Home KIMATAIFA ANGUKO LA ISABEL DOS SANTOS: MWANAMKE TAJIRI KULIKO WOTE AFRIKA

ANGUKO LA ISABEL DOS SANTOS: MWANAMKE TAJIRI KULIKO WOTE AFRIKA

4886
0
SHARE

 

NA BALINAGWE MWAMBUNGU


VIONGOZI wengi wa Kiafrika, hasa wenye kujitwalia madaraka (despots), huwa wanatabia ya kutumia nafasi zao kuwatajirisha watoto, au ndugu zao wa karibu, kwa kuwamegea sehemu ya mapato ya nchi, ama moja kwa moja, au kupitia kandarasi za serikali na mashirika ya umma au kuwateua ndugu zao kushika madaraka katika taasisi kubwa. Vinginevyo, wao wenyewe hujilimbikia mali na fedha ambazo wanazificha katika mabenki ya kigeni nje ya nchi.

Kwa miaka mingi, Uswiss ndio lilikuwa kimbilio lao, lakini baada ya nchi hiyo kujiridhisha kwamba fedha hizo zilikuwa zinachukuliwa kwa hila, imebadili sera. Nchi husika ikiweza kuthibitisha kwamba fedha hiyo ni mali ya umma, na ilidokolewa kutoka kwenye mapato yatokanayo na rasilimali za nchi husika, huwa inazirudisha. Mfano ni Jenerali Sani Abacha wa Nigeria, ambaye alichota mamilioni ya fedha kutokana na mauzo ya mafuta, na kuzificha Uswiss, zilirudishwa Nigeria baada ya kifo chake.

Ni viongozi wachache katika Afrika ambao wamefanya kazi kwa uwadilifu na kuondoka madarakani wakiwa na mikono misafi. Mfano ni Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Kenneth Kaunda wa Zambia, Quet Masire wa Botswana, Joachim Chisano wa Mozambiki, Sam Nuyoma wa Namibia, Nelson Mandela wa Afrika Kusini.

Jomo Kenyatta wa Kenya, alimwachia mtoto wake Uhuru, ardhi kubwa sana na mali, Marcias Nguema wa Equatorial Guinea,  Omar Bongo wa Gabon, Abdulaye Wade wa Senegal,  Jose Edwardo dos Santos wa Angola, ni kati ya viongozi wa Kiafrka ambao walijitajirisha pamoja na watoto na ndugu zao, huku wananchi wakiogelea kwenye umaskini.

Mtoto wa Rais Angola, Edwardo dos Santos, alimpa mtoto wake wa kike Isabel, mamlaka makubwa kwenye shirika la mafuta la Angola, akampa kibali cha kipekee cha kuuza almasi ya nchi, na kumpa kandarisi kubwa kubwa.

Baada ya Rais Dos Santos kustaafu, Isabel amejikuta katika kashifa mbali mbali ikiwemo ya kupewa  kandararasi za serikali kinyemela, bila kufuata utaratibu wa tenda.

Isabel ambaye anasemekana ni mwanamke tajiri kuliko wote Afrika, akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani 2.8bilioni, amejikuta akiandamwa serikali na kuondolewa katika nyadhifa alizokuwa nazo wakati wa utawala wa baba yake.

Katika muda mfupi wa miaka miwili, mikataba minono minne yenye thamani zaidi ya $22 bilioni, imebatilishwa na Rais Jenerali João Lourenço. Isabela, ambaye enzi baba yake, alikuwa haguswi na aliishi ‘binti mfalme’.

Wachambuzi wanasema kuwa ufalme wake sasa unakaribia kuanguka. Baba yake, Rais Jose Edwardo dos Santos, ambaye alitawala Angola kwa miaka 38, amestaafu akiwa na utajiri wa $20bilioni.

Inaelezwa kuwa isingekuwa uimara wa Kamati Kuu ya chama tawala cha  MPLA (Movement for People’s Liberation of Angola), Rais Dos Santos, alikusudia kumwachia Isabel kiti cha urais. Ndivyo Wafrika tulivyo. Alifanya hivyo Omar Bongo wa Gabon kwa kumteua mwanaye Ali Bongo Odimba kuwa mrithi wake, dikteta Teodoro  Obiang Mangue, wa Equatorial Guinea,  alimteua mwanaye Teodorin kuwa makamu wake na kumpa utajiri mkubwa.

Rais Dos Santos alimpa binti yake Isabel biashara kubwa kubwa ikiwa ni pamoja na mradi mkubwa wa kulijenga jiji la Kuanda kuwa la kisasa—Luanda Metropolitan Master Plan’ wenye thamani ya Dola15 bilioni kupitia kampuni yake ya Urbinvest na hakuna aliyehoji.

Hapakuwa na tenda ili makampuni mengine, na yenye ujuzi na uwezo zaidi yawanie. Laki haya hayakutokea Angola tu, kwa sababu hata hapa kuna miradi mikubwa ambayo haikupita katika mfumo wa kibiashara na inatekelezwa, hakuna anyejua kama kuna akina Isabel nyuma yake na hakuna anaye hoji.

Kwa kawaida fedha ya umma inaweza kutolewa kununua, au kulipia huduma, lazima itokane na bajeti iliyopitishwa na Bunge, na lazima tenda ipite katika mchakato wa kisheria.

Rais Dos Santos, akijua kwamba ni ‘lala salama’ yake, na alikwisha pitisha sheria zinazompa kinga ya kutoshitakiwa, alipindisha utaratibu wa tenda na kumpa mtu aliyemtaka! Lakini katika hali kama hiyo, lazima kuna washirika ambao wanafanya kazi kisiri na kupata mradi wao. Maana katika biashara—hasa biashara kubwa za kimataifa, lazima wawepo ‘wapiga debe’ na madalali, ili mambo yaende kama sawa. Marekani kwa mfano, mtu harusiwi hata kuuza nyumba yake au gari, bila kupitia kwa dalali au wakala.

Dos Santos alifanya mambo hayo kwa usiri, sasa baada ya kuondoka madarakani, yote yakaanikwa.

Tayari Isabel ameondolewa kwenye wadhifa wa Mtendaji Mkuu (CEO) wa National Oil Company Sonangol, nafasi aliyopewa mwaka 2016 kabla ya baba anakaribia kustaafu.

Aidha, amenyang’anywa mamlaka pekee (exclusive rights), ya kuuza almasi ya Angola nje ya nchi.

Kampuni ya mawasiliano ya UNITEL, ambayo Sonangol ilikuwa inamiliki asilimia 50 ya hisa, ilazimishwa kumgawia Isabel asilimia 25 na hakuna ushahidi kwamba aliwahi kuzilipia hisa hizo.

Hivi sasa, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, (International Court of Arbitration) itakaa mjini Paris, Ufaransa kuamua kesi ya Dola 3.5 billion dhidi ya familia ya Isabel.

Kampuni ya Portugal Telecom Ventures, ambayo ilikuwa inamiliki wa hisa asilimia 25 ya UNITEL, imefungua mashitaka na inadai Dola 600 milioni kama malimbizo na pia inamdai  Isabel dos Santos yeye mwenyewe kutokana na kusimamia mapato na uendeshaji wa  kampuni.

Wakati wa utawala wa baba yake, Isabel inasemekana aliitumia UNITEL kama kibubu chake—piggy bank. Kati ya mwaka 2012 na 2013, UNITEL iliikopesha International Holdings kiasi cha Dola 465 milioni, kampuni hiyo ni mali ya Isabel dos Santos, asilimia 100 na alitumia fedha hiyo kwa ajili ya matanuzi na manunuzi nchini Ureno. Aidha, alisaini mikataba kama mwakilishi  wa mkopeshaji yaani UNITEL, na  mkopaji UNITEL International Holding, mikataba ambayo ilitakiwa kuiva baada ya miaka 10 kwa riba ya 1%.

Kama kwamba hiyo ilikuwa haitosi, kampuni nyingine mali ya Isabel inayoitwa Tokeyna, ilinunua karadha za UNITEL kwa jina lake na ukaguzi ulionesha kuwa katika mchakato huo, kampuni hiyo ya mawasiliano, ilipata hasara ya Dola 315 milioni.

Hata hivyo, mnamo mwaka 2014, Isabel dos Santos huyo huyo, hakuchukua gawio lake la Dola 322 milioni, badala yake akalibadilisha kuwa mkopo kwa  UNITEL wenye riba ya asilimia 12. Matokeo yake, UNITEL ilipata hasara ya Dola 315 milioni, kutokana na mkopo aliopewa Isabel dos Santos, na yeye akapata faida safi ya Dola 35 milioni kwa kuikopesha UNITEL mwaka moja baadaye.

Mwaka jana, Isabel alitoa Dola 458 milioni kutoka benki kama gawio na kutoka kampuni hiyo ya mawasiliano na Dola 265 milioni za mkopo alioipa kampuni mwaka 2017, na kuiacha kampuni hiyo bila fedha.

Inasemekana kuwa kampuni ya mafuta ya Sonangol, inakusudia kumwondoa kwenye hisa za UNITEL kwa kulazimisha kulipa fedha zote alizokwapua. Hili litamaanisha kwamba litakuwa anguko lake kutoka kwenye moja ya mabenki makubwa binafsi nchini  Angola, Banco Fomento de Angola (BFA), ambamo kampuni ya mawasiliano ina hisa  51%.

Bila fedha kutoka ng’ombe wa maziwa wa Angola, utawala wa kifalme wa Isabel nchini Ureno, ambako ndiko alikuwa anachimbia fedha zitokanazo na vitegauchumi vya kimataifa, hautakuwa endelevu.