Home Makala Bunge la Spika Ndugai haliwezi kuwa la moto

Bunge la Spika Ndugai haliwezi kuwa la moto

1537
0
SHARE

Na Balinagwe Mwambungu

WIKI iliyopita nilizungumzia Bunge letu ndani ya mfumo wa vyama vingi, hususan Bunge lililopita yaani Bunge la 10 lililokuwa linaongozwa na Spika Anne Makinda (2010-15), kwamba lilikuwa tofauti na Bunge la Tisa chini ya Spika Samuel John Sitta.

Nachelea kusema kwamba Bunge la 11, chini ya Spika Job Ndugai, tusitegemee kuwa litakuwa Bunge la mafanikio makubwa kwa kuwa limeanza na mpasuko mkubwa ambao haujawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Nasema tusitegemee kuwa litakuwa Bunge ‘vibrant’—lenye kusisimua kama lilivyokuwa Bunge la kwanza la vyama vingi chini ya uongozi wa Spika Pius Msekwa. Hili Bunge ndilo lililoandika kanuni za Bunge na haki za Wabunge. Kifupi tu niseme kwamba hili ndilo Bunge lililoweka misingi ya Bunge katika mfumo mpya wa vyama vingi.

Wabunge wa upinzania, japo walikuwa wachache, walikuwa makini na walimchachafya Spika Msekwa pamoja na kwamba alikuwa Spika mzoefu. Kitu kinachokumbukwa zaidi ni pale Wabunge wapya ambao walikuwa wanasheria, wakiwamo Masumbuko Lamwai na Mabere Marando, walikosoa Kiapo cha Mbunge na ilibidi kirekebishwe mara moja.

Wapinzani kwa ujumla wao, walikataa kiapo ambacho Mbunge anaapa kuwa ‘nitakuwa mtii kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano’—wakisema haiwezekani wakaitii Serkali ambayo kimsingi, wao ndio wanapaswa kuisimamia.

Kwa kujikumbusha tu, baada ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi, Chama cha Mapinduzi (CCM), kilikuwa na jumla ya Wabunge 186 wa kuchaguliwa na 28 wa Viti Maalumu na jumla ya Wabunge 214.

Chama kikuu cha upinzani Civic United Front (CUF) kilikuwa na jumla ya Wabunge 28, viti maaalumu 4 na wakuchaguliwa 24. Chama kilichofuata kilikuwa NCCR-Mageuzi kikiwa na Wabunge 16 wa kuchaguliwa na 3 wa Viti Maaalumu. Jumla kilikuwa na Wabunge 19.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilikuwa na Wabunge 3 tu wa kuchaguliwa na 1 wa Viti Maalumu. United democratic Party (UDP), kilikuwa na Wabunge

3 wa kuchaguliwa na 1 Viti Maalumu. Nimeonesha idadi ya Wabunge wa Upinzani, ili msomaji aelewe ni kwa nini CCM na Rais John Magufuli wako ‘apprehensive’—waha hofu.

Chadema kimepaa kutoka Wabunge watatu wa kuchaguliwa na mmoja wa viti maalumu mwaka 1995-2000 na kufikisha Wabunge 70 baada ya Uchaguzi wa 2015 na kuvifunika CUF ambacho ndicho kilikuwa Chama Kikuu cha Upinzani 1995-2000, kikifuatiwa na NCCR-Mageuzi kilichokuwa na Wabunge 19.

Katika uchaguzi Mkuu uliopita, kama si uwepo wa Edward Lowassa na Frederick Sumaye, na vyama vinavyounda ukawa kujenga ngome ya pamoja, CUF na NCCR-Mageuzi huku Baraza, vingepotea kabisa.

Aidha, wasiwasi wa CCM ni kwamba Chadema wakiachwa waendelee na utaratibu wao wa kukipeleka chama vijijini, ni wazi kwamba wataweza kupata wanachama wengi, hasa vijana, kama ilivyoonesha kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.

Chadema ambacho kilipewa lebo ya “chama cha Wachagga” kilikuja juu baada ya Dk Willibrod Slaa kujiunga. CCM ambao walikuwa wanavituhumu vyama vya upinzani kwamba ni vya kikabila, na walipoona kwamba Chadema kinazidi kukubalika, wakadai kwamba ni chama cha Ukanda wa Kaskazini.

Lakini uchaguzi wa mwaka jana umeonesha kwamba Chadema ni chama cha kitaifa na kinachoendelea kujitanua kanda zote za Tanzania.

Kwa mara ya kwanza kilipata jimbo moja katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika uchaguzi uliofutwa wa Oktoba 25, 2015. Chadema hivi sasa kina nguvu Kanda ya Ziwa, ambako ndiko anakotoka Rais Magufuli wa CCM.

Na kwa wale wanaopenda kudadisi, Rais Magufuli amelielewa hilo, na ‘marufuku ya siasa’ aliyoitangaza inalenga kukidhoofisha.

Rais ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM kitaifa, amenza kuzunguka mikoani, kukitangaza chama chake, huku wenyeviti wengine wa kitaifa akiwawekea zengwe—eti wafanye siasa walikoshinda uchaguzi. Yeye tayari amefanya ziara mbili katika Kanda ya Ziwa katika kipindi cha miezi 10.

Katika uchaguzi uliopita, Rais Magufuli alipata kura 8,882,935, ambayo ni sawa na asilimia 58.46 ya kura zote zilizopigwa vizuri na CCM kikapata jumla ya viti  252 vya Wabunge.

Edward Lowassa aliyegombea kwa tiketi ya Chadema, alipata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97 ya kura na kina jumla ya Wabunge 70.

Kwa mwanasiasa yeyote makini, anajua kwamba huwezi kuwadharau watu zaidi ya milioni sita waliokunyima kura na kuwaambia waache siasa na wasifanye mikutano ya hadhara hadi uchaguzi mkuu wa 2020.

CCM hivi sasa wanakuna vichwa—kupinga kauli ya Rais au waumie kimya kimya kwa vile wanamwogopa. Hii marufuku inawaumiza na wao pia. Hawatafanya mikutano katika majimbo na kata ambako walishindwa, hakuna mwanasisiemu mwenye ujasiri wa kumwambia Magufuli kwamba amewakwaza.

Lakini hii marufuku haiwahusu Chadema pekee. CUF ambacho ni cha pili kwa vyama vikuu vya upinzania kikiwa na jumla ya Wabunge 4, ACT-Wazalendo chenye Mbunge mmoja, na NCCR-Mageuzi chenye Mbunge mmoja pia, vinapaswa kuunganisha nguvu na kupaza sauti kwa pamoja. Ikumbukwe kwamba CUF kingelikuwa na Wabunge wengi zaidi kama usingefanyika ‘uporaji wa ushindi’ kule Zanzibar.

Naliona Bunge la mwezi ujao kuwa ni lenye mparaganyiko, japo Spika Job Ndugai anasema anatafuta dawa ya kuwaleta Wabunge pamoja.

Hii itawezekana tu kama Wabunge wa pande zinazosigana, watajitathmini na kutambua kwamba wapo pale bungeni Dodoma kwa nia moja tu—kuisimamia Serikali na kuona kwamba inatekeleza miradi ya maendeleo kama iliyoahidi.

Wabunge wa upande wa chama tawala, wajitathmini pia na kujisahihisha—waache kuwa wasemaji wa upande wa Serikali—kwa  kuendelea kupeleka itikadi za chama chao, hawalitendei haki taifa. Kama Magufuli anasema yeye ni Rais wa wote, na CCM kwa kuwa ndicho chama tawala, kiseme vivyo hivyo—kwa kuwa ni chama tawala.

Wabunge wa CCM waache kuogopa upepo wa mabadiliko—bali wajifunge vibwebwe, na kusimama kidete kupambana na kutetea hoja murua na zenyetija kwa wananchi waliowapeleka kuwawakilisha. Wabunge waiache Serikali ijibu hoja za wawakilishi wa wananchi, bila kujali hoja imeletwa na upande gani.

Ni kwa njia hii tu, tunaweza kusema tunajenga demokrasia ya kweli katika nchi yetu. Kuwazuia wanasiasa wasifanye siasa, kwa dhana tu kwamba eti huenda wakafanya vurugu, ni dhana isiyo na mashiko—kwa kuwa inakisiwa tu–ni woga tu uliojengeka pasipo kuwa na ushahidi. Hatuendi hivyo.