Home Habari kuu Baada ya furaha matokeo kidato cha nne 2019 nini kinafuata?

Baada ya furaha matokeo kidato cha nne 2019 nini kinafuata?

461
0
SHARE

DK. Kijo Bisimba

HIVI karibuni Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilitoa matokeo ya mitihani ya darasa la nne, kidato cha pili na nne  iliyofanyika mwaka 2019.

Nimefuatilia matokeo hayo yalivyopokelewa na wengi na hasa ya kidato cha nne na imeonekana mwaka huu ufaulu umeongezeka kwa zaidi ya asilimia moja, huku wasichana wakifanya vizuri zaidi kuliko wavulana na kushika nafasi za juu karibu zote kumi.

Pia imeonekana shule binafsi zimeendelea kufanya vizuri zaidi ya shule za serikali. Kuna shule ya wasichana mkoani Mbeya ya St Francis imeshangaza kwa wahitimu wake wote kupata daraja la kwanza kwa kiwango cha alama saba ambayo ndio alama ya juu mtu anayoweza kuipata.

Aidha mikoa mitatu ya Kilimanjaro, Iringa na Arusha imeonekana kuwa kinara katika matokeo yote matatu ya darasa la nne, kidato cha pili na cha nne, nayo ni Kilimanjaro, Iringa na Arusha.

Lakini katika hayo yote nimeona pia ajabu ya kijana Yohana Lameck Lugedenga wa Shule ya Sekondari Igaganulwa, ambayo ni ya kata iliyoko Bariadi mkoani Simiyu aliyefaulu kwa kupata alama zote A katika masomo yote tisa aliyofanyia mtihani na kupata daraja la kwanza kwa alama hizo saba pia.

Kwa shule za umma pia yupo kijana Yohana Assa wa Malangali Mufindi mkoani Iringa naye alikuwa mtu wa tano kitaifa, yaani yuko katika kumi bora akiwa pekee ndiye aliyetoka katika shule ya umma, wengine tisa wakiwa wametokea shule binafsi.

Kwanza nianze kwa kuwapongeza sana wote waliohusika hadi tukaweza kupata matokeo hayo mazuri na binafsi, niwapongeze watahiniwa wote waliofanya mitihani na waliofaulu vizuri na hata wale waliofaulu kiasi.

Hoja yangu kubwa katika matokeo haya ni kujiangaliza sana katika suala la elimu ya nchi yetu kwa ujumla, nimemwona Mkuu wa Wilaya aliyekwenda kumtembelea kijana Yohana wa Simiyu, akatuonyesha mazingira ya yule kijana hali ya nyumba yao na kwamba alitelekezwa na baba na hata nguo za shule ni walimu wake ndio walikuwa wanamnunulia lakini mwisho akakamilisha kwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa sera ya elimu bure.

Tunapoona pongezi kama hizi kwa rais najiuliza ni kweli au ni dhihaka. Ni kweli kwamba hilo neno elimu bure limesaidia wengi kwenda mashuleni lakini wapo pia wengi walioshindwa kwenda kwa kukosa vifaa.

Kama alivyosema, huyu Yohana kwa vile alikuwa ana uwezo sana walimu wake ndio walikuwa wanamnunulia sare za shule, nina hakika wapo wengi ambao walishindwa kuendelea kwa kukosa sare za shule pia.

Tuendelee kujiuliza iweje shule zetu ambazo elimu ni bure ufaulu uwe chini hivyo kuliko shule ambazo si za serikali na wanaosoma huko wanalipiwa fedha nyingi sana.

Kuna uhusiano wa malipo na ufaulu. Je Yohana aliyefaulu kutoka si kwenye mazingira magumu ya nyumbani tu lakini hata ya shuleni kilichomwezesha ni nini hasa?

Hata Yohana wa Mufindi ni nini kilichomwezesha kufaulu pekee kuwa katika kumi bora kutoka shule za serikali?

Tukiyaangalia haya matokeo na ufaulu ulivyo tuanze kuchambua mambo yanayoweza kuchangia wanafunzi waweze kufanya vizuri. Kuna wakati watu walikuwa wanaamini kuwa wasichana hawana uwezo kama wavulana kiasi kwamba wasichana wakapewa upendeleo wa kuwezeshwa kuingia elimu ya juu katika ufaulu mdogo kuliko wanaume.

Lakini sasa hivi tunaona wasichana waliopewa mazingira mazuri ya kupata elimu wameweza kufanya vizuri zaidi ya wavulana, kwa sababu uwezo wa akili ni sawa ila mazingira ya kuelimishwa ndio huweza kuathiri mtu anavypokea.

Wanafunzi walioko shule za binafsi  mazingira yao ya kuelimishwa ni tofauti kabisa na zile za umma. Walimu wao wanaangaliwaje? Wanafunzi wanatunzwaje? Shule zina mazingira ya aina gani? Tuviangalie hivyo kisha turudi tujiulize kwa hawa ambao wako katika mazingira magumu ya nyumbani na ya shule na bado wamefanya vizuri sana maana yake ni nini? 

Kuna suala la uwezo binafsi, mazingira ya kupatia elimu na juhudi za mamlaka kuhamasisha. Kwanini mikoa mingine iwe vinara dhidi ya mingine yote?

Tuliwahi kusema kuwa elimu ndio kila kitu kwa jamii.  Maana yake ni kwamba pasiwepo na ubaguzi katika elimu. Hizi shule za serikali nazo zina madaraja zipo za kata na zipo nyingine sijui  zinaitwaje.

Kuna uhaba mkubwa wa walimu kwenye baadhi ya shule, pamoja na elimu kuwa bure. Kuna uhaba mkubwa wa vifaa kama maabara, kwingine maabara zipo lakini watendaji wa kuziendesha pamoja na vifaa havipo.

Wakati sisi tunasoma kila wakati huwa nakumbusha kulikuwa na shule binafsi pia lakini hazikuweza kuzishinda shule za serikali na pia mwanafunzi asingekubali kwenda kusoma shule binafsi kwani huko walikuwa wanapelekwa wale waliokuwa hawakufaulu vya kutosha.

Sasa hivi waliofaulu vya kutosha ndio huenda shule binafsi. Kwa shule za umma wanaoenda waliofaulu vizuri sana ni wale  ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwapeleka hizo shule binafsi.

Wakifika huko katika shule za serikali viwango vyao huporomoka kwa kuwa mazingira ni yale yanayoporomosha badala ya kujenga.

Sasa inabidi tuamue kama kweli tunataka  elimu ya nchi hii iwe bora kwa watoto wetu wote na ili Taifa letu likue kimaendeleo. Elimu ikiwa ni kwa baadhi tu ndivyo hivyo  hivyo na hali ya maendeleo itakavyokuwa. Hivi huyu kijana aliyekuwa anasaidiwa sare za shule na walimu wake ataweza kuendelea na masomo kidato cha tano bila shida? Uzoefu wangu nilioupata nikiwa katika utafiti wakati nafanya shahada yangu ya uzamivu inanionyesha huyu kijana anaweza akaishia kutembelewa na mkuu wa wilaya.

Mfano mzuri nilikutana na kijana mdogo huko Kijiji cha Ndulamo Kata ya Iwawa Makete, aliyekuwa na uwezo mkubwa kimasomo lakini alikuwa yatima anayejilea mwenyewe. Nilipozungumza na kamati ya  watoto wanaoishi katika mazingira magumu ya kijiji walinihakikishia huyo mtoto akifaulu  hawezi kukosa msaada wa kumwendeleza.

Nilienda huko miaka minne baadaye  nilimkuta yule kijana akiwa kijijini akanieleza alikosa mtu wa kumwezesha kununua vifaa vilivyohitajika kuingia kidato cha kwanza. Hivyo wenzake wakati huo walishafika kidato cha nne yeye alikuwa yupo tu. Mifano ni mingi.

Jambo muhimu kwa nchi yetu ni kuweza kuangalia uwiano katika elimu na kipindi hiki ambacho bado hatujaweza basi vijana wenye uwezo mkubwa kama akina Yohana waangaliwe katika upekee wao.

Nchi nyingine wana fungu maalumu la wale wanaofaulu vizuri sana wanapatiwa msaada maalumu [bursary], wanasomeshwa. Elimu bure hapa inaishia kidato cha nne hivyo kidato cha tano kwa mtu aliyekuwa hawezi kununua sare ni shida, itabidi asaidiwe wakati tunapindua meza kuikabili sekta hii ya elimu tusiwe na matabaka ya aina za shule na wanaoelimisha nao wasikosewe haki zao kiasi cha wao kushindwa kuifanya kazi yao kwa weledi. Wachambuzi waendelee kuyachambua matokeo haya ili waje na suluhisho la kitaalamu na la kudumu.