Home kitaifa Bunge, CAG wingu zito

Bunge, CAG wingu zito

1189
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA

MVUTANO wa kiutendaji kati ya Bunge na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad unatajwa kuibua wingu zito lenye sura ya kuiingiza nchi kwenye mgogoro wa Kikatiba. RAI linachambua.

Kwa zaidi ya wiki sasa, mjadala mkuu unaorindima kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ni uamuzi wa Bunge kuazimia kutofanya kazi na CAG, huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akieleza kuwa taasisi yake itafanya kazi na ofisi ya CAG, lakini haiko tayari kushirikiana na Prof. Assad.

Ufafanuzi huo wa Spika pamoja na uamuzi wa Bunge, umetajwa kukoleza mjadala kwa hoja kuwa CAG ambaye kwa sasa ni Prof. Assad anatambuliwa na Katiba Ibara ya 143 na 144 na vipengele vyake vyote huku, Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ikiwa haijatajwa hata mara moja kwenye Katiba nzima.

Matakwa hayo ya Kikatiba yanatajwa kuzidisha wingu kwenye azimio la Bunge dhidi ya CAG, kwamba kwa namna yoyote ile haliwezi kukwepa kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi huo wa hesabu za Serikali.

Hata hivyo wingu linatanda zaidi kwenye uamuzi wowote utakaochukuliwa na Bunge juu ya ripoti hiyo ya CAG, kuipokea na kuijadili kutaleta tafsiri kuwa chombo hicho cha kutunga sheria kinakosa msimamo kwenye azimio lake.

Kutoipokea na kukacha kuijadili kutaibua mgogoro wa Kikatiba ambao unaweza kukwamisha nia njema ya Rais Dk. John Magufuli ya kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ikumbukwe kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 143 na Ibara ya 144 na vipengele vyake vyote inamtambua CAG.

Aidha Ibara ya 143(2)(b) na ibara ndogo ya (4) ya Ibara ya 143 zinamuhusisha moja kwa moja CAG na Bunge.

Ibara ndogo ya (2)(b) ya Ibara ya 143 inatamka wazi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na jukumu juu ya mambo yafuatayo: (b) kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na Sheria iliyotungwa na Bunge na ambazo zimetumika, zimetumiwa kwa ajili ya shughuli zilizohusika na matumizi ya fedha hizo na kwamba matumizi hayo yamefanywa kwa kufuata idhini iliyotolewa kuhusu matumizi hayo.

Ibara hii inadhidhirisha wazi kuwa CAG ndio jicho pekee la Bunge katika kusimamia kile ilichokiidhinisha kupitia sheria ilizozitunga, kwa maana kutokufanya nae kazi kunatajwa kuwa sawa na taasisi hiyo ya kutunga sheria kujitia upofu katika kusimamia majukumu yake.

Katika kudhihirisha kuwa CAG ni muhimu kwa Bunge, Ibara ya 143 (4) imemwagiza Rais kuwasilisha ripoti ya CAG kwa Bunge ndani ya siku saba mara baada ya kuanza kwa kikao cha kwanza cha  Bunge.

“Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu  atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii. Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.

“Iwapo Rais hatachukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge, basi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge (au Naibu Spika ikiwa kiti cha Spika ki wazi wakati huo au ikiwa kwa sababu yoyote Spika hawezi kutekeleza shughuli za kazi yake) ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge.” Imeweka wazi Ibaraya ya 143(4).

Wingu lililotanda sasa ni je, Bunge litakuwa na utayari wa kuijadili taarifa ya CAG ambayo vyovyote iwavyo itakuwa imesainiwa na Prof. Assad ambaye tayari amewekewa azimio la kususwa na Bunge huku Spika akisema wako tayari kufanya kazi na ofisi yake!

Wachambuzi wa mambo wanabainisha kuwa uamuzi wa Bunge hauna tija kwa nchi kwa sababu hauwezi kumtenganisha Prof. Assad na ofisi ya CAG, kwa sababu CAG ni Assad na Assad ni CAG, hivyo kumsusa ni kutaka kuliingiza Taifa kwenye mgogoro wa kikatiba ambao haujawahi kutokea.

Aidha wingu zaidi litaibuka pale Bunge litakapoipokea ripoti hiyo na kutoijadili, hatua hiyo itatoa mwanya kwa wananchi kuanza kuijadili na kuichambua kwani itakuwa na baraka za kuwa taarifa kwa jamii (Public notice) kwa wananchi kama alivyopata kusema Prof. Assad Mwenyewe.

Tayari baadhi ya wanasheriana, wasomi na wanasiasa wameeleza kuwa kushindwa kwa namna yoyote kwa Bunge kushughulikia ripoti ya CAG ambayo tayari imeshawasilishwa kwa Rais  kutaibua mgogoro wa Kikatiba.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), ni miongoni mwa watu waliohoji sababu ya kuchelewa kuwasilishwa kwa taarifa ya CAG bungeni.

“Kwa sababu taarifa iliyotolewa na ofisi ya Spika inaonesha kwamba, Machi 28 mwaka huu Rais alipokea ripoti za ukaguzi kutoka kwa CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2018. Na kikao cha kwanza cha Bunge kilianza tarehe mbili mwezi huu, ambapo taarifa alizopokea Rais hazijawasilihswa na Katiba imezungumzia siku saba, haijazungumza siku saba za kazi au zisizo za kazi.

“Naomba mwongozo wako ni kinuni katika orodha ya shughuli za leo (Jumatatu) hakuna ripoti ya CAG kwenye hati zilizowasilishwa mezani. Ni tarehe ngapi hasa Rais atagaaiza wahusika walete ripoti ya CAG bungeni kabla hazijapita siku saba ambazo zimetamkwa kwa mujibu wa Katiba,” alisema Mnyika.

Hoja hiyo ya Mnyika ilijibiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ambaye alisema licha ya Mnyika kuonesha kujua kuitafsiri Katiba na kunukuu vifungu vya sheria, lakini hakwenda mbali zaidi  kusoma sheria nyingine.

“Sheria nyingine ambazo zinaambatana na maagizo hayo ya Kikatiba na kisheria katika kufanya tafsiri ya siku ambazo zimeandikwa katika Katiba na sheria zinazohusika na uwasilishwaji wa ripoti ya CAG na hasa sheria ya tafsiri za sheria na hivyo kuonyesha wazi kuwa Serikali haitaki kuwajibika ama haijawajibika.”

Aidha Mhagama aliomba mwongozo, kwamba linapotokea jambo kama hilo kiti kinapaswa kuwa tayari kutoa tafsiri na sheria hizo zote ili Mnyika asiendelee kulipotosha Bunge na kuiacha Serikali iendelee kujipanga katika utekelezaji wa jambo hilo.

Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge, alimweleza Mnyika kuwa wanaongozwa na orodha ya shughuli za Bunge na kumtaka asome na sheria ya tafsiri.

“Nakusihi kasome sheria ya tafsiri inayoeleza siku na naamini Serikali haijaenda nje ya tafsiri.” alisema Chenge.

TLS YATOA NENO

Akizungumza na RAI Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Rugemeleza Nshala, alisema sakata hilo limetawaliwa na utata, lakini kuna haja ya kutoa nafasi kwa Serikali na Bunge kutimiza wajibu wao.

Alisema kama Rais ataipeleka ripoti ya CAG wakashindwa kuipokea hiyo ni wazi itakuwa changamoto, lakini pia kama Bunge litaipokea na kutoijadili hiyo itakuwa giza zaidi.

“Jambo la kujiuliza ni kwamba baada ya Rais kuipokea kashaipeleka bungeni, kama Rais hajawapa, ni mtihani na kama imefika bungeni na kukaliwa kimya ni mtihani zaiodi. Kwa sababu Katiba imeeleza kuwa CAG anampatia Rais na Rais yeye ndiye anatakiwa aipeleke kule, tusubiri tuone.”

Hata hivyo aliweka wazi kuwa anaamini Bunge litaifanyia kazi ripoti hiyo na kwamba huenda zipo taratibu zinakamilishwa ili ianze kufanyiwa kazi.

Nshala alisema kwa sababu kujadiliwa kwa ripoti ya CAG ni maagizo ya kikatiba isipojadiliwa Bunge linaweza kuvunjwa.

“Siyo kitu kidogo kile jamani. Rais hana mamlaka yoyote juu ya CAG, huwa ana mamlaka ya uteuzi tu basi, CAG ni nafasi nyeti sana kwa hiyo ni bora busara itumike kuweza kumaliza mgogoro huu. Ripoti za CAG siyo kitu cha kupuuzwa.

“Ni kukaribisha mgogoro wa Kikatiba bila ya sababu. Huwezi kuwa unafanya ukaguzi halafu ripoti isipelekwe bungeni, maana yake hapo ni kukiukwa Katiba maana Katiba imeagiza ripoti lazima ipelekwe bungeni, na haijasema kama Bunge halifanyi kazi na CAG isipelekwe, hapana lazima ipelekwe” alisema Nshala.

Nshala alisema kama ripoti ya CAG itashindwa kujadiliwa bungeni mwathirika mkuu ni Mtanzania maana ndiye analipa kodi.

 “Cha maana ni kwamba vyombo vyote hivi Bunge, Serikali lazima wote waheshimu Katiba, kwamba yale mambo ambayo yamewekwa kwenye Katiba yafuatwe bila kujali ni nani. Hayo ni maagizo ya Katiba hata kama mtu huyapendi. Sasa kwa sababu hupendi hilo hata lile la kumchagua Rais nalo limetokana na Katiba huwezi ukachagua hiki na kile ukakiacha, kwenye Katiba inabidi vyote viheshimiwe” alisema Nshala.

Mwanasheria Fatuma Karume, kwa upande wake alisema kuwa suala la CAG kudhibiti na kukagua hesabu za Serikali ni lazima kwa sababu anatumia fedha za wananchi na yeye anakuwa kama mtazamaji kwa kuzikagua na kisha kutoa ripoti kwa Rais ambaye ataiwasilisha bungeni ili ijadiliwe.

Fatuma alisema anadhani wabunge hawakufikiri mpaka mwisho au wanataka kumpa msukumo CAG ajiuzulu, lakini kama atakataa kujiuzulu na wao wakakataa kuijadili ripoti hiyo watakuwa wanavunja Katiba.

“Chini ya Katiba yetu ripoti ya CAG inamaana anamkagua Rais, anakagua namna Rais anaendesha Serikali na anavyotumia fedha za umma. Kwa hiyo kwenye Katiba yetu walioandika Katiba waliona inaweza kufika hadi Rais anakataa kupeleka ile ripoti bungeni, akikataa kuipeleka CAG anaweza kumruka Rais na akaipeleka bungeni yeye mwenyewe.

Kwa upande wake Wakili wa kujitegemea Innocent Mwelewa, alisema licha ya Bunge kusema kuwa wao wako tayari kufanya kazi na ofisi ya CAG na si Profesa Assad changamoto ni kwamba ripoti ya CAG huwa mara nyingi inawasilishwa na CAG mwenyewe siyo msaidizi na kwamba huwasilishwa na msaidizi endapo CAG mwenyewe yuko safari au kunatatizo jingine lolote.

Alisema shida kubwa iliyopo sasa ni kama ripoti hiyo haijawasilishwa bungeni na kwamba cha msingi ni Bunge lipokee hiyo ripoti ya CAG na kuijadili na kwa sababu CAG yeye anachokifanya ni kuonesha  bajeti ya Serikali iliyoipitishwa mwaka uliopita kama imetumika sawasawa au haijatumika sawasawa.

“Kama haijatumika sawasawa wao wanatakiwa kuihoji Serikali kwanini hasa imekuwa hivi, kutokufanya kazi  na CAG ni sawasawa na bajeti zao kuwa wamezitupa kwenye jalala, maana hawatajua imetumikaje kwa hiyo changamoto kubwa iliyopo ndiyo hiyo” alisema Mwelelwa.

Kuhusu mgogoro wa kikatiba unaoweza kujitokeza Mwelelwa alisema ni kwamba CAG anatambulika na Katiba na ana majukumu yake kikatiba huku Bunge nalo linatambulika kikatiba na lina majukumu yake na kwamba vyombo hivyo vyote viwili lazima vitekeleze majukumu yake kwa kufuata Katiba.

“Endapo Bunge litashindwa kuipitia ripoti ya CAG maana yake limeshindwa kutekeleza majukumu yake Kikatiba. Kikatiba ni lazima Bunge lipitie ripoti ya CAG na kuiwajibisha Serikali pale ambapo linadhani haiko sawasawa, sasa ikishindwa kuipitia hiyo ripoti na kuifanyia kazi maana yake Bunge limeshindwa kutimiza majukumu yake Kikatiba.

“Jukumu la Bunge Kikatiba ni kuisimamia Serikali, maana yake linasimamia Serikali kwa niaba ya wananchi, yeyote aliyempigia kura mbunge amempa mamlaka kwamba aisimamie Serikali kwa niaba yake, maana wananchi wanatoa kodi wakishatoa kodi wanataka maendeleo yafanyike.

“Sasa maendeleo haya yatafanyikaje? Yatafanyika kwa kuhakikisha mbunge anaangalia ile kodi ya mwananchi imelipwaje, hiyo kodi ya mwananchi imetumikaje, sasa kama kodi uliyoilipa hujui imetumikaje, kiongozi uliyemteua akasimamie anashindwa kufanya kazi na mwananchi asijue hela yake imetumikaji, tayari mgogoro wa kikatiba unaanza” alisema Mwelelwa.

Mwelelwa alisema CAG atakuwa ametekeleza majukumu yake kwa kuandaa ripoti na kuiwasilisha, lakini mbunge atakuwa ameshindwa kuipitia ile ripoti kwa mujibu wa Katiba.

“Kwa mfano bajeti imepitishwa ni trilioni tano, ikatumika trilioni sita maana yake kwake hayo ni matumizi mabaya kwa sababu hiyo si bajeti ya Serikali na mambo yanakwenda kwa bajeti. Maana yake Bunge litakuwa halijafanya kazi zake kwa mujibu wa Katiba maana yake ni kwamba litakuwa limevunja Katiba” alisema.

Mtaalamu wa masuala ya siasa Dk. Richard Mbunda aliliambia RAI kuwa endapo Bunge halitaijadili kwa namna yoyote ile ripoti ya CAG ni wazi itakuwa imejinyima haki yake ya kimsingi ya kuisimamia serikali katika matumizi ya fedha za umma.

Hata hivyo Dk. Mbunda alisema anadhani kinachofanyika sasa hivi kwa viongozi ni kuongoza nchi kwa utashi wao na si kufuata matakwa ya Katiba.

“Ni mtazamo wangu, nadhani viongozi wanaongoza nchi kwa utashi wao si kwa kufuata Katiba na ndio maana wanafanya maamuzi ambayo yanapingana na Katiba na naamini hata hili linaweza likaisha hivi hivi, watu wakapiga kelele kisha wakaa kimya.

“Namkumbuka sana marehemu Mchungaji Mtikila (Mchungaji Christopher Mtikila) ambaye alikuwa haliachi jambo la kikatiba lipite hivi hivi, alikuwa ni lazima aende mahakamani, lakini simwoni mtu wa namna hiyo, badala yake mambo yatapita bila kuchukuliwa hatu.”

ASSAD: BUSARA ITUMIKE

Akizungumzia hatua ya kususwa na Bunge, Prof. Assad alisema anaamini kama Bunge limefanya uamuzi huo basi lina mamlaka ya kufanya hivyo na ina sababu zake, lakini kimsingi alikwenda kwenye Kamati na alizungumza nao vizuri.

“Mi nafikiri kama limefikia huko basi kuna kila sababu ya yale mazungumzo yetu ya kwenye kamati yawe wazi kwa kila mtu, ili kila mtu ajue nimeulizwa kitu gani na nimejibu kitu gani ili kila Mtanzania aweze kufanya tathmini yake halafu waweze kupima kama hili lilipofikia ni sawa sawa ama si sawa sawa.

“Kwa hiyo rai yangu ni hiyo tu kwamba ile hansard ya kamati ya maadili iwekwe wazi kila mtu aone maswali gani niliyoulizwa na majibu yangu yalikuwa yapi.

“Katiba inanipa mimi majukumu ya kufanya na majukumu yake yanatekelezwa na Bunge, kama Bunge limeamua kutofanya kazi na mimi ni vigumu sana kutofautisha mimi na ofisi kwa sababu Katiba inaitaja ofisi yangu na haiitaji Nation Audit office.

“Kwa hiyo nafikiri ni jambo zito sana hilo, na kama nilivyosema linahitaji tathmini kali ya watu ambao wana maturity kutazama athari zake ni zipi, sasa tukifanya maamuzi ambayo hatujatazama athari zake, linaweza kuwa tatizo kubwa zaidi badala ya kuwa solution.

“Mimi nafikiri tukae chini tutazame, halafu tuone athari ni zipi ili kuepuka matatizo ambayo tunaweza kuyasababisha. Naamini kuna watu wenye busara na wametumia busara zao, wasiwasi wangu ni kwamba huenda likawa tatizo kubwa tofauti na inavyoonekana sasa hivi.

“Technical (kiufundi) tunaweza kuwa na mgogoro wa Kikatiba, kwamba ripoti zimeshawasilishwa kwa Rais na mimi siwakilishi ripoti bungeni.

“Kwa hiyo Rais atawasilisha bungeni ripoti katika siku stahiki na kama Bunge likikataa kuzipokea hilo ni tatizo kubwa zaidi.

“Wasiwasi wangu ni huo na zikiwasilishwa bungeni zinakuwa public documents ninyi mnapata fursa ya kuzungumza, hilo pia linaweza kuwa tatizo, tafsiri ya hatutafanya kazi na CAG ni tafsiri pana sana inatakiwa tuijue vizuri.

Kuhusu kufanya uamuzi mgumu, Assad alisema hana uamuzi wowote zaidi anaomba dua ili watu waongoze vizuri, wafanye maamuzi ambayo yanafaida na nchi hii. “Sina cha kufanya zaidi mimi nina misingi yangu ya Katiba na nitaendelea kuizingatia.”

Wachambuzi wa mambo wanabainisha kuwa ripoti hiyo ya CAG pamoja na sakata lake dhidi ya Bunge inatarajiwa kuendelea kurindima kwa namna yoyote ile wiki hii na huenda ikashika kasi zaidi siku zijazo kama busara haitatumika kushughulikia suala hilo.

Hata hivyo mapendekezo yametolewa kwa viongozi wote kuitekeleza kwa vitendo Ibara ya 9 (b) inayoelekeza kulinda na kutekeleza sheria za nchi.