Home Michezo Kimataifa Bayern bado wamkomalia kinda Chelsea

Bayern bado wamkomalia kinda Chelsea

1909
0
SHARE

MUNICH, Ujerumani

BAADA ya Franck Ribery na Arjen Robben kuondoka ndani ya kikosi cha Bayern Munich, wababe hao wa Ujerumani wamemgeukia winga wa Chelsea, Callum Hudson-Odoi.

Mabingwa wa Ligi Kuu Ujermani, Bundesliga, Bayern Munich wamerudi kwa mara nyingi na ofa nono zaidi ya pauni milioni 45 kwa ajili ya kumnasa winga kinda mwenye umri wa miaka 18.

Kwa namna moja au nyingine, vigogo hao wa Ujerumani wanamtazama Odoi kama mrithi sahihi wa mawinga hao walioitumikia Bayern Munich kwa zaidi ya miaka saba.

Odoi mwenye umri wa miaka 18 anafukuziwa vikali na mabingwa hao wa Ujerumani ambao walianza harakati za kusaka saini yake tangu Januari, mwaka huu.

Hiyo ni ofa ya tano inatumwa na Bayern Munich baada ya zingine nne kukataliwa na Chelsea ambao wanaamini winga huyo ataziba nafasi ya Eden Hazard aliyesajiliwa Real Madrid.

Odoi raia wa England alicheza michezo 24 katika michuano yote msimu uliopita na kupelekea kuitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa kinachonolewa na Gareth Southgate.

Hata hivyo, kocha wa Chelsea, Frank Lampard amesema kuwa winga huyo ni chaguo la kwanza katika kikosi chake wala hawezi kumuuza kwa sasa.

“Odoi ni mchezaji mzuri, atatusaidia sana hapo baadae kwa sasa hatuwezi kumuuza, nitaongea naye na naamini ataendelea kuwa hapa,” alisema.

Taarifa kutoka Chelsea zinasema kuwa timu hiyo ipo tayari kumpa jezi namba 10 ambayo ilikuwa ikivaliwa na Hazard.