Home kitaifa ANTHONY MTAKA: MADALALI WA IKULU WANAMCHAFUA RAIS MAGUFULI

ANTHONY MTAKA: MADALALI WA IKULU WANAMCHAFUA RAIS MAGUFULI

1160
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI,

SIMIYU ni mojawapo ya mikoa mipya ambayo imeanza kuchipua vema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012. Mkoa huo ambao ulimegwa kutoka mkoa wa Shinyanga upande wa mashariki ni mojawapo ya mikoa iliyojaliwa kuwa na mifugo mingi.

Hivi karibuni Rais Magufuli alifanya ziara mkoani humo na kuzindua miradi kadhaa ikiwamo viwanda viwili ambavyo ni vya maziwa na chaki jambo ambalo lilimlazimu Rais kumwagia sifa Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka.

Licha ya kuzindua viwanda viwili pekee Rais Magufuli alidhibitisha kuwa huwa ni vigumu kutoa pongezi na sifa kwa watumishi wa umma, ila Rais Magufuli bila kumung’unya maneno alionesha furaha yake kutokana na mwamko huo.

RAI lilizungumza ana kwa ana na Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka ambaye pamoja na mambo mengine alibainisha baadhi ya miradi ambayo mkoa unaendelea kuiandaa ili kufikia ndoto ya kuwakomboa wananchi kiuchumi.

RAI: Mkoa wa Simiyu umekuwa na mafanikio ya kutolewa mfano katika utekelezaji wa sera ya Taifa ya uanzishaji viwanda, ni nini hasa siri ya mafanikio haya?

MTAKA: Mkoa wa Simiyu mkoa mchanga ambao ulianzishwa mwaka 2012. Baada ya kutua Simiyu niliwaambia wenzangu kuwa wamemuona namna Rais anachozungumza ni kile anachomaanisha, hata alivyoshape utumishi ndani ya serikali. Wengi walizoea kuwa ukiteuliwa kuwa mkurugenzi, mkuu wa wilaya au wa mkoa unaona kama hicho cheo ni chako au cha kudumu hali iliyochochea migogoro kati yao. Lakini sasa hakuna hilo.

Ndio maana Magufuli alipokuwa kwenye mchakato wa kuteua akasema mnagombania nini mimi ndio mteuzi!. Rais ametuvusha kutoka kwenye utumishi wa umma kuja kwenye utendaji, Rais Magufuli ameteua viongozi bila kujali vyeo ili kuchanganya na kuonesha kuwa uteuzi ni jambo la muda.

Na Rais anataka Tanzania ya viwanda ndio maana nikawaambia wanaSimiyu sasa tunataka mkoa wa aina gani?

Kwa mfano hapa Simiyu tunazalisha pamba asilimia 60 je, tunazalisha bidhaa gani?, Pia mkoa wetu ndio unaongoza kwa kuwa na mifugo mingi hivyo tunaitumia vipi?. Nikawaambia lazima kutafsiri dira yetu badala ya kukopi mitazamo ya nchi nyingine kama China au Japan.

Ninataka mkoa wa Simiyu uwe ni mkoa ambao utazalisha bidhaa mbalimbali nchini. Tunajifunza pia kwa waliofanikiwa kwa mfano, Japan wamefanikiwa kwenye mpango wa Odo, ambao unamaanisha wilaya moja bidhaa moja na sasa wamefikia kwenye kijiji kimoja bidhaa moja. Lakini kama sisi tumerasimisha ardhi za kimila kwanini tusirasimishe bidhaa zetu, hivyo nikawaambia hatuwezi kuwa watu wa kutangaza fursa, tuwaachie vyombo vya habari watangaze fursa sisi tuoneshe njia, hivyo tukaweka orodha vitu tunavyoweza kuzalisha.

Tulianza na chaki kwa sababu ndani ya mkoa tunanunua  chaki za Sh milioni tano mpaka saba kwa mwezi, hivyo tukiangalia chaki inatokana na gypsum ambayo inazalishwa Singida. Hivyo tumeshirikiana na SIDO, TIRDO na wadau wengine wakiwamo sekta  binafsi kwa ajili ya kuanzisha Saccos kwa vijana mkoa mzima.

Tumebuni mipango ya kupata vyanzo vipya vya mapato, na sasa tumeanza kuzalisha chaki ambazo tunaziuza Zanzibar, na mikoa mingine zaidi ya 10.  Katoni moja ya chaki hapa Simiyu tunauza Sh 25,000 lakini kule Dar es Salaam chaki zinauzwa Sh 40,000 hadi 45,000.

Pia wilaya inayoongoza kwa mifugo ni Meatu, na kule wanauza maziwa kwa matoroli ikifika mchana maziwa yanaganda. Hivyo tukaona nayo ni fursa tumesajili kampuni tumeshirikiana na Sido na wadau wengine tumetengeneza mpango ambao sasa kiwanda tayari kinaanza kuzalisha bidhaa za maziwa.

Tumebadilisha gia angani, baada ya ukame kutokea, njaa nayo imeanza kutokea na hii changamoto ya ukame imetuletea changamoto kwamba tuanze kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kwa sababu haiwezekani sehemu kama Kilimanjaro walie ukame au pale Mwanza walie ukame wakati kuna Ziwa Victoria na muda wote wanabeba maji kufua, kuoga kuogelea sasa kwanini wasione ni fursa kufanya kilimo cha umwagiliaji.

Sasa tumeanza na wilaya moja tu kuonesha kama mfano, ili kilimo cha kisasa tunachopigia kelele kwenye runinga sasa tuoneshe kwa mfano, Ethiopia wameamua, wanasukuma maji wafuge samaki, wapate umeme na mambo mengine na sisi tutaanza kilimo cha umwagiliaji.

Lakini mradi mwingine mkubwa tunaotarajia kuuanzishwa ni kiwanda kitakachozalisha bidhaa zinazotumika katika matibabu kama bandeji, pamba na nyingine nyingi. Kiujumla bidhaa zinazotokana na pamba ambazo zinatumika kwenye sekta ya afya.

Tuliona kuwa kwa ukanda huu wa ziwa viwanda vya nguo vipo sasa tumeamua kuzalisha bidhaa za pamba zinazotumika katika sekta ya afya.

Tumefanya maamuzi kwa kushirikiana na TIB Benki ambao wametoa Sh milioni 150 kwa ajili ya upembuzi. Lengo letu baada ya kukamilisha mradi wa bidhaa za afya kwa sababu ni mkubwa utagharimnu zaidi ya bilioni 250. Tutaanza kwenye kuzalisha viwanda vya small scale kwenda kwenye medium na baadaye large.

Kuna mabadiliko tumefanya, barabara ya Busega – Mwanza sasa watu watafanya biashara masaa yote tumewawekea ulinzi wa uhakika. Hii ni kwa sababu tunataka kukusanya kodi lazima tuwawekee mazingira mazuri.

Tunataka kupambanua maono, dira yake anayoitaka Rais Magufuli, tunataka pia uwe mkoa unaojipambanua kama mkoa unaoonesha uchumi wa nchi.

Tunataka Simiyu ije kama mkoa mpya utakaokua kiuchumi, sasa ili uende Dar es Salaam si lazima uende Mwanza unapitia tu pale Bariadi. Teknolijia zote ambazo watu huona kwenye televisheni tunataka waje kuona Simiyu.

Niliwapiga marufuku wakuu wa wilaya kutokwenda kwenye kufungua makongamano na semina, nimekataa kwenda kupiga marufuku marumbesaa, nimewaambia wakaoneshe mfano kwa vitendo kwa kutekeleza miradi tuliyoiandaa.

RAI: Unazungumziaje ushirikiano wa wafanyabiashara na viongozi wa mkoa wako katika ukusanyaji wa kodi na hata ushiriki wa kutekeleza miradi mnayoiandaa?

MTAKA: Wafanyabiashara wanashiriki, kwa sababu lengo na nia yetu ni kuwakomboa wananchi katika umaskini. Watanzania tupende vya kwetu kwamba kama unataka kununua bidhaa zetu, kwa mfano katoni ya chaki Dar es slaam ni Sh 45000 lakini Simiyu tunauza Sh 25000 hivyo hatuwafukuzi ila lazima watanunua vya kwetu tu.

RAI: Umekuwa katika timu ya wasaidizi wa Rais  wa awamu ya tano tangu alipounda serikali yake. Nini tathmini yako kuhusu utendaji na utekelezaji wa majukumu ya serikali kwa kipindi ilichokaa madarakani?

MTAKA: Rais ameipambanua nchi katika hali ya utofauti sana, sisi tumezoea kukosoa ila tuangalie mtu anagombea Uganda au Senegal anasema mnichagua nitakuwa kama Magufuli, Senegal wana Magufuli day.

RAI: Katika serikali ya awamu ya nne, ulikuwa mkuu wa wilaya ya Mvomero na Hai, Je, ulijifunza nini katika kipindi cha uongozi wako?

MTAKA: Mvomero hapakuwa mahala pazuri pa kufanya mambo ya maendeleo kwa sababu asilimia 70 ni kusuluhisha  migogoro ya wakulima na wafugaji, kwa miaka mitatu niliyokaa nilijikuta kuwa msuluhishi tu wa migogoro. Hivyo ni lazima kufika mahali kutambua kuwa amani ni suala la msingi. Ilinifundisha vitu vingi kuwa tunayo nafasi ya kuondokana na migogoro iwapo tutakuwa na uwezo wa kuongeza thamani ya mazao na mifugo wetu.

RAI: Simiyu ni mojawapo ya mikoa yenye kuenzi mila potofu kama vile dagashida ambayo hutumiwa kuwaadhibu hata watumishi wa umma iwapo wasipofuata tamaduni za wenyeweji, zaidi ya hilo kuna changamoto gani nyingine umekutana nazo baada ya kuongoza mkoa huo kwa mwaka mmoja sasa?

MTAKA: Ni kweli nimekaa mikoa mbalimbali kama vile Kilimanjaro ambao kuna makabila mbalimbali ila tofauti ya Simiyu ni kwamba kuna watu wenye tamaduni moja inayofanana.  Ni tamaduni ambazo wanaona ni mambo sahihi.  Kwa mfano wao wanataka iwapo kuna msiba huwezi kwenda kazini kuomba ruhusa lazima uendane na tamaduni zao sivyo wanakutenga. Sasa tamaduni hizo zimeisha tunazungumza maendeleo.

Tunataka Simiyu itamkwe midomoni mwa watu kama mkoa wa mfano kimaendeleo.  Sasa watu wajenge nyumba bila kuogopa kulogwa, pia tuendelee kutokomeza mauaji ya maalbino na mambo mengine.

RAI: Kwa kuwa ni kada wa CCM, unayazungumziaje mabadiliko aliyoyafanya mwenyekiti Rais John Magufuli?

MTAKA: Kama kuna kitu ambacho CCM imepata faida, ni mageuzi aliyofanya mwenyekiti kwamba tumevaa koti kabla ya baridi, kwa sababu hata Mwalimu alifanya mabadiliko mwaka 1992, wengi walikataa ila akawaambia kubalini. Kulikua na vyeo visivyo na ulazima. Vikao vingi visivyo na tija. Hapakua na sababu ya kutumia bilioni moja kufanya vikao.

RAI: Unakifiri ni kweli vyeo vya wakuu wa mikoa na wilaya ni vya kisiasa visivyo na tija kama wapinzani wasemavyo?

MTAKA: Huo ulikuwa ni mtazamo wa Mbowe, na sasa nataka amuulize leo Lowassa na Sumaye. Kwa sababu kina Mbowe na wenzake hawajanusa hata harufu ya utumishi serikali na kujua upo vipi, kwa hiyo wamuulize hao mawaziri wakuu kuwa faida za wakuu wa mikoa na wilaya zipoje?.

Kwa sababu huwezi kukaa miaka 10 ndani ya serikali alafu utoke useme hakuna kitu maana yake ulikuwa na sifuri kichwani. Ila ili serikali iende lazima ujue utakwenda vipi.

RAI: Umefanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali ukiwa bado kijana, unatoa wito gani kwa vijana wenzako kufikia mafanikio kama yako?

MTAKA: Wito wangu lazima unapokaa kwenye madaraka ujue kuwa yupo aliyekaa kabla yako, dhaman haibebwi kwenye mabega. Na huwa natafsiri kama rais anazungumza na sisi kwanini sisi tusizungumze na wananchi?. Wananchi watatuunga mkono kwa sababu tunawashirikisha, mimi sio one man show. Ndio maana tupo hapa na wakuu wa wilaya.

RAI: Hivi sasa katika mikoa mingi kumetokea hali ya ukame hivyo kusababisha upungufu wa chakula, hali ipoje mkoani Simiyu?

MTAKA: Hata kama mvua ingekuwa inanyesha lazima gharama ya chakula ingepanda, hata wakulima wanaelewa wakivuna dunia 20 wanauza tano, na nyingine wanaweka ili waje kuuza katika kipindi hiki kwa bei ya juu. Kwa hiyo gharama ya chakula ingekuwa ni ileile. Watu walizoea rahisi wakati siku zote vyakula hupanda bei na hata wakati wa mfungo huwa tunawaomba kutopandisha bei. Kiujumla niseme mkoani kwangu hali ni shwari.

RAI: Yapo madai kutoka makundi mbalimbali ya watu katika jamii yetu kuwa baadhi ya wasaidizi wa Rais wanamuogopa kiasi cha kushindwa kumshauri vizuri na hata kumpa taarifa potofu. Hili unalizungumziaje?

MTAKA: Taarifa potofu! hao wanaosema hayo maneno walizoea kuwa madalali wa ikulu wanawadanganya watu mitaani na kuchukua hela zao, tuna madalali wengi sana ambao waliitumia Ikulu. Rais Magufuli hadanganyiki kwa sababu hajatoka nje ya Tanzania, wala si mgeni, amesoma hapahapa kuanzia vidudu mpaka amepata udaktari na amekuwa waziri hapahapa kwa miaka 20.

Sasa huwezi kumdanganya kwa sababu anasoma kwenye mitandao ya kijamii na mambo yote anayaona. Kwa mfano hili la chakula kupanda bei ni sawa na lile la  kwa sababu watu walizoea zamani sukari na mahindi ilikuwa ni dili, sasa madili hayapo. Watu walikuwa wanaendesha V8 wakati hawana kazi wanayoifanya, ukiuliza utaaambiwa ni papaa.