Home Makala Kimataifa ‘BINTI’ WA MUGABE KUGOMBEA URAIS ZIMBABWE

‘BINTI’ WA MUGABE KUGOMBEA URAIS ZIMBABWE

1745
0
SHARE
Rais Robert Mugabe na Joice Mujuru katika picha ya pamoja ya furaha zama hizo

HARARE, ZIMBABWE

Makamu wa Rais wa zamani wa Zimbabwe Joice Mujuru alikuwa swahiba mkubwa sana wa kisiasa wa Rais Robert Mugabe. Alikuwa mstari wa mbele kabisa kumtetea rais huyo na sera zake.

Mujuru mwenye umri wa miaka 61 alipandishwa wadhifa kutoka uwaziri hadi kuwa Makamu wa Rais mwaka 2004. Alikuwa mtetezi mkubwa wa Mugabe wakati uchumi wa nchi hiyo ulipokuwa unadidimia, na amekuwa akimuunga mkono na kumfanyia kampeni kali katika chaguzi tatu, chaguzi ambazo wapinzani nchini humo na watazamaji wa kimataifa walisema hazikuwa huru na haki.

Mwaka 2007 Mujuru aliwahi kuliambia gazeti la Telegraph la Uingereza kwamba kwa namna walivyokuwa karibu na Mugabe, alikuwa anajihisi kama ‘binti’ yake tu.

Lakini miaka mitatu baada ya kujiondoa kutoka chama tawala cha Mugabe (ZANU-PF) kutokana na madai kwamba alikuwa anapanga njama za kumuua Mugabe, mawasiliano kati yake na rais huyo yakatoweka kabisa.

Anasema tangu ajitoe kutoka chama hicho mwaka 2014, hajapigiwa simu na Mugabe, naye pia hajampigia simu – yaani hawajaongea kabisa.

Akiwa London wiki iliyopita akihamasisha Wazimbabwe walioko nje ya nchi kumtosa Mugabe, Mujuru aliliambia jarida la Newsweek kwamba hana mawasiliano na Mugabe kabisa na kwamba hajutii uamuzi wake wa kujiondoa ZANU-PF kwani aligundua kuwa Mugabe alikuwa anataka kumtumia tu kisiasa.

Mwaka jana 2016 alianzisha chama chake cha siasa – National People’s Party (NPP) – ingawa wapinzani wenzie wana shaka naye hasa kutokana na baadhi ya kauli zake za kusifia sera fulani za Mugabe.

Aidha katika mkutano mmoja mkubwa uliojumuisha vyama vya upinzani mjini Harare mwezi uliopita Mujuru hakuwapo jukwaani ingawa wafuasi wake wengi walikuwepo – kitu ambacho kilianzisha minon’gono.

Hata hivyo wachunguzi wa mambo wanasema uswahiba wa muda mrefu wa kisiasa uliokuwapo baina yake na Mugabe umemsaidia Mujuru kwa kumemjenga hadi kuwa mwanasiasa mashuhuri zaidi nchini Zimbabwe.

Lakini sasa hivi Mujuru anavyojitayarisha kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2018, uchaguzi ambao wengi wanaona utatoa fursa ya mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini humo, mwanamama huyo anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwaaminisha wananchi wake kwamba anaweza kuwaletea hali tofauti ya ile iliyopo chini ya ‘mlezi’ wake wa zamani – Mugabe.

Anasema katika uchaguzi ujao Wazimbabwe wataona uzoefu wake katika serikali ya Mugabe kama ni turufu ya kisiasa na siyo doa katika hadhi yake.

Anasema: “Wazimbabwe wamekuwa wananifahamu kwa muda mrefu, tangu nilipokuwa waziri mwenye umri mdogo, na wanafahamu vizuri jinsi nilivyokuwa natimiza wajibu wangu.”

Na sasa hivi Zimbabwe inakabiliwa na matatizo makubwa ya uchumi kwani haujatulia sawasawa baada ya mfumuko wa bei na kuanguka thamani ya sarafu yake (Dola ya Zimbabwe) mwaka 2008/2009. Wakati ule sarafu hiyo ilikuwa inaanguka thamani kwa asilimia bilioni 80 kila mwezi na mkate mmoja uligharimu Dola za Zimbabwe milioni 10.

Sasa hivi asilimia 63 ya Wazimbabwe wako chini ya mstari wa umasikini na robo ya wananchi wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame.

Wachumi wengi wanasema nyingi ya changamoto hizo zinatokana na sera mbovu za kiuchumi za kiongozi huyo. Kati ya 2000 na 2008, Pato la Taifa (GDP) la Zimbabwe’s lilianguka kwa asilimia 50 kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia.

Kutokana na hali hii wananchi wengi wameanza kujihamasisha kwa mabadiliko kwa idadi ambayo haikuwahi kuonekana huko nyuma. Milolongo ya mavuguvugu yanayompinga Mugabe yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.

Maandamano makubwa yalihamasishwa kupitia mitandao ya jamii na Evan Mawarire (40) – kasisi mmoja wa Harare ambaye daima huvaa nguo za bendera ya nchi hiyo. Naye amesema atagombea urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Wakati huo huo mwanasiasa mkongwe nchini humo Morgam Tsvangirai amekuwa akifanya ziara katika maeneo ya vijijini akimtaka Mugabe aachie madaraka na afanye marekebisho makubwa katika sheria za uchaguzi.

Hata hivyo wachunguzi wa mambo wanaona bila ya umoja katika upinzani itakuwa vigumu sana kuuondoa utawala wa ZANU-PF.