Home Makala BOT INAPOSHINDWA KUWA MLEZI WA KWELI WA MABENKI

BOT INAPOSHINDWA KUWA MLEZI WA KWELI WA MABENKI

722
0
SHARE

NA HILAL K. SUED


Karibu katika kila sekta ya umma nchini kuna madudu. Madudu haya yapo kwa sababu mfumo wa utawala uliopo unalazimisha kuwapo. Utawala unashindwa kujifunza kwa sababu watendaji wanajua fika kwamba hakuna chochote kinachoweza kutokea kwao kwa sababu ya kulindana kulikopitiliza.

Chukulia suala la ufisadi kwa mfano. Matukio madogo madogo ya jinai hiyo hayakuwa yanashughuilikiwa ipasavyo na hivyo kuanza kufisha hadhi ya utawala kiasi kwamba hata wale viongozi wa umma wasafu wanaona hakuna tena maana yoyote kwa wao kutii sheria.

Na sababu kubwa ya kufanyika madudu ni kukosekana kwa vyombo huru na imara (regulatory mechanisms) vinavyosimamia sekta na taasisi muhimu – kwani vilivyopo vimekuwa dhaifu mno na vinaokana vinaingiliwa na siasa.

Nimesema karibu kila sekta kuna madudu, hata ile ya shughuli za kibenki – hususan mlezi wake – Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hali ambayo moja kwa moja inaathiri uchumi wa nchi.

Hatimaye wiki iliyopita BoT ilichukua hatua ambayo ilipaswa kuchukua miaka mitatu iliyopita – iliifutia leseni ya biashara Benki ya FBME (Federal Bank of the Middle East) na kuteua Bodi ya Bima ya Amana kuwa mfilisi. Nimesema ‘hatimaye’ kwani madudu ya benki hiyo yalianza kubainika tangu 2014.

BoT yenyewe ina historia mbaya sana hapa nchini. Mwaka 1984 jengo lake lote liliungua moto pamoja na nyaraka muhimu na fedha. Hadi leo hii haikuelezwa sawasawa sababu hasa ya kuungua benki hiyo, ingawa pengine ni rahisi kuhisi ‘uunguaji’ huu ulikuwa ni kwa lengo gani.

Na miaka 20 baadaye BoT ilikumbwa na kashfa nyingine ya gharama za ujenzi wa minara yake pacha, kwamba gharama hizo zilikuzwa sana, kashfa ambayo hatimaye afisa mmoja mwandamizi wa benki hiyo alipatikana na hatia – ya ‘utumiaji vibaya madaraka’ na kufungwa gerezani. Wengi walisema huyu afisa alikuwa ametolewa kafara tu.

Aidha BoT iliwahi kuhusishwa na uanzishwaji wa kampuni moja ya kitapeli – Mwananchi Gold – iliyodaiwa kwamba kazi yake kubwa ilikuwa ni kusafisha dhahabu inayozalishwa hapa nchini na kupelekwa nje. Uchunguzi wa kina haukufanywa kuhusu madai hayo na kampuni hiyo iliyeyuka kimya kimya.

Halafu kukaibuka mlolongo ya ‘uchotwaji’ – au tuseme wa mabilioni ya fedha katika nyakati na mazingira tofauti kutoka BoT kama vile ule uchotwaji uliofanywa na kampuni ya Deep Green Finance. Suala lililotia fora kwa uwingi wa fedha zilizochotwa ni lilie la mabilioni yaliyowekwa BoT na Tanesco katika akaunti ya Escrow, ambapo inadaiwa BoT iliruhusu ‘kuchotwa’ zaidi ya bilioni 300 na mwekezaji mmoja wa nje bila ya utaratibu na uhalali pia.

Katika mwaka wa mwisho wa utawala wa Benjamin Mkapa (2005) aliyekuwa Gavana wa BoT Daudi Ballali (sasa marehemu) aliruhusu wizi mkubwa wa fedha kutoka akaunti yake ya madeni ya nje (EPA), wizi ambao unadaiwa ulikuwa na lengo la kupata fedha kwa ajili ya kampeni za uchaguzi za CCM.

Hata hivyo kuna baadhi watu wengine wakishirikiana na maafisa wengine wa BoT walitumia mwanya huo nao kuiba kivyao. Ni baada ya msukumo mkubwa wa magazeti na vyama vya upinzani ndiyo uliwezesha serikali ya CCM kuchukua hatua dhidi ya wezi, ingawa ilionekana wazi hatua hizo zilikuwa ni kiini macho tu, kwani wahusika wakubwa waliojulikana hawakuguswa.

Na katika hiyo hiyo kashfa ya wizi wa EPA, ilibainika kwamba benki ya wazalendo ya CRDB ndiyo ilitumiwa katika kuhifadhi baadhi ya mabilioni ya wizi baada ya kuchotwa kutoka BoT. BoT haikuchukua hatua yoyote dhidi ya CRDB.

Hali kadhalika BoT haikuchukua hatua dhidi ya benki za Stanbic na Mkombozi ambazo nazo, katika sakata la Escrow, zilitumika kupitisha baadhi ya mabilioni yaliyochotwa na kulipwa kwa waty binafsi, wakiwemo maafisa wa serikali, waziri mmoja mwandamizi, viongozi wa dini na hata majaji wa Mahakama Kuu – malipo yaliyokuwa na viashiria vya milungula.

Utendaji huu wa BoT wa kuburuza miguu au kuacha kabisa kutoa maamuzi ya haraka si kitu kigeni kwa taasisi hiyo muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi, kwani historia inaonyesha hali kama hii ilishatokea huko nyuma.

Mapema mwaka 1994 benki ya Meridien BIAO ambayo ndiyo ilikuwa benki ya kwanza binafsi ya kigeni kuruhusiwa kufungua tawi hapa nchini ilikumbwa na kashfa kubwa ya utapeli wa kutorosha hela za wateja.

Meridien BIAO ilikuwa ina matawi katika nchi kadha za Afrika lakini makao yake yalikuwa katika visiwa vya Bahamas na mmiliki wake alikuwa Andrew Sardanis, mzaliwa wa Cyprus ambaye baadaye alichukuwa uraia wa Zambia.

Benki hiyo ilianza kuporomoka huko Ghana, Gambia na Swaziland ambako wateja walianza kuzungushwazungushwa walipotaka kuchukuwa fedha zao. Hatimaye hali hiyo ikaikumba Zambia, nchi jirani yetu, na hapo ndipo wateja wa Tanzania nao walipoanza kwenda kuchukuwa pesa zao, nao wakaanza kuzungushwa.

Lakini pamoja na hili kuripotiwa katika magazeti hapa nchini, BoT, chini ya Gavana wake wakati huo Dk Idris Rashid, haikushituka kabisa na hata iliweza kufanya ujasiri wa kusambaza taarifa rasmi kwenye vyombo vya habari – tena kwa matangazo ya kulipia, kwamba tawi la Tanzania la benki ya Meridien BIAO lilikuwa imara, wateja wasihofu na hivyo hawakuwa na sababu ya kukimbilia kwenda kuondoa pesa zao. Taarifa hiyo ilitiwa saini na Dr Rashid mwenyewe.

Kumbe ile ilikuwa taarifa ya uongo kabisa kwani hali ilikuwa ni kinyume na kile alichokiandika. Meridien BIAO (Tanzania) ililazimika kufunga milango yake wiki mbili hivi baadaye kwa kukosa pesa za kuwalipa wateja waliokimbilia kwenda kuchukuwa pesa zao. Wateja wengi walipoteza pesa zao.

Tukio la kuporomoka benki hiyo chini ya usimamizi wa Gavana Idris Rashid liliweka historia ya Watanzania kutapeliwa na benki ya kwanza ya kigeni hapa nchini tangu kutaifishwa kwa mabenki ya kigeni katika miaka ya 60.

Kenya na Zambia zilichukuwa hatua dhidi ya maafisa wao walionekana kukiuka taratibu za kibenki na hata baadhi yao kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Huko Kenya maafisa kadha wa Benki Kuu ya nchi hiyo nao walifikishwa mahakamani kwa kusaidia Meridien BIAO kutorosha kwenda nje zaidi ya KSh 450 milioni kutoka katika akaunti za wateja.

Hali kadhalika, kule Zambia maafisa kadha wa Benki Kuu walitiwa mbaroni kuhusiana na kosa kama hilo hilo, kutorosha zaidi ya dola za Kimarekani 90 milioni kwenda nje.

Hapa Tanzania hakuna afisa au mkuu yeyote wa serikali au BoT aliyewajibishwa kutokana na kuanguka kwa Meridien BIAO ingawa inasadikiwa mamilioni ya wateja yalitoroshwa pia.

Hivyo hata katika uzembe huu wa sasa kuhusu FBME, hakuna afisa yeyote wa BoT atakayechukuliwa hatua yoyote na inawezekana mabilioni ya hela yametoroshwa kutoka nchini.

Kama nilivyosema hapo mbele suala la jinai katika sakata la Benki ya FBME liligunduliwa 2014 baada ya kubainika kujiingiza katika shughuli haramu – pamoja na kutakasa fedha (money laundering) na uhamishaji fedha za nchi (illicit money transfer) na hata kuhusika na fedha za magaidi na za kikundi cha Mafia cha huko Italia.

Kwanza kabisa jina la benki hiyo pekee tu linadanganya – kwamba benki hiyo ilionekana kama ni tawi la benki moja kubwa ya Mashariki ya Kati.

Sivyo kabisa – benki hiyo haipo kabisa Mashariki ya Kati, ilianzishwa hapa Tanzania na ndipo yapo makao makuu yake na ina matawi katika kisiwa cha Cyprus hali ambayo inaibua shuku kubwa katika dhamira na utendaji wake.

Isitoshe, hata wamiliki (wanahisa wake wawili) ni ndugu na wote si raia wa Tanzania, hivyo hata uanziswaji wake hapa nchini unatiliwa mashaka kwani ni kinyume na sheria ya uanzishwaji wa mabenki inayosimamiwa na Benki Kuu (BoT) kwamba lazima miongoni mwa wanahisa wawepo ambao ni wazalendo.

Na tusisahau pia kwamba benki hii ya FBME ilirithi mali za benki nyingine mbili ambazo zote zilifungwa na Benki Kuu kutokana na madai ya kukiuka sheria za benki. Benki hizo ni Trust Bank na mrithi wake Delphis Bank.

Hali hii pekee ingeweza kumfanya msimamizi wa mabenki hapa nchini yaani BoT kuitazama benki ya FBME nayo kwa jicho la tatu kwani viashiria vya kufanyika madudu vilikuwapo. BoT ilikuwa usingizini hadi nchi ya nje – Marekani – ndiyo ikamgutusha mlezi huyo kutoka usingizini kwamba benki hiyo imekuwa ikifanya madudu mengi.