Home Habari ANNA MGHWIRA ATOA YA MOYONI

ANNA MGHWIRA ATOA YA MOYONI

1403
0
SHARE
Anna Mgwira (kulia) akizungumza na Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kabla ya kuhamia CCM.

NA SAFINA SARWATT, KILIMANJARO


KWA mara ya kwanza tangu ajiunge na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ameibuka na kutoa kauli nzito zilizomsukuma kujiunga na chama tawala.

Kabla ya kujiunga na chama hicho, Mghwira alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo ambaye pia alipeperusha bendera ya chama hicho kwenye mbio za urais, akiwa ndiye mwanamke pekee kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu.

Akiwa ndani ya ACT-Wazalendo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, hatua iliyoibua mjadala mzito uliotokana na itikadi yake ya kisiasa.

Hatua hiyo awali ilionekana kama dhamira ya kumrejesha CCM mwanamama huyo mwenye taaluma ya sheria na theolojia.

Katika mazungumzo yake na RAI yaliyofanyika juzi, Mghwira alisema alipokuwa upinzani alijifunza mengi  na alipata hasara ya kutumika kisiasa kwa kutetea masilahi ya watu binafsi.

“Watu wanatanguliza masilahi yao mbele kwenye kila kitu, ninyi wenyewe ni mashahidi hasa kwa mkoa huu wa Kilimanjaro wenye viwanda vingi na rasilimali nyingi, vipo wapi leo viwanda hivyo?

“Vimekufa kwa sababu watu walitanguliza masilahi yao binafsi wakaendesha siasa zao chafu mkawaachia na kukaa kimya, wakati si kawaida watu wa Kilimanjaro,” alisema Mghwira.

“Naomba ndugu zangu tuungane na tuwe chachu katika kurejesha rasilimali zetu, tukirejesha wafaidika wakuu ni sisi, mfano KNCU tu kwa mwezi tunapata zaidi ya billion 15, lakini leo hii kiwanda kinadaiwa badala ya sisi kudai, mchwa walitafuna viwanda vyetu na sisi tukakaa kimya,”  alisema.

AMSHANGAA ZITTO

Mghwira alisema ameshangazwa na kauli ya Kiongozi Mkuu wa chama chake cha zamani, Zitto Kabwe kuwa alimwibua na wataendelea kuwaibua wengine licha ya kuhamia CCM na kusema hizo ni kauli za wakosaji.

“Kauli ya Kiongozi wa chama nilichotoka ya kwamba waliniibua  na CCM walinichukua kirahisi tu, hivyo wataibua wengine, ukimwibua mtu mtumie kwani hakuna mtu aliyependa kutoka ndani ya chama chake kirahisi bila sababu za msingi tuachane na siasa chafu,” alisema.

Alisema haamini kuwa siasa ni uwongo na michezo mchafu, bali ndani ya siasa kuna watu wabaya wasiokuwa na nia njema na maendeleo ya nchi.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo inaonekana kuwa na siasa chafu kutokana na wanasiasa kuweka masilahi yao mbele na kutumia mali za umma vibaya.

“Tukiruhusu wachafu washike jukwaa tutachafuka wote kwa sababu hao ndio wanaotusemea na hatuwezi kwenda wote lazima aende mwakilishi na akitumia vibaya uwakilishi wananchi lazima maendeleo yetu yakwame,” alisema.

Alisema kwamba siasa za Tanzania bado zinayumba, hazijapata msimamo imara na kwamba tunakoelekea vyama vya siasa vinaanza kuyumba na kukosa dira, kutokana na makada wa vyama kuhamia CCM na Chadema.

”Watu wanahama vyama kutoka Chadema kwenda CCM hutasikia mtu akihama kwenda CUF, NCCR Mageuzi na TLP hili ni kwa sababu vyama vyenye nguvu ni viwili tu. Sijasema watu wasihame ila ukweli ni kwamba CCM ndiyo chama pekee ambacho kinatekeleza dira ya Taifa. Na siku zote mchezaji mzuri huchagua timu kubwa yenye wachezaji wazuri,”  alisema. 

Alisema ili tufikie mafanikio ni lazima tukubali makosa tuliyofanya kwani kukubali kosa ni moja ya hatua kubwa kupiga kuelekea kujirekebisha.

“Sisi ndiyo tuna uwezo mkubwa wa kujenga Kilimanjaro mpya na tukijenga Kilimanjaro mpya tumechangia katika kujenga Tanzania mpya tunayoidai,” anasema Mghwira.

Anasema kuwa ujenzi wa mali za umma  na utunzaji wa rasilimali zetu ambazo Mungu ametujalia zinahitaji uwajibikaji na uaminifu wa hali ya juu.

“Muda wote nipo kwa ajili ya wananchi wa Kilimanjaro na kwa masilahi ya taifa mimi sina hulka ya kubagua watu, nikitaka kufanya siasa nitaendea kwenye jukwaa la siasa lakini ushauri wangu tuwajibike ipasavyo.

“Nikurudi kwenye ilani ya CCM imenyambua dira ya maendeleo ya Taifa ya 2020/2025  kwa hiyo haikinzani na dira ya Taifa  ndio maana nashaanga wanaolalamika.

“Kinachotakiwa ndani ya dira ni vitendo zaidi kuliko kuwa vitabu vikubwa vilivyojaa maelezo mbalimbali ambavyo havitekelezeki.  Vyama vilivyobaki  vitaendelea kupiga kelele lakini mwisho siku tutakutana pale pale katika kutekeleza ilani ya CCM,”  anasema Mghwira.

HISTORIA YAKE KISIASA

Mghwira alianza kama mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na ilipoundwa CCM, Mghwira alipunguza kujihusisha na siasa hadi mwaka 2009 alipojiunga na Chadema.

Licha ya kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chadema ikiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake pamoja na Katibu wa Baraza la Wanawake, mwaka 2012,  aliingia katika mchakato wa kugombea ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki  lakini akakwama  katika kura za maoni.

Ndipo mwaka 2015, alipoamua kujiunga na chama cha ACT –Wazalendo na kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa chama na hata mgombea urais.

Hata hivyo, baada kushindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, kujaza nafasi iliyowachwa na Said Mecky Sadiki.

Anna Mghwira anakuwa kiongozi wa pili wa chama hicho kinachofuata siasa za mrengo wa kushoto kuteuliwa kuingia kwenye serikali ya Rais Magufuli, akitanguliwa na Profesa Kitila Mkumbo, ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Maji na Umwagiliaji.