Home Habari Barua yangu ya wazi kwa Rais Magufuli

Barua yangu ya wazi kwa Rais Magufuli

2079
0
SHARE

DEOGRATIAS MUTUNGI

NIANZE andiko hili kwako Rais Dk. John Magufuli kwa kukupa pole na majukumu mazito uliyonayo katika kusimamia maendeleo endelevu ya taifa letu ambayo yanamlenga mwananchi wa kawaida.

Aidha Rais Magufuli nakupongeza kwa kufanikisha kutekeleza miradi midogo kwa mikubwa ya maendeleo kwa asilimia kubwa na hivyo kuwa Rais anayekubalika zaidi katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki na kati.

Pia Rais unakubalika miongoni mwa jamii ya Watanzania kama kiongozi mwenye haiba ya pekee katika kuthubutu na kusimamia falsafa ya watu kufanya kazi kwa misingi ya uchumi wa taifa na kwa kipato chao wao wenyewe.

Ndugu Rais kinachokutambulisha kwa Watanzania ni udhubutu wako wa  uzalendo na usimamizi wa rasilimali za umma. Aidha unatambulika kama kiongozi mwenye misimamo isiyoyumbishwa na siasa za Magharibi zenye harufu ya ukoloni mamboleo.

Najua wapo wanaokubeza lakini kumbuka hata Lee Kuan Yew wa Singapore alibezwa na kubatizwa majina mengi lakini leo Singapore ni taifa tajiri duniani kiuchumi. Joseph Stalin wa Urusi ya zamani (USSR), alibezwa lakini itizame Urusi ya sasa kiuchumi, Mao Zedong wa China alibezwa lakini imulike china ya leo ndio kimbilio la Afrika kuomba misaada, Kwa hiyo kubezwa katika utumishi wa umma ni jambo la kawaida wala halikwepeki hata kidogo.

Hata hivyo umma wa Watanzania wanakufananisha na viongozi nguli wa Afrika waliopigania uhuru wa mataifa yao kwa sababu walipinga unyonyaji, dhuluma na walihubiri utaifa kwanza, Mwalimu Nyerere alifanya hivyo, Nkwame Nkrumah alifanya hivyo, Patrick Lumumba alifanya hivyo, Louis Rwagasole alifanya hivyo, Nnamdi Azikiwe alifanya hivyo na wengineo wengi walifanya hivyo na sasa wewe unafanya hivyo.

Mheshimiwa Rais kwa heshima kubwa nimeamua niandike barua hii kwako ambayo kimantiki inalenga kuwasilisha ujumbe wenye maudhui yenye tija kwa nchi yetu kwa kizazi cha sasa na hapo baadaye. Hata hivyo andiko hili linabeba hitaji muhimu kama sio kiu cha Watanzania walio wengi.

Ndugu Rais, Mwalimu Nyerere kwenye baadhi ya hotuba zake nyingi aliwahi kusema “kiongozi imara na shupavu utamtambua kwa kumuangalia machoni na kwa matendo yake” bila shaka Watanzania wanalitambua hilo kupitia kwako ni kwa jinsi gani unaguswa na kero zinazokwamisha maendeleo ya umma.

Rais Magufuli nakufahamisha kuwa andiko langu hili linajikita katika agenda kuu mbili, mosi ni ombi langu kwako la kukubali kufufua mchakato wa Katiba mpya na pili ni kukubali kutoa mwaliko wa vyama vya upinzani na kufanya mazungumzo nao hapo Ikulu. Nitajenga hoja chanya na maridhawa kwa agenda zote mbili.

Ndugu Rais, nikianza na agenda ya kwanza ya kufufua mchakato wa Katiba mpya, hii ni agenda nyeti na lazima nikiri kabisa kuwa natambua uwepo wa kauli yako uliyoitoa, kuwa unajenga nchi kwanza na huna mpango na agenda hii ya Katiba mpya kwa sasa.

Kwa asilimia kubwa nakubaliana na wewe na nasema wazo lako kamwe halikuwa baya, kweli ulichosema kuhusu kujenga nchi Watanzania tumeona kwa vitendo, nchi umeijenga na umefanikiwa kuleta mabadiliko kwa muda mfupi aidha mapinduzi yaliyofanyika yanaonekana kwa macho na hakuna anayebisha, kupitia dhana ya kujenga nchi utu, nidhamu na uzalendo vimeshika hatamu.

Lakini hoja yangu inasimama ndani ya kauli na matendo yako ya kifalsafa unayoyasimamia kisiasa na kiitikadi,  ndugu Rais Magufuli kama umeweza kufanya mapinduzi na mabadiliko ya kimaendeleo kwa kipindi hiki cha muda mfupi na kufanya Watanzania walio wengi waridhike na kasi yako ya uchapakazi ukiwemo upande wa siasa za  upinzani, ambazo kwa muda mrefu zilijenga hoja mbadala ya kupata kiongozi mwenye udhubutu na mwenye fikra za kuleta mabadiliko ya kweli katika siasa zetu za ndani.

Upinzani ulijenga hoja juu ya ombwe la uongozi madhubuti na usimamizi wa sheria za nje na kulinda rasilimali za taifa, sasa nyakati zimetimia na yote yanatekelezwa, kwa mantiki yake upinzani unakubali kile unachokifanya na kukiishi kama rais wa nchi.

Sasa ndugu Rais swali ni je? Kwanini falsafa zako za kiutendaji na uwajibikaji zisiwe ndani ya Katiba yetu itakayo muongoza kila kiongozi ajaye kutekeleza haya mazuri unayoyasimamia na kuyatekeleza kwa sasa ambayo kimantiki yanalengo la kupanua wigo wa masilahi ya Watanzania wote.

Ndugu Rais umekuwa ukikiri uwepo wa ugumu wa usimamizi wa kile unachokifanya kwa sasa lakini umehimili kwa vishindo vyote, Je ajaye atahimili yawezekana ndio au hapana, hili kukwepa jibu la hapana kwanini tusiweke nadharia hizi kwenye andiko letu la katiba?

Ndugu Rais ni wazi kuwa unachokifanya kwa sasa kwa umma wa Watanzania ni kama zawadi ya kisiasa ambayo ina mafaniko lukuki kwenye maisha yao, hata hivyo ufanisi huu ni matokeo ya mawazo yako binafsi yenye misimamo madhubuti inayopenya kwenye mifumo ya kiserikali na taasisi zake na kuweza kuwa sehemu ya falsafa za uwajibikaji wa mamlaka kwa umma.

Ndugu Rais yote ufanyayo ni ya heri kwetu kama yatadumu kwa viongozi wajao, lakini si ubatili mtupu kama viongozi wanaokuja hapo baadaye hawataweza kuziishi falsafa zako na kwanini mazuri haya yawe ya awamu moja badala ya kuwa endelevu kwa masilahi ya taifa letu.

Ndugu Rais kama ujuavyo binadamu tunapita lakini dunia itabaki milele, je ni kwanini usikubali ombi langu la kutupa Katiba mpya ili historia ikukumbuke kwa alama ya kuruhusu mchakato wa mahitaji ya umma kuwa sehemu ya katiba.

Ndugu Rais tunawakumbuka nguli hawa wa falsafa Plato na Socrates, hususani Plato aliyechapisha kitabu maarufu sana cha Republic takribani karne 4K.K (Kabla ya Kristo), kwa sababu ya falsafa zao kuchapishwa kwenye maandiko, tunazisoma vyuoni na kuziishi, ili tuenzi falsafa zako na kuziishi sisi Watanzania tunaomba Katiba bora itakayosimamia mambo yaliyo bora kwa taifa letu.

Ndugu Rais, kwa sababu hatujui kiongozi ajaye atakuwa na hulka gani katika kusimamia falsafa za uwajibikaji na utendaji uliotukuka, ni rai ya andiko hili kukuomba kurejea upya mchakato wa Katiba yetu itakayoainisha mambo muhimu katika kusimamia rasilimali zetu kama unavyofanya hivi sasa, Rais Magufuli ni vigumu sana kumpata kiongozi mzalendo kama wewe anayeweza kusimamia mambo ya msingi bila kuelekezwa na Katiba ya nchi.

Basi mantiki kama ndio hiyo, Watanzania tunaomba kwa vyovyote vile usituache hivi bila uwepo wa Katiba mpya, ndugu Rais si dhambi kubadilisha kauli yako maana kiu ya Watanzania kwenye mchakato wa Katiba ni kubwa sana.

Ndugu Rais nina imani na wewe kuwa agenda yangu hii ya kwanza utaisoma na kuitafakari kwa kina na kwa kudra za Mwenyezi Mungu utaifanyia kazi, kwa ufupi nawasilisha agenda ya kwanza yenye ombi la Katiba mpya.

Baada ya kufafanua kwa kina umuhimu wa agenda ya kwanza, Ndugu Rais naomba nihamie kwenye agenda ya pili. Agenda hii inasimama katika dhana ya kutoa mwaliko kwa vyama vya upinzani.

Ndugu Rais, natumia andiko hili kukujulisha kinachoendelea mtaani kwa sasa pengine, sisi tunaoishi uswahilini tunaelewa fika kuwa jamii zetu sasa hazifungamani na kuelewana vizuri kwa sababu ya utofauti wa kiitikadi, kuna visasi na visa vya hapa na pale vinavyojengwa na wanasiasa wetu.

Ndugu Rais zipo taarifa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinanyanyasa vyama vya upinzani katika dhana ya demokrasia, chuki imetawala watu wamenuna kwa sababu wanaaminishwa ndivyo sivyo.

Wapo baadhi ya wanasiasa wanafitinisha wananchi juu ya dhana ya ubakaji wa demokrasia nchini, swali langu kwao ni je wanaitambua Katiba yetu ya mwaka 1977, kama jibu ni ndio basi warejee Ibara hii (3)1  Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Kama hivyo ndivyo nongwa za kisiasa zinatoka wapi?

Ndugu Rais, pengine hupati ukweli huu lakini ukweli upo wazi kuwa sasa siasa zetu zinaanza kupandikizwa kirusi cha kubaguana sisi kwa sisi, kwa sababu ya tofauti zetu kiitikadi jambo hili si jema kwa mustakabali wa taifa letu.

Ndugu Rais ninalo ombi ndani ya agenda hii ya pili, ombi langu kwako Rais Magufuli ni kuomba ukutane na vyama vyote vya upinzani kabla ya uchaguzi ujao mwaka 2020.

Ndugu Rais kudhubutu kufanya hivyo ni ushindi tosha dhidi ya wanasiasa uchwara wanaojenga dhana potofu za uchonganishi kulingana na utofauti wa itikadi zetu, kwao ni mtaji kwetu raia ni mauti, kwa mantiki hiyo Rais Magufuli nakuomba pia kwa dhati ulipokee pendekezo langu hili la kukutana na vyama vya upinzani bila shaka wanazo kero zenye mantiki katika uhai wa kulisogeza taifa letu mbele.

Ninaamini wakisikilizwa kwa umakini kama taifa kisiasa tutakuwa tumesaidia kuondoa chuki, visasi na ghiriba za kisiasa ambazo kadiri muda unavyosonga mbele zinakomaa, wahenga wanasema ni bora kuziba ufa kuliko kujenga ukuta.

Ndugu Rais, kwa heshima kubwa nawasilisha andiko hili lenye mfumo wa barua kwako, aidha uandishi wa andiko hili umesukumwa na uzalendo ikiwa pia na mustakabali wa amani na umoja wa taifa letu.

Ndugu Rais, ifahamike kuwa ombi si dhambi ni jambo la heri kabisa, kwa sisi wakristo hutumia maombi kama sehemu ya kuwasiliana na Mungu rejea “Ikawa neno la Bwana likamjia Isaya, kusema enenda ukamwambie Hezekia, mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako.” (ISAYA 38:4).

Mungu ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania

  0717-718619

                                                                                                       dmutungid@yahoo.com