Home Habari Bernard Membe afunguka

Bernard Membe afunguka

2565
0
SHARE

>>Afanya mahojiano maalum na Rai

MWANDISHI WETU

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya awamu ya nne Bernard Membe amevunja ukimya na kumshangaa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Dk. Bashiru Ally kwa kukalia kimya barua yake ya wito.

Akizungumza na RAI nyumbani kwake mwishoni mwa wiki, Membe alisema: “Nilituhumiwa na Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally kuwa ninaihujumu Serikali ya Awamu ya Tano na kunitaka nifike ofisini kwake kujibu tuhuma baada ya kudai hana namba yangu ya simu.

“Na mimi kwa kumheshimu Katibu wangu wa chama tarehe 7, Desemba mwaka jana nilimpelekea barua kwa dispatch (ushahidi) na kusainiwa nikimuomba kunipangia siku, muda na tarehe ya kufika kwake lakini cha kushangaza ameendelea kukaa kimya.”

Aidha, Mwanadiplomasia huyo amedai kushangaa kusikia kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Humphrey Polepole kuwa mjadala huo umefungwa rasmi.

“Nimemsikia Polepole kupitia Radio Clouds akisema ‘mjadala wa Membe umefungwa rasmi.’ Sasa ninamhoji ni yeye aliyeuanzisha mjadala huo hadi aufunge? Lakini pia kulikuwa kuna mjadala rasmi wa Membe?”

Akizungumza katika kipindi cha ‘Power Breakfast’ cha kituo cha Radio Clouds cha jijini Dar es salaam, Polepole akizungumzia masuala mbalimbali ya chama hicho alipoulizwa sakata la Membe na Bashiru limefikia wapi alijibu kwa msisitizo, “naomba niwaambie Watanzania na wana CCM kuwa mjadala wa Membe umefungwa rasmi.”

Membe aliendelea kusema: “Nilitegemea baada ya Katibu Mkuu kunitaka nifike kwake angefanya hivyo maana hata nilipotaka mtuhumu wangu mkubwa Bwana Mussiba (Cyprian) naye awepo Katibu Mkuu alinitaka nisimuwekee masharti, nikakubali kukutana naye bila huyo Mussiba ili nijibu mapigo.

“Hata hivyo, huyo mtuhumu wangu tayari nimemfungulia kesi Mahakama Kuu nikimtaka athibitishe kauli yake dhidi yangu kupitia gazeti lake la Tanzanite au anilipe sh 10 Bilioni kama fidia ya kunichafua.”

Aliongeza kuwa; “Baada ya tarehe 7 Desemba kumekuwepo na vikao vya juu kama Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na hata Kamati ya Maadili ambavyo vingetumia nafasi hiyo kujadili suala hili ambalo kwangu mimi na wana CCM wenzangu si dogo maana unapomuona simba anakukimbia usidhani uko salama, jaribu kumpa mgongo uone, utajikuta umeraruriwa vipande vipande, na hivyo kama kuniita kumeshindikana kwa nini nisihisi kuna ‘plan B’ na hivyo nichukue tahadhari?”.

Aidha, RAI lilimtafuta Dk. Bashiru ili kuzungumzia iwapo ameipokea barua hiyo na Membe na lini atampangia kumuhitaji, lakini kila alipotafutwa kwa njia ya simu hakupokea wala kujibu ujumbe mfupi.

Hata hivyo, RAI lilifanikiwa kuzungumzia na Polepole ambaye alisema suala hilo kwa upande wake halifahamu wala hajui kama kuna barua yoyote imeletwa na Membe.

Chanzo cha sakata

Siku za karibuni gazeti moja la kila siku liliandika mfululizo machapisho yaliyodai Membe anamhujumu Rais Magufuli asitekeleze majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo huku ikidaiwa Membe anajipanga kugombea nafasi ya Urais mwaka 2020 kupitia Chama Cha Mapinduzi, CCM.

Kufuatia tuhuma hizo, Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally akiwa mkoani Geita alitoa wito kwa Bernard Membe ambaye kwa wakati huo alikuwa nje ya nchi kufika ofisini kwake kujibu tuhuma hizi dhidi yake na kujieleza ni kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu.

Naye Membe kwa haraka kupitia ukurasa wake wa ‘twitter’ alijibu, “inawezekana ni uchanga katika ofisi lakini ninamheshimu Katibu wangu, nitaenda lakini ninataka na Mussiba awepo maana burden of truth (ushahidi) amebeba yeye na hapo ndipo nitajibu mapigo.”

Hata hivyo, siku chache baadaye Katibu Mkuu Ally alisema, “CCM haifanyi kazi kwa mitandao ya kijamii bali kwa vikao lakini pia Membe ni mwanachama wa kawaida wa CCM kama walivyo wengine.”

Akitoa taarifa ya vikao vya Kamati Kuu mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu Bashiru Ally aliulizwa kuhusu sakata la Membe ambapo alijibu, “nimeagizwa kuzungumzia yale tu tuliyojadili, hatukujadili suala la Membe kwa hiyo msiniulize kuhusu Membe.”

Wazee wastaafu walonga

Mbali na Spika Mstaafu wa Bunge Pius Msekwa kujitokeza hadharani kumtetea Membe huku akimkosoa Katibu Mkuu wa CCM kupindisha kanuni na taratibu za chama,

Ukimya wake wamponza

Taarifa kutoka kwa makada mbalimbali wa chama-tawala zinadai ukimya wa Membe na hasa kuacha kujitokeza hadharani kumuunga mkono Rais Magufuli kama ilivyotokea kwa Edward Lowassa, Rostam Aziz, Jakaya Kikwete huenda ndiko kunamuweka katika mtazamo hasi.

“Unajua Mwenyekiti wetu anapambana kufa na kupona kuhakikisha nchi inasonga mbele kimaendeleo sasa angehitaji watu kujitokeza hadharani kumuunga mkono lakini huyu bwana (Membe) toka 2015 baada ya kukatwa jina lake amekaa kimya kana kwamba hayupo sasa hili lazima ikusumbue mwenzio anafikiri nini ukizingatia angepitishwa yeye leo angekuwa ndiye Rais,” anasema Gaston Masele ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa.

Hata hivyo, katika mazungumzo yake na gazeti hili kuhusu ukimya wake, Membe amesema; “ninajua Watanzania wangependa kusikia ninaongea, nitaongea baada ya kukutana na Katibu wangu Mkuu Dk. Bashiru Ally akinipangia siku na saa ya kukutana.”