Home Michezo Athuman Bilal: Kiboko ya Yanga anayejiita ‘nabii’ asiyekubalika

Athuman Bilal: Kiboko ya Yanga anayejiita ‘nabii’ asiyekubalika

1248
0
SHARE

MOHAMED KASSARA

MIONGONI mwa timu zitakazobaki kwenye kumbukumbu za mashabiki wa Yanga msimu huu wa Ligi Kuu Bara, ni Stand United ya mjini Shinyanga.

Stand, timu pekee pekee iliyoweza kuvuna pointi tatu mbele ya Wanajangwani hao, inanolewa na Athuman Bilal ambaye awali alikuwa msaidizi wa kocha raia wa Burundi, Niyongabo Amars.

Amars alibwaga manyanga na kuiacha timu hiyo katika hali mbaya lakini tangu Bilal alipopewa kazi, mambo yameonekana kuwaendea vizuri, ikiwamo kuwachapa Wanajangwani bao 1-0.

RAI limememfikia na kufanya mahojiano na kocha huyo mzawa kufahamu mengi kutoka kwake na timu hiyo.

RAI: Ulikabidhiwa timu na umefanikiwa kuibadilisha haraka, nini siri ya mafanikio hayo?

Bilal: Siri kubwa ya mafanikio ya misingi niliyoiweka baada ya kujua timu ipo katika wakati mgumu.

Ilibidi niweke mipango ya muda mfupi itakayotuwezesha kupata pointi katika michezo inayofuata.

Kingine ni kuwafahamu wachezaji wangu wanataka nini. Tunajua tupo katika wakati mgumu wa kifedha, hivyo wachezaji wanatakiwa kujengwa kisakolojia ili wapambane.

Nashukuru nilijaribu kufanya hivyo na vijana wakanielewa, hivyo ikawa rahisi kushinda mchezo dhidi ya Yanga na kupata pointi katika michezo mingine migumu.

RAI: Uliwezaje kuwandaa wachezaji wako wakati mchezo wa Yanga na kufanikiwa kuvuna pointi zote tatu?

Bilal: Nilikaa na vijana wangu na kuwaambia umuhimu wa kupata ushindi dhidi ya Yanga. Niliwaambia kama ukata hata Yanga wanao, ndiyo maana wanatembeza bakuli.

Hivyo basi, tusijisikie wanyonge kwani tunakutana na timu ambayo ipo katika hali kama yetu, tusiwaogope.

RAI: Ugumu uko wapi katika kuwahamasisha wachezaji bila fedha?

Bilal: Ni changamoto kubwa sana, ni jambo gumu kumuhamasisha mchezaji acheze bila kuwa na uhakika wa malipo yake.

Lakini nashukuru vijana wangu wananielewa, kikubwa ninachowaambia ni kuhakikisha wanatumia vema fursa inayopatikana ili kujitengenezea ulaji sehemu nyingine,

Hivyo, kila mmoja amekuwa akijituma kwani maisha ya soka yanajulikana, unaweza kupata timu nyingine kama utaoonyesha kiwango kizuri.

RAI: Umekabihiwa jukumu la ukocha mkuu,je ipi mipango yako?

Bilal: Mpango wa kwanza ni kuhakikisha tunapambana kwa kila hali kwa ajili ya kuhakikisha tunabaki Ligi Kuu msimu ujao.

Tumepata matokeo kwenye michezo kadhaa iliyopita lakini ukweli ni kwamba tuna kazi ya ziada katika michezo iliyobaki.

Ligi imekuwa na ushindani mkali, hasa hii duru ya lala salama. Tunahitaji kuendelea kupigana kufanikisha hilo.

RAI: Changamoto gani umepitia tangu utue Stand United?

Bilal: Kwa kweli changamoto ni nyingi sana hasa ya kutoaminiwa, mimi ni kama nabii amabaye sikubaliki kwetu.

Kwanini nasema hivyo, hii siyo mara yangu ya kwanza kukabidhiwa majukumu haya, mara ya kwanza ilikuwa wakati alipoondoka Patrick Liewig. Nilichukua timu katika hali mbaya na kupigana hadi ikabaki Ligi Kuu.

Cha ajabu, baada ya kuniamini, msimu uliofuata aliletwa Amars kuwa kocha mkuu na mimi kuwa msadizi.

Tuliendelea kufanya kazi, lakini baadaye nilisimamishwa kutokana na kile walichodai nilishiriki kupanga matokeo katika mchezo dhidi ya Yanga uliomalizika kwa Stand kufungwa mabao 4-3.

Hata hivyo, bado sikuonesha tofauti yoyote, walikaa wenyewe na kuamua kunirudisha kwenye timu.

Sasa hivi ameondoka Amars wamenipa jukumu la kuhakikisha timu inabaki Ligi Kuu msimu ujao, usishangae pia wakatafuta kocha mwingine msimu ujao baada ya timu kubaki.

Wanapaswa kuanza kutuheshimu sisi wazawa tunaofanya kazi kubwa bila kupewa fadhila zinazostahili.