Home Makala BOMBA LA MAFUTA KULETA FURSA MPYA YA BIASHARA AFRIKA MASHARIKI?

BOMBA LA MAFUTA KULETA FURSA MPYA YA BIASHARA AFRIKA MASHARIKI?

755
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU,

MOJA ya mikoa ambayo imedorola kiuchumi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ni mkoa wa Tanga. Hali hiyo imechangiwa na kufa kwa viwanda vingi vilivyokuwa vikichagiza maendeleo ya mkoa huo katika awamu ya kwanza na ya pili za kiutawala nchini.

Hali ilikuja kuwa mbaya mkoani humo baada ya kukaribishwa rasmi kwa sera ya ubinafsishaji ambayo ilisababisha viwanda vingi kukabidhiwa kwa watu binafsi ambao nao waliviua.

Hatua hiyo ilisababisha kasi ya ukuaji wa mji wa Tanga kudumaa hali iliyouacha mkoa huo ukiwa umepauka kwa muda mrefu sasa.

Kumekuwa na jitahada mbalimbali za kufufua viwanda mkoani humo, hata hivyo bado mwendo umekuwa ni wa kusuasua.

Jambo la kupendeza machoni pa wengi ni ushirikiano jadidi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na ujio wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga,  Tanzania.

Hii ni fursa kubwa ya kimaendeleo kwa mkoa wa Tanga na nchi kwa ujumla.

Ujio wa bomba hilo pamoja na harakati za kurejesha Tanzania ya viwanda, ni wazi vitaamsha vuguvugu jipya la maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na mkoa wa Tanga kwa ujumla wake.

Mradi huo ni muhimu sana kwa nchi na mkoa wa Tanga kwani hata Kenya kwa kuzingatia umuhimu wa mradi huo nao walikuwa mstari wa mbele kuuwinda.

Afisa wa masuala ya sheria kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Goodluck Shirima, alieleza kuwa mpango wao wa kuhakikisha mradi wa bomba la mafuta unatatekelezwa kwa uharaka ili ukamilike kabla ya mwaka 2020.

Anasema mradi huu utaendeshwa na kampuni maalumu ya kuendesha mradi ambayo Tanzania kupitia TPDC itakuwa na umiliki wa hadi asilimia 10 katika shughuli mbalimbali.

“Hatua mbalimbali za kuwezesha mradi zimeanza ikiwa pamoja na kutoa elimu kwa mwekezaji juu ya utwaaji wa ardhi na tathmini ya athari za mradi kwa mazingira, pamoja na mafunzo kuhusu mikataba inayotarajiwa kuingiwa.

“Majadiliano ya mkataba wa usimamizi wa mradi baina ya serikali ya Tanzania na Uganda yanaendelea, kazi za awali zinaendelea ikiwamo uwekaji wa alama katika njia litakapopita bomba inaendelea kufanyika.

“Kwa asilimia kubwa bomba litapita mbali na makazi ya watu na halitasababisha uharibifu wa mazingira wala athari kwa hifadhi na mbuga za wanyama ambalo pia litakwenda sambamba na miundombinu kama barabara na reli,” anasema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella kuwa tayari mkoa huo unaandaa mazingira ya kutekeleza mradi husika ambapo tayari barabara ya kuelekea eneo hilo imekwishachongwa.

“Tunajenga mazingira ya kutekeleza mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi, lakini pia tunao wajibu wa kuboresha Bandari yetu kwa ajili ya utekelezaji huo. Yale tunayoweza kufanya sisi kama Serikali tayari tunaanza wakati tukisubiri Marais na Mawaziri wa nchi husika kusema ni lini ujenzi huu utaanza rasmi. Kwetu ni fursa na tunataka maendeleo.”

Aliyekuwa Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Henry Arika anasema katika maandalizi ya mradi huo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imetenga jumla ya Sh bilioni 9.2 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya bandari hiyo ili kuwezesha mapokezi ya vifaa vya mradi husika.

Anaongeza mbali na kuboresha miundombinu fedha hizo pia zitatumika kuongeza kina cha gati ili kuwezesha Meli kubwa zitakazobeba vifaa vya ujenzi kuweza kutia nanga kwa urahisi.

“TPA inatarajia kupokea wastani wa tani 250,000 za shehena za vifaa kupitia Bandari yetu wakati wa maandalizi na ujenzi wa bomba hilo, hivyo maboresho kwetu ni muhimu sana. Tunajua kazi kubwa iliyo mbele yetu, tunajipanga na tunajiandaa kuhakikisha kwamba mizigo inapita kwa ufanisi na usalama,” anasema Arika.

Anafafanua kuwa, ili kuimarisha usalama na kupanua wigo wa eneo la kuhifadhi mizigo, tayari Mamlaka hiyo imetenga eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 2,600 litakalotumika kwa shughuli za kuhifadhia shehena ya mizigo kabla ya kusafirishwa, ikiwemo pia maandalizi ya ujenzi wa mashine maalum ya ukaguzi (scanner) kwa ajili ya kukagulia mizigo ili kuimarisha usalama.

Hata hivyo, Kaimu Kamishna wa Nishati anayeshughulikia masuala ya Petroli, Wizara ya Nishati na Madini, Mwanamani Kidaya, anaonyesha kufurahishwa na namna Mkoa huo ulivyoanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi husika na hivyo kuwataka wananchi kuwa tayari kuupokea mradi huo ikiwemo kutumia fursa zitakazojitokeza kupitia mradi husika.

Wakati Diwani wa Kata ya Chongoleani ambapo ndio eneo ambalo mradi huo utapita, Mswahili Njama anasema wananchi wa kata hiyo wana usubiri mradi huo na wataunga mkono katika ufanikishaji wake ili kutoa fursa utakelezaji wake ufanyike bila kuathiriwa na chochote ili uweza kufanywa kwa ueledi mkubwa.

“Mimi nisema kuwa wananchi wangu wapo tayari kushirikiana katika uendeshaji wa mradi huo kwani faida yake ni kubwa hasa kwa uchumi wa mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla na hiyo ndio njia pekee inayoweza kurejesha hadhi ya mkoa huu ya miaka ya nyuma “Anasema.

Katika hatua nyengine wananchi wa maeneo mbalimbali jijini Tanga wameelezea kufurahishwa na mradi huo ambao wamesema kuwa utasaidia kurejesha hadhi ya viwanda iliyokuwa nayo mkoa huu lakini pia kufungua fursa za kiuchumi kwao na jamii zinazowazunguka.

Alphonce Mboya ni mfanyabiashara jijini hapa na mkazi wa Msambweni anasema ujio wa mradi huo utasaidia kuongeza thamani ya mkoa wa Tanga ikiwemo mzunguko wa fedha na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa ujumla.

Anasema kuwa kutokana na uwepo wa mradi huo utaiwezesha Tanga kuweza kuwika kiuchumi lakini pia kurudisha ufanisi mkubwa katika Bandari ya Tanga ikiwa ni mkakati wa kuirudishia ufanisi wake kama mwanzoni.

“Unajua bandari yetu ya Tanga inafanya kazi nzuri sana lakini baada ya kufungwa kwa baadhi ya viwanda hali iliyosababisha shehena ya mizigo nayo kushuka hivyo mradi huo utasaidia kuwezesha kuongezeka kwa kasi na hivyo mji wetu kurudisha heshima yake ya miaka ya nyuma “anasema.

Mafanikio yote haya ni Dhahiri yatagusa kundi kubwa la vijana walioko Tanzania. Mkoa wa Tanga pia unapakana na Kenya na kupita kwa bomba hili kutaongeza nguvu ya biashara kwa vijana hawa. Jitihada za kuwaandaa vijana katika mkoa huu ambao pia huzalisha matunda kwa wingi ni muhimu kuanza sasa.

Kama maandalizi yatafanyika mtaji utakaotokana na uwepo wa bomba hili smabamba na shughuli za uchimbaji wake, zitaweza kutanua vipato vya vijana. Vipato hivi ili view endelevu lazima vitanuliwe kwa ama, kuonesha fursa za kibiashara zilizopo nje ya Tanzania ama kuwashirikisha vijana wa kike kwa kiume bila kusahau walemavu kujifunza kutanuka ili kuboresha maisha yao.

Bomba hili ni fursa kwa Tanga na Tanzania na linaweza kuwa mwanzo mzuri wa kuandaa wajasiliamali ambao watakuza mitaji yao na kuifanya kumudu ushindani katika Afrika Mashariki.