Home Habari Bajeti ya uchaguzi Serikali yaeleza ilivyotekeleza mpango wa maendeleo

Bajeti ya uchaguzi Serikali yaeleza ilivyotekeleza mpango wa maendeleo

599
0
SHARE

MWANDISHI WETU – DODOMA

SERIKALI imewasilisha tathimini ya mwenendo wa hali ya uchumi na utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa mwaka wa fedha wa 2019/20 inayolenga kutumia Sh. trilioni 34.88 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.

Bajeti hiyo inaweka kipaumbele kuwa ni Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwa wabunge jijini Dodoma wiki hii, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema kuwa mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2020/21 ni ya mwisho katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/17 – 2020/21.

Dk. Mapango alichanganua kuwa kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 21.98 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 12.90 za matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote.

Dk. Mpango alisema kuwa bajeti ya maendeleo inajumuisha Sh. trilioni 10.16 fedha za ndani, sawa na asilimia 78.8 ya bajeti ya maendeleo na Sh. trilioni 2.74 fedha za nje. Matumizi hayo yanajumuisha gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Oktoba mwaka huu Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani. Hii ni baada ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kumaliza muhula wake wa kwanza wa miaka mitano tangu alipoingia madarakani mwaka 2015.

“Kwa upande wa Serikali, tumejipanga kikamilifu katika maandalizi ikijumuisha mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo. Napenda kuchukua nafasi hii kuwasihi Watanzania wote washiriki uchanguzi huu muhimu na wazingatie umuhimu wa kuendelea kudumisha amani ya nchi yetu.

 “Kila anayehusika atekeleze wajibu wake kulingana na nafasi yake tukianzia kwa viongozi wa madhehebu ya dini, wagombea wa nafasi mbalimbali, wapiga kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama, wasimamizi wa uchaguzi, vyombo vya habari na hata waangalizi wa kimataifa watakaokuwepo nchini wakati huo. Napenda kuwahakikishia Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuwa uchaguzi utazingatia haki na utafanyika kwa usalama, amani na utulivu wa hali ya juu,” alisema.

Akizungumzia mpango huo wa maendeleo, alisema kuwa una dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.

Aidha, alisema kuwa mapendekezo haya yamezingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 ambayo katika kipindi hicho cha utekelezaji wa mpango, mafanikio makubwa yamepatikana kupitia uongozi Rais Magufuli.

Waziri Mpango alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2016 hadi mwaka 2019, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka.

Alisema kuwa ukuaji huu ulichochewa na sekta ya ujenzi kufuatia kuongezeka kwa uwekezaji hususan katika miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za maji; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; kuimarika kwa shughuli za habari na mawasiliano.

“Kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. Mwenendo mzuri wa ukuaji wa Pato la Taifa umechangia kuongezeka kwa ajira 6,032,299, ambapo ajira 1,975,723 ni kutoka sekta rasmi na ajira 4,056,576 ni kutoka katika sekta isiyo rasmi.

“Mfumuko wa bei umeendelea kubaki ndani ya wigo wa tarakimu moja wa wastani wa asilimia 4.4 kati ya mwaka 2016 na mwaka 2019. Kati ya Julai 2019 hadi Januari 2020 mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.7 ambao uko ndani ya lengo la ukomo la mfumuko wa bei wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wa asilimia 5,” alisema Dk. Mpango.

UJAZI WA FEDHA                                                   

Dk. Mpango alisema kuwa  ujazi wa fedha umeendelea kukua kwa kasi kulingana na mahitaji ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Alisema katika mwaka 2019, ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi uliongezeka na kufikia Sh. bilioni 28,313.1 kutoka Sh. bilioni 25,823.5 mwaka 2018, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.6, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.5 mwaka uliotangulia.

Alisema ukuaji huo unadhihirisha kuwepo kwa fedha za kutosha kuendesha shughuli za uchumi, na kuongezeka kwa uwezo wa sekta ya kibenki kutoa mikopo kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, ujenzi na madini.

Alifafanua kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka na kufikia Sh. bilioni 19,695.4 mwaka 2019, kutoka Sh. bilioni 17,726.8 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 11.1, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 4.9 mwaka 2018.

Aidha, rasilimali katika sekta ya kibenki ziliongezeka na kufikia Sh. bilioni 33,067.4 kutoka Sh. bilioni 30,374.0 mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.9.

“Vile vile, ubora wa rasilimali za sekta ya kibenki uliimarika kama inavyodhihirishwa na kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu kutoka asilimia 10.7 Desemba 2018 hadi kufikia asilimia 9.8 ya mikopo yote Desemba 2019. Serikali kupitia Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kupunguza uwiano wa mikopo chechefu ili kufikia lengo la asilimia 5,” alisema. 

 MAUZO YA BIDHAA

Alisema mauzo ya bidhaa na huduma nje, yalikuwa dola za Marekani milioni 9,712.6, ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 8,398.3 mwaka 2018. Thamani ya mauzo ya bidhaa zisizo asilia iliongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 4,236.6 mwaka 2019 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 3,209.3 zilizopatikana mwaka uliotangulia

AKIBA YA FEDHA

Waziri huyo alisema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa Desemba 2019, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 5,567.6, kiasi kinachotosheleza kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.4.

Alisema kiwango hicho ni zaidi ya lengo la nchi la kuwa na akiba ya kutosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa muda wa miezi 4, ikiwa pia ni juu ya lengo lililokubalika katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi isiyopungua 4.5 na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika la miezi isiyopungua sita

Alisema hadi Januari 2020, Serikali imefanikiwa kukopa Sh. trilioni 3.04 kutoka soko la ndani sawa na asilimia 100.9 ya lengo la Sh. trilioni 3.01. Kati ya kiasi hicho, Sh. trilioni 2.23 zilitumika kulipia mikopo ya ndani iliyoiva na Sh. bilioni 806.8 zilitumika kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo.

MIRADI YA MAENDELEO

Alisema kuwa katika mwaka 2019/20 jumla ya Sh. trilioni 12.25 zilitengwa kugharimia miradi ya maendeleo, kati ya hizo Sh. trilioni 9.74 zilikuwa fedha za ndani na Sh. trilioni 2.51 ni fedha za nje.

“Hadi Januari 2020, jumla ya shilingi trilioni 6.22 zilitolewa kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo sawa na asilimia 71.9 ya lengo la shilingi trilioni 8.67. Aidha, Serikali imetumia shilingi trilioni 5.80 kulipia deni la Serikali lililotokana na mikopo iliyotumika kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Baadhi ya miradi hiyo ni: mradi wa maji Arusha; mradi wa maji Ruvu Chini; mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi, mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kv 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga; upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Zanzibar; Mradi wa Kuboresha Huduma katika mji wa Zanzibar; Mradi wa Serikali Mtandao Awamu ya Pili Zanzibar.

“Ujenzi wa Jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere; ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara, Kigoma, Shinyanga, Sumbawanga na Mwanza; ukarabati wa reli ya Kati; na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam,” alisema

Dk. Mpango alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia mwaka 2016/17 hadi Januari 2020 chini ya utawala wa Rais Magufuli.

“Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge: Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 75 na kwa kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) asilimia 25.

“Hadi Septemba 2019, mradi huu umezalisha takribani ajira 13,117. Aidha, zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni 664.7 zimetolewa kwa wazabuni na makandarasi wa ndani 640. Jumla ya shilingi trilioni 2.96 zimetumika kugharimia mradi huu zikijumuisha shilingi bilioni 237.5 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020;

“Ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere – Mw 2,115: kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi (njia ya kusafirisha umeme, barabara kwa kiwango cha changarawe, mfumo wa maji, mawasiliano ya simu na nyumba za makandarasi); ujenzi wa daraja la muda namba 2,” alisema

 MPANGO WA MAENDELEO 2020/21

Alisema mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21.

Aliitaja kuwa viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, miradi itakayotekelezwa katika eneo hilo inalenga kujenga viwanda vinavyotumia kwa wingi malighafi zinazopatikana nchini zikiwemo za kilimo, madini na gesi asilia ili kukuza mnyororo wa thamani.

UKOMO WA BAJETI 2020/21

Alisema Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, iliyoidhinishiwa ina jumla ya Sh trilioni 33.11, ikijumuisha Sh. trilioni 20.86 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 12.25 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya mapato ya ndani yalitarajiwa kuwa shilingi trilioni 23.05. Kati ya mapato hayo, Serikali ililenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 19.10, mapato yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 3.18,” alisema.