Home Makala Bandari za Ziwa Nyasa kupaisha usafirishaji saruji, makaa ya mawe nje

Bandari za Ziwa Nyasa kupaisha usafirishaji saruji, makaa ya mawe nje

1491
0
SHARE

Na ESTHER MBUSSI -ALIYEKUWA NYASA    

ZIWA Nyasa ni moja ya maziwa makubwa Afrika Mashariki na la tatu kwa ukubwa baada ya Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.

Ziwa Nyasa liko mkoani Ruvuma na limepakana na nchi za Malawi na Msumbiji na kwa Tanzania liko katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma.

Kama ilivyo kwa maziwa mengine makuu ya Victoria na Tanganyika, ambayo yamerahisisha usafiri wa majini kwa kuwa bandari zenye meli zinazohudumia abiria na kupakia shehena mbalimbali, Ziwa Nyasa pia linazo bandari zake.

Bandari hizo zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ziko 15 ambazo kwa namna moja au nyingine zimesaidia wakazi wa maeneo hayo na nchi jirani.

Bandari hizo ni Itungi, Kiwira na Matema zilizopo mkoani Mbeya, Lupingu, Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde na Manda mkoani Njombe, na Bandari za Ndumbi, Lundu, Nkili, Njambe, Liuli na Mbamba Bay za mkoani Ruvuma.

Makao Makuu ya Bandari zote za Ziwa Nyasa yako katika Bandari ya Kyela (Bandari ya Itungi) mkoani Mbeya ambapo Meneja wa bandari hiyo ambaye pia ni Msimamizi wa bandari zote, Abeid Gallus anasema licha ya kusafirisha abiria katika bandari hizo lakini shehena kuu ambayo husafirishwa ni makaa ya mawe.

MAKAA YA MAWE NI NINI?

Makaa ya mawe ni aina mojawapo ya madini na chanzo kikuu cha nishati ya umeme ambayo huchimbwa kwenye miamba.

Miamba hii ilitokea kutokana na mabaki ya mimea ya kale iliyogeuzwa kuwa aina ya mwamba katika mchakato unaochukua mamilioni ya miaka.

Madini haya yanapatikana katika mikoa ya Ruvuma, Songwe na Njombe.

Mkoani Ruvuma, madini hayo yanachimbwa wilayani Mbinga na Nyasa.

BANDARI YA KIWIRA

Akizungumzia umuhimu wa biashara hiyo katika kupaisha uchumi wa bandari za Ziwa Nyasa, Gallus anasema biashara ya usafirishaji shehena ya makaa ya mawe inatarajiwa kushamiri zaidi kuliko wakati wowote baada ya kukamilika kwa Bandari za Kiwira mkoani Mbeya na Ndumbi iliyoko wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma.

Anasema ujenzi huo unaoenda sambamba na ujenzi wa Meli mbili za mizigo za MV Ruvuma na MV Njombe zenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kwa wakati mmoja kila moja.

Gallus anasema licha ya kurahisisha usafiri wa mizigo katika ziwa hilo pia utachangia kuongeza shehena inayohudumiwa katika bandari za ziwa hilo.

“Lengo la mradi huo ni kupanua eneo la kuhifadhi shehena hususani makaa ya mawe ambayo yatakuwa yakisafirishwa kwa wingi hadi Bandari ya Kiwira na kuchukuliwa na malori kwa ajili ya kusambazwa kwa wateja.

“Shehena kuu katika Bandari za Ziwa Nyasa ni makaa ya mawe ambayo hupitia katika Bandari ya Ndumbi iliyoko wilayani Nyasa hadi Kiwira na baadaye kusafirishwa na malori katika viwanda vilivyopo Mbeya.

“Aidha shehena ya makaa ya mawe pia husafirishwa kwenda katika bandari zilizopo nchi jirani ya Malawi kwa ajili ya matumizi katika viwanda nchini humo lakini pia shehena nyingine zinazopita katika Bandari za Ziwa Nyasa ni saruji, mabati, dagaa na mizigo mchanganyiko,” anaeleza.

Anasema Bandari ya Kiwira ni lango kuu la usafirishaji mizigo katika Ziwa Nyasa ambapo asilimia 90 ya shehena zinazohudumiwa na mamlaka hupitia hapo.

“Bandari ya Kiwira ndiyo bandari muhimu katika upitishaji wa makaa ya mawe kutoka katika Wilaya ya Nyasa na Mbinga zilizopo mkoani Ruvuma.

“Pia bandari hii inatumika kuhudumia mizigo mchanganyiko inayosafirishwa kwa njia ya maji katika ukanda wote wa Ziwa Nyasa,” anasema Gallus.

Anasema kwa kuzingatia umuhimu wa bandari hiyo, serikali inatekeleza miradi miwili muhimu ya upanuzi wa bandari hiyo ili kuboresha ufanisi.

Anaitaja moja ya mradi kuwa ni ujenzi wa skafu ngumu unaogharimu Sh bilioni 2.45 zinazotokana na mapato ya ndani ya TPA ambao ni mradi wa miezi tisa na unatarajia kukamilika Septemba mwaka huu.

Anasema lengo kuu la mradi huo ni kupanua eneo la kuhifadhi shehena hususani makaa ya mawe.

Meneja huyo pia anaeleza kuwa licha ya kutoa huduma ndani ya nchi, Bandari za Ziwa Nyasa upande wa Tanzania zinatumika kusafirisha shehena na abiria kwenda katika nchi jirani kupitia Bandari Kuu za Nkhata bay, Monkey bay, Chipoka na Karonga zilizopo nchini Malawi na Bandari ya Metangula iliyopo nchini Msumbiji.

Naye Mhandisi wa Bandari za Ziwa Nyasa, Khamisi Nyembo, anasema meli hizo zikianza kazi zitafanya safari nne kwa mwezi usafiri ambao utarahisisha usafiri wa makaa ya mawe kutoka Bandari ya Ndumbi hadi Kiwira.

Kwa upande wake mmiliki wa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Liweta, uliopo Kijiji cha Liweta, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Richard Mahundi, anasema changamoto iliyopo katika usafirishaji wa makaa hayo ni miundombinu kwani barabara bado mbovu lakini kwa sasa inaenda kuondolewa na usafiri wa meli hizo.

Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Liweta.

“Kwa sasa tunasafirisha tani 5,000 kwa mwezi lakini meli itaturahisishia kubeba walau tani 2,000 kwa wiki na mteja wetu mkubwa ni Kiwanda cha Saruji Mbeya (Mbeya Cement).

“Pamoja na hayo tunamuomba waziri mwenye dhamana atuangalie kwa jicho la tatu wachimbaji wazawa kwa sababu wazawa bado hatujapewa nafasi kama Rais Magufuli alivyodhamiria kuwainua wachimbaji wadogo wazawa,” anasema Mahundi.

Aidha, anazungumzia meli hizo mbili za mizigo Gallus kuwa zinatarajiwa kupunguza idadi kubwa ya malori yanayopita barabarani kwa kuwa mzigo mwingi utakuwa ukipitishwa kwa njia ya maji na pia itaipunguzia serikali gharama za ukarabati wa mara kwa mara.

Bandari ya Kiwira.

BANDARI YA NDUMBI

Pamoja na mambo mengine, Gallus anasema mamlaka pia inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Ndumbi kwa kuweka gati la kudumu, jengo la ofisi, sakafu ngumu kwa ajili ya kuhifadhia makaa ya mawe na ujenzi wa nyumba ya mtumishi.

“Ujenzi huu utaboresha shughuli za uhudumiaji wa shehena ya makaa ya mawe ambapo wastani wa tani 6,000, zinatarajiwa kuhudumiwa kwa mwezi sawa na makusanyo ya Sh milioni 300 kwa mwezi.

“Lakini pia mamlaka imedhamiria kufungua ushoroba wa Mtwara kupitia bandari ya Mbamba Bay ambapo tayari imeshaweka miundombinu ya barabara hadi Mbinga na inatarajiwa hadi kufikia mwaka 2020 kipande cha lani cha Km 67 kutoka Mbinga hadi Mbamba Bay kitakuwa kimekamilika,”anasema.

MIRADI YA MELI

Pamoja na mambo mengine, Ziwa Nyasa gallus anazungumzia mradi wa meli za abiria ya MV Mbeya II, itakayofanya safari zake katika Ziwa Nyasa unaotarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu kuwa utarahisisha usafiri wa abiria waliokuwa wakitumia mashua.

Anasema meli hiyo iliyogharimu Sh bilioni 9.1, ina uwezo wa kupakia mizigo tani 200 na abiria 200 kwa wakati mmoja, inatarajiwa kuwaondolea changamoto ya usafiri abiria wanaoishi katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na Ziwa Nyasa kwa ujumla.

Gallus anasema kukamilika kwa meli hiyo ya abiria itaenda kuondoa adha ya usafiri ziwani kwa sababu kwa sasa hakuna chombo chochote cha kuaminika kinachofanya kazi ziwani.

“Watu wengi wamekuwa wakitumia maboti au mashua lakini hakuna chombo madhubuti kinachofanya kazi ziwani, kwa hiyo ujio wa meli ya MV Mbeya II unaenda kuondoa changamoto hiyo ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na ziwa hili ni hatari kidogo kwani lina mawimbi makubwa kwa hiyo inaenda kumarisha usalama wa mizigo na abiria wanaokwenda sehemu mbalimbali,” anasema.

Anasema ujenzi wa meli hiyo ulianza Julai mwaka 2017, chini ya Kampuni ya Songoro Marine na umefikia zaidi ya asilimia 82kwa hatua ya kufunga mitambo, kuweka vyumba, kufunga viti na umaliziaji.

Kwa upande mwingine anazungumzia meli zilizopo katika ziwa hilo kwa ujumla kuwa hivi sasa lina meli tatu zikiwamo mbili za mizigo moja ya abiria.

Anazitaja meli hizo za mizigo kuwani MV Njombe na MV Ruvuma ambayo kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1,000 na tayari zimeshakamilika na zimeanza kufanya kazi tangu Julai mwaka 2017 kwa ukanda wa Ziwa Nyasa na MV Mbeya II ya abiria.

“Hadi hivi sasa meli hizo zimeshafanya safari saba zikiwamo nne za majaribio na tatu za kibiashara ambazo inaendelea nazo,” anasema Gallus.

Aidha, anasema mradi mzima wa meli hizo na miundombinu mingine inayoendelea katika bandari mbalimbali za Ziwa Nyasa hususani Itungi na Kiwira, itazifanya Ziwa Nyasa kuanza kujitegemea kiuchumi tofauti na sasa ambapo inategemea ruzuku kutoka serikalini.

Meli ya MV Mbeya.