Home Makala BADALA YA MCHUCHUMA, TUMALIZIE UMEME WA UPEPO

BADALA YA MCHUCHUMA, TUMALIZIE UMEME WA UPEPO

4569
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


TANZANIA imekuwa mojawapo ya nchi iliyojaliwa uwapo wa vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme. Vyanzo hivyo ni pamoja na maji, upepo, gesi, makaa ya mawe na nishati nyingine jadidifu.

Licha ya kuanzishwa kwa vyanzo mbalimbali, hadi sasa kumekuwapo na vyanzo vingi ambavyo vimeanzishwa na kusahauliwa au kutelekezwa, kutokana na sababu mbalimbali.

Moja ya chanzo ambacho kilipigiwa upatu bila kutazama kwa kina athari zake, ni uchimbaji wa makaa ya mawe kule Mchuchuma, mkoani Njombe.

Makaa hayo yaliyopo Kata ya Mkomang’ombe, wilayani Ludewa, sasa yataanza kuchimbwa hivi karibuni, bila kuzingatia kwa umakini, athari za kimazingira.

Eneo hilo ambalo linakadiriwa kuwa na tani za makaa ya mawe zaidi ya milioni 536, pia limerandana na Liganga palipo na madini ya chuma. Kwa zaidi ya miaka 30 sasa, limeendelea kuwaweka roho juu juu wakazi wa vijiji vitakavyoathiriwa na uchimbaji huo.

Tangu kugunduliwa kwa madini hayo na wakoloni, na kufuatiwa na awamu tano za uongozi nchini, kila kiongozi kwa wakati wake, amekuwa akiwaandaa kisaikolojia wakazi hao kukaa mkao wa kuhamishwa kupisha uchimbaji huo.

Hata hivyo, katika kipindi cha awamu ya kwanza kama ilivyokuwa kwa uongozi wake Mwalimu Julius Nyerere, aliondoka madarakani mwaka 1985 na kumwachia Rais Ali Hassan Mwinyi ambaye alikaa madarakani miaka 10, lakini madini hayo hayakuguswa.

Vivyo hivyo Rais Benjamini Mkapa ambaye alikuja na sera ya ubinafsishaji, hadi alipomaliza muhula wake wa miaka 10 na kumwachia Rais Jakaya Kikwete.

Rais Kikwete naye licha ya kuanzisha michakato mbalimbali ikiwamo Serikali kwa kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), na Kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Ltd (SHG) ya China kuingia ubia kwa ajili ya kuanza uchimbaji, hata hivyo hadi sasa hakuna kinachoendelea huku wakazi wa eneo hilo wakiaminishwa kuyahama makazi yao.

Bilioni tano zatengwa

Wakati danadana hizo zikiendelea kupigwa tayari Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ameuaminisha umma kuwa wizara yake imetenga Sh.5bn. kwa ajjili ya kulipa fidia kwa wakazi hao.

Akijibu hoja za baadhi ya Wabunge waliochangia hotuba yake, Mei mwaka huu, Mwijage anasema mwekezaji yupo na Serikali inautambua mradi huo.

“Serikali ilishaingia makubaliano na mbia kampuni ya China ambayo imewekeza pesa karibu Dola za Marekani 60m. Wamesaini kitu kinaitwa ‘performance contract’, ndio tukaja na sheria, tukapitia mara mbili tukakubaliana kwamba tupitie ule mkataba tuboreshe vifungu.

“Watalaamu wakaanza kufikiria kama kuna ukakasi na masilahi kwa taifa, wakakuta kuna vifungu hatujajadiliana lakini mwekezaji yupo”.

Anasema licha ya kwamba mkataba huo ni siri, ila kuna mambo mawili ya msingi ambayo waliyabaini baada ya kuupitia mkataba huo.

“Ule mkataba wa kwanza ulioingiwa mwaka 2011, mwekezaji alikuwa anataka akusanye VAT aitumie baada ya miaka 20 atulipe. Sasa ukikutana na watendakazi wa leo wanataka VAT wakatoe elimu bure, wakanunue madawa, wanapata ukakasi! Kwa hiyo tukakaa nao.

“Pia niwaambie chuma cha Mchuchuma na Liganga, watalaamu wa uchambuzi wa migodi wanasema katika mgodi huo, dili sio chuma kuna madini mengine ambayo kitarakimu yana tija zaidi”.

Serikali ibadili uamuzi

Kutokana na kusuasua kwa mradi huo, ambao pia unaaminika kuwa athari za kimazingira baadhi ya wadau wanaishauri Serikali kuanza kutekeleza mradi wa madini ya chuma (Liganga), na kuachana na mradi wa makaa ya mawe, ili kulinda mazingira asilia ya maeneo husika na kupunguza gharama zinazotarajiwa kutumika.

Mmoja wa wadau hao kutoka Njombe, ni Benward Lihawa ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya mazingira, anasema utekelezaji wa miradi hiyo unaonekana kujawa na ujanja ujanja mwingi, hali inayozidisha hasira kwa wananchi.

“Inaonesha serikali kuu inaelekeza kitu tofauti na uongozi wa chini kwa wananchi ndio maana wanasuasua namna hii. Ingekuwa vema gharama za sasa zikaelekezwa kwenye miradi endelevu kuliko kuwatesa wananchi wa Ludewa,” anasema.

Hoja hiyo pia inaonekana kuungwa mkono na Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu, ambaye wakati akichangia hotuba ya wizara hiyo, anasema Sera ya Viwanda imeipa kisogo miradi ya Liganga na Mchuchuma—jambo linaloilazimu Serikali kuagiza chuma nje ya kwa ajili ya ujenzi wa reli na malighafi za viwanda vya nondo nchini.

Komu ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), anasema mwenendo huo unadhihirisha kuwa uwekezaji unaofanywa kwenye Sekta ya Viwanda, hasa miradi hiyo hauwezi kuonesha dalili njema iwapo hakutakuwapo na maji ya kutosha kupunguza athari za mazingira katika eneo hilo.

“Sasa miradi ya gesi asili haijatumika vya kutosha, lakini cha ajabu serikali imekimbilia kuwekeza kwenye Stiggler’s Gorge na kuanzisha vita na mataifa mengine duniani, ambapo ni sawa na kuhamisha goli, hapakuwa na ulazima huo—hasa ikizingatiwa miradi mikubwa iliyoanzishwa haijatumika ipasavyo wala kutengamaa,” anasema.

Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Maendeleo Tanzania (NDC), Abel Ngapemba, mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh trilioni 6.564.

Licha ya gharama hizo, tayari ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG), zimeshabainisha kuwapo kwa viashira hafifu katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika ripoti hiyo ya mwaka 2016, zinabainisha kuwa mwaka 2011, NDC, kampuni ya Sichuan Hongda na kampuni ya Tanzania China International Mineral Rescource (ITCIMRL), zilisaini mkataba wa ubia wa kuendesha kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources, ikiwa ni kampuni iliyoanzishwa kwa kusudi la utekelezaji wa mradi wa Mchuchuma na Liganga.

Inaelezwa kuwa katika aya ya 2.9 ya mkataba, Sichuan Hongda ilikubali kuchangia kiasi kisichozidi Dola za Kimarekani milioni 600, ikiwa ni mtaji kwa MCIMRL, ili zitumike kulingana na maendeleo ya utekelezaji wa mradi.

“Kwa kuongeza, kampuni itatafuta mkopo wa kuweza kufikisha makusanyo ya Dola za Marekani bilioni 2.4 utakaoidhinishwa na mali za kampuni ya ubia zitakazojumuisha haki za uchimbaji zinazomilikiwa na kampuni ya ubia zenye uhusiano na mradi na udhamini wa Hongda,” inaeleza sehemu ya taarifa.

CAG anaeleza kuwa hakuna utaratibu uliowekwa wa kuhakiki na kuthibitisha kiasi cha fedha kilichotolewa na Hongda hadi sasa kama sehemu ya mtaji iliyokubali kutoa wa Dola 600 milioni kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.

“Kama mkopo unadhaminiwa na rasilimali za Tanzania, NDC kwa niaba ya serikali lilipaswa kuwa na mwanahisa mkuu wa TCIMRL kulingana na thamani ya rasilimali ambazo hazijatumika zenye thamani zaidi kiasi cha fedha ambayo ilikubaliwa na Hongda.”

CAG anaeleza kuwa kukosekana kwa utaratibu wa kuhakiki na kuthibitisha gharama za matumizi ya mwekezaji wa mradi, kuna matokeo hasi kwenye muda wa marejesho pamoja na gharama ambazo NDC lilizitumia kwa kuzingatia gharama zote zilizotumika na mwekezaji, huchukuliwa kama gharama anazotakiwa kurejeshewa kutokana na mapato yatokanayo na uzalishaji.

Kutokana na hali hiyo, ndio maana baadhi ya wadau wanaona sasa kuna haja ya kutekeleza miradi endelevu ambayo ina umeme wa uhakika na isiyoathiri mazingira.

Mojawapo ya vyanzo hivyo, ni umeme wa upepo mkoani Singida ambao mradi huo ulizinduliwa mwaka 2015, lakini mpaka sasa hakuna utekelezaji wenye malengo stahiki.

Mradi huo unaokadiriwa kugharimu Dola za Kimarekani milioni 132, unakadiriwa kuzalisha Megawati zaidi ya 300.

Mradi huo pia unaungwa mkono na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba, anasema mpango utarahisisha wananchi hasa wa viojijini kupata umeme kwa bei rahisi.

Makamba alitoa kauli hiyo wakati wa Kongamano la Wadau wa Nishati ya umeme hivi karibuni ambapo pamoja na mambo mengine, anasema lengo la Serikali ni kuwa na vyanzo endelevu vya nishati.

“Kwa kuwa umeme huo utazalishwa kwenye maeneo ya vijijini, wananchi wanatakiwa kupata umeme kwa bei rahisi kulingana na uchumi wao na sio kuuziwa umeme kwa bei juu, na zaidi wizara yake inapenda kuweka  wazi kuwa huu mradi una faida kubwa sana kulingana na mfumo wa nchi ulivyo,”anasema Makamba.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kuzalisha umeme wa upepo Afrika Mashariki Six Telecoms, Rashid Shamte, naye anasema mradi huo unamanufaa kwa sababu kwa awamu ya kwanza watatoa umeme megawati 100 na itaendelea mpaka kufika megawati 300.

“Tutaunganisha kwenye gridi ya taifa, na huu mradi utakuwa na faida kwa wananchi pamoja na wale watakaotolewa kwenye maeneo yao watafaidika kwa kulipa stahiki zao,” anasema.