Home Makala Ardhi dhambi ya asili inayoitafuna Afrika Kusini

Ardhi dhambi ya asili inayoitafuna Afrika Kusini

1591
0
SHARE

NA ERICK SHIGON

Licha ya miongo miwili kupita tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, bado Wazungu nchini humo wanamiliki ardhi kubwa ya nchi hiyo.

Wazungu wa Afrika Kusini ambao ni asilimia nane ya jumla ya idadi ya watu nchini humo, wanamiliki asilimia 72 ya mashamba, tofauti na asilimia nne pekee ya mashamba yaliyoko mikononi mwa wananchi asilia—watu weusi, ambao ndio wengi zaidi nchini humo.

Migogoro ya ardhi baina ya wakazi (weusi dhidi ya weupe) wa nchi hiyo kubwa kiuchumi barami la Afrika, ilianza kujitokeza miaka ya 1600, mara baada ya watu kutoka Ulaya walipozuru nchini humo.

Hali hiyo imemlazimu Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, kutangaza kuwa Chama tawala cha African Natuoal Congress (ANC), kinatarajia kuifanyia marekebisho Katiba ya nchi hiyo, ili kutekelezwa mpango wa ugawaji upya ardhi kwa watu weusi.

Rais Ramaphosa alisema kitendo cha Wazungu kuwapokonya ardhi wakazi wa asili miaka ya 1600, sawa na dhambi ya asili, hivyo lazima ardhi irejeshwe bila fidia, ili kuponya majeraha ya muda mrefu, ila itatekelezwa kwa uangalifu mkubwa, ili zoezi hilo lisiharibu uchumi.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Ramaphosa amepokelewa kwa mtazamo tofauti ndani na nje ya nchi hiyo, hali iliyoibua mijadala katika mataifa ya Marekani na Ulaya.

Rais wa Marekani, Donald Trump, aliibua mjadala juu ya suala hilo baada ya kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa twitter, akidai kuwa amemwagiza Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Mike Pompeo, kufutilia suala hilo huku Serikali ya Afrika Kusini, ikijibu kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa “itaharakisha urasimishaji wa ardhi kwa wazawa kwa umakini, kwa kuwahusisha watu wote ambapo haitapelekea kuligawa taifa”.

Hata hivyo, wapo wanaopinga marekebisho ya Katiba katika Ibara 25 ambapo wanadai kuwa hakuna haja ya kurekebisha kwa sasa katika Ibara hiyo, kwani fidia ni jambo lisilo la lazima, na kama yatafanyika marekebisho, basi ni kwa matakwa ya kisiasa tu.

Aidha, itakumbukwa kuwa Machi mwaka huu, Waziri wa Uhamiaji wa Australia, Peter Dutton, naye alizusha mjadala baada ya kusema kuwa nchi yake, inapaswa kuwapa kipaumbele wakulima Wazungu wa Afrika Kusini wanaotafuta hifadhi kwa sababu wanapitia hali ya kutisha.

Aidha, katika hali ya kushangaza, Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, wiki hii amekituhumu chama tawala cha ANC kwa kuachana na sera ya kutokuwa na ubaguzi, na badala yake chama hicho kinakuwa chama cha watu weusi peke yake, kutokana na sera yake ya ardhi kiliyoamua kuchukua.

Kauli hiyo ya Mbeki, imekuja katika kipindi hiki ambacho Rais Ramaphosa, ameendelea kwa kusisitiza kuwa Katiba ya nchi hiyo, itarekebishwa, ili kuruhusu uchukuaji wa ardhi kutoka kwa Wazungu bila ya kulipa fidia, ili igawanywe kwa watu weusi.

Mbeki amesema chama tawala cha ANC, kilipigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo, ili kuleta usawa na uhuru kwa watu wote, bila kujali rangi wala eneo mtu anakotoka.

Chapisho la Mbeki, linalodaiwa kuvuja kwa umma, ameeleza kutoridhishwa na njia ambayo chama hicho kimeamua kuichukua—kuwanyang’anya  ardhi kwa nguvu Wazungu na kuwakabidhi raia weusi wa nchi hiyo bila malipo.

Harakati za kutwaa ardhi kutoka kwa Wazungu na kuwapatia watu weusi ambao ndio asili wa Afrika Kusini, hazijaanzishwa leo na viongozi wa nchi hiyo, kwani kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha EFF, Julius Malema, ameshaanzisha harakati kadhaa za kutwaa ardhi hiyo.

Pia katika kampeni zake amekuwa akichochea wananchi kutwaa ardhi za Wazungu kimabavu, jambo ambalo limewahi kukemewa na Mahakama Kuu nchini huyo.

Malema alipendekeza Waafrika wapewe ardhi bure; yaani Mzungu mwenye ardhi popote pale nchini inayotakiwa na Mswahili, anyang’anywe tu bila malipo yoyote, kwani babu yake Mzungu naye aliwanyang’anya Wafrika.

Histori ya migogoro ya ardhi

Tatizo la migogoro ya ardhi ndani ya nchi hiyo, lilianza kujitokeza zaidi ya miaka 360 iliyopita mara baada ya watu kutoka Ulaya walipozuru nchini humo.

Kundi la kwanza la makaburu kutoka Uholanzi lililotia timu Afrika Kusini likiongozwa na Jan Van Riebeeck akiongoza kampuni ya Dutch East India Company (DEIC) mwaka 1652. Hili ndiyo kundi la kwanza makaburu kutinga Afrika kusini katika kipindi cha Ubepari mchanga ulipokuwa ukianza kuota mizizi, mataifa ya Ulaya yakiongozwa na kiranja wao Uingereza.

Katika kipindi hicho, mataifa ya Ulaya yalikuwa yakizunguka duniani kufanya biashara na uporaji, unyonyaji wa rasilimali kama pembe za ndovu, dhahabu, almasi, chuma, shaba na ngozi za wanyama katika kuelekea safari ya mapinduzi ya viwanda yaliyotokea katika kipindi cha miaka ya 1750.