Home Michezo Bado tumwite Mourinho ‘special one’?

Bado tumwite Mourinho ‘special one’?

333
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

NI mechi tano za Ligi Kuu zimepita sasa bila Tottenham kupata ushindi, mechi ya mwisho ikiwa ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Burnley, tena Jose Mourinho na vijana wake wakilazimika kusawazisha kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Dele Alli.

Matokeo hayo ya kwenye ligi yanakuja huku Tottenham ikiwa imeshang’olewa Kombe la FA. Safari yao ilikwamishwa na Norwich City katika mchezo wa raundi ya tano.

Dalili zote zinaonesha wanakwenda kuumaliza msimu huu wakiwa mikono mitupu, hasa kwa kuwa hata kule Ligi ya Mabingwa Ulaya wameshafungashiwa virago, wakisukumwa nje na RB Leipzig.

Mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora ilichezwa jijini London na Tottenham wakachapwa bao 1-0. Matumaini yakawa ni kwenda kupindua meza katika mchezo wa marudiano lakini juzi wakatandikwa ‘tatu bila’.

Huku majeraha ya wachezaji muhimu yakifahamika kuwa sababu kubwa, unaweza kuiona tofauti kubwa kati ya Tottenham hii na ile ya Mauricio Pochettino msimu uliopita. Unazungumzia kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.

Chini ya Mourinho, imeonekana kuwa tofauti na matarajio waliyokuwa nayo mabosi wa Tottenham, kwamba angehamishia mafanikio yake klabuni hapo.

Hadi sasa, Tottenham wako nje ya timu nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku mbinu zake uwanjani zikishindwa kuwashawishi walio wengi.

Kocha aliyeshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu za Porto na Inter Milan, achana na yale ya Ligi Kuu akizinoa Chelsea na Real Madrid, sasa anapitia wakati mgumu, hata kuibua shaka kuwa hastahili kuendelea kuitwa Special One.

Tofauti na alivyozoeleka misimu kadhaa iliyopita, ni mechi 11 pekee alizoshinda kati ya 25 alizokaa kwenye benchi la ufundi la Tottenham.

Kuziweka sawa takwimu zilizopo, kati ya muchezo hiyo aliyoiongoza Tottenham tangu alipomrithi Pochettino, amefungwa nane na kutoa sare sita.

Kama hiyo haitoshi kuthibitisha upepo mbaya unaovuma kwa kocha huyo, juzi dhidi ya Leipzig ilikuwa mechi yake ya sita mfulululizo kuondoka uwanjani bila ushindi.

Ikiwa umeifuatilia kwa karibu safari yake ya ukocha, hasa kuanzia alipokuwa na Porto ya nchini kwao, Ureno, ni jambo jipya kwake na kwa watu wanaomfahamu.

Kwamba haijawahi kutokea kuona timu yoyote inayonolewa na kocha huyo raia wa Ureno ikifikisha idadi hiyo ya mechi bila kupata ushindi.

Kwa mazingira hayo, kumbuka pia majanga yaliyomkuta pale Old Trafford ambako alitimuliwa, ni sahihi kuendelea kulitumia jina la Special One kumtaja Mourinho?

Wanaoweza kumkingia kifua, kwamba aendelee kufahamika kwa jina hilo, watakwambia anapaswa kupewa muda, walau msimu mmoja zaidi kuthibitisha kuwa bado ni Special One au la.