Home Habari Bajeti ya Serikali yazidi kuchambuliwa

Bajeti ya Serikali yazidi kuchambuliwa

1415
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

WIKI moja tangu Serikali ilipowasilisha bungeni mapendekezo ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/20 ambayo ni Sh trilioni 33.1, mjadala mzito umeibuka huku baadhi ya wasomi na wadau mbalimbali wa maendeleo  wakiendelea kuichambua katika mtazamo mpana wa maendeleo ya nchi.

Bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni Juni 13, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, pamoja na mambo mengine Serikali ilitangaza kufuta tozo mbalimbali 54.

Tozo hizo ambazo wasomi na wadau wanaona zitachangia uwekezaji wa ndani kukua, ni pamoja na zile zilizokuwa zikitozwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na katika sekta ya mifugo.

Pia zipo zile za ukaguzi wa maduka mapya ya bidhaa za chakula, ambayo ilikuwa Sh 50,000 kwa duka.

Pamoja na hali hiyo, suala la umeme unaouzwa Zanzibar Serikali ilitangaza kufutwa kwa kodi ya VAT ya asilimia 18, huku  watumiaji wa Tanzania bara wakiendelea kulipa asilimia 18 ya VAT.

Katika bajeti hiyo ya Serikali, TRA imepigwa marufuku kufunga biashara kwa sababu ya madeni na kwamba uamuzi huo sasa utafanywa kwa kibali maalumu cha kamishna na si vinginevyo.

Bajeti ya mwaka huu ni tofauti na bajeti zilizopita, ambazo mara nyingi zilikuwa zikiongeza ushuru katika bia na sigara, hii haujaongezwa wala kupunguzwa.

Tozo zilizoongezwa katika bajeti ya sasa ni pamoja na ile ya leseni ya udereva ambayo  imepandishwa kutoka Sh 40,000 hadi 70,000, ada ya usajili wa magari Sh 10,000 – 50,000, bajaji Sh 10,000 – 30,000 na pikipiki Sh 10,000 – 20,000.

Kufutwa msamaha wa kodi taulo za kike, pia nywele za bandia  kutoka nje kuingia kwa mara ya kwanza katika tozo ya asilimia 25, wachambuzi hao wanaona zimeifanya bajeti ya sasa kuwa na sura nyingine.

WACHAMBUZI

Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini (Repoa), Dk. Lucas Katera, katika uchambuzi wake, hasa uamuzi wa Serikali kuondoa tozo mbalimbali, alisema bajeti hiyo imegusa maisha ya Mtanzania wa kawaida.

 “Mfano wakulima wadogo ambao wanafuga kuku na wavuvi wameondolewa tozo, wafanyabiashara wa kati wameondolewa tozo za kero kama za TBS, TFDA na Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema Dk. Katera.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, alisema wao wanaipongeza Serikali kwa kuongeza mishahara ya watumishi kutoka Sh trilioni 6 bajeti iliyopita hadi Sh trilioni 7.

Alisema kutokana na ongezeko hilo, wana imani sasa kilio cha walimu kimesikika.

Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Michael Massawe, akizungumzia kuhusu kuongezwa kwa tozo za usajili wa bodaboda katika bajeti ya 2019/20, alisema wamepokea na kwamba hawana namna.

“Tumelipokea japo ni maumivu, lakini hatuna namna, tunajua mwanzo tutaumia ila baadaye tutazoea. Lakini pia tunaiomba Serikali pale inapochukua uamuzi wa namna hii, iangalie mahitaji yetu kwa sababu tunakuwa hatufikii malengo yetu,” alisema Massawe.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema bajeti hiyo ni kama inang’ata na kupuliza kwa sababu kuna mambo mazuri yanayofurahisha, mengine yanaumiza.

 “Bajeti imeorodhesha mambo ambayo yalikuwa changamoto, mfano upotevu wa mapato, hasa bandari bubu, ugumu wa kukusanya kodi kwenye sekta zisizo rasmi.

“Sijaona mipango ya kuzuia upotevu wa fedha kwenye bandari bubu, ni vyema kungekuwa na ulinzi madhubuti na mpango maalumu kuhakikisha hizo bidhaa hazipotei,” alisema Henga.

DK. BASHIRU

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, aliichambua bajeti hiyo na kusema kwamba imeakisi mambo ya msingi yaliyowekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho tawala.

“Ni mapendekezo mazuri yanayolenga shabaha zetu katika Ilani ya CCM. Tuliahidi kukabiliana na matatizo ya kiuchumi, ajira, umasikini, rushwa ufisadi, amani na utulivu.

“Kama mlivyosikia, sekta zilizopewa kipaumbele kama viwanda, biashara, kilimo na kodi zimeonyesha matarajio makubwa, kwani miradi yetu mikubwa itatekelezwa vizuri,” alisema Dk. Bashiru.

Kutokana na hali hiyo, aliwaomba wabunge wa CCM na upinzani kujadili vizuri bajeti hiyo, lengo likiwa ni kuboresha mapendekezo hayo ya bajeti kuu.

PROFESA SEMBOJA

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, alisema bajeti hiyo imeonesha utofauti kwa sababu haijaenda nje ya mategemeo na uwezo wa Serikali katika kutumia rasilimali zilizopo na kuwezesha wananchi kuwa wawekezaji katika ukuaji wa uchumi.

Alisema kwa kawaida bajeti hutafsiriwa katika mapato na matumizi ya Serikali na kwamba kazi ya Serikali inajulikana kuwa ni kushughulikia masuala ya sera, sekta zote za maendeleo, ulinzi na usalama.

“Ukiangalia katika bajeti hii, mimi ningesema ni bajeti moja nzuri, imekuwa ina ‘details’ (maelezo) zote bila kuwa na wasiwasi. Bajeti ya zamani ilikuwa wanaongeza na kupunguza basi, na hakukuwa na maelewano kati yao na sekta binafsi,” alisema.

MFURUKI

Mwenyekiti wa Kampuni ya InfoTech Investment Group Ltd, Ali Mufuruki, ambaye alizungumza na kituo kimoja cha redio, alisema bajeti hiyo ni nzuri na imejibu maswali ya wafanyabiashara.

“Kwa kifupi ni bajeti nzuri ambayo inaonekana hasa kusapoti wafanyabiashara kwa kujibu maswali ambayo tulikuwa tukiuliza kwa muda mrefu, kuhusu usimamizi wa kodi ambao unatakiwa kuwa wa haki,” alisema.

KAMATI YA BUNGE

Mapema wiki hii, Kamati ya Kudumu ya Bajeti ilitaja maeneo muhimu ambayo yatasaidia kupatikana kwa vyanzo vipya vya mapato, ikiwemo urasimishaji wa sekta isiyokuwa rasmi.

Maeneo hayo yalitajwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, George Simbachawene, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20 pamoja na tathmini ya utekelezaji  wa bajeti ya Serikali  kwa mwaka 2019/20.

Simbachawene alisema kuna idadi kubwa ya wafanyabiashara wadogo wanaojihusisha na shughuli ambazo hazipo katika mfumo rasmi, hivyo kusababisha ugumu katika kuzilea ili zikue na baadae kuchangia katika mapato ya kodi.

“Kamati inaamini kwamba hatua hizo zikikamilika zitarahisisha utambuzi kwa nia njema ya kujenga na kuendeleza sekta isiyo rasmi ili iweze kukua na mchango kuonekana katika pato la taifa,” alisema.

Pia alitaja eneo jingine kuwa ni katika huduma za kifedha ambapo kamati imeishauri Serikali kuziongezea mtaji Benki ya Kilimo (TIB) na Benki ya Rasilimali (TADB).

“Uwekezaji katika sekta ya viwanda na sekta ya kilimo, hasa kilimo cha mazao ya biashara, huhitaji fedha nyingi na kuchukua muda mrefu kutoa faida na umegubikwa na vihatarishi vingi,” alisema.

Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe (CCM), alitaja chanzo kingine ni kwenye diplomasia ya uchumi.

“Eneo hili ni muhimu katika kusaidia Serikali kupata mapato kupitia uhamasishaji wa vivutio vilivyopo ili kupata wawekezaji wa kigeni kwenye sekta ya kilimo, uvuvi, utalii, miundombinu, biashara  na huduma,” alisema.

Katika hatua nyinge, Kamati imeishauri Serikali ihakikishe inaunganisha taasisi zote zenye majukumu yanayofanana (OSHA, TBS, TFDA, Fire) ili kurahisisha  utekelezaji katika maeneo mbalimbali.

KAMBI YA UPINZANI

Naye Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde, alisema bajeti mbadala ya kambi hiyo itakuwa ni ya zaidi ya Sh trilioni 29.

Alisema vipaumbele katika bajeti yao ni sekta za elimu ambayo imetengewa zaidi ya Sh  trilioni 4, kilimo zaidi ya Sh trilioni 5, viwanda zaidi ya Sh trilioni 4, maji zaidi ya Sh trilioni 2, afya zaidi ya Sh trilioni 2 na mengineyo Sh trilioni 8.

Pia kambi hiyo ilidai kwamba bajeti ya Serikali imejikita kwenye maendeleo ya vitu na sio ya watu.

Silinde pia alidai kwamba mfumo wa ulipaji kodi umekuwa ukilalamikiwa kwa miaka mingi na wafanyabiashara ambao ndio huwa wanalipa kodi, hivyo mfumo huo sio shirikishi.

“Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa pendekezo,  kutokana na kuendelea kupungua  kwa makusanyo ya kodi licha ya Serikali hii ya awamu ya tano kutumia mbinu nyingi za kukusanya mapato, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kikosi maalumu cha kukusanya kodi,” alisema.

Pia kambi hiyo ilisema kwamba usimamizi  ni dhaifu katika usimamizi wa deni la taifa.

WABUNGE WACHAMBUA

Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), aliiomba Serikali kuwasaidia wakulima wa zao la pamba kutokana na wanunuzi kujipangia bei.

“Tuache siasa katika zao la pamba, tunawanyanyasa wakulima, kwenye zao la pamba misimu yote unapotaka kuanza msimu wa pamba mara unasikia umepanda, unasikia wanauza 1,400 mpaka 1,500. Serikali iingilie kati hii sio bure, wanunuzi wanataka kuwaibia wananchi,” alisema Ndassa.