Home Makala BOMU LA AJIRA KUTEGULIWA KWA STADI ZA MAISHA?

BOMU LA AJIRA KUTEGULIWA KWA STADI ZA MAISHA?

910
0
SHARE

NA AMINA OMARI, TANGA

INAAMINIKA kuwa vijana waliokuwa nje ya shule ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari ya kuingia katika vishawishi vya tabia hatarishi kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu  stadi za maisha zenye kuwaongoza katika kufanya maamuzi sahihi.

Inaelezwa wazi kuwa ukosefu wa elimu ya stadi za maisha ndio umechangia  vijana wengi kujiingiza kwenye tabia ya utumiaji wa dawa za kulevya, ngono zembe, biashara za kujiuza pamoja na tabia mbalimbali ambazo ni hatarishi kwa afya zao pamoja na jamii inayowazunguka.

Vilevile ukosefu wa elimu ya stadi ya maisha unachangia vijana wengi kutokuwa wabunifu hali inayowasababishia kushindwa kutumia fursa zilizowazunguka.

Kutokana na hali hiyo wataalamu wa masuala ya kijamii wamebaini kuwa stadi za maisha ni moja ya njia zinazoweza kuleta mabadiliko chanya kwa kijana.

Njia hii uhusisha uwezo wa kujenga tabia njema ili kuepukana na matatizo yaliyopo katika maisha ya kila siku.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kwa takribani miaka miwili wamekuwa wakiendesha  mradi wa elimu ya stadi za maisha kwa vijana walio nje ya shule nchi nzima.

Mradi huo umejikita katika  kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu stadi za maisha ili waweze kuwa wabunifu ili wajiajiri kupitia fursa zinazowazunguka katika maeneo yao.

Hivi karibuni Kanda ya Kaskazini ilipata fursa ya kufikiwa na mafunzo hayo  ili kuwapa vijana elimu na ujuzi wa stadi za kukabiliana na changamoto za kila siku katika maisha yanayowazunguka.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Ulemavu, Erick Shitindi, anasema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, inaonyesha kuwa nguvu kazi ya Taifa ni takribani watu mil 22 na kati yao asilimia 56 ni vijana.

“Kwa kuwa wapo vijana wengi ambao ndio nguvu kazi ya Taifa ambayo haitumiki, ndipo tulipoamua mpango mahususi wa kuhakikisha nguvu kazi hiyo inatumiwa ipasavyo katika kuleta maendeleo ya kiuchumi.

“Licha ya changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa ajira, mimba za utotoni, utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na magonjwa kama VVU bado kundi hilo linahitaji uangalizi wa karibu ikiwemo mipango madhubuti ya kuwaendeleza kiuchumi,” anasema.

Anasema kutokana na nguvu kazi hiyo kutotumika ipasavyo katika shughuli za uzalishaji mali ndipo Serikali ilipoamua kuja na mradi huo ili kuwawezesha kujitambua wenyewe ili kuamua hatima ya maisha yao.

“Mifumo yetu ya elimu kutokuwa na mafunzo ya stadi za maisha imechangia kwa kiasi kikubwa kutoweka mazingira wezeshi kwa vijana kuweza kujitegemea mwenyewe mara baada ya kumaliza masomo,” alibainisha Shitindi.

Anasema kwa kupitia elimu hiyo vijana sasa wataweza kujitambua ikiwemo kubadilika kifikra na kuweza kujipanga kwa ajili  ya kubuni miradi mbalimbali kulingana na fursa zilizopo kwenye maeneo yao ili kujikwamua kiuchumi.

“Ni vizuri tuwe na mafunzo hayo hasa kwa vijana walio nje ya shule ili waweze kupata kitu cha kufanya ikiwemo kuwabadili kifikra badala ya kuishia kukaa vijiweni na kujihusisha kwenye tabia hatarishi,” anasema.

Anasema wawakilishi hao wa vijana watakuwa na jukumu la kuwaunganisha vijana katika maeneo kulingana na stadi zilizoko katika maeneo yao na kuweza kuibua fursa za kiuchumi na kuanza kuwabadilisha fikra ziendane na kasi ya maendeleo.

Hata hivyo, Shitindi anasema kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2014, kiwango cha ukosefu wa ajira kimeshuka hadi kufikia asilimia 10.5 wakati mwaka 2006 kilikuwa asilimia 18.

“Changamoto kubwa iliyokuwepo nchini kwa sasa ni kwamba tuna wasomi wengi lakini hawaendani na uhitaji wa soko la ajira kutokana na  wengi wao kukosa ujuzi stahiki,” anabainisha Shitindi.

“Hivyo Serikali inawawezesha vijana kupata stadi za kazi ili waweze kushindana katika soko la ajira kwa urahisi kwani kupitia elimu hiyo wataweza kubadilisha tabia za vijana na kuwafanya kuwa wachapakazi ili kushindana katika soko la ajira,” anasema Katibu huyo.

Hivyo, anasema kutokana sasa nchi inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda, hivyo kupitia mafunzo hayo vijana katika kanda zao wanaweza kuja na ubunifu wa kuwa na viwanda vidogo vidogo ili kujiwezesha kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, James Kajugusi, anasema kila kijana ana sifa za kujiunga na mafunzo ya stadi za maisha zitakazowawezesha kukataa visingizio kama vile umasikini, maradhi na masuala yanayoshauriwa na marafiki ambayo yanaweza kuwaingiza katika vishawishi.

Kajugusi anasema mafunzo ya stadi za maisha yamelenga kupata waelimishaji wa kitaifa wa stadi za maisha watatu kutoka kila mkoa katika mikoa yote ya Tanzania bara ambao watawafikia waelimishaji rika wa kila mkoa ili kuweza kufikisha elimu waliyoipata kwa vijana wa rika mbalimbali katika mikoa, wilaya, kata, vijiji, vitongoji, mitaa, vijiwe na sehemu rasmi za shughuli za vijana.

Anasema elimu hiyo imegawanyijka  katika makundi matatu ambayo ni stadi za maisha kwa ajili ya kujitambua, kwa ajili ya fikra na kwa ajili ya mahusiano baina ya watu, hivyo kwa pamoja aina hizi huweza kutoa majibu kwa vijana kuwa wao ni nani, wanataka kwenda wapi na watafikaje hapo wanapotaka kwenda.

Anasema ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia vijana wengi, wameweza kutengeneza miongozo na kuisambaza katika ngazi za halmashauri ili kuwafikia walengwa.

Anasema kupitia miongozo hiyo wataweza kuwatambua vijana katika sekta mbalimbali walizokuwepo na kuweza kuwawezesha kielimu, ikiwemo kuwaongeza ubunifu katika kazi zao.

“Licha ya kujua dhana nzima ya stadi za maisha, wataweza kujifunza njia za kufikisha elimu kwa wenzao pamoja na kushirikiana katika kuzitambua fursa zilizopo na kuzitumia,” amesema Kajugusi.

Anasema anaamini kuna fursa nyingi za ajira hususani vijijini na mijini lakini kutokana na vijana wengi kutokuwa na elimu ya stadi ya maisha, wengi wao wameshindwa kuzitambua na kuzitumia ipasavyo.

Hata hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Zena Said, anasema kada ya vijana kwa hapa nchini wamekuwa ni sehemu ya watu ambao kazi yao kubwa ni kulalamika tu badala ya kufanya kazi.

Anasema kwa sababu ya tabia walizonazo za baadhi yao kutopenda kujishughulisha, wanajihisi ni kama sehemu ya watu ambao wametengwa na jamii.

“Bado vijana walio wengi wana mawazo mgando kuwa baada ya kumaliza masomo  ni lazima atajiriwa, hivyo wengi wakiishi kukaa mitaani bila kazi lakini kama wangeweza kujiajiri kwa kutumia elimu waliyonayo wangeweza kujikwamua kiuchumi,” anasema.

Anasema kuja kwa mpango huo anaamini utaweza kumaliza changamoto za ukosefu wa ajira, kwani sasa vijana watawajibika kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo.