Home Makala ANTHONY MAVUNDE: TUMEPATA MATUMAINI MAPYA YA KUTOKOMEZA VVU

ANTHONY MAVUNDE: TUMEPATA MATUMAINI MAPYA YA KUTOKOMEZA VVU

4865
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


WAKATI mwenendo wa fedha za kutokomeza Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi kutoka kwa wahisani na wadau wa maendeleo ukipungua nchini, Watanzania milioni 1.4 wanaishi na VVU huku wanawake wa rika zote wakiendelea kuathiriwa zaidi kuliko wanaume.

Hayo yanajiri katika kipindi hiki wakati Tanzania kwa mwaka inakadiriwa kutumia Sh trilioni 1.2 kwa ajili ya shughuli za udhibiti wa VVU na Ukimwi nchini ikiwamo kununua dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs).

Kwa mujibu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids), asilimia 93 ya fedha hizo hufadhiliwa na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi, kati ya hizo asilimia 86 hutolewa na Marekani kupitia programu yake ya PEPFAR na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund ATM).

Tanzania hutoa asilimia saba tu ya fedha za udhibiti wa Ukimwi, hata hivyo katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2018/19 Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni tatu, ili kuendelea kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) ulioanzishwa mwaka 2015 kwa lengo la kutokomeza janga hilo nchini.

Ili kupunguza utegemezi huo, kampuni ya Geita Gold Mine (GGM), kwa kushirikiana na Tacaids kwa kupitia Mfuko wa Kili Challenge, kila mwaka huandaa mpango wa kupanda Mlima Kilimajaro ujulikano kama ‘Kili Challenge’ kwa lengo la kuchangisha fedha kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU.

Akizindua mpango huo hivi karibuni Naibu wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde, anasema ili kufikia malengo ya kutokomeza maambukizi ya Ukimwi mbinu mbadala na ubunifu wa hali ya juu unahitajika.

Anasema hadi sasa zaidi ya watu 700 kutoka duniani kote wameshiriki katika mpango huo wa kihistoria la upandaji Mlima kupitia programu hii ya “Kili Challenge” na kukusanya fedha nyingi kwa miaka yote ambazo zimesaidia maeneo mbalimbali na makundi ya wajane, watu wanaoishi na VVU, watoto yatima, vijana, pamoja na taasisi zinazotoa huduma muhimu za Ukimwi.

Anasema fedha hizo zimetumika kuboresha huduma za Hospitali mbalimbali nchini zikiwemo za Mkoa wa Geita na Kibong’oto Mkoani Kilimanjaro na ujenzi wa vituo vinne vya maarifa kwenye njia kuu za usafirishaji.

“Hivyo programu hii pia imepanua wigo wa kusaidia Taasisi zinazojikita kuhudumia wachimbaji wadogo wadogo pamoja na maeneo ya wavuvi ambako tafiti zinaonyesha kwamba wako kwenye mazingira hatarishi ya kuambukizwa VVU.

“Tacaids imekuwa ikishirikiana kwa karibu na GGM kuhakikisha jambo hili linatekelezwa kwa tafsiri ya kuoanisha changamoto za mapambano dhidi ya Ukimwi na ugumu wa upandaji wa Mlima Kilimanjaro kupitia njia ngumu ya Machame na uzungukaji wa Mlima Kilimanjaro kwa baiskeli.  Jitihada katika kupambana na ugumu wa kupanda na kuzunguka Mlima Kilimanjaro huwa ni ushindi wa kufanikiwa kumaliza na hiyo huongeza chachu ya mapambano yenyewe dhidi ya Ukimwi,” anasema.

Anasema matarajio ya serikali  kwa kupitia Kili Challenge, malengo ya 90-90-90 yatafikiwa; yaani asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao za maambukizo ya VVU; asilimia 90 ya walioambukizwa na kujua hali zao wanaanza kupatiwa dawa (ARVs) na asilimia 90 ya waliopo kwenye mpango wa kupatiwa dawa wamefubaza VVU ifikapo 2020.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tacaids, Leornard Maboko anasema pamoja na hatua zilizofikiwa kwenye mwitikio dhidi ya VVU na Ukimwi tangu ugunduliwa miaka 38 iliyopita, Ukimwi bado ni tatizo kubwa kijamii na kiuchumi nchini.

“Kwa mfano, bado kuna maambukizi mapya yanayokadiriwa kufikia 81,000 kila mwaka, ambapo kiwango cha maambukizi ni asilimia 4.7 na takribani watu milioni 1.4 wanaishi na VVU nchini.

“Katika jitihada za kujenga mwitikio kabambe wa kitaifa, Tacaids imeendelea kushughulikia changamoto za unyanyapaa, usawa na ukatili wa kijinsia ili kulinda haki za watu walioathirika kwa njia moja au nyengine na janga la VVU na Ukimwi,” anasema.

Naye Makamu wa Rais miradi endelevu wa kampuni ya AngloGold Ashanti na GGM, Simon Shayo, anaishukuru serikali kwa kuunga mkono jitihada za Kili Challenge tangu ilipoanzishwa mwaka 2001, hadi mwaka huu, ikiwa inatimiza miaka 17 tangu ianzishwe.

“Mwaka huu mashujaa 78; yaani Wapanda Mlima 45 na Waendesha baiskeli 33 waliacha familia na shughuli zao na kufanya maamuzi ya kupanda na kuuzungunga Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuhamasisha na kukusanya fedha dhidi ya Ukimwi na kuhusisha nchi malimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Misri, Afrika kusini na Marekani.

“Kila siku na kila mwaka mpango huu haujaacha kuweka alama katika jamii, kwani hadi sasa Sh bilioni 14 zimekusanywa kwa kupitia Kili challenge. Fedha zimenufaisha zaidi ya mashirika 40 yasiyo ya kiserikali pamoja na taasisi mbalimbali za serikali kupitia Tacaids mamilioni ya watanzania wamenufaika kutokana na programu hii,” anasema.

Aidha, katika hafla ya kuwapokea mashujaa waliopanda na kuuzungaka Mlima Kilimanjaro Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema anatambua na kuthamini mchango na kazi nzuri inayofanywa na GGM kwa ushirikiano na wadau wake, pia  kwa kushirikiana na  Tacaids katika mapambano dhidi ya Ukimwi ili kutimiza malengo ya Kimataifa ya kuutokomeza ugonjwa wa huo ifikapo 2030.

“Hivyo natoa wito kwa watu binafsi, makampuni na wadau wa maendeleo kushikamana ili kuendelea kuchangia mfuko huo ambao una lengo la kutokomeza Ukimwi nchini tukiiga mfano ulioonyeshwa na Kampuni ya GGM kwa miaka 17 sasa,” anasema.