Home Habari Bandari kufumuliwa tena

Bandari kufumuliwa tena

1459
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

HALI tete katika bandari ya Dar es Salaam inayotokana na kupungua kwa mizigo, kuzorota kwa teknolojia, pamoja na kushuka kwa mapato yanayotokana na shughuli za Bandari hiyo ni viashiria tosha kuwa uongozi wa Bandari hiyo ama Wizara iliyo na dhamana na bandari unahesabu siku ili kufumuliwa tena.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo upungufu wa meli zinazotia nanga bandarini hapo, huku pia ikibainika kuwepo kwa mitambo ya ukaguzi isiyofanya kazi,  kushuka kwa makusanyo kunakotokana na uduni wa teknolojia pamoja na kupungua kwa mizigo, masuala ambayo yameonesha kuwakera viongozi wakuu wa awamu ya tano, hivyo kuonesha dhahiri kuwa uongozi wa bandari hauendani na kasi ya utawala uliopo sasa madarakani.

Asilimia 42 ya mizigo inayokwenda nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es Salaam imepungua, huku kukiwa na siku ambazo meli moja tu ndiyo hutia nanga kupakua mizigo inayoingia nchini na ile ya nchi za jirani, zinazotumia bandari ya hiyo.

Ziara ya wiki hii ya Rais John Magufuli katika bandari hiyo inaelezwa kuwa ilisukumwa na utete wa mambo hayo na inaaminiwa ilifanyika kwa lengo la kujiridhisha baada ya taarifa za awali kuonesha mapungufu ya kiutendaji, kiteknolojia na kimkakati katika bandari hiyo.

Rais alifika Bandarini akiwa anatambua analofanya na analotaka kulifanya. Hata aina ya maswali aliyokuwa akiuliza yaliashiria kuwa anafahamu uchafu unaoendelea na kwamba unamkera.

“Lakini nikuulize waziri… wewe unafahamu mafuta haya yanapokuja ndio tunacollect hata fedha za road fund, ambazo ndizo zinatengeneza barabara zako, zinafanya maintenance, kweli… kwa muda huo wote tangu agizo lilipotolewa na Waziri Mkuu huwezi hata kufuatilia? Aliuliza Magufuli na kujibiwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa kuwa; “ nilifuatilia mheshimiwa mara mbili na tukakubaliana kwamba kama flow mita hizi hazifanyi kazi, wanunue flow mita mpya ili zifungwe,” alijibu.

Hata hivyo Magufuli hakuridhishwa na majibu hayo na kumuuliza tena; “Sasa kwanini hujanunua flow mita mpya, kama ni bei yake ni Sh 800,000, tunapoteza fedha nyingi mno, wanafanya udanganyifu mno, waziri mkuu amekuja hakuna kinachofanyika, mtu tu wa kupima anazuia whole process lakini kama hiyo flow haiwezi kufanyika hamna hata ninyi watalaam wa kuweza kuifanya?” aliuliza Magufuli huku waziri huyo akiendelea kujitetea mbele ya Rais kwa majibu yasiyoridhisha.

Rais Magufuli alipofika bandarini hapo na hasa katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo inayopita katika makontena, alibaini ubabaishaji pamoja na kukuta mashine za ukaguzi zikiwa hazifanyi kazi, hali inayoelezea kuwa, upo uhaba wa mizigo unaosababisha kushuka kwa mapato ya bandari, lakini pia hata mapato madogo yanayopaswa kukusanywa, hayakusanywi yote kutokana na mashine hizo za kukagulia mizigo inayopita bandarini hapo kutokufanya kazi.

Katika ziara hiyo, Rais pia aligundua kutokufanya kazi kwa mita za kupimia mafuta yanayopakuliwa melini (Flow Meters), jambo ambalo lilishatolewa maelekezo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, miezi kadhaa iliyopita na hivyo kuonesha uongozi wa Mamlaka ya Bandari kuwa mzito katika kutekeleza maagizo ya serikali. Mita hizo za kupimia mafuta kama zingekuwa zinafanya kazi, zingesaidia kufahamika malipo halali ya kodi inayotokana na mafuta yanayoingia nchini, lakini kutokuwepo kwake kunasababisha zoezi la ulipaji kodi hizo kufanyika kwa kukadiria, jambo ambalo ama linaipunguzia serikali mapato au kuwaumiza waagizaji wa mafuta.

Tukio lingine lililobainika na ambalo linaonesha kuwepo nia ya kufumua tena uongozi wa bandari ama vitengo vyake ni lile la Mkataba aliouita Rais Magufuli wa ‘kijanja’ ulioingiwa na Bandari na Wizara husika na Kampuni kimataifa ya kuhudumia shehena ya makasha bandarini (TICTS) ambayo inapakia na kupakua mizigo katika gati namba nane hadi 11. Rais ameitaka Wizara na Uongozi wa Bandari kujadiliana ili kurekebisha mkataba huo  ambao anadai hautoi nafuu kwa serikali.
Maagizo haya ya Rais yanatolewa sasa ikiwa ni miezi sita imepita tangu Waziri Mkuu kutoa maagizo kama hayo bandarini hapo, maagizo ambayo hayakutekelezwa hadi ziara hiyo ya Rais.

Baada ya Waziri Mkuu kufanya ziara tatu bandarini hapo, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari, Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi wa bandari, Awadh Massawe.

Magufuli alimteua Profesa Ignas Aloys Rubaratuka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia Mwezi Aprili mwaka huu, huku Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akimteua Mhandisi Deusdedit Kakoko kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA kuanzia Juni mwaka huu.

Pamoja na hatua hizo bado hali imeendelea kuwa tete katika bandari hiyo hali iliyoliamsha Bunge huku Kamati ya sekta ya Viwanda, Biashara na Mazingira ikitangaza uamuzi wa kuwakutanisha wadau  kujadili mdororo huo wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kamati hiyo ilitangaza kukutana na wadau  na Serikali  kujadili namna ya kuiwezesha bandari hiyo kurejesha mizigo ambayo kwa sasa inaonekana kupungua kutokana na sababu mbalimbali.

Kamati hiyo ilikutana na  wadau  na uongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambako ilibainika mkanganyiko wa taarifa kutoka kwa kila upande.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA, Deusdedit Kakoko, alikiri kupungua  mizigo katika bandari hiyo huku akielezea kuwa sababu za kupungua kwa mizigo bandarini hapo ni kudorora kwa uchumi wa China, kushuka  bei ya mafuta, gesi na shaba.

“Hofu ya wateja inayotokana na kuanzishwa  sheria ya VAT kwenye huduma zinazotolewa kwenye mizigo ya nchi jirani ambayo haitozwi kodi katika nchi zenye bandari shindani,” alisema Kakoko.

Alisema jambo jingine ni hofu ya wateja kuhusu utaratibu wa himaya moja ya ushuru wa forodha na kwamba mzigo unaohudumiwa kwenye mfumo huo unatozwa kodi kwa asilimia 100.

Mtikisiko huo uliwaamsha baadhi ya wasomi akiwamo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Profesa Mwesiga Baregu, ambaye alisema nchi inakoelekea ni pabaya hasa kama kunatokea mtikisiko katika nyanja muhimu kama bandari.

Alisema ni vigumu kwa nchi kusimama kama hakutakuwa na jitihada za kurekebisha mambo ambayo yanachangia kudumaza uchumi.

“Wateja wanaotumia bandari kama ya Dar es Salaam, wakishaamua kuelekeza mizigo yao katika bandari nyingine kama vile Mombasa au Beira ni vigumu kuwarudisha kwa sababu kule wanatumia gharama ndogo kurahisisha ufanikishaji wa biashara zao.

“Hivyo ni dhahiri matatizo yanayoikabili bandari yanaifanya serikali kuelekea pabaya, inatakiwa kujirekebisha mapema ili kunusuru uchumi wa nchi yetu hasa ikizingatiwa sasa kunao ushindani mkubwa wa bandari ikilinganishwa na nchi nyingine,” alisema.