Home Habari Barabara ya Tanga-Pangani mateso kwa Naibu waziri

Barabara ya Tanga-Pangani mateso kwa Naibu waziri

3722
0
SHARE

NA OSCAR ASSENGA, PANGANI

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso amesema ujenzi wa barabara ya Tanga –Pangani Saadani umekuwa ukimtesa na hata wakati mwengine kumnyima usingizi kwa kuwa ndio chanzo cha kukwamisha maendeleo katika wilaya ya Pangani.

Aweso ambaye ni Mbunge wa Pangani (CCM) alitoa kauli hiyo hivi karibuni mjini humo katika ziara ya Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigell.

Aweso alisema  barabara hiyo inahitaji ifunguke sawa na ilivyo Bagamoyo ambayo imepiga hatua kubwa za kimaendeleo baada ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami.

Alisema kama fedha zake za mshahara wake zingetosha angezisamehe ili ziweze kutumika kujenga barabara ya Tanga hadi Saadani ili kuondosha kero hiyo kwa wananchi wake na kufungua fursa za kiuchumi.

“Kwa kweli ujenzi wa barabara hii unaniumiza sana ingawa Rais amesema ujenzi wa barabara hiyo utaanza na kuondoa kilio hicho kwa wakazi wa mji wa Pangani “ alisema.

Alisema wakati Rais John Magufuli alipokuja mkoani Tanga alimueleza juu ya changamoto ambazo zimekuwa zikiikabili wilaya hiyo ikiwemo ya barabara ambayo iwapo itajengwa itasaidia kufungua fursa za kiuchumi kwenye mji wa Pangani na mkoa kwa ujumla.

“Katika tukio la kuzima Mwenge wa Uhuru, naomba tujipange agenda yetu iwe ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani hadi Saadani kwani mafanikio ya Pangani ni mengi ikiwamo viwanda maeneo mengine,” alisema.

Hata hivyo, alisema amewapigia magoti mawaziri wengi lakini mpaka sasa bado ujenzi huo haujafanyika jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya wilaya hiyo kongwe nchini.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigella aliwaahidi wananchi wilayani Pangani kuwa atamshawishi Rais Magufuli kupitia barabara ya Dar es Salaam-Bagamoyo-Saadan-Pangani hadi Jijini Tanga wakati wa kilele cha mbio za Mwenge ili ajionee kero wanayoipata wananchi juu miundombinu hiyo.

Rais Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha mbio za Mwenge mwaka huu Jijini Tanga Oktoba 14.

Shigella alisema hakuna njia mbadala ya kuisaidia Wilaya hiyo ya Pangani na vitongoji vyake bila ya ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo imekuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi hao.

“Lazima nikiri hali mbaya ya barabara hiyo lakini pia ili tuweze kuikomboa Wilaya hii lazima tuhakikishe ujenzi wake unaanza na niwaeleze ukweli hatua za mradi wa barabara hii ziko katika hatua nzuri” alisema Shigella.

Alisema alishafanya jitihada zote ikiwa pamoja na kufika katika mamlaka mbalimbali za Serikali , Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hadi wizara ya fedha ili kuweza kupata majibu sahihi juu ya hatma ya mradi wa barabara hiyo na matokeao yake yako mazuri.

Hata hivyo, aliwaomba wananchi hao kuwa na uvumilivu kwa kuwa mchakato wake upo tayari kwani Oktoba mwaka huu zabuni ya  kuwatafuta wakandarasi wa mradi huo zitatangazwa rasmi ili mradi uanze.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Pangani Mashariki, Akida Boramimi (CUF) alisema ahadi zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali kuhusiana na ujenzi wa barabara hiyo huwa hazitekelezeki.

Alisema anapata mashaka juu ya kauli hizo na wananchi wanapaswa kuamini kuwa ahadi zinazotolewa na viongozi hao ni kauli za kiserikali hivyo kutokutekelezwa kwake kunaonyesha ishara mbaya.

“Labda barabara hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuombea kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wananchi wapo watawasikiliza tena kutokana na barabara hii  ambayo imekuwa mtaji kwao,” alisema.