Home Makala Bajeti imejaa matundu  

Bajeti imejaa matundu  

1057
0
SHARE

 

IMG_0216Na Happy Joseph, Kilimanjaro

KATIKA  bajeti iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano hivi karibu yapo mambo yanayostahili kupongeza na mengine kukosoa kwa hoja  kwa sababu yanaweza kuwaumiza wananchi.

Katika makala haya naanza kuchanganua mambo mazuri  kisha nitakosoa namna bajeti hiyo ilivyo na jinsi kasoro hizo  zitakavyoweza  kutatuliwa.

Maeneo ya ukwepaji kodi

Walioandaa bajeti wametazama maeneo kadha wa kadha ambayo yalikuwa changamoto hasa katika ukwepaji wa kodi.

Maeneo hayo ni maduka yanayotumiwa na vyombo vya usalama, misamaha ya kodi itolewayo kwa wafanyabiashara, mashirika ya dini na taasisi zisizo za kiserikali.

Pia bajeti imeainisha maeneo kama ya kutuma na kupokea hela kwa njia ya simu, pamoja na kwenye uwekezaji.

Kwa kiasi kikubwa serikali imejitahidi kudhibiti maeneo hayo kwa kubadilisha mfumo wa ukusanyaji ambao kwa kiasi kikubwa kodi iliyokuwa ikipotea katika maeneo haya itaweza kupatikana

Mosi, kufutwa kwa kodi na ushuru. Kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakilalamikia tozo za ushuru katika mazao yao maarufu kama produces. Tozo la ushuru huu kwa mazao ya kilimo ilikuwa ni asilimia 5 ya bei ya bidhaa husika. Kwa kufuta kodi hii, wakulima wanaweza kunufaika kwa uzalishaji wao

Pili, Tozo la kodi katika kiinua mgongo cha wabunge. Serikali imefanya jambo bora kabisa kwa kutoza kodi pato hili ambalo kimsingi ni kubwa kwa kuwa  muda wa utumishi wa wabunge ni mfupi kulinganisha na watumishi wengine wa serikali ambao hutumikia muda mrefu na kiinua mgongo hakifiki hata robo tatu au pengine nusu ya kiinua mgongo cha wabunge.

Tatu, Mfumo. Naipongeza awamu ya tano kwa kuzingatia na kuweka mkazo ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kutumia mfumo na njia za kibenki kwa kuwa njia hii inarasmisha ule ukusanyaji na mapitio sahihi ya fedha za serikali

CHANGAMOTO ZA BAJETI

Kwanza ni suala la vipaumbele, ambapo katika bajeti hii mgawanyo wa fedha umeonesha kuwa kipaumbele cha sasa cha serikali ni miundo mbinu iliyotengewa asilimia 25.4 ya bajeti yote. Kimsingi ni njia bora ya kuimarisha uchumi, japokuwa ndilo eneo

ambalo lina mazingira makubwa ya ufujaji wa fedha za serikali. Awamu iliyopita serikali iliweza kuimarisha kwa kiasi kikubwa miundombinu iliyopo hapa nchini kiasi kwamba mimi binafsi sijaona haja ya serikali kuipa kipaumbele cha kwanza katika bajeti hii.

Pili, sekta ya elimu ambayo imepewa kipaumbele cha pili kwa kutengewa asilimia 21.1 ya bajeti yote, ingefaa kuwa kipaumbele cha kwanza kwa kuwa serikali ndio kwanza imeanza kutoa elimu bure na kuona changamoto zilizojitokeza.

Sambamba na hilo serikali ipo katika mpango wa kutumia mtaala mpya ifikapo Julai, na mpaka sasa bado inahaha kwenye upatikanaji wa madawati, vifaa, na hata fedha za ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu umekuwa mtihani.

Kwa kuthibitisha hilo, zipo shule zilizoshindwa kujimudu kwa kutumia ruzuku inayotolewa na serikali ambapo kwa miezi sita kuna shule hazijafikisha laki mbili kwa majumuisho ya ruzuku yote ya miezi sita, licha ya kuwepo kwa mahitaji yasiyo na fungu ya mlinzi, pamoja na fedha za vitabu na vifaa vingine vya kujifunza na kufundishia.

Suala la madawati pia limekuwa changamoto kubwa na serikali haijapanga lolote kukabiliana na changamoto hii ndio maana waziri mkuu ametamka kuwa halmashauri zitumie mbao zilizokamatwa kutengeneza madawati.

Kuna maswali hapa, fedha za fundi zinatoka wapi? Vipi kuhusu halmashauri ambazo hazijakamata mbao? Je waziri mkuu ana uhakika kwamba mbao zilizokamatwa katika halmashauri, tutolee mfano halmashauri ya wilaya ya Hai zikitumiwa zinatosha kutengeneza madawati yatakayotosheleza upungufu uliopo?

Tatu, kilimo, uvuvi na ufugaji ambavyo ni kama mshingi wa kipato kwa mtanzania wa kawaida kimetengewa asilimia 4.9 ya bajeti. Hii si sawa kwa sababu, kwa sera ya nchi hii kuboresha viwanda, tunahitaji kwa kiasi kikubwa malighafi za uzalishaji viwandani.

Sawa serikali imepanga kuboresha miundombinu, ili isafirishe nini? Waziri amesema kuwa ili bajeti hii itekekezeke vema, msingi mmojawapo ni “hali nzuri ya hewa” kwa maana kwamba bado serikali haijaweka maanani kilimo cha umwagiliaji ambacho kinaweza kuleta uhakika wa upatikanaji wa mavuno

Sambamba na hilo, waziri hajaweka wazi ni kwa namna gani pembejeo zitawafikia wakulima kwa wakati ili waweze kuzitumia kwa tija. Pia bado kuna udhaifu mkubwa katika mipango ya ardhi ambayo imekuwa ikizua tafrani kukicha kati ya wakulima, wafugaji na wawekezaji.

Hii pia inathibitishwa na gharama ambazo serikali huingia kulipa fidia wananchi ili uwekezaji ufanyike eneo husika, jambo ambalo linadhihirisha kuwa, mpango madhubuti wa kutenga maeneo kwa ajili maalum haupo.

Katika nchi za wenzetu mfano China, waliweka sera ya makazi iitwayo ‘Closing Policy’ ambayo iligawa miji na vijiji. Wananchi walipewa nafasi ya kuchagua makazi yao yawe wapi kulingana na shughuli zifanywazo.

Kwa wale wa mjini, hawakuruhusiwa kumiliki maeneo, bali serikali ilimiliki maeneo yote ya mji na kuyagawa kwamba yapi yawe maeneo ya biashara na yapi yawe maeneo ya makazi, yapi maeneo ya viwanda.

Maeneo ya makazi yalijengwa na taasisi za umma, pamoja na binafsi kwa mpango maalumu uliowekwa na serikali na kupangishia wale waliochagua kuishi mjini. Waishio mjini walipaswa kuwa na kazi maalumu inayowawezesha kulipa kodi na kujikimu kimaisha. Pia huduma za kijamii zilipangwa kulingana na sera hii ya makazi.

Kwa wale wa vijijini, wao walipewa maeneo na kutakiwa kuyaendeleza kwa kilimo. Kila mwaka serikali ilifanya tathmini ya uzalishaji ambao unafanywa na kutoza kodi wale wasioyaendeleza na pia kuwaongezea maeneo wale waliozalisha kwa wingi. Njia hii iliweza kuisaidia serikali kwenye nyanja zifuatazo:

  • Kufahamu pasipo shaka makazi ya kila mtu
  1. Kugawa rasilimali kuendana na makazi yaliyopo
  2. Kufahamu maendeleo ya uzalishaji na kuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi
  3. Kuepuka migogoro ya ardhi na makazi
  4. Kuwa na miji iliyopangwa vizuri
  5. Kuhimiza uzalishaji kulingana na eneo husika
  6. Kuwa na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji yasiyoingiliwa na wananchi, jambo litakaloondoa ulipwaji wa fidia

Nne, sekta ya umeme imetengewa asilimia 5.3 na maji asilimia 4.8 ambapo ni jambo zuri japo kiasi hiki hakiwezi kuiwezesha nchi hii kufikia malengo ya serikali ya kuwa nchi ya viwanda.

Tano, asilimia 70.7 imeelekezwa kwenye miundombinu, afya, elimu, maji, umeme, kilimo na uvuvi, na asilimia 30 imeelekezwa kwenye matumizi mengine kama makundi maalum, maendeleo vijijini, ambapo kiasi cha bilion 59 zimetengwa kwa ajili ya tafiti, na ufanywaji wa tathmini ya viwanda.

 

Kwa mujibu wa waziri, mwaka huu wa fedha ni wa “kuandaa mazingira” basi…. Namnukuu… “Mheshimiwa Spika, kama alivyoelekeza Mhe. Rais wakati wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge lako Tukufu, Serikali itahakikisha viwanda vilivyopo vinafanya kazi. Katika mwaka 2016/17, Serikali itakamilisha tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuweka mikakati ya namna bora ya kuviendeleza. Baadhi ya viwanda hivyo ni viwanda vya nguo, viwanda vya mazao ya mifugo, viwanda vya kusindika mazao yakiwemo mazao ya mpira, korosho, tumbaku, miwa na mpunga. Katika kutekeleza jukumu hilo, fedha za maendeleo zimetengwa katika Mafungu mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza mashamba; na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, na ya mifugo. Pamoja na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda, Serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya wawekezaji waliokiuka masharti ya mikataba ya mauzo ya viwanda walivyobinafsishiwa.”

Sita, kimsingi fedha iliyotengwa haiwezi kutosha kwenye maandalizi na ufunguzi wa hivi viwanda vilivyopo. Nadhani inaweza kusukuma gurudumu la kufanya tathmini lakini kuhakikisha vinafanya kazi hapana. Kwanza kwa kuwa serikali haijui nini hasa changamoto za kufunga viwanda hivi, ndio maana tathmini na utafiti unahitajika, kisha ndipo changamoto zilizoainishwa zitatuliwe jambo ambalo serikali haijawa tayari kwa sasa. Nafananisha na mtu anayepanga kuzaa watoto kadhaa, akiwa katika maandalizi ya harusi bila kuwa na uhakika kama uwezo wa kuzaa upo au haupo.

Saba, serikali kuondoa kodi kwa malighafi za kutengeneza viberiti  katika kodi za forodha imenistaajabisha kwa kuwa sisi hatuna kiwanda cha vibeeriti.

Kiwanda chetu kimefungwa kwa madai ya kutokuwa na miti ya kutosha pamoja na dhana ya uharibifu wa mazingira. Tunashindwa kuiga teknolojia rahisi ya kutengeneza viberiti kwa kutumia karatasi zilizokwishatumika na nta ya nyuki kama wenzetu wa Kenya wafanyavyo hadi kiwanda kinafungwa, na hakuna dalili yoyote ya kufufua kiwanda hiki, hapa hapajakaa sawa.

 

Mgawanyo wa mapato serikali kuu na serikali za mitaa

Kuna mambo kadhaa ambayo yamenishangaza sana katika awamu ya tano hasa kwenye suala la mahusiano kati ya serikali kuu na zile za mitaa kimapato. Kumekuwa na kauli za kufuta halmashauri ambazo hazikufikia zaidi ya nusu ya makusanyo ya mapato yao. Hapa bila kutazama changamoto zilizopo katika halmashauri, waziri mwenye dhamana anatoa tamko kuonekana anafanya kazi.

Tangu mwaka jana kabla ya uchaguzi, halmashauri nyingi zilisimamisha shughuli za ukusanyaji wa mapato yake kupisha uchaguzi mkuu. Ukusanyaji wa mapato ulionekana kama ungezipunguza kura za chama tawala na kudhoofisha ushindi hivyo ukusanyaji ulisimama.

Pamoja na hayo, magari ya halmashauri pamoja na watumishi wa halmashauri walikuwa miongoni mwa nguvukazi ya Tume ya uchaguzi na lazima serikali ione kuwa sehemu ya ukusanyaji ilikwamishwa na mchakato wa uchaguzi, sasa unapotishia kuzifuta huku ukwamishaji ukiwa umesababishwa na serikali yenyewe si sawa.

Aidha, serikali imepokonya halmashauri chanzo cha mapato yake ya ndani ambacho ni kodi ya majengo (Property Tax) ambayo ni chanzo kikuu cha mapato katika halmashauri nyingi hasa majiji. Binafsi sioni sababu yoyote zaidi ya mgongano wa maslahi kisiasa kwa kukichukua chanzo hiki kwa kuwa ni kama kuua halmashauri za majiji.

Serikali imeziongezea halmashauri majukumu ya kusimamia elimu bila malipo kwa kuzitaka zihusike kulipa fedha za mlinzi, maji, umeme, na madawati. Pia halmashauri zinakabiliwa na madeni mengi ambayo kwa hali ya sasa zitashindwa kujiendesha. Mzigo mwingine ni kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya makundi maalum ambayo ni vijana na wanawake.

Naona kama huu ni mpango wa kuua serikali za mitaa. Kwa sasa halmashauri hazina fedha, badala yake makusanyo yanaingia katika mfuko mkuu wa serikali, kisha matumizi yagawanywe kulingana na bajeti.

Hii si sawa kwa kuwa, kabla ya mfumo huu serikali ilitakiwa kupeleka fungu halmashauri kila robo mwaka (OC) lakini fedha hizi zimekuwa zikichelewa kila mwaka na kusababisha shughuli zinazotegemea fungu hili kukwama ama kuzorota kiufanisi. Sasa kama fedha hizo chache zilikuwa zinasumbua sembuse hizi ambazo zinatolewa kwa mafungu tofauti tofauti.

Bajeti za halmashauri zimepunguzwa kiasi kwamba shughuli za halmashauri zitakwama. Mfano, katika ofisi ya viwanda, biashara na masoko yenye majukumu kama kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wafanyabiashara, kukusanya mapato ya halmashauri na kutoa leseni, kutembelea maeneo ya uwekezaji na kushauri wafanyabiashara, inapewa shilingi milioni 3 kwa mwaka.

Hapo ni majumuisho ya matumizi ya ofisi kama malipo ya likizo, mafunzo ya kitaaluma (professional development), mafuta ya dizeli na kadhalika. Aidha, umetumwa waraka kuwa zitengwe milioni 2 kwa ajili ya kuwezesha mafunzo yatolewayo na taasisi fulani iliyopendekezwa na serikali ije kutoa mafunzo. Sasa tunawezaje kutegemea kuona maendeleo ya viwanda, biashara na masoko?

Wigo wa kodi

Hadi sasa serikali imeendelea kutazama vyanzo vidogo vya mapato hasa vile vinavyomgusa mlaji moja kwa moja. Mfano, serikali kujikita kwenye kodi katika vileo na vinywaji baridi, kunamuumiza zaidi mwananchi wa kawaida pamoja na kudumaza biashara ya vinywaji hivi hasa vileo.

Pamoja na kuwa ongezeko la kodi linaweza kulenga kupunguza matumizi ya vileo au bidhaa za anasa, lazima serikali ifanye tathmini ya kina kuona madhara yake. Kabla ya bajeti, wazzalishaji wa pombe hapa nchini waliweka bayana jinsi mapato yao yalivyoshuka kwa asilimia 30 kutokana na sheria kali zilizowekwa.

Tukumbuke hawa ni wafanyabiashara na wana historia nzuri ya ulipaji wa kodi. Iwapo watakuwa wanajiendesha kwa hasara, wanaweza kusimamisha shughuli zao za uzalishaji jambo ambalo litaigharimu nchi kwa mapato na vile vile wananchi ambao watalazimika kununua bidhaa toka nchi jirani. Na serikali itakusanya kodi kutoka wapi ikiwa wenye viwanda watavifunga?

Kuwa na utaratibu mzuri wa matumizi ya pombe na bidhaa za anasa si kosa, ila namna gani ya kupunguza matumizi haya ndipo kosa laweza kufanyika. Serikali haipaswi kumnyima mtu kutumia mvinyo bali kumwekea mazingira ambayo yatamfanya  mwananchi akose huo muda. Mfano, kuna watu wanafanya kazi ya ulinzi, na hawa muda wao wa kujidai ni asubuhi hadi mchana. Sasa ukiwataka wanywe kuanzia saa tisa, hapo kazi itaendaje?

Vilevile serikali haijasema popote kwenye mazao ya misitu, utalii, na rasilimali kama madini watakusanya kiasi gani na ni namna gani watadhibiti utoroshwaji wa nyara za serikali zinazotupotezea fedha nyingi. Zaidi ya kusema itatoa mafunzo kwa wakaguzi ili wajue namna ya upimaji wa madini, bado serikali haijawa wazi kuweka bayana nini kinapatikana huko.

Kwa wingi wa rasilimali hii, kama udhibiti na usimamizi wa madini ungekuwepo, hakukuwa na haja kabisa ya kukopa. Lakini kwa kuwa hakuna hiyo nia ya kuvunja mikataba mibovu ya madini, binafsi ninashawishika kuwaza kuwa, serikali inawaogopa wamiliki, au vyanzo hivi vikuu vya mapato vimeshauzwa.

 

Kulimbikiza madeni

Bajeti hii inaeleza kuwa matumizi ya serikali yameongezeka kwa kulinganisha na mwaka uliopita, jambo ambalo linapingana na sera ya kubana matumizi inayonadiwa na serikali kila kukicha. Bajeti iliyopita ilitumia kiasi cha trilioni 16.57 kwa matumizi ya kawaida na mwaka huu serikali itatumia trillion 17.72 kwa matumizi ya kawaida. Pamoja na kuwa makisio ya bajeti ya mwaka huu ni makubwa, haimaanishi na matumizi ya kawaida yaongezeke kwa kuwa, mwaka uliopita, fedha hizo zilitumika pia kwenye shughuli za uchaguzi na mwaka huu hakuna.

Hakuna popote ambapo serikali imetenga fedha za kulipa malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi wa umma ambayo serikali iliahidi kuyalipa. Vilevile, kuna maeneo serikali inaonesha imedhibiti kodi wakati imebadilisha maneno tu.

Mfano, wanaulinzi na usalama wamefutiwa kodi katika maduka yao huku waziri akipendekeza walipwe posho itakayokuwa mbadala wa ule msamaha ili waweze kumudu kununua bidhaa kwa bei ya kawaida. Kimsingi ni kama kuhamisha mzigo kichwani ukauweka mabegani.

Suala la udhibiti wa mfumuko wa bei bado limekuwa changamoto hasa kwa bidhaa ya sukari. Kinachonishangaza ni kitendo cha serikali kutoa bei elekezi ya rejareja na kuacha kuitazama ‘supply chain’ ya bidhaa husika si sawa. Kwa mtiririko wa kawaida, kiwanda kinamuuzia wakala, na wakala anamuuzia muuzaji wa jumla naye atamuuzia wa rejareja, na wa rejereja atamuuzia mtu mmojammoja.

Sasa inakuwaje bei ya rejereja ijulikane na ya jumla isijilikane? Au ya kutoka kiwandani isijulikane? Hapa ndipo serikali ilikwama na bei elekezi ya 1,800 kwa kilo ikafeli. Badala ya serikali kusahihisha kosa hilo, imekuja tena na bei elekezi ya Sh 2, 200 hadi 2,400. Sasa ipi ni bei ya jumla? Wa jumla naye atauziwa na kuuza bei gani?

Ipo haja ya serikali kuacha kufikiri kuwa ni dhambi kwa watu kutoa maoni kuhusiana na kasoro zinazoonekana. Na kusiwe na dhana kwamba viongozi wa sasa ni malaika na wanachofanya hawawezi  kukosea. Hii ni nchi yetu sote, na tunaijenga kwa kushirikiana, kukosoana na kurekebisha mapungufu.

 

Ilani za miaka 5 hazifai

Kwa bajeti hii nina hakika madhumuni ya elimu hayataweza kutimizwa kwa ukamilifu katika bajeti hii kwa kuwa fedha za ruzuku zinazotolewa na serikali hazikidhi matumizi halisi. Vilevile mzigo uliopewa kwa halmashauri ni mkubwa mno kulinganisha na mapato yaliyopo.

Mfano idara ya elimu inaomba bajeti ya milioni 100 au zaidi lakini inapewa milioni 40, ambayo mafuta ya dizeli ni milioni 30, ukiachilia mbali matumizi mengine. Je unadhani ufuatiliaji utafanyikaje? Watumishi hawapandi daraja wala kupata ongezeko la kila mwaka (increment) unatarajia wafanye kazi namna gani?  Vitabu vya mtaala mpya vimefika mwezi huu, na kutarajiwa kuanza Julai ni utaratibu wa wapi wa kuanza mafunzo katikati ya mwaka?

Hakukuwa na haja serikali kulazimisha kuanza kutoa elimu bila malipo kabla ya kujipanga. Huwa anguko la mipango hutokea pale serikali inapolazimisha jambo fulani ili kutimiza ahadi za kisiasa.

Vyama vya siasa kwa ujumla havina nafasi kubwa kwenye kuboresha elimu. Binafsi nadhani vyama vya siasa vinachangia zaidi kuharibu mfumo wa elimu. Mchango uliopo ambao ni mdogo sana ni kuisukuma serikali, japo serikali inaweza isikubali kusukumwa kwa kuweka vizingiti mbalimbali.

Uharibifu niuonao hasa ni ule wa matumizi ya Iilani ya chama. Kila chama kina ilani yake, na ilani huwa hazifanani. Ina maana kwamba kama kila chama kingepewa eneo la kutekeleza ilani yake, tungekuwa na mseto wa ajabu sana. Ina maana kwamba, matumizi ya ilani hayafai kwa chochote katika nchi hasa kwa mfumo wa ilani tulionao, ambao ilani ndiyo inakuwa kipimo cha maendeleo katika nchi.

Nchi za wenzetu huwa na ilani zao, lakini zinazoongozwa na sera ya nchi. Nchi inakuwa na vipaumbele na nini kifanyike na tufikie hatua ipi, kisha vyama vinaleta ilani zao kusema sisi tutafikia malengo hayo kwa kufanya moja, mbili, tatu.

Lakini mpaka sasa sisi hatujui nchi inatakiwa iwe katika hatua gani, na ndio maana ni ngumu kusema chama kimefeli. Utaulizwa kimefeli kwa kulinganisha na mifano ipi? Hapa tulipofikia lazima tuwe na sera ya nchi isiyobadilika, itakayutumika kurekebisha ilani za vyama. Sera ieleze kwa nini, kwa kiwango gano na jkwa muktadha upi.

Badala vyama viseme nini kama ilivyo sasa, vitatakiwa viseme kwa namna gani. Chama kuamua kitawapa nini wananchi ni kosa kubwa sana na ndio uchochoro wa kudhorotesha maendeleo.

Mifano ipo mingi, chama kinasema, muhula huu ni wa viwanda, au muhula huu ni wa elimu bila malipo, au waziri anaamka huko anasema mtaala unabadilika, kwa kuwa tu hakuna sera inayomdhibiti, tunaona mabadiliko yasiyo na tija.

Kama nilivyosema, ilani zinaleta mwanya wa matumizi mabaya ya madaraka kwa kuwa waziri aweza kubadilisha chochote. Mfano, akiunda urafiki na wachapishaji vitabu, mtaala unabadilishwa, vitabu vya zamani vinafutwa na wachapishaji wapya wanaletwa jambo linaloondoa tija ya elimu.

Nakumbuka nilisoma kwa kutumia vitabu vya Taasisi ya Elimu iliyokuwa inatoa vitabu na vimeandikwa ‘Hakiuzwi’. Vitabu hivyo ubora wake haujawahi kuonekana wala kukaribiwa na watunzi waliojitokeza baada ya mtaala kubadilishwa na kuruhusu kila mtunzi kutunga anachojisikia na kupewa ithibati. Huu ni mwanya wa rushwa, kwa kuwa kuna vitabu ambavyo havikuwa naubora wowowte na vilipewa ithibati.

Nashauri, wataalam wa elimu na wa sekta mbalimbali wajumuishwe kutunga sera za nchi ambazo zitatoa dira ya nchi kwa miaka mingi. Wataalam hawa wahusishwe na wale waliosoma nje waliobahatika kujifunza sera za wenzetu ili kuweza kupanga mipango ya muda mrefu.

Ilani za miaka 5 hazitufai kabisa. Ndio maana viongozi watakuwa hisia za kufanya mambo yanayoonekana lakini ya muda mfupi. Wenzetu wako tayari kufanya jambo ambalo litakumbukwa milele hata kama asipumuwepo madarakani, lakini sisi tupo tukinusanusa mambo madogomadogo kwa kujinufaisha na siasa.

 

Changamoto ya usawa wa kulipa Kodi

Nimalize kwa kujumuisha katika hoja hii muhimu katika maisha yetu. Kati ya mambo ya maana kabisa ambayo serikali imeyakumbuka kwenye bajeti ni kupanua wigo wa usawa kwenye ulipaji kodi. Maeneo yaliyoguswa ni kiinua mgongo cha wabunge na kufuta msamaha kwenye maduka ya wanausalama (jeshi na polisi).

Kuhusu maduka hayo, ukweli ni kwamba waliokuwa wanayatumia si wanausalama peke yako. Wananchi wa kawaida walikuwa wakitumia migongo ya hao wanausalama na hivyo serikali ilikosa mapato.  Japokuwa maduka haya bidhaa zake zitatozwa kodi, mapendekezo ya serikali ni kuwapa posho itakayowasaidia kujikimu kununua bidhaa kama wananchi wa kawaida.

Hapo kunaweza kuwa na changamoto, kwamba ni kiasi gani ‘kitatosha’ kwa wao kuweza kumudu. Na hapa serikali isipokuwa makini inaweza kupata hasara zaidi kuliko hivi sasa kwa kuwa posho zina mambo mengi.

Kuhusu kiinua mgongo cha wabunge, ukweli serikali imejikaza, japokuwa wabunge wengi wanaonesha kutoliunga mkono. Tukitazama kwa jicho la kiuchumi, wabunge wanapata fedha nyingi kuliko watumishi wa kawaida.

Sitaki kusema mshahara ufanane, hapana, namaanisha kuwa kazi wanayoifanya hailingani na fedha wanayopata. Kiinua mgongo chao kwa miaka mitano ni mara dufu na zaidi ya akipokeacho mtumishi aliyetumikia serikali katika umri wake wote aliokuwa na nguvu hadi zikamwishia.

Kwa jicho la kisheria, wabunge ndio watungao sheria hizi, na wameitumia nafasi hiyo kujipendelea, na bado wanashikilia rungu hilo kujipendelea. Kisiasa, tunaweza kuona wabunge wa upinzani wanasusia posho ya kikao, lakini ukweli ni kwamba hiyo posho hawahitaji sana kama ambavyo Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson anavyofikiri.

Wabunge ambao kazi yao ni pamoja na kujadili na kupitisha bajeti, vikao vyao bado wanalipwa posho jambo ambalo linaleta picha kwamba kuna watu na viatu katika kuitumikia hii nchi. Sera ya kubana matumizi inapaswa iwahusu Watanzania wote na si tabaka la chini. Serikali isiwe na ‘double standard’ katika utekelezwaji wa sera zake.

Mfano kikao cha mtumishi ni kazi yake  na kikao cha Bunge ni “Extra Duty” kwa mbunge. Nawaomba wananchi wenzangu tupaze sauti hadi zipasue ngoma za masikio ya hawa wabunge wanaotunga sheria za kujipendelea.

Binafsi, tozo la kodi kwa kadiri ya mapendekezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango naliunga mkono. Aidha, nimefurahishwa na hatua ya Waziri wa Fedha kuridhia hatua ya Rais Makamu wa Rais, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya kulipishwa kodi. Lakini ni vema kodi hiyo ikaelekezwa hata kwenye mishahara yao, isiishie kwenye viinua mgongo tu.

Kama suala la kodi lingeulizwa kwa wananchi kwamba walipe au wasilipe, je, kodi zingelipwa? Kama vile ambavyo wananchi wanaagizwa, na wabunge wapokee jambo hili kwa moyo mweupe. Wananchi hatusemi kiinua mgongo kipunguzwe kwa maana ya kile kiasi, bali kiasi kiwe kilekile, lakini kilichotozwa kodi.

Aidha, sijawasikia wafuasi wa Ukawa na wabunge wengine wa upinzani wakiunga mkono mapendekezo hayo. Ukawa wasijifiche chini ya kutoka nje, kwamba hawakupata mahali pa kusemea. Labda ningekuwa mimi mbunge wa upinzani, ningebaki wakati wa mjadala huu ili nipate nafasi ya kuunga mkono hili jambo.

 

Suluhisho la usawa wa kodi

Mosi, mapendekezo ya kodi au sheria zinazowagusa wabunge zisipewe nafasi ya kujadiliwa na hao watunga sheria kwa kuwa kutakuwa na “Conflict of Interest”.

Pili, wananchi wawe makini sana kwenye mambo haya ya kitaifa yanayowawezesha kuwatambua viongozi wao, na wakikataa, nasi wananchi tuwakatae.

Tatu, Serikali iondoe posho zote za wabunge ambazo wamenyimwa watumishi wengine.

Nne, serikali itazame kwa kina suala la wanausalama kwa kutumia mbinu nyingine na si ya posho. Wanausalama wanafahamika kwa kuwa wamesajiliwa, maduka yao yanaweza kubaki ila wakapewa kiwango cha mwisho cha manunuzi kwa mwezi au mwaka. Mfumo wa utambuzi wa picha zao na vitambulisho vyao view vinakaguliwa kwa njia ya Eletroniki na iwapo manunuzi yametimia kwa mwezi huo huwezi kununua tena.

Naamini njia hii itaweza kudhibiti manunuzi yao na mapato ya serikali. Haitakuwa rahisi mwanausalama kumpa mtu kitambulisho mtu mwingine wakati sura si yake. Haitakuwa rahisi mwanausalama kumnunulia rafiki yake vitu wakati yeye hataweza kuvipata akifika mwisho wa manunuzi.

Baruapepe; happy.joseph67@yahoo.com