Home Makala BUMACO: SERIKALI IWASIKILIZE WAFANYABIASHARA ILI KUOKOA UCHUMI  

BUMACO: SERIKALI IWASIKILIZE WAFANYABIASHARA ILI KUOKOA UCHUMI  

769
0
SHARE

NA SAFINA SARWATT, MOSHI


TANGU Rais John Magufuli aingie madarakani Novemba 5, mwaka 2015, kila sekta imeguswa na mtikisiko wa ujio wa kiongozi huyo kwa namna mbalimbali.

Magufuli ambaye aliingia na gia kubwa ya kukusanya kodi na kuwabana wafanyabiashara wakubwa na wadogo, matokeo yake sasa yameanza kujitokeza baada ya kampuni nyingi kufungwa, huku wafanyabiashara wadogo wakifunga maduka yao katika masoko makubwa kama Kariakoo.

Licha ya Rais Magufuli kudai wanaotikisika na ujio wake kuwa walikuwa wapiga dili, hali sasa imezidi kuwa mbaya kiasi cha baadhi ya wafanyabiashara kumwomba atafakari maamuzi yake vema kabla ya kuchukua hatua ili kuliokoa Taifa.

Mojawapo ya sekta iliyokumbwa na mtikisiko wa Rais Magufuli, ni sekta ya bima ambayo kwa namna moja au nyingine ni mojawapo ya sekta muhimu kwa maendeleo ya binadamu yeyote kwani bima inagusa kila jambo unalofanya.

RAI wiki hii limezungumza na Kampuni ya Bima ya Bumaco ambayo ni miongoni mwa kampuni za wazawa zinazotoa huduma katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Mtwara, Mwanza na Mbeya.

Bumaco ambayo imejizatiti kufanya bishara licha ya kuwepo kwa ushindani wa kibiashara kutokana na wingi wa makampuni ya bima za majanga nchini, moja ya siri kubwa kwake ni uthubutu na ubunifu kulingana na aina ya wateja wake kwa kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuwafikia Watanzania kwa asilimia kubwa.

Clement Kwayu ni Mkurugenzi wa Bumaco Tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro, ambaye katika mazungumzo yake na RAI hivi karibuni, anasema biashara ya bima ya majanga kwa hapa Tanzania bado ina changamoto kubwa ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi kuhusu bima hiyo tofauti na nchi za nje ambazo kila mwananchi ni lazima kutumia huduma hiyo.

Anasema licha ya kampuni hiyo kufanikiwa kuendesha biashara zake nchini Tanzania, bado  elimu inahitajika juu ya bima ya majanga.

“Kwa mfano Bumaco ilianza kama wakala halafu ikawa kama dalali sasa imekuwa kampuni ambayo makao makuu yake yapo jijini Dar es Salaam. Tupo kwa lengo la kuhudumia jamii ya Watanzania kwa kutoa huduma za bima zenye uhakika.

“Uzoefu wetu katika masuala ya bima umeifanya Kampuni ya Bumaco kuwa ya ushindani kwa kutoa huduma  bora kwa Watanzania,” anasema Kwayu.

Anasema ukuaji huu wa kampuni umechangiwa na hali nzuri ya utendaji wa watumishi kufanya kazi kama timu ili kuhakikisha wanawafikia wateja wao na kuwapa huduma za kuridhisha.

“Dira ni  kutoa huduma zenye uhakika kwa Watanzania na kuboresha namna ya utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuongeza idadi ya wateja. Tunaendesha shughuli zetu kwa maadili ya hali ya juu ili kujenga imani kwa wateja wetu,” anasema.

Anasema Serikali inatakiwa kuyapa kipaumbele makampuni ya wazawa na kuwaboreshea mazingira mazuri ya kibiashara.

Kwayu amezitaja aina za bima zinazotolewa na kampuni hiyo kuwa ni bima ya moto, uhandisi, vihatarishi vyote vya wakandarasi, fidia kwa wafanyakazi, bima ya ajali binafsi, bima ya ajali ya kikundi, bima ya umma, bima ya nyumba na mali, bima ya  vioo, bima kubwa ya magari, bima ndogo ya gari, dhamana, dhamana ya uaminifu, bima ya fedha, vihatarishi vyote, vifaa vya kielektroni, bima ya waajiriwa, bima za baharini, fidia ya utaalamu  pamoja na mamlaka ya bima ya mikopo ya vikundi.

Akizungumzia  changamoto, anasema uelewa mdogo wa wananchi  kuhusu bima za majanga ni tatizo.

“Watanzania wengi hawajawa na uelewe juu ya bima ya majanga na hata wale wachache ambao tayari wana uelewa wamekuwa wakikimbilia makampuni ya nje kwa madai kuwa vya nje ndivyo vizuri,” anasema.

“Wengi wanadhani kukata bima ya majanga ni kwa magari tu kwamba kukatia bima mali zao ni kama kupoteza fedha.

“Mfano bima ya majanga ya kilimo, nyumba pamoja na vitu vya ndani, hiyo ni miongoni mwa bima ambayo watu wengi wanaona kuikata ni kupoteza fedha zao,” anasema.

Wingi wa makampuni mengi ya nje pia imekuwa changamoto kubwa, hali inayochangia makampuni mengi ya wazawa kushindwa kukabiliana na ushindani huo kibiashara.

Anasema elimu ya bima ya majanga ilichelewa kuingia nchini, hali ambayo inawapa ugumu kuelewa faida za bima za majanga ambayo ni muhimu sana kwa jamii pale wanapopatwa na majanga ya mvua, ajali na kuunguliwa kwa vitu.

“Kampuni yetu imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa Watanzania juu ya umuhimu wa bima ya majanga wakati tatizo linapotokea, lakini pia inategemea na aina ya bima uliyokata na kuangalia thamani ya vitu,” anasema Kwayu.

Akizungumzia hali ya biashara nchini, anasema hali kwa sasa si nzuri kutokana na mdororo wa kiuchumi na kwamba kuna haja ya Serikali kulitazama hili kwa kukaa na wafanyabiashara ili makapuni yanayolipa kodi yasifungwe.

“Ukitaka kujua hali ya kibiashara si nzuri, angalia bidhaa zinazoingizwa nchini ni chache na kama bidhaa zinaingizwa chache lazima bei itakuwa juu,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo, si wafanyabiashara wote wanaoweza kupambana na hali hiyo, hivyo ni lazima biashara nyingi zitafungwa.

Wafanyabiashara watakuwa na nidhamu ya kuingiza bidhaa kulingana na uhitaji wa soko kwa wakati husika na si kuingiza bidhaa ambayo haipo.

Kikwazo kingine ni utiriri wa kodi za Serikali, Serikali imewekeza zaidi kwenye kodi  kuliko  uzalishaji, hali ambayo ni hatari kwa ukuaji wa biashara.

Anasema Serikali inatakiwa kuangalia zaidi suala ya uzalishaji kuliko kodi ili kukuza makampuni ya ndani yanayofanya biashara.

 

“Kodi katika nchi hii imekuwa ikitumika kama sera bila kuangalia hasara itakayokuja kujitokeza baadaye endapo hali itaendelea hivyo, kwani hata kodi haitakuwepo tena na matokeo yake ni nchi kuwa masikini,” anasema.

“Serikali inatakiwa kuwekeza zaidi katika shughuli za kilimo na ufugaji na si kuwekeza katika ukusanyaji wa kodi tu ambapo wafanyabiashara wakifunga biashara hakutakuwa na mapato.

Akizungumzia Tanzania  ya viwanda, anasema Watanzania wengi bado hawana teknolojia  ya uzalishaji hivyo kutachukua muda kufikia malengo hayo.

“Usipokuwa na tija ya uzalishaji katika nchi yako, hutaweza kukuza uchumi na sera ya uchumi katika nchi bado haijaimarika,” anasema.

Serikali kurudisha fedha zake benki kuu ni kufifisha ukuaji wa uchumi kutokana na benki kuu kazi yake si kufanya biashara, bali ni kusimamia sarafu maamuzi hayo ni kuinyima fursa mabenki ya kibiashara kushindwa kufanya biashara.

Anasema sera hiyo haijakaa vizuri na kwamba kwa kiasi kikubwa imewazuia na kuzibana benki  za biashara kukosa fedha za kukopesha wafanyabiashara wakubwa, hivyo kuchangia  kupungua kwa mzunguko wa fedha na kusababisha mdororo wa kiuchumi.

Anasema benki kuu ina wataalamu  wengi na hana shaka  na utendaji wao ila hana uhakika na maamuzi yanayofanyika.

“Uchumi katika nchi ni kila kitu  na uchumi ukiyumba na maendeleo yanayumba na kwamba ni wakati wa Taifa  kutafakari,” anasema.

Anasema Tanzania haiwezi kupiga hatua katika uchumi wa viwanda endapo Serikali itaendelea na msimamo wake wa kufanya maamuzi bila kusikiliza maoni ya wafanyabishara.