Home Latest News Bunge la Bajeti lilidoda, halikuwa na mvuto

Bunge la Bajeti lilidoda, halikuwa na mvuto

1356
0
SHARE
Wabunge wa upinzani walitumia njia ya kuziba midomo yao kwa plasta, lengo likiwa ni kuupinga uongozi wa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

NA INNOCENT HEZEKIAH

HATIMAYE Bunge la Bajeti limemalizika. Kila Mtanzania amejionea yaliyotokea, lakini kwa watu wengine tunaofikiria na kuchekecha zaidi akili zetu, tumeona mambo yanayoashiria mwelekeo mbaya.

Bunge ni chombo ambacho kinatakiwa kuwa huru na kila mwananchi anapaswa kufurahia uwakilishi wa Mbunge wake. Kama Bunge linageuzwa kuwa kivuli badala ya mtu halisi, ni lazima tutakuwa na matokeo mabaya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Naamini Watanzania ni watu makini wanaoweza kuchambua pumba na mchele, ili kujua Wabunge gani wanawakilisha yale wanayotaka. Watanzania wanafahamu hali halisi iliyopo bungeni.

Tumeona bajeti imepitishwa. Tumeona pia maumivu makali ya kodi yakianza kuwaumiza wananchi, huku kukiwa na sintofahamu juu ya utozaji wa kodi uliopitishwa na Bunge.

Ukifuatilia mikanganyiko iliyotokea katika mjadala wa Bunge la Bajeti lililomalizika mwezi uliopita, hususan mambo ya utozaji Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), na mambo mengine yaliyopitishwa hasa katika ongezeko la tozo kwenye sekta ya utaliii, ni wazi kwamba Serikali inahitaji watu makini wa kuishauri kifungu kwa kifungu mpaka kufikia suluhu.

Bahati mbaya kwetu wa Tanzania, Wabunge waliokuwa mstari wa mbele kufanya hayo kwa undani kabisa, walikuwa ni Wabunge wa upinzani pamoja na kuwa wengi wameonyesha wana uwezo mkubwa sana katika kupambanua na kujenga hoja, lakini pia ni wajibu wao wa msingi katika Bunge, ili kuisimamia Serikali ifanye mambo yake kwa tija na kwa manufaa mapana kwa taifa letu.

Kimsingi kutokuwepo kwa wapinzani bungeni, kunatugharimu Watanzania tutake susitake. Kuna baadhi ya Wabunge wa chama tawala walijitahidi sana kuchukua nafasi iliyokuwa imeachwa wazi na Wabunge wa upinzani kwa kutoa michango yao mujarabu katika kuboresha Bajeti,  lakini sauti zao zilikuwa hazifiki mbali, hivyo kuzimwa na walio wengi.

Katika hili napenda kwa dhati kutoka moyoni mwangu, kumpongeza Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe na Mbunge wa Muleba, Profesa Anna Tibaijuka, kwa kuwa na maono ya mbali. Katika Bunge lililopita, hakika michango yao itabaki kuwa kumbukumbu vizazi na vizazi.

Kwa mantiki hiyo, kukosekana kwa wajumbe wa upinzani katika Bunge la Bajeti lililopita, ni pigo jinginge kwa ustawi wa taifa letu. Mengi yamesemwa na kuzungumzwa, lakini kikubwa Watanzania wanaona tofauti kubwa iliyojitokeza pale Wabunge wa upinzani walivyokuwa ndani ya Bunge.

Kiukweli, Bunge lilionekana kuwa la kiwango cha juu hata upande wa Serikali ulikuwa unajipanga kwa hoja mujarabu ili kutoa majibu yenye tija, lakini kukosekana kwa upinzani, Bunge letu lilikuwa la kawaida sana na kwa mtazamo wangu, upande wa Serikali haukuwa ukihitaji kujiandaa sana ili kukabiliana na hoja za Wabunge.

Tanzania kwa sasa na hata baadaye, tunahitaji upinzani imara na madhubuti kwa maendeleo ya nchi yetu, hili halina mjadala na ni afya kwa ustawi wetu.

Mbinu zozote za kuzuia wapinzani kufanya kazi yao ni kurudisha juhudi za maendeleo yetu nyuma kwa makusudi au kwakutojua.

Rai yangu kwa Serikali; iwe radhi kupokea ushauri kutoka kwa wapinzani maana wao ni wabia wa maendeleo ya taifa letu. Pia viongozi walio madarakani, watambueni kuwa mamlaka waliyonayo, ni Mungu kawapeni, hivyo yatumieni vizuri maana hata nyinyi mnasifa za ubinadamu na ni binadamu kama walivyo wengine.

Viongozini wanaweza kuugua, wanaweza wakaumwa, wakapoteza maisha, wanachukia, wana majonzi, wanapata ulemavu na kila sifa ya ubinadamu wanayo, kwa hiyo wajiepushe na kujiweka daraja la Muumba wa mbingu na nchi .

Ni lazima viongozi kuwatendea wananchi wao sawa sawa na wao wapendavyo kutendewa.  Viongozi msiwatende watu vile msivyopenda kutendewa nyinyi, maana Mungu huwapatilia waovu hata kizazi cha tatu na kuendelea. Epukeni kuwaletea shida wajukuu zenu na vitukuu vyenu kwa matendo yenu ya leo.

Sisi wote ni ndugu, sisi wote ni Watanzania, sisi wote tuna haki katik nchi yetu, maana ndio nchi tuliyopewa na Mungu, uovu haupiti hivi hivi ukisha maliza ulikotumwa, urudi ulikoanzia.
Mungu wabariki viongozi wetu wape hekima, iliwatuongoze kwa amani na upendo. Mungu ibariki Tanzania.