Home Habari Bakwata mpya Mwanza yaja na mikakati ya kuboresha uchumi

Bakwata mpya Mwanza yaja na mikakati ya kuboresha uchumi

796
0
SHARE

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza limedhamiria kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa waumini wa misikiti yote mkoani humo kwa kuimarisha upendo, mshikamano na kuendelea kutenda mambo mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu.

Shehe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassan Kabeke ambaye aliteuliwa rasmi Oktoba 10 mwaka jana kushika wadhifa huo na Baraza la Ulaama Taifa kupitia kwa mwenyekiti wake ambaye ni Mufti wa Tanzania, Alhaji Shehe Abubakar Bin Zuberi Bin Ally Mbwana, anaeleza mikakati ya kuijenga Bakwata mpya kwa mkoa wa Mwanza katika mahojiano na mwandishi; NASHON KENNEDY

Swali: Ukiwa ndio kwanza umeteuliwa na Mufti wa Tanzania, Alhaji Shehe Abubakar Bin Zuberi Bin Ally Mbwana kupitia Baraza la Ulaama Taifa, nini vipaumbele vyako kwenye uongozi wako?

Jibu: Moja ya vipaumbele vyangu kama Shehe wa Mkoa wa Mwanza ni kuimarisha uchumi wa Bakwata, mkoa wa Mwanza na elimu ya mafundisho ya dini. Binafsi miongoni mwa mambo yanayonikera ni hali duni ya maisha hivyo dhamira yangu ni kuhakikisha kuwa katika kipindi cha uongozi wangu mikakati ya kiuchumi inaimarishwa zaidi?

Swali: Kupitia mikakati yako hiyo, unatarajia kutekeleza mambo yapi?

Jibu: Nitakuja na mipango madhubuti ya kuimarisha uchumi wa Bakwata kwa kuanzisha miradi itakayokuwa na lengo la kubadilisha maisha ya mashehe wetu, walimu wa madarasa na maimamu wa misikiti ambao kimsingi ndio zao la dini ya uislamu na misingi yake.

Swali: Kwanini umelenga zaidi madrasa na misikiti?

Jibu: Madrasa na misikiti ndio eneo dhaifu kutokana na walimu na mashehe kushindwa kufundisha elimu ya dini na hata ujira wao ni mdogo wanazidiwa na watumishi wa ndani jambo ambalo linanifanya nihangaike katika kipindi cha uongozi wangu kwa kushirikiana na wenzangukwa kumtanguliza Allah ili tuone ni namna gani tunaweza kulitafutia tiba tatizo hilo.

Ili kuboresha hali za walimu wa madrasa, mashehe, maimamu na waumini wetu tutakuwa na vyanzo madhubuti vya mapato vitakavyosaidia Bakwata na waislamu na haiwezekani na katika kipindi cha uongozi wangu sitaki kuona Bakwata tunakuwa ombaomba.

Kwa sasa Bakwata ina hali mbaya kiuchumi na ni taasisi pekee isiyo na wanachama wanaolipa ada wakati chombo hiki kinawapa heshima, hivyo kwa mkoa wetu katika kutekeleza dira ya kuleta maendeleo, viongozi wa ngazi ya mkoa tutachangia Sh 8000 kwa mwezi ikiwa ni sawa na Sh 2000 kwa wiki fedha hizo zitawekwa kwenye akaunti maalumu kwa ajili ya ustawi wetu na lengo letu ni kwamba ndani ya mwaka tujenge jengo la kitega uchumi, tuwe na uwezo wa kulipa mishahara ya walimu wa madarasa na mashehe sanjari na kutatua kero zao.

Swali: Tumeshuhudia kwa baadhi ya madhehebu na taasisi nyingi za kidini zikiwemo dini ya kiislamu, watu wanapopata madaraka hubadilika kitabia na kimwenendo, nini kauli yako juu ya hilo?

Jibu: Kwanza niwahakikishie waumini wangu, viongozi wenzangu na Mufti wa Tanzania, Alhaji Shehe Abubakar Bin Zuberi Bin Ally Mbwana, kwamba jambo kama hilo katika utumishi wangu haliwezi kutokea, nitatekeleza majukumu yangu kwa kufuata kanuni na taratibu zilizopo.

Pili niwaondoe hofu, maana wapo baadhi ya watu wanaosema kuwa mimi ni mkali, la hasha, ukali wangu unajidhihirisha pale ninapokuwa natenda haki. Binafsi nauchukia ufisadi, wizi na umasikini hata Mufti wa Tanzania, kilio chake kikubwa kimekuwa ni kutaka kuwatoa waislamu kwenye udhalili (unyonge), katika hili la kuimarisha uchumi niko radhi nilaumiwe kama nisipotenda haki na Mwenyezi Mungu anihukumu.

Swali: Suala la unyonge lipo sana misikitini kwa baadhi ya waumini kama ulivyosema, nini kifanyike kuondoa hali hiyo?

Jibu: Ndugu waislamu hawana sababu ya kuwa wanyonge na wasinione mimi ni mkali bali nitautumia ukali wangu huo kwa kuwaondoa kwenye unyonge wao.

Na niwaombe viongozi na waumini watumie neema tuliyopewa na Mwenyezi Mungu katika kutafuta pepo na nyumba ya ahera.

Swali: Vipi kuhusu malalamiko ya baadhi ya waislamu kutengwa katika elimu?

Jibu: Kuhusu elimu ambayo imegawanyika katika sehemu kuu tatu, niwaombe ndugu zangu waislamu waache kulalamika kuwa taasisi yao inahujumiwa na kuchafuliwa kwa lengo la kupoteza akidhi yetu.

Wakati walio na dhamana ya kufundisha elimu ya dini mashuleni hawatimizi wajibu wao na kusababisha vijana wanaoa na kuolewa kwa misingi ya dini ya kiislamu kukosekana.

Kwa kusimamia yote haya kama ndiyo tafsiri ya ukali wangu, lazima waumini watambue kuwa jukumu nililonalo lazima nihakikishe kuwa naijenga Bakwata mpya kwa ajili ya waumini, mashehe, maimamu na walimu wa madrasa.

Swali: Tayari umekuja na kauli mbiu yako ya Jitambue, Badilika na Acha mazoea, kauli mbiu hii inalenga nini katika Bakwata mpya?

Jibu: Kauli mbiu hii imejikita katika kutekeleza na kama Bakwata kujipambanua kwa mambo makubwa saba, ambayo ni elimu, kutambua ndoa na sensa ya waislamu, kuboresha huduma za kijamii, kuishi pamoja ndani ya imani tofauti, kumaliza migogoro ya kidini na kijamii, kuimarisha jumuiya za baraza na kutoa tafsiri juu ya kinachodaiwa elimu ya ugaidi kupitia elimu. Nikianza na ugaidi, tafsiri sahihi ya ugaidi inakuwa haifahamiki kwenye maeneo mengi.

Wananchi wamekuwa wakielewa isivyoelewa Serikali na Serikali inaelewa wasivyoelewa wananchi, wakiwemo waislamu na wasiokuwa waislamu. Hali hii imefanya waislamu waone wanasemwa vibaya na pengine Serikali kuonwa inatazamwa vibaya.

Sisi kama Bakwata kwa kushirikiana na taasisi ya Chemchem Trust Foundation na kwa kutumia gharama kubwa tumeandaa kongamano kubwa lililotoa elimu ya watu kufahamu maana ya ugaidi hali iliyowafanya waumini na wasiokuwa waumini kuelewa dhana hiyo na baadhi yao wameomba makongamano ya aina hiyo yafanyike tena.

Kwa upande wa migogoro ya kidini, ambayo mingi imekuwa inaanzia ndani ya majumba ya ibada, Bakwata tumefanya kazi kubwa eneo hili na mgogoro uliokuwepo baina ya waislamu wa Nyakato Buzuruga na wananchi uliodumu katika kipindi cha miaka 15 tumeumaliza kwa amani waumini na wananchi wamekumbatiana.

Halikadhalika pia kupitia Kamati ya Amani ya Wilaya ya Sengerema, imeshughulikia mgogoro wa uchinjaji wa Nyehunge na kuumaliza kwa siku tatu haya ni mambo makubwa ambayo tumeyafanya, hatua hii kutokana na mgogoro huo wa Nyehunge inathibitisha kuwa katika dhana ya kuishi pamoja na imani tofauti za kidini, imethibitisha kuwa nchi yetu haina dini lakini wananchi wake wana dini.

Na kwa msingi huo uongozi wa Bakwata Mkoa wa Mwanza kwa kushughulikia matatizo hayo unayoonyesha ni kwa jinsi gani Watanzania wanavyoweza kuishi kwa amani ndani ya dini moja.

Nichukue pia fursa hii kuzungumzia mitafaruku inayoendelea hivi sasa kutofautiana baina ya waislamu ya kuanza kufunga na kuchelewa kufunga wakati wa ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa ramadhan.

Hapa vimeibuka baadhi ya vikundi vya waumini na kusema kuwa sikukuu ya Idi ni ya Bakwata na kwamba Bakwata ni chombo cha Serikali. Mimi nasema watu hao wanaosema Bakwata ni chombo cha Serikali wana nia ya kutaka kuwaaminisha waislamu waone Bakwata kuwa sio chombo chao bali ni chombo cha Serikali.

Kimsingi mtu anayesema hivyo ana lengo la kuifitinisha Bakwata na Serikali yenyewe na ukweli wa mambo ni kwamba Bakwata ni chombo cha Serikali kwa maana ni taasisi ya kidini iliyosajiliwa na Serikali ya Tanzania kwa mujibu wa sheria. Na kutokana na usajili huo Bakwata ni chombo cha Serikali na serikali siku zote ni ya wananchi na Bakwata inawasimamia wananchi ambao ni waislamu wa Tanzania.

Kwa upande wa elimu, tumeanzisha idara ya madrasa ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia elimu ya dini kuanzia ngazi za awali kwa kuwatambua walimu hao na mtaala wanaotumia sanjari na kuunganisha mtaala huo na elimu ya dini mashuleni kwa wanafunzi wa sekondari kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu.

Tumeamua pia kutambua ndoa za waumini wetu sanjari na kufanya sensa kwa waumini, hii ni baada ya kushuhudia mashauri mengi yakipelekwa mahakamani yanayohusu hali za watu (waumini), ndoa na hitilafu za kifamilia na mahakimu wamekuwa wakitumia muda mrefu kwa mashauri haya.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Bakwata imeunda kamati za sensa na ndoa ambapo kwa sasa inaendelea na zoezi la kuzitambua ndoa zote za waislamu mkoani Mwanza na hali za maisha ya wanandoa.

Zoezi hili litaisaidia sana Serikali katika kuandaa takwimu zake za kimaendeleo lakini pia kuzipunguzia mahakama zetu muda wa kutafuta ushahidi wa hali za watu za ndoa kwa mashauri yanayowasilishwa kwao.

Mwisho namshukuru Mufti wa Tanzania Abubakar Zuberi bin Ali na Baraza la Ulamaa kwa kniteua, kuniona na kuniamini kwamba nafaa kumsaidia kwenye nafasi hiyo kubwa ambayo si ya kukimbiliwa na naahidi kuwa kwenye uongozi wangu sitabadilika na nitakubali kushauriwa.

Pia niishukuru Serikali Mkoa wa Mwanza kupitia kwa Mkuu wa Mkoa, John Mongela, wakurugenzi watendaji na wakuu wa wilaya zote kwa ushirikiano wanaonipatia ikiwemo Kamati ya amani ya viongozi wa madhehebu ya dini mkoa wa Mwanza.