LA CHADEMA LASUKWA

ANGUKO LA CHADEMA LASUKWA

5921
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI            |            


HATUA ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuendelea kuwa chama kikuu cha siasa nyuma ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatajwa kuwa sumu kubwa kwa chama hicho hali inayosababishia kusukwa kwa mkakati wa kukimaliza. RAI linachambua.

Mkakati unaosukwa sasa unafananishwa na ule uliowahi kukikumba chama Cha NCCR-Mageuzi mwaka 1996 na Chama cha Wananchi CUF, 2016.

Duru za habari zinabainisha kuwa kwa sasa Chadema inawaka ndani kwa ndani na kama hakutakuwa na jitihada za kusimama imara ni wazi chama hicho hakitafika salama mwaka 2020.

Tayari chokochoko zimeanza kuelekezwa kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho, ambapo yapo makundi ndani ya chama yameanza kuunda mitandao yao ili kufanikisha dhamira ya kumng’oa mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe, ambaye anatajwa kuwa mtu mwenye misimamo isiyoyumba.

Misimamo na uimara wa Mbowe tangu alipochukua nafasi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake Marehemu Bob Makani mwaka 2004, inatazamwa kama kikwazo kikubwa cha kuiyumbisha Chadema.

Wanaopanga mikakati hiyo wanaamini kuwa haitawawia rahisi kufanikisha dhamira ya kuidhoofisha Chadema kama Mbowe ataendelea kuwapo kwenye nafasi hiyo kwani mara nyingi amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha chama hicho hakipasuki wala kuanguka.

Ukweli wa hilo unanasibishwa na kile alichokifanya Mbowe Mwaka 1995 wakati huo akiwa kijana, ambapo Edwin Mtei na Bob Makani wote wawili walichukua fomu ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wote walionekana kuwa na nguvu.

Mpambano huo ulileta sitofahamu kubwa ndani ya Chadema, hata hivyo Mbowe akiwa mwanasiasa kijana alitoa ushauri kwa chama kwamba kisisimamishe mgombea urais ili kuepusha mpasuko ndani ya chama na badala yake wamuunge mkono mgombea wa urais kupitia NCCR Mageuzi Agustine Lyatonga Mrema ambaye wakati huo alikuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa wananchi wengi.

Ushauri huo wa Mbowe uliungwa Mkono na wanachama na viongozi wa Chadema na kuwafanya Mtei na  Makani kuachana kabisa na mchakato huo wa kuwania urais na chama kumuunga mkono Mrema.

Hatua hiyo ya mwaka 1995 na ile ya mwaka 2000 ya kukishauri chama kutosimamisha mgombea urais ili kumuunga mkono mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, zinadaiwa kuwa hatua muhimu ya kuonesha uimara na misimamo ya mwanasiasa huyo.

Katika kuhakikisha kizingiti hicho kinavukwa kwa weledi wa hali ya juu, wasuka mikakati wameamua kuzitumia chaguzi za ndani za chama hicho ambazo kwa sasa ziko ngazi ya chini, kusimika watu wao kwenye nafasi mbalimbali ili iwe rahisi kunadi hoja ya kumtaka ang’atuke au kumshinda kwa namna yoyote ile kwenye sanduku la kura.

Wanaotajwa kutumika kuendesha mkakati huo baadhi yao wanadaiwa kuwa watu wa karibu na Mbowe na wengine ni wananafasi za uongozi walizozipata kwa mgongo wa Mwenyekiti huyo.

Wanachama wanaotajwa kutaka kumgeuka Mbowe wanahusishwa na makundi mawili, kundi la Chadema asilia kwa upande mmoja na kundi la Chadema wa kuja kwa upande wa pili.

Makundi haya yanajitofautisha kwa kauli na matendo yao, zipo taarifa kuwa si wanachama wa makundi yote haya wanataka Mbowe ang’oke, lakini pia si wote wanaotaka abaki hali inayosababisha mgawanyiko ndani ya chama na kwenye makundi hayo.

Hoja zinazobebwa na wasiomtaka Mbowe ni kwamba ameongoza chama hicho kwa muda mrefu, hivyo anapaswa kung’atuka ili kupisha fikra mpya.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vincent Mashinji ameyaonya makundi hayo na kuyaahidi kuwa kamwe hayatopata nafasi ya kupenyeza mbinu na hila zao katika uchaguzi wa chama hicho.

“Naomba nisaidie kuwafikishia ujumbe kwamba…wale wanaofikiria kuwa wao ni kundi fulani au kundi lile, Chadema haina room hiyo na hawana nafasi ndani ya chama,” alisema Dk. Mashinji alipozungumza na RAI wiki hii.

Aidha, akifafanua kwa kina kuhusu makundi hayo yanayodaiwa kutaka kuugawa uchaguzi, Dk. Mashinji alisema kinachoendelea sasa kuhusu makundi hayo mawili ni propaganda zinazotengenezwa na baadhi ya makada wa CCM.

Alisema ndani ya Chadema hakuna mwanachama wa kuja na asilia kwa kuwa kila mtu ni asilia ndani ya chama, haijalishi muda wala saa alizoingia.

“Unaweza kuingia asubuhi saa mbili, saa tatu ukachaguliwa kuwa mwenyekiti wa taifa, hata kama uliingia miaka 10 iliyopita unaweza kuchaguliwa, kwa hiyo haijalishi muda uliyoingia.

“Kama kuna hisia za watu wenye kundi hilo wanafikiria hivyo, au kama kuna watu wanaojitenga kimakundi, niwaambie wazi kuwa wapo kwenye maamuzi mabaya, kwa sababu Chadema hamna kitu cha namna hiyo, ndio maana mimi ni Katibu Mkuu na wangesema hivyo wangeanza kutafuta nani tulikuwa naye kwenye maandamano mwaka 1997.

“Pia ndio maana Lowassa aliingia asubuhi, jioni akawa mgombea urais. Jambo la muhimu ni kwamba nani anabeba ajenda yetu kwa watanzania na yuko tayari kuipigani na kuivusha Chadema,” alisema.

SUMAYE, DK. MASHINJI WATAJWA

Katika kuchagiza hoja ya kumng’oa Mbowe inadaiwa tayari wasuka mikakati wameshaanza kupendekeza watu wao ambao wanaamini itawawia rahisi kwao kuwanadi na kufanikisha malengo yao.

Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ya chama hicho, Frederick Sumaye anatajwa kuwa mtu sahihi atakayeweza kumrithi Mbowe.

Mbali na Sumaye mwingine ni Dk. Mashinji ambaye kwa kauli yake amekiri kuhusishwa na jambo hilo la kutaka kumrithi Mwenyekiti wake.

“Kuna wengine wamenitaja hata mimi, sielewi wanapotaja wanakuwa na interest gani, lakini nikiwa kama Mtendaji Mkuu wa chama ninachoangalia kwa makini ni kanuni zetu na jinsi ya kutangaza nia ya kugombea cheo.

“Katika ngazi ya Taifa mtu anayetaka kugombea anatakiwa kuitaarifu ofisi ya Katibu Mkuu, sasa kama hawajatutaarifu itakuwa ni stori za watu wanaotunga na kuhisi labda fulani anafaa, ila na sisi kwenye chama tuna taratibu zetu,” alisema.

UCHUNGUZI

Pamoja na Dk. Mashinji kutoa tahadhari kwa wenye nia ovu na chama, lakini pia amebainisha kuwa ili kukwepa viongozi mamluki wa chama kuanzia ngazi za chini, wanaendelea kuwachunguza makada wote walioonesha nia ya kutaka kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama hicho.

Aidha, alisema milango iko wazi kwa wanachama wa chama hicho kujitokeza kuwania nafasi yoyote ndani ya chama kwa kuzingatia taratibu na kanuni za pale wanapotangaza nia na kamwe wasiogope kujitokeza.

“Tunataka tuende vizuri, chama kijengwe kwenye misingi imara, kwa hiyo tunatumia muda wetu, hatuna presha tunakwenda taratibu tunamchunguza kila mtu anayetaka kuwa kiongozi kwamba ana nia gani, anapenda kukijenga chama, hata sasa nipo Nachingwea kwa kazi hiyohiyo.

“Sasa tuko kwenye uchaguzi ngazi za chini kwa hiyo kisheria na kwa katiba yetu tupo ndani ya muda hata mpaka mwaka 2020 ila tuliamua tu kusogeza mapema ili kama tutamaliza mapema uchaguzi wa ngazi za chini, kabla ya kufikia mwisho wa mwaka huu tutafanya uchaguzi mkuu wa ngazi ya viongozi wa kitaifa,” alisema na kuongeza;

“Hakuna sababu ya wanaotaka uongozi kutangaza kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa mtu anayefanya hivyo anapoteza sifa za kupitishwa kugombea. Kwa hiyo suala la mtu kutaka kutoa mchango wake katika ukuaji wa chama ni suala ambalo hatuwezi kulizuia.”

Alisema katiba ya Chadema haina ukomo wa Mwenyekiti wa sasa kuendelea kugombea hivyo inamruhusu kuendelea kugombea tena na tena.

Hili litakuwa jaribio la tatu la kutaka kumng’oa Mbowe, kumbukumbu zinaonesha jaribio hilo liliwahi kufanyika katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi wa ndani wa mwaka 2009, ambapo marehemu Chacha Wangwe ndie aliyekuwa akitajwa kuwa mwiba kwa Mwenyekiti wake.

Hata hivyo, Wangwe hakufikia dhamira yake hiyo baada ya kufariki kwa ajali usiku wa Julai 28,2008 alipokuwa njiani kuelekea Dar es Salaam, akitokea bungeni Dodoma, ambako alihudhuria kikao cha Bunge cha asubuhi na baadae kufunga safari ili awahi kumzika Mzee Bhoke Munanka.

Mwaka 2013 kuelekea kwenye uchaguzi wa ndani wa mwaka 2014 lilifanyika jaribio jingine lililoongozwa na kundi la Zitto Kabwe ambao kwa pamoja walidaiwa kutengeneza mkakati wa kumng’oa Mbowe kwenye nafasi yake hiyo.

KAULI YA SOSOPI

Dk. Mashinji alisema kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi kuwa wapo tayari kuongozwa na Mbowe hata miaka 10 ijayo ni maoni yake binafsi.

Alisema hatua zinazochukuliwa na Bavicha pamoja na matamko yanayotolewa na viongozi hao ni mojawapo ya chachu ya kuwafunza vijana kutokana na makosa wanayoyatenda sasa wakiwa ndani ya Bavicha.

“Muda wa miaka 35 ukifika na kutoka kwenye baraza tunakuwa tayari tumepika viongozi ambao wameiva,” alisema.

ANGUKO LA VYAMA VYA SIASA

Historia ya kisiasa nchini hasa siasa za upinzani, inaonesha wazi kumekuwa na utamaduni wa migogoro ya ndani ya vyama imekuwa ndio njia rahisi ya kusuka mikakati ya kuviangusha vyama hivyo.

Ukweli wa hilo unanogeshwa na anguko la NCCR-Mageuzi mwaka 1999-2000, chama hicho ambacho kilikuwa na nguvu kubwa kilijikuta kikisambaratika na kupotea kabisa kwenye siasa za ushindani.

Sababu kuu ikiwa ni kuibuka kwa makundi mawili moja likiongozwa na Mrema na jingine likiongozwa na Mabere Marando.

Muongo mmoja baadae CUF nayo ilianza kutumbukia shimoni, hata hivyo jitihada kadhaa za kukinusuru chama hicho ambacho kwa sasa kimegawanyika kabisa zilifanyika.

Pamoja na jitihada hizo CUF haikuweza kusimama imara kama ilivyokuwa mwaka 2000, na hali imekuwa mbaya zaidi mwaka 2016 mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho nusura kianguke mwaka 2015 baada ya kuibuka kwa mgawanyiko mkubwa uliohusisha makundi ya wagombea urais.

Kama si uimara wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Jakaya Kikwete na busara za wazee wa CCM huenda leo hii, chama hicho kingekuwa pinzani.

Historia ya kuvitikisa vyama vya upinzani vyenye nguvu sasa inaonekena kuelekezwa kwa Chadema, ambacho kwa zaidi ya miaka 10 sasa kimekuwa chama kikuu cha upinzani nchini.