Home Makala BARBRO JOHANSSON: UTITIRI WA KODI UNATUKWAMISHA KUFUFUA NDOTO ZA WASICHANA

BARBRO JOHANSSON: UTITIRI WA KODI UNATUKWAMISHA KUFUFUA NDOTO ZA WASICHANA

1117
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


SHULE ya Sekondari Barbro Johansson Model Girls ni mojawapo ya shule za wasichana zilizopo nchini kwa malengo ya kufufua ndoto na matumaini ya wasichana waliokosa fursa ya kusoma kutokana na ufukara.

Shule hii iliyoanzishwa mwaka 2000 na Hayati Balozi Wilson Tibaijuka pamoja na wadau wengine akiwamo Balozi John Rupia kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), licha ya kuanza katika mazingira magumu ya wakati huo sasa imejitanua na kutahini zaidi ya wanafunzi 600.

Awali shule hiyo iliyopo Kata ya Kwembe, Kibamba jijini Dar es Salaam ilianza na wanafunzi 40 pekee hasa ikizingatiwa miaka ya 1990 wasichana wengi walikuwa hawapatiwi fursa ya kusoma kwa madai kuwa hawana uwezo kiakili jambo hili limekuwa likipingwa sana na wadau wa elimu kwa kubainisha kuwa wasichana hawakupewa mazingira rafiki ya kusoma.

Jambo hilo pia linaungwa mkono na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Halima Kamote, ambaye anabainisha kuwa baada ya mdororo wa elimu miaka hiyo ya 1990 wavulana wengi walipata fursa katika shule za madhehebu ya kidini – ‘kimissionary ‘.
Anasema ingawa walianza kuchukua watoto wa masikini tu, katika mwendelezo ilibidi kuchanganya wanafunzi wa masikini na wa wazazi wenye uwezo ili shule iwe endelevu na hata ufadhili usipokuwapo shule iwe na uwezo wa kujiendesha.

“Shule imekuwa taasisi kubwa tuna walimu 34 na wafanyakazi wasiokuwa walimu 27. Shule inafanya vizuri kwani lengo la kuendelea kusaidia watoto maskini bado tunaendelea nalo, sasa wanafunzi tunaowafadhili wapo asilimia 12.5 ya wanafunzi wote tulionao ingawa ni kiwango cha chini ila idadi imeshuka kutokana na ugumu wa kutafuta fedha za kuwafadhili hawa watoto,” anasema.

Changamoto
Asilimia kubwa ya wazazi wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa za karo za wanafunzi katika shule mbalimbali, dai hili linajibiwa na Mwalimu Kamote kwamba wazazi wanatakiwa kutambua kuwa shule binafsi hazipati ruzuku au msaada wowote kutoka serikali, hivyo gharama zote za uendeshaji zinaangukia kwa wamiliki wa shule hizo.

“Uendeshaji wa shule si rahisi kwa sababu shughuli zote zinatokana na ada wanayolipa wazazi, niseme elimu si kitu rahisi kwamba mtu alipe Sh 20,000 kwa mwaka apewe elimu. Lazima tutambue kuwa mtoto kuingia darasa atahitaji elimu kutoka kwa mwalimu ambaye lazima alipwe mshahara wenye kukidhi maisha.

“Kwa mfano shule hizi za bweni watoto wanakaa zaidi ya siku 276. Inabidi kulishwa, kupatiwa sare za shule, matibabu kila kitu lazima wapewe, kama madaftari, vitabu, hivyo hakuna kitu cha bure. Na tunachozingatia ni mtoto kuelewa kwa kufanya mazoezi kwa vitendo. Sasa vitu vyote hivi vinatengeneza gharama kwa mtoto mmoja, kuanzia kulala, kuamka hadi kupatiwa elimu,” anasema.

Aidha, anasema ada nayo imekuwa mzigo kwa wazazi kwa sababu serikali imeongeza utitiri wa kodi kwa shule binafsi nchini hivyo kuonesha kama vile utoaji wa elimu si huduma tena bali ni biashara.

“Kwa mfano kwenye shule mbali na kodi ambayo ni stahiki za wafanyakazi ambayo ni asilimia 10 ya pensheni, kuna Mfuko wa fidia kwa mfanyakazi ambao tulipa asilimia moja ya mishahara, lakini ikumbukwe kuwa kwenye taasisi nyingi tunalipia bima ya afya ambayo ni asilimia tatu mwajiri na tatu mwajiriwa, kuna kodi ya ardhi ambayo pia imepanda, kuna kodi ya SDL-‘ Skills Development Levy ambayo ni asilimia tano ya mishahara yote unayolipa licha ya kuwa tumekuwa tukiipinga kila mara lakini tumeshindwa ma manispaa wamekuwa wakitudai.

“Kuna Property tax ambayo mwaka 2000 tulianza milioni 1.5, lakini ikapandishwa hadi milioni tano mwaka 2013 ila sasa mwaka huu 2016 wamekuja wanatuambia tulipe milioni 18. Hizi gharama zote zitatoka wapi? zitatoka kwa mzazi anayemlipia mtoto. Hivyo kama mtoa huduma tunaemsaidia serikali kuelimisha umma, bado hatujangaliwa kwa jicho stahili kwenye upande wa kodi.,” anasema.

Anasema kwa kuwa mzazi ni Mtanzania anayelipa kodi asingestahili kutakiwa kulipia gharama kubwa kumsomesha mwanawe lakini kutokana na ubora wa elimu kuwa katika kiwango cha chini wa shule za serikali wengi wanalazimika kuwapeleka shule binafsi kwa kijibana ili mradi watoto wao wapate elimu bora..
“Pia kuna changamoto ya kupata walimu stahiki kwani lazima utafute walimu sahihi… sipendelei sana kutafuta wa Kenya kwa sababu hapa kwetu wapo wanaofaa kwani tunawatengeneza. Licha ya kuwapo kwa uhaba wa walimu wa sayansi kwa upande wetu tumekuwa tukijitahidi na kufanikiwa hata kupata tuzo mbalimbali katika fani hiyo ya sayansi.

Matarajio
Hata hivyo, anaongeza kuwa shule hiyo yenye eneo la hekari zaidi ya 50 sasa ina majengo ya kutosha.
“Lakini pia tumenuia kuongeza idadi ya wanafunzi hivyo kuna bweni jipya limekamilika mwaka huu ambalo litakuwa na nafasi za kutosha za kulala. Pia tumepanga kuongeza darasa mojakwa mwaka kesho  na likikamilika tutaongeza wanafunzi kuanzia 720 hadi 800.

“Pia tumeanza kutahini wanafunzi wapya na wazazi wanaweza kuchukua fomu za kujiunga na shule kwenye tovuti yetu. Lengo letu ni kuwasaidia wasichana nao wapate elimu bora ndio maana hatuwachuji watoto kama shule nyingine ambazo zinachukua wale watoto wenye ufaulu wa juu pekee.

“Tumenuia kumfikisha mtoto katika uwezo wa juu wa kufikiri, si lazima apate daraja kwanza pekee kwa sababu tunaanza kumjenga kimaadili, kimaarifa, kujiamini. Kwa hiyo ukimleta mtoto wako Barbro, hatuchagui wale ambao ni wa daraja la kwanza tu bali tunawajenga waweze kujielezea, kusimamia haki zao na kujitambua,” anasema.