Home Makala BOMBA LA MAFUTA TANGA LILIIBUA MVUTANO KATI YA TANZANIA, KENYA

BOMBA LA MAFUTA TANGA LILIIBUA MVUTANO KATI YA TANZANIA, KENYA

900
0
SHARE

NA SUSAN UHINGA, TANGA

TANZANIA imefanikiwa kukamata mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi yanayotoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Mradi huo unaotazamiwa kugharimu kiasi cha Dola za Marekani bilioni 3.55, ni wa aina yake na wenye tija kubwa kwa Tanzania.

Kama nilivyotangulia kusema katika makala ya wiki iliyopita kuwa nia kuu ya kuandika makala hizi zinazohusu ujenzi wa bomba hili ni kuujuza umma wa Watanzania umuhimu na faida kubwa za mradi huu ambao kama wananchi hawatazifahamu, upo uwezekano mkubwa wa kutoa nafasi kwa wananchi wa nchi jirani na hata za mbali kuja kuchangamkia fursa hii adimu na adhimu.

Ukweli ni kwamba idadi kubwa ya Watanzania hasa vijijini wanautazama mradi huu kwa jicho la kawaida, hali inayoweza kuwanyima uwezo wa kuingia kwenye ushindani wa kuzoa fursa zote zitakazojitokeza kwenye mradi huo.

Kwa kulitambua hilo, RAI limeiona haja ya kutumia safu hii kueleza mapambano ya mradi huo, kuchambua na kufafanua tija ya mradi huo kwa kutoa nafasi ya kuzungumza na wataalamu na watu wa kada mbalimbali, lengo likiwa ni kuwajuza na kuwaandaa Watanzania kuchangamkia fursa hiyo.

Wiki hii tutauangazia mradi huo ulivyoteteresha uhusiano wa kirafiki na kindugu kati ya Kenya na Tanzania.

Fukuto la ujio wa mradi huu liliibuka rasmi kipindi cha mwisho cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne iliyokuwa chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Katika kipindi hiki paliibuka mgogoro wa kimasilahi, uliohusisha nchini marafiki Kenya na Tanzania, chanzo kikiwa ni kila moja kuhitaji kunyakua mradi huo.

Kenya ilitaka mradi huo upitie kwenye Bandari yake ya Mombasa, huku Tanzania ikitaka upitie Tanga, hali hiyo iliibua mgogoro wa chini kwa chini na wa wazi, ambao uliilazimisha Serikali ya Uganda nyakati nyingine kukosa maamuzi.

Taarifa zilizotoka Machi 28, 2016 zilibainisha wazi kuwapo kwa mvutano kati ya Tanzania na Kenya.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Prof Justin Ntalikwa, alikiri kuwepo kwa mvutano huo hata hivyo aliwahakikishia Watazania kuwa upo uhakika wa asilimia 98 kwa Tanzania kuuchukua mradi huo.

“Kwanza tuna uzoefu mkubwa katika ujenzi wa haya mabomba, tuna mabomba kama manne hivi ambayo tayari tumeshayajenga, uwepo wa bandari ya kina kirefu iliyopo Tanga ambayo inaweza kuchukua meli mbalimbali ambazo zinakuja kuchukua hayo mafuta, vilevile nchi yetu ina usalama zaidi ikilinganishwa na hao wenzetu tunaoshindana nao.” Hiyo ilikuwa ni kauli ya Prof. Ntalikwa.

Aidha, alichothibitisha kukutana na wafanyabiashara ili kujadili ni jinsi gani wanaweza kuchangia katika kuchukua fursa mbalimbali zitakazojitokeza baada ya kuupata mradi huo.

“Kwenye huo mradi kuna fursa ambazo ni pamoja na kupata tenda mbalimbali katika kazi zitakazojitokeza, ajira zitakazoweza kupatikana kwa ajili ya watu wetu Tanzania na pia kuna kodi mbalimbali zitapatikana kwa kulipwa kupitia huo mradi,” anasema.

Makubaliano ya kujengwa kwa bomba hilo litakalojulikana kama East African Crude Oil Pipeline (EACOP), yaliafikiwa wakati wa mkutano kati ya Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Uganda Yoweri Museveni mapema mwaka jana.

Vikao vya utekelezaji  wa mradi huo unaoanzia Hoima, Kabaale nchini Uganda hadi Chongeleani Tanga nchini Tanzania vilianza kwa wataalamu wa nchi hizi mbili kukutana Julai 4, 2016 kabla ya kikao cha Mawaziri wa nchi husika

Wataalamu waliohudhuria kikao hicho kwa upande wa Tanzania walitoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Kwa upande wa Uganda waliwakilishwa na Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini, wadau wa sekta ya nishati kutoka idara mbalimbali za Serikali na Wawekezaji wa kampuni za Total, CNOOC na Tullow.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, kwa kushirikiana na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhandisi Irene Mukoni, walisaini makubaliano ya kikao kuhusu utekelezaji wa mradi huo mbele ya waandishi wa habari katika kikao kilichofanyika Hoima Uganda,  Julai 5, mwaka jana ambapo walijadili maendeleo ya mpango kazi wa bomba hilo.

Profesa Muhongo ambaye bahati mbaya alikuja kutumbuliwa, lakini mchango wake bado utasalia kwenye kufanikisha mradi huo ambapo anasema kuwa vikao vya Julai 5, mwaka jana vilikuwa vya mafanikio makubwa yakiwemo Kampuni ya CNOOC (China) na TULLOW (UK) kukubali kushiriki kwenye ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1443.

Alisema hapo awali makampuni hayo yalikuwa yakiunga mkono bomba hilo la mafuta kupita Kenya na kueleza kuwa kwa uamuzi huo, timu ya ujenzi wa bomba imekamilika huku bomba hilo likipewa jina EACOP.

Mawaziri hao wawili walifanikiwa kuwaongoza wataalamu wa Tanzania na Uganda katika kikao cha kujadili utekelezaji wa Mradi huo, huku Prof. Muhongo akisema kuwa wakiwa nchini Uganda Julai 6, mwaka jana walitembelea eneo la Ziwa Albert na kujionea visima vilivyochorongwa tayari kwa uzalishaji wa mafuta ghafi (crude oil) ambapo makisio ni uwepo wa mapipa bilioni 6.5 (reserve) na yanayoweza kuchimbwa ni mapipa bilioni 2 (recoverable).

“Bomba hili la mafuta litakuwa na gharama ya Dola za Marekani bilioni 3.55 na litakuwa na urefu wa kilomita  1,443 ambapo litasafirisha mapipa 200,000 kwa siku,” alisema Profesa Muhongo.

Aidha, Profesa Muhongo alisema  Serikali ya Uganda itajenga kiwanda cha kuchakata mafuta hayo katika eneo la Kabaale  na Ujumbe kutoka Tanzania ulitembelea  eneo la ujenzi huo.

Vilevile, alisema Serikali ya Uganda imetoa jumla ya asilimia 40 ya hisa za kiwanda hicho cha kuchakata mafuta kwa Serikali 5 za Afrika Mashariki (kabla ya Sudan Kusini kujiunga),  ambapo Tanzania imetengewa na kukaribishwa kununua asilimia 8 za hisa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 150.4.

Ili kufanikisha ununuaji wa hisa hizo, Profesa Muhongo alitoa wito kwa Serikali na sekta binafsi kushirikiana.