Home Habari BUNGARA: Korosho imetusababishia kufungwa midomo

BUNGARA: Korosho imetusababishia kufungwa midomo

1946
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa wabunge wa mikoa ya Kusini, Seleman Bungara amesema licha ya wabunge hao ‘kufungwa midomo’, wamefurahishwa na maamuzi ya wakulima wa korosho kwa kugoma kuuza zao hilo kwa bei ya dhuluma.

Bungara ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), amesema tangu Bunge la Bajeti lilipomalizika, wabunge hao hawashirikishwi chochote na serikali ikiwamo mikutano ya wadau ambayo hutumika kupanga bei dira ya korosho.

Akizungumza na RAI juzi, Bungara maarufu ‘bwege’ alisema licha ya kutoshirikishwa katika mikutano hiyo, maamuzi waliyochukua wakulima ni ishara tosha kuwa waliandamana kupinga bei dira ya awali ambayo ilipangwa na serikali.

Alisema katika mkutano wa wadau wa korosho ambao ulifanyika mapema mwezi uliopita bila kuwashirikisha wabunge wa mikoa ya Lindi na Mtwara, ulipanga bei dira ya korosho kuwa Sh 1,550 kwa kilogramu moja.

Hata hivyo, alisema Uamuzi aliouchukua Rais Dk.John Magufuli wa kupanga bei mpya dira ya Sh 3,000 kwa kilo moja pia ni ishara tosha kuwa sasa serikali ilijichanganya katika kupanga bei dira.

“Kwanza sisi wabunge wa mikoa ya kusini baada ya Bunge lililomalizika, hatujashirikishwa katika vikao vya wadau wa korosho, wakati miaka yote tulikuwa tunashirikishwa. Kulikuwa na kikao Dar es Salaam, tulipewa barua rasmi lakini ghafla tukaambiwa kikao kimeahirishwa na wabunge hatutatakiwa kushiriki. Barua hizo za wito zilipitia Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Lakini pili wadau wanapokaa vikao, huangalia gharama za msimu kwenye zao la korosho, ndipo wanajua bei dira hii wakulima hawatopata hasara, kwa hiyo Bodi ya Korosho ilikaa na wadau pamoja na Waziri wa Kilimo, wanunuzi, wakulima, vyama vya ushirika  kwa maana ya serikali yote wakapanga kwamba bei dira ni Sh 1,550, lakini baadae ikatokea wafanyabiashara wakanunua kwa zaidi ya Sh 2,700, yaani walinunua juu ya bei dira iliyopangwa na wadau wa korosho.

“Wakulima wakagoma! Kwa hiyo mtu wa kwanza kusifiwa ni mkulima aliyegoma kwa sababu bei dira ilitangazwa muda mrefu serikali ilikuwa inajua walikaa kimya na ilipofikia wakulima wamegoma, ndipo walishtuka na kuamua kuungana nao” alisema.

Alisema kutokana na hatua huyo anawapongeza wakulima kwa kuonesha msimamo.

“Suala la kushuka kwa soko au kupanda kwa soko linaleta ukakasi kwa sababu Rais kuja kutangaza bei dira ni Sh 3000 wakati mwanzo walisema 1,550, hiyo inaonesha kulikuwa na mpango wa kuwadhulumu wakulima na niwapongeze wakulima kwa kuonesha msimamo wao. Tunafurahi wakulima wetu wametuelewa,” alisema.

Aidha, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) alisita kuzungumzia maamuzi yaliyotolewa hivi karibuni na serikali dhidi ya sakata hilo la korosho na kusema kuwa ameshalizungumzia sana suala la Korosho.

“Sitaki kulizungumzia suala la Korosho kwa sababu nimeshalisemea sana ndani na nje ya Bunge,” alisema

Nape ni mmoja wa wabunge kinara waliokuwa wakipinga mabadiliko ya sheria ambayo yalifuta mgawo wa asilimia 65 za ushuru wa korosho inayouzwa nje kwenda Mfuko wa Maendeleo ya Korosho na asilimia zilizobaki kwenda Serikalini.

Aidha, Mbunge Mteule wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CCM), alisema anaunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli kwa kutangaza bei dira kuwa Sh 3000.

Mbunge huyo ambaye awali alikuwa CUF kabla ya kuhamia CCM na kuchaguliwa tena mapema mwezi huu alisema; “pia nimefurahi kuona Rais ameungana na wakulima kukataa bei inayowadhulumu. Amechukua maamuzi sahihi kwa wakati muafaka hivyo ni jambo zuri la kupongezwa.

“Wafanyabiashara walikuwa na mazoea ya kuwadhulumu sana wakulima ndio maana hata msimu huu walitaka kuwadhulu na sasa wameonesha nia,” alisema.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisema Serikali haipaswi kukwepa lawama kwenye suala la uuzaji wa korosho na ni vizuri ikubali kuwa imefanya makosa.

Zitto ambaye alizungumza na vyombo vya habari wiki iliyopita alisema; “Badala ya Serikali kulichukulia zao la korosho kama la kimkakati imekuwa haisikii, haielewi na sasa imeharibu kuku anayetaga mayai ya dhahabu katika nchi yetu,” alisema.

Alisema korosho ndio zao pekee la kuiokoa nchi na kupingana na habari kwamba Serikali imepata wanunuzi wa korosho kutoka Marekani watakaonunua kilo moja kwa Sh5,000.

Zitto alisema taarifa alizonazo kutoka Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na wanunuzi, uzalishaji wa zao hilo utashuka kwa asilimia 40.

“Mnaweza kuona fedha za kigeni tunazoenda kupoteza kwa uamuzi wa Serikali kuchukua fedha zote za export levy (ushuru wa mauzo nje) badala ya kupeleka zinakostahili,” alisema.

Alisema kukwama huko kwa minada ya korosho akihusisha na makosa ya Serikali kutosikiliza wabunge.

Itakumbukuwa kuwa wakati wa Bunge la Bajeti, wabunge walipinga mabadiliko ya sheria ambayo yalifuta mgawo wa asilimia 65 za ushuru wa korosho inayouzwa nje kwenda Mfuko wa Maendeleo ya Korosho na asilimia zilizobaki kwenda Serikalini.

Walisema mgawo huo ulisaidia wakulima kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na pembejeo na kwamba ulianzishwa kwa mapendekezo ya wadau wa korosho, tofauti na mazao mengine yanayouzwa nje.

Hata hivyo, mjadala wa zao hilo, ambalo sasa linalimwa mikoa mbalimbali nchini lakini kitovu kikiwa ni Lindi na Mtwara, ulianza kushika kasi bungeni na hata hoja za wabunge hao hazikuweza kufua dafu kwani sasa Serikali inachukua asilimia 100 ya fedha za ushuru wa zao hilo.

Aidha, baada ya Bunge, Rais John Magufuli alisema katika moja ya mikutano ya hadhara kuwa alipanga kuwatimua uanachama wa CCM wabunge wa mikoa ya Lindi na Mtwara akiwamo Waziri Mkuu, Majaliwa kama sheria hiyo isingepita.

Mgomo wa wakulima

Oktoba 22 mwaka huu ilielezwa kuwa wakulima mkoani Mtwara waligomea mnada wa korosho na kufuatiwa na mgomo kama huo katika minada mingine miwili, kabla ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufanya kikao na wakuu wa mkoa inayolima korosho kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Minada mitatu ya korosho ya Tandahimba na Newala; Masasi na Mtwara; na Ruangwa, Nachingwe na Liwale, ilikwama baada ya wakulima, ambao mwaka jana walijivunia mamilioni ya fedha kutokana na bei safi iliyofikia zaidi ya Sh3,000 kwa kilo, kukataa bei mpya ya chini ambayo ni kati ya Sh1,700 na Sh2,700 kwa kilo.

Aidha, katika kikao cha Serikali na wanunuzi wa zao hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Magufuli aliagiza bei ya korosho itakayonunuliwa kwa wakulima isipungue Sh3,000 na kwamba iwapo wafanyabiashara hao watang’ang’ania bei, Serikali inaweza kununua na kutafuta soko zuri yenyewe.

Pia Rais alitangaza kupunguza baadhi ya tozo zinazoumiza wanunuzi, ikiwa ni pamoja na ushuru wa halmashauri ambao ulikuwa ukitozwa na halmashauri tofauti kwa shehena moja.