Home Tukumbushane Busara za wazee ziendelee kutafutwa

Busara za wazee ziendelee kutafutwa

3060
0
SHARE

Rais John Magufuli katika mkutano na wazeee wa Dar es Salaam.

NA HILAL K SUED

Watu wa jamii na tamaduni nyingi duniani huchukulia ushauri wa watu wao wa umri mkubwa (wazee) kuwa ushauri wa muhimu sana. Watu humtafuta mzee kwa busara zake na muongozo katika masuala mbali mbali yanayohusu maisha yao kwa sababu busara ni kitu cha thamani kubwa tunachopaswa kukitafuta na kukizingatia.

Na kwa sehemu kubwa ya maisha ya binadamu, kila kizazi kipya kilijifunza kuhusu maisha kutoka masimulizi ya uzoefu na busara kutoka kwa wazee. Watu hawa (wazee) wanaheshimika kwa sababu ya umri wao mkubwa na wamekuwa wakihangaika kuwalea vijana, na kwa ujumla kupigania kuwepo kwa dunia ya amani na iliyostaarabika.

Hata misahafu pia imezungumza nafasi ya wazee katika jamii: “Hivyo nawaasa wazee miongoni mwenu… kuwachunga kondoo wa Bwana kati yenu… kufanya kazi ya kuwaangalia…” (1Petro 5: 1–2).

Hapa kwetu ni nadra sana kutafuta busara za wazee kama vile ilivyokuwa wakati wa utawala wa baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere – hasa katika kutafuta mwongozo mwanana katika sera za kijamii na za uchumi, kwani utamaduni wa kutoa busara hiyo mara nyingi hukosekana.

Hivyo iwapo wazee katika jamii yoyote wanapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa, basi Watanzania wasijihesabu kwamba wamejaliwa kuwa na neema hiyo.

Sidhani kuna wengi miongoni mwetu wamekisoma kitabu kiitwacho “Didnt Get Old to Become Stupid” (yaani “Sikutafuta Uzee Ili Nije Kuwa Mpumbavu.” Kwa wale ambao wamekisoma bila shaka walielewa maana ya kuzeeka katika nchi nyingine – kwa mfano Tanzania.

Kwa mfano katika miaka ya mwanzo ya 90 Rais wa awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi hakupata matatizo yoyote kutoka kwa wazee pale alipokuwa ‘anaiuza’ kwa wananchi ile sera ya serikali yake ya kuchangia elimu ya vijana wao hadi kiwango cha chuo kikuu.

Katika mkutano mmoja wa ndani, wazee walipiga makofi pale aliposema itawabidi wachangie elimu ya vijana wao. Hivi baadaye wazee hao hawakuja kuona kilichokuwa kinatokea kwa vijana wao waliokuwa wakifukuzia elimu ya juu? Wengi hawakuweza kufikia chuo kikuu kwa kukosa ada. Suala hili la elimu ya juu kwa vijana wetu bado linalitesa taifa – pamoja na utajiri wake mwingi wa mali asili n.k.

Na kuhusu utawala unaokuwapo madarakani ambapo katika hali ya kawaida wazee waliopo katika jamii ndiyo hutarajiwa kutoa maneno ya ushauri, muongozo na angalau kuwakemea ikibidi wale walio juu madarakani dhidi ya ufisadi na kutokuwapo kwa utawala bora, badala yake baadhi yao ndiyo kwanza huwa washiriki wa vitendo hivyo, kama siyo kujiingiza moja kwa moja.

Labda kama wana sababu nyingine za msingi za kufanya hivyo, kwa nini waachie kazi hiyo kufanywa na vyombo vya habari – hususan magazeti – na Wabunge wachache wapiga filimbi kutoka kambi zote mbili za medani ya siasa?

Lakini hata hawa, ili jamii iwachukulie kwa umakini, pia wanahitaji kuungwa mkono na wazee – hasa wale wa chama kilichopo madarakani. Hii ni kwa sababu kutokana na umri wao mkubwa na kwamba katika miaka yao ya nyuma baadhi yao walishika nyadhifa kubwa kubwa katika serikali na utumishi wa umma kwa ujumla, wamehitimu kuitwa ‘wazee wa busara’ ambao jamii huwachuklia kwa heshima kubwa na mara kwa mara huwatupia macho kwa ajili ya muongozo.

Hapo juu nimegusia suala la kukua kwa ufisadi kwamba sababu moja ni kukosekana kwa ‘ukemeaji’ dhidi ya kansa hiyo kutoka kwa wazee. Wamekuwa kimya mno. Swali kubwa ni – kwa nini iwe hivyo? Kwa nini walikuwa wakiiacha kansa hiyo kuendelea bila kujali hatari iliyokuwa inatengenezwa?

Sehemu moja ya jamii ambayo imekuwa ikiathirika na ukimya wao ni vijana. Maelfu na maelefu ya vijana ambao huingia mitaani kutoka mashuleni na vyuoni kila mwaka ni watu wasiojua hatima yao kimaisha, labda wajiingize katika shughuli ambayo maelfu ya wenzao kabla yao wamekuwa wakifanya – kukumbatia shughuli za ‘umachinga.’

Hii ni kwa sababu kwa miaka kadha mabilioni ya fedha kutoka hazina ya taifa yamekuwa yakichotwa kila mwaka na wajanja wachache, na mabilioni mengine kuibiwa kupitia mikataba mibovu ya uchimbaji madini, na uporaji wa mali asili zetu.

Fedha hizo zingeweza kutumika kutengeneza mazingira mazuri ya upatikanaji ajira kwa vijana wetu – kama vile viwanda – viwanda vya aina ya ile alivyoanzisha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wake.

Lakini labda hakuna wakati ambapo ushauri wa wazee unahitajika sana kama wakati huu. Kumekuwapo na migongano kati ya makundi ya kijamii, vyama vya saisa na taasisi za serikali — hususan, Jeshi la Polisi — kiasi kwamba hivi sasa imejengeka hofu kwamba polisi ambao kazi yao kuu ni kulinda usalama wa raia, hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Kumekuwapo na ongezeko la watu kuumizwa, kuharibiwa mali zao, kuuwawa katika mazingira ya kutatanisha. Kumetokea kikundi cha ‘watu wasiojulikana’ ambao wamesababisha sintofahamu na kujenga hofu katika jamii.

Kutokana na hli hii wito umekuwa unatolewa na taasisi mbali mbali, likiwamo Baraza la Maskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Kituo cha cha Demokrasia Tanzania (TCD), na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwamba ipo haja ya kuyatolea kauli ya pamoja matukio mabaya yanayoharibu sifa nzuri za nchi yetu.

Aidha magazeti mbali mbali katika tahriri zao nayo yametoa wito wa kuwepo maridhiano – serikali na wadau mbali mbali wakae pamoja kuitafakari hali hii ili kuipatia ufumbuzi kwa masilahi ya taifa.

Tulitarajia wazee nao wangejitokeza na kuweka sauti zao kwani naamini kabisa wengi wao hawapendezwi na matukio haya. Ni watu ambao wanaweza kusikilizwa.

Ni watawala pekee ndiyo wana uwezo wa kuchukua hatua ya kwanza. Lakini inaonekana hawataki kuketi pamoja na wadau wengine katika kufanya “soul searching” – vipi hali inakuwa hivi. Hawataki kukubali kwamba ‘amani na utulivu’ ni suala la pande mbili (two-way traffick) – yaani raia na utawala wenyewe. Pande zote hizi mbili zinawajibika katika kuijenga na kuirutubisha amani hiyo.

Wanapaswa kuondokana na dhana kwamba siku zote suala la amani ni wajibu wa raia peke yao – yaani raia pekee ndiyo huwa watuhumiwa wa kwanza na wakubwa wa kutoweka kwa amani na si utawala pamoja na vyombo vyake vya dola.

Tukubaliane kitu kimoja – kwamba katika nchi yoyote duniani amani hailetwi kwa kusisitizwa au kuimbwa majukwaani, au hata kwa mahubiri katika majumba ya ibada. Aidha si kitu cha kutamka mithili ya maagizo katika Taurati kuhusu kuumbwa kwa dunia “..na iwepo amani” na kweli ikawepo!

Amani hujengwa kutokana na misingi madhubuti ya haki na usawa na kuisimamia kwa dhati na kwa haki misingi hiyo, na pia kuzisimamia vyema taasisi zinazosimamia misingi hiyo. Kama misingi ya haki haisimamiwi vizuri na kuanza kuporomoka amani inakuwa mashakani.