Home kitaifa Bila CUF uchaguzi utakuwa shakani

Bila CUF uchaguzi utakuwa shakani

3170
0
SHARE

RAI katuni makalaKATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ni miongoni mwa viongozi wachache nchini wenye mioyo ya uvumilivu, ustahimilivu, usikivu na subira iliyovuka mipaka.

Maalim amekuwa akionyesha hali hiyo ya uungwana hata pale anapobaini kwamba mahasimu wake wa kisiasa wanatafuta maridhiano kwa njia za kilaghai kwa nia ya ama kukikwamisha chama chake au mwenyewe binafsi.

Pamoja na kujua ukweli huo lakini kiongozi huyu amekuwa tayari kuzibeba hila na ghiriba za mahasimu wake ikiwamo na chama tawala kwa ukubwa wake nia ni kuhakikisha Zanzibar inabaki salama.

Uvumilivu wa kiongozi huyo umekuwa ukidhihiri kutokana na kuonyesha hekima ya uamuzi kwa kila uchaguzi unaofanyika hata pale chama chake kinapohisi kimechezewa rafu kwa kunyimwa ushindi.

Wakati haya yakiendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatakiwa kukumbuka kwamba wanatakiwa kuzuia matukio yaliyotokea mara baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na kusababisha kufutwa kwa uchaguzi wa majimbo 16 ya Mkoa wa Mjini Magharibi.

Jambo hilo liliwaudhi CUF na kusababisha kuitisha maandamano yaliyotikisa Januari 27, 2001 hali iliyofanya watawala kutumia watu ya 2,000 kuwa wakimbizi, Mombasa Kenya.

Mambo yote haya yalitulia kutokana na busara za Maalim Seif kukubali kukaa meza moja ya muafaka baina yake na watawala na hatimaye kukubali kuitazama Zanzibar yenye amani kwanza na vyama baadaye.

Uamuzi huo hasa ndio uliozaa uchaguzi wa amani wa mwaka 2005 na kusababisha nchi hiyo kuandika historia ya kuwa na serikali ya maridhiano iliyomfanya Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Katika uchaguzi huo Maalim alikubali kumuachia Dk. Ali Mohamed Shein ushindi wake na hakujali kama alishinda kihalali au si halali ila aliheshimu kwa sababu matokeo yalitangazwa na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) iliyo na mamlaka ya kufanya hivyo.

Kama Rais wa Zanzibar, Dk. Shein alikubali hisani ya kuachiwa utawala kwa kupitia ZEC kwanini hivi sasa asitumie uungwana huo wa hata chembe ili kutoa haki kwa mwenzake kwa kutumia matokeo halali yaliyokuwa yamebaki kutangazwa?.

Pamoja na wengi kuamini kwamba mtu pekee mwenye uwezo wa kumaliza mgogoro wa Zanzibar ni Rais John Magufuli kwangu ni tofauti kwani naamini mwenye dhamana hiyo ni Dk. Shein ambaye ndiye anayekubali kuona suala la kulazimisha linafanyika kwake na mwenyewe kulinyamazia.

Si Dk. Magufuli aliye na mamlaka ya kutatua mvutano wa kisiasa nchini Zanzibar bali mwenye uwezo huo ni Dk Shein ambaye anaweza kuiruhusu Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.

Shein anaouwezo wa kuwataka ZEC kutangaza mshindi halali pasipo kwenda kwenye uchaguzi wa marudio wa Machi 20 kama ilivyofanyika kwa kufutwa kwa uchaguzi ule ambao ulikuwa halali na wenye amani kwa mujibu wa waangalizi wa ndani na Kimataifa.

Dk. Shein ndiye mwenye maamuzi ya kuamua hatima ya Zanzibar kama iwe na amani au vurugu kwa kung’ang’aniza kurejewa kwa uchaguzi ambao haukuwa na sababu zilizokuwa na tija za kufanya hivyo.

Hali ya CUF kukataa kuingia kwenye uchaguzi wa marudio na kusisitiza kutangazwa kwa matokeo ya majimbo tisa yaliyokuwa yamebaki inaonyesha hali mbaya kwa Zanzibar ijayo.

Ni hatari sana iwapo uchaguzi huo utalazimishwa kufanyika huku wanachama na wapenzi wa CUF hawajakubalina na adhima hiyo ambayo kwa wapenda amani na tunaotazama mambo kwa mapana yake tunaona demokrasia imechezewa.

Inapotokea nchi inayojipambanua kufuata misingi ya demokrasia ikifinya na kubaka demokrasia katika masuala makubwa kama haya nia yake inakuwa ni kutafuta vurugu.

Maalim amekuwa mpole kupita kiasi kwani pamoja na kushuhudia Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha akifuta uchaguzi kwa sababu ambazo zimetia shaka na kutoa maswali kwa watu wanaofikiri sawasawa basi niridhike kusema nia ya wahusika haikuwa nzuri.

Kwa mvutano huo pekee umesababishia Tanzania kukosa msaada wa Dola za Marekani milioni 472.8 uliokuwa utolewe na Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Marekani.

Kukosekana kwa fedha hizo zimewasababisha Watanzania wapya wanaofikia 300,000 kukosa kuunganishwa kupata umeme.

Sitaki kuamini CCM ambayo imekuwa ikijipambanua kama muumini wa kujali utu leo imekubali kuona wakikosa fedha hizo zote za maendeleo ya watu wake kwa kuona bora wakae giza kuliko CCM kuondoka madarakani.

CCM hiyo hiyo imeona bora kutokea mivutano ambayo mara nyingi mwisho wake huwa mbaya kuliko kuruhusu wapinzani kuingia Ikulu.

Hadi sasa hakuna njia ambayo Maalim Seif na CUF haikutumia katika kuhakikisha inapatikana suluhu ya mvutano wa kisiasa unaoendelea Zanzibar.

Pamoja na kwamba Maalim amekuwa na imani ya rais Magufuli ambaye kwangu sina imani naye katika mvutano huo wa kisiasa unaoendelea kwa sababu hata mwenyewe naye pia ni miongoni mwa ‘wale wale’ (CCM) na hajaonyesha dalili za kupinga kinachoendelea cha maandalizi ya kurudiwa uchaguzi.

Jambo ambalo naamini limebaki kwa Maalim Seif ni kutangaza maandamano ambayo ni haki ya Mtanzania kikatiba ikiwa ni njia ya kujielezea na kulitaka jeshi hilo, kujiandaa kuyalinda kwa sababu ni jukumu lao.

Kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 ibara ya 18 (a), kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake pia kwenye Ibara ya 20 (1) inasema “kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine”.

Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2002 Ibara ya 11 inatambua maandamano na mikusanyiko kama sehemu ya shughuli za vyama vya siasa.

SHARE
Previous articleKIBONZO:
Next article‘Hata Bunge letu ni jipu’