Home Michezo Kimataifa Arsenal kumfungulia milango Koscielny

Arsenal kumfungulia milango Koscielny

997
0
SHARE

LONDON, England

KLABU ya Arsenal wapo tayari kumuuza beki wao Laurent Koscielny ambaye hivi karibuni aligoma kujiunga na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao yanayoendelea huko nchini Marekani.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa Washika bunduki hao watafungua mashtaka kwa utovu wa nidhamu ulioonyeshwa na nahodha wao kwa kushindwa kurejea kwenye timu kwa wakati.

Beki huyo raia wa Ufaransa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kuwatumikia mabingwa hao wa zamani wa England.

Kocha wa Arsenal, Unai Emery, hivi karibuni alisema bado timu hiyo inamtegemea beki huyo ambaye anataka kutimkia nchini Ufaransa katika klabu ya Lyon.

“Kwa upande wangu kama kocha, Koscielny ni mchezaji muhimu kwetu, kilichobaki sasa pande zote mbili tukae chini tujadiliane cha kufanya kuliko uamuzi aliochukua,” alisema.

Ingawa, Arsenal imekuwa ikisaka beki wa kati katika dirisha hili la usajili ambalo litafungwa Agosti 8, mwaka huu, siku moja kabla ya Ligi Kuu England kuanza.

Washika bunduki hao wanamfukuzia kwa kasi beki wa kushoto wa Celtic, Kieran Tierney huku ofa yao ya pauni milioni 25 ikitolewa nje na wababe hao wa Scotland.

Pia, Arsenal wanakaribia kukubali kumsajili beki wa kati wa Saint Etienne, William Saliba, endapo dili hilo likikamilika beki huyo ataendelea kusalia kwa mkopo ndani ya kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Ufaransa, Ligue 1.

Taarifa zinadai kuwa wapinzani wakubwa wa Washika bunduki hao, Tottenham wanamfukuzia kwa kasi beki huyo mwenye umri wa miaka 18 huku wakiweka mezani kitita cha pauni milioni 20.