Home Makala BUNGE KUMUONDOLEA MUSEVEN KIKWAZO CHA UMRI

BUNGE KUMUONDOLEA MUSEVEN KIKWAZO CHA UMRI

1115
0
SHARE

KAMPALA, UGANDA


Februari 20, mwaka huu, Yoweri Kaguta Museveni alitangazwa kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha kuwania urais kwa mara ya tano mfululizo.

Hata hivyo, iwapo Museveni ataendelea kukaa madarakani baada ya uchaguzi ujao utakaofanyika mwaka 2021, itabidi aruke kiunzi kimoja cha kikatiba.

Kifungu cha 102(b) cha Katiba ya Uganda ya mwaka 1995, kinatamka kwamba: “Mtu yeyote hawezi kuwa na sifa za kuchaguliwa kuwa rais iwapo atakuwa na umri usiopungua miaka 35 na usiozidi miaka 75.”

Rais Museveni atakuwa ana umri wa miaka 76 mwaka 2021. Lakini mwaka jana, rais huyo, kwa mbali na katika hali isiyo ya bayana, amekuwa anajaribu mikakati ya yeye mwenyewe kubakia madarakani baada ya 2021 au kuhakikisha anarithiwa na mtu anayemtaka.

Desemba mwaka jana, Jaji wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo, Steven Kavuma ambaye kicheo ni wa pili miongoni mwa majaji wa Uganda, alidaiwa kula kiapo (affidavit) kwamba umri wake ulikuwa miaka minne pungufu kuliko umri wake unaotambulika rasmi wa miaka 69.

Majaji wote nchini Uganda wanalazimika kustaafu wakifikia umri wa miaka 70, hivyo akaona ni vyema ‘azaliwe’ upya. Madai haya yaliibua mjadala mzito katika mitandao ya kijamii nchini Uganda, huku wananchi wakijiuliza, kuna jambo linajificha katika hatua aliyochukua jaji huyu?

Jaji Kavuma ni mwanachama mwasisi wa chama kinachotawala cha National Resistance Movement (NRM) na aliwahi kushika wadhifa wa uwaziri wa nchi katika masuala ya ulinzi mwanzoni mwa miaka ya 2000 na alidaiwa kuwa na ukereketwa uliopitiliza kwa chama chake.

Mchakato wa kuteuliwa kwake kuwa Naibu Jaji Mkuu mwaka 2015, ulipingwa vikali mahakamani. Nicolas Opiyo, mwanaharakati wa masuala ya haki za binadamu nchini humo, aliliambia gazeti la The Monitor kwamba, ilionekana wazi alikuwa anakingiwa kifua na Rais Museveni mwenyewe.

Je haya yote yalikuwa ni maandalizi kuhusu dhamira ya Rais Museveni? Siku rasmi ya kuzaliwa Museveni ni Septemba 15, mwaka 1944, lakini kutokana na kumbukumbu zake zilizopo kuhusu malezi yake kijijini na wazazi wasiokuwa na elimu, tarehe hii ilikisiwa tu kutokana na matukio ya kihistoria ya eneo hilo. Hivyo, Museveni anahitaji kupunguzwa mwaka mmoja tu wa umri wake wa sasa ili agombee tena urais mwaka 2021.

Wazo la kubadilisha umri wa mtu si la kushangaza sana, anasema Opiyo: “Mambo haya ni ya kwaida sana miongoni mwa watumishi wa umma ambao hawataki kustaafu baada ya kufikisha umri wa kustaafu.”

Masuala haya yanatiwa nguvu na barua ya Februari 6, mwaka huu kutoka Wizara ya Utumishi wa Umma  ambayo inasema: “Maombi mengi yameletwa na maofisa mbalimbali kubadilisha tarehe zao za kuzaliwa, hasa wale ambao wanakaribia kustaafu”.

Matukio haya bila shaka Museveni anayaangalia kwa shauku kubwa. Lakini kuhusu dhamira yake, kuna hatua zimeanza kuchululiwa. Agosti mwaka jana, hoja binafsi ya muswada ilitolewa bungeni na Mbunge wa chama tawala (NRM), Robert Ssekitooleko.

Hata hivyo, hoja hii ilitupiliwa mbali na Spika Rebecca Kadaga bila hata ya kijadiliwa. Hoja ilitaka kuongezwa rasmi kwa muda wa kustaafu kwa majaji na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi.

Wachunguzi wa mambo wanasema hiyo ilikuwa ni jaribio la kwanza la kutaka Kifungu 102(b) cha Katiba kirekebishwe ili kuondoa ukomo wa umri wa marais kugombea uchaguzi.

Hata hivyo, Uganda ina historia ya mambo kama haya. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2001, Museveni alikabiliwa na kikwazo kingine cha Katiba, ukomo wa urais wa vipindi viwili. Ndipo pakatokea msukumo mkubwa bungeni wa kuuondoa ukomo huo ingawa wakati wote Museveni alikuwa anajiweka mbali na kampeni hizo za bungeni.

Hatimaye kuondolewa kwa ukomo wa vipindi wa urais ulipitishwa bungeni mwaka 2005, mwaka ambao pia uliruhusu mfumo wa vyama vingi.

Katika Bunge hili la Uganda, chama tawala (NRM) kina akidi ya theluthi mbili, kwa hivyo iwapo hoja ya umri wa ugombea urais italetwa tena, basi kutakuwa hakuna pingamizi.