Home Latest News Anthony Martial tumaini jipya Man Utd

Anthony Martial tumaini jipya Man Utd

1754
0
SHARE

ANTHONY Martial ameanza kuirejesha Ligi Kuu ya England katika utamu wake baada ya kuonesha dalili ya kuibeba klabu yake mpya ya Manchester United katika ushindani wa kweli.

Kama ilivyokuwa mwaka 2004 katika msimu huo wa majira ya joto, Man Utd iliwasajili kwa mara ya kwanza wachezaji wawili wapya chipukizi, Wayne Rooney pamoja na Cristiano Ronaldo, ambao kwa wakati huo walikuwa wachanga, lakini wenye vipaji vikubwa. Rooney aliwasili siku ya mwisho ya Agosti mwaka huo akitokea klabu ya Everton kwa ada ya pauni milioni 27 akiwa bado chipukizi mwenye njaa ya mafanikio, hiyo ilijionesha msimu huo kwenye michuano ya Ulaya. Baada ya kushuhudiwa kinda huyo akijiunga na klabu hiyo, muda mchache mwaka huo huo naye Ronaldo aliungana naye lakini yeye ilikuwa kwa ada ya pauni milioni 12 ikiwa ni kiasi kidogo ukilinganisha na cha Rooney.

Katika msimu huo tayari Ronaldo alionesha kipaji ambacho kiliendelea kuishawishi United kuamini kwamba walifanya usajili wa mchezaji sahihi katika muda sahihi, kwani alionesha kuwa na kipaji cha pekee. Mreno huyo alifanikiwa kufunga mabao mawili tu katika ligi hiyo katika miezi saba ya mwanzo ndani ya klabu hiyo, lakini alimaliza msimu kwa kuifungia timu yake mabao ambayo yalisaidia kuibuka mabingwa wa michuano ya Kombe la FA dhidi ya klabu ya Millwall, kabla ya kurejea nyumbani kwao ambapo aliongoza katika ushindi na kulipeleka taifa lake kwenye michuano ya Ulaya ya 2004.

Baada ya miaka mitano, Ronaldo pamoja na Rooney walikuwa wachezaji wenye mafanikio kwa kuisaidia timu yao kutwaa vikombe na nishani mbalimbali, hiyo ikiwa misimu mitatu mfululizo wakiwa mabingwa wa ligi kuu, wakifanikiwa kuingia fainali cha klabu bingwa mara mbili, pamoja ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2008 dhidi ya klabu ya Chelsea. Kwa ujumla chipukizi hao wawili waliweka rekodi ya kipekee na kuwa na heshima kwa mashabiki wao, huku wakitunukiwa zawadi iliyowatambulisha kama wachezaji wa kizazi kipya ndani ya klabu hiyo. Ronaldo akaibuka kuwa mchezaji wa kwanza kwenye klabu hiyo kunyakua tuzo ya mwanasoka bora duniani baada ya miaka 40 tangu George Best kufanya hivyo.

Lakini awali nyota hao walipokuwa wanajiunga na klabu hiyo wakiwa chipukizi walipewa matumaini ya kuja kufanya vizuri zaidi hivyo baada ya miaka 11 kupita klabu hiyo imerudi kwenye wakati mgumu kwa kusajili vipaji vipya kama vile Memphis Depay pamoja na Anthony Martial.

Si vibaya kufahamu kwamba mwaka 2004 Rooney pamoja na Ronaldo hawakuwa tayari kuibeba klabu hiyo, lakini waliweza kufanya hivyo baada ya miaka minne kupita klabu hiyo ilipofanya vizuri michuano ya Ulaya. Hadi sasa Memphis amecheza michezo nane, huku Martial akicheza dakika 205 tu, lakini tayari wamefanikiwa kuonesha kwamba wanaweza kuirudisha timu hiyo kwenye mstari ili kupambana katika mashindano ya England pamoja na Ulaya. Hata hivyo, dakika 75 alizocheza katika Ligi Kuu hiyo Martial ameweza kufikisha mabao matatu, ikiwa ni idadi sawa na ile ya mabao ya Wayne Rooney aliyofunga ndani ya miezi saba iliyopita, huku Memphis akifanikiwa kuwashawishi mashabiki kwa kushinda mabao matatu katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. Martial alikuwa kivutio zaidi kwenye ushindi wa mabao matatu, huku akitupia peke yake mabao mawili na Memphis akipiga shuti lililomkuta Juan Mata na kufunga akikamilisha ushindi huo dhidi ya Southampton hivi karibuni.

Chipukizi hao kwa sasa wana miaka kati ya 19 na 21 bado wanayo nafasi kubwa, upo wakati watapotea kwa muda, lakini vipaji vyao vitawalinda. Hadi sasa Memphis tayari ameshashiriki mechi 19 za kimataifa na kufanikiwa kufunga kwenye Kombe la Dunia ambapo ilichangia kuwa mchezaji bora wa mwaka wa taifa lake kama ilivyo kwa Martial, akiwa ni miongoni mwa washiriki wa kimataifa akiwa amecheza mechi tatu katika timu ya Ufaransa.

Huku akicheza mechi mbili za michuano ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na klabu yake ya zamani Monacco, wakati kwa wachezaji kama Rooney na Ronaldo walihitaji misimu mitatu ili kufikia hatua hiyo. Ukifuatilia miaka 11 iliyopita Rooney na Ronaldo walikuwa watulivu na wenye uzoefu wa kutosha wakiwa chini ya aliyekuwa Kocha wa klabu hiyo, Sir Alex Ferguson, aliyedumu nao kwa zaidi ya miaka 18 wakiwa pamoja na Paul Scholes, Roy Kean, Gary Neville, Ryn Giggs pamoja na Ruud Van Nistelrooy.

Tofauti yao na Memphis pamoja na Martial wamejiunga Old Trafford ikiwa si ile iliyokuwa awali ambayo kwa sasa ipo chini ya Kocha Louis van Gaal, akiwa bado anatafuta uimara wa kikosi hicho baada ya miezi 14. Pia kwenye klabu hiyo wamebakia wachezaji wawili tu, Rooney pamoja na Michael Carrick, ambao wana uzoefu wa kutosha juu ya timu hiyo wanaotegemewa kushirikiana vyema na nyota hao.

Licha ya matumizi makubwa ya fedha dhidi ya kuwasajili nyota hao pamoja na kushindwa kuziba nafasi ya Angel Di Maria, Robin van Persie hata Javier Hernenandez, kunaweza kukawa na mategemeo makubwa kwa Martial na Memphis na si vinginevyo. Martial pamoja na Memphis kwa sasa ndio wanaochukua nafasi ya Ronaldo na Rooney kwenye timu hiyo, hivyo United wanahitaji kuonesha mipango dhidi yao kwenye misimu miwili ijayo ili kushinda na kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu.