Home Makala Bush alijua Marekani ingeshambuliwa

Bush alijua Marekani ingeshambuliwa

1635
0
SHARE

Na William Shao

KWA tuliofuatilia mfululizo wa makala haya tangu mwanzo hadi hatua hii tumeona mambo kadhaa, tukapata majibu kadhaa na tukabaki na maswali kadhaa. Baadhi ya maswali hayo ni yale ambayo tunaweza kupata majibu yake na mengine hatutapata majibu kamwe.

Maswali mengi yatakayoendelea kuulizwa yatahusu kile kilichotokea Septemba 11, 2001, lakini angalau kuna kiasi cha mambo ambacho sasa tunakijua kuhusu tukio hilo. Sehemu moja ya kiasi hicho ni ile ambayo haina ubishi.

Kwa mfano, hakuna ubishi kwamba ni kweli tukio hilo lilitukia, na lilitukia Septemba 11, 2001, na lilitukia katika miji ya New York na Washington DC., Marekani, na lilihusisha ndege nne zilizokuwa na abiria.

Lakini bado kuna ubishi wa nani waliliandaa tukio hilo, kulitekeleza na nini shabaha yake. Ingawa kuna ubishi wa aina hiyo, angalau dunia inaanza kupata mwanga wa kile kilichotokea, ingawa haitapata mwanga wa ukweli wa mambo yote.

Sasa tunajua kuwa familia ya Bush ilikuwa—na pengine bado—ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa familia ya bin Laden—au angalau ndivyo ilivyokuwa. Sasa tunajua kuwa utawala wa George W. Bush ulikwamisha juhudi za kuchunguza ushiriki wa familia ya bin Laden katika kuufadhili mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na kuvifadhili vikundi vya kigaidi.

Tumesoma kuwa baadhi ya wanafamilia wa familia ya bin Laden waliokuwa nchini Marekani waliondolewa nchini humo bila kubughudhiwa wakati ndege zote binafsi zilikuwa zimepigwa marufuku kuruka. Tunajua kuwa kuondolewa kwa familia hiyo kulifanyika siku kadhaa baada ya tukio la Septemba 11 wakati kila Mwarabu aliyeonekana popote katika ardhi ya Marekani alikuwa akitiliwa shaka.

Tunajua siku chache kabla ya Septemba 11 Kaimu Mkurugenzi wa FBI na Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Ugaidi, John O’Neill, alijiuzulu wadhifa wake Julai 2001 kwa sababu alikwamishwa asimchunguze Osama bin Laden na mtandao wake.

Tunajua kuwa watu wa familia ya George Bush ina uhusiano wa kibiashara na watu kama Khalid bin Mahfouz ambao wanadaiwa kuwa ni ama magaidi au ni wafadhili wa ugaidi na kwamba aliwahi kutajwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuwa alikuwa akifadhili magaidi—hususan Osama bin Laden.

Sasa tunajua kuwa kuondolewa kwa Taliban huko Afghanistan kulikusudiwa ili kutoa mwanya kwa ajili ya kujenga bomba la mafuta litakaloyasafirisha mafuta hayo kutoka eneo hilo na kuyapeleka kule ambako Wamarekani na Waingereza wanataka.

Tumeona kuwa kuishambulia Afghanistan hakukuhusiana kwa vyovyote na ‘ugaidi’ wa Septemba 11, 2001. Tunajua kuwa mtandao wa bin Laden nchini Afghanistan uliimarishwa na CIA.

Tumeona kuwa majina ya waliotajwa na FBI kuwa ni ya watekaji hayakuwa katika orodha ya majina ya abiria waliosafiri katika zile ndege zilizoangamia Septemba 11, 2001. Yote hayo yanajulikana kwa sasa. Lakini tutajua mengi mengine, na mengine, na mengine, na mengine, na mengine mengi ikiwa tunataka kuyajua.

Tuendelee. Kushindwa kuzuia tukio la ‘kigaidi’ la Septemba 11 hakukutokana na kutokuwa na taarifa za mapema kuhusu tukio hilo. Imani iliyojengeka kwa walimwengu wengi duniani—si wote—ni kwamba Marekani haikujua kuwa ingeshambuliwa hadi pale iliposhambuliwa.

Kile ambacho walimwengu wanalazimishwa wakiamini ni kwamba taifa la Marekani, na viongozi wake, na walinzi wake wote, na teknolojia yake yote, na ujasusi wake wote, na polisi wake wote, na utajiri wake wote, na historia yake yote, walishtukizwa na magaidi hadi kikatukia kile kilichotukia.

Ni rahisi kukubali hivyo, hususan ikiwa hatutaki kuhangaika kulitafakari kwa makini jambo hilo na kuvuka ng’ambo ya taarifa unazosoma na kuambiwa. Swali rahisi ni je, Serikali ya Bush haikujua kuwa ingeshambuliwa? Kabla hujafikiri kuwa jawabu lake ni ‘NDIYO’, tafakari kwa makini sana yafuatayo.

Makamanda watatu wakuu wa Serikali ya Marekani hawakuwa nje ya nchi yao siku hiyo, bali walikuwa nchini Marekani—tena kazini. Makamanda hao ni wale waliokuwa na uwezo wa kuamua nini kifanyike nchini Marekani, jinsi kitakavyofanyika, muda gani kifanyike na nani afanye nini.

Makamanda hao ni George Walker Bush (Rais), Donald Henry Rumsfeld (Waziri wa Ulinzi) na Richard Bowman Myers (Mkuu wa Majeshi ya Marekani). Je, hawakujua kilichokuwa kinaelekea kutukia nchini mwao kabla hakijatukia?

Kuna habari zinazosema Rais alipata “maonyo” mengi miezi kadhaa kabla ya Septemba 11, 2001 kwamba ‘magaidi’ wangeishambulia Marekani kwa kutumia ndege, lakini hakuna kilichofanyika kuzuia ‘ugaidi’ huo.

Mwanajeshi wa Jeshi la Anga la Marekani, Luteni Kanali Steve Butler, alisema Bush alijua kuwa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 yangetukia, lakini hakufanya lolote kuyazuia. (Rejea kiungo hiki: http://goo.gl/HKDJZz)

Luteni Kanali Butler alikuwa pia mkuu wa masuala ya wanafunzi katika Taasisi moja ya kijeshi nchini humo. Baadaye aliandika barua iliyochapishwa katika gazeti ‘The Herald’ la Monterey katika matoleo mawili ya Mei 21 na 26, 2002 akimtuhumu Bush kuruhusu kufanyika kwa mashambulizi hayo ili atimize malengo yake ya kisiasa. (Rejea http://goo.gl/RVHCxZ)

Sehemu ya barua hiyo ilisomeka hivi: “Kwa kweli Bush alijua hatari iliyokuwa ikiijia Amerika. Hakufanya lolote kuwaonya Warekani kwani alilihitaji sana tukio hili kwa sababu ya vita dhidi ya ugaidi. Baba yake alikuwa na Saddam na sasa yeye anamhitaji Osama … Urais wake hauendi popote.

Hakuchaguliwa na watu wa Amerika, lakini aliwekwa Ikulu ya Marekani na watu wa mahakama kuu wasiopenda mabadiliko. Uchumi ulikuwa ukitumbukia kwenye shimo la kawaida la ‘Republican’ na alihitaji chochote kuuhalalisha urais wake.”

Mara baada ya barua hiyo kuchapishwa, Butler alisumbuliwa sana kiasi kwamba mkewe, Shelly Butler, alisema jeshi la Marekani lilimsababishia mumewe “huzuni nyingi” kutokana na barua hiyo. Aliachishwa kazi kwenye taasisi hiyo na kupangiwa kazi nyingine. (Rejea http://goo.gl/3c2FOl)

Butler ni mwanajeshi aliyepigana katika Vita ya Ghuba mwaka 1991. Wakati huo aliyekuwa Rais wa Marekani ni George H. Bush. Kwa kuzingatia kuwa Butler alikuwa afisa mwandamizi katika jeshi la Marekani, haiwezekani alikuwa akitoa madai ambayo hakuyajua. Inaelekea alijua fika kuwa Bush na The Pentagon walijua kabisa ni kitu gani kilikuwa kinaelekea kutukia nchini Marekani na pia walijua kingetukia wakati gani.

Siku ile ile ya tukio, Septemba 11, 2001, habari nyingi kuhusu Bush kuwa na taarifa za mashambulizi ya ‘kigaidi’ kabla hayajatokea zilianza kusambaa. Vyombo vya habari vilivyokuwa na mwelekeo wa watawala na ambavyo vilirudia tu yale ambayo watawala walisema ndivyo ambavyo havikuliona hilo.

Vyombo vichache zaidi ambavyo huchunguza kwa umakini sana kabla ya kutoa habari zake, ndivyo vilivyoanza kuripoti habari za kwamba kabla ya Septemba 11, 2001 Rais Bush aliambiwa—kwa hiyo alijua—kuwa kulikuwa na uwezekano wa kuteka ndege nchini Marekani, lakini hakufanya lolote kuzuia hali hiyo isitokee.

Lakini hata kama alijua au la hakutoi kidokezo chochote cha kuonesha kuwa kitendo hicho kilifanywa na Osama bin Laden na, au, mtandao wake wa kigaidi wa al-Qaeda.

Hapa ndipo yanapozuka maswali ya mashaka. Je, mpango wa kuishambulia Marekani Septemba 11 uliandaliwa nchini Afghanistan au ni Marekani kwenyewe? Kama Bush aliambiwa na hakuchukua hatua, hiyo inamfanya asilaumiwe yeye au serikali yake? Ingawa tunaweza kukubali kuwa Bush alionywa kuhusu kufanyika kwa ugaidi huo, tutambue kuwa kuna mengi zaidi ya hilo.

Mwaka 2002 vyombo vingi vya habari vilianza kutoa habari zilizodai kuwa Serikali ya Bush ilionywa. Miezi minane baada ya tukio hilo, Ikulu ya Marekani ilikiri kuwa Bush alionywa na Usalama wa Taifa la Marekani kabla ya Septemba 11 kwamba mtandao wa kigaidi wa Osama bin Laden ulikuwa na mpango wa kuteka ndege nchini Marekani.

Hizo ni habari zilizokuwa zikisambazwa—kwamba Osama ndiye aliyekuwa akiuandaa mpango huo. Hivyo ndivyo vyombo vya habari viliripoti, hususan televisheni ya ‘CBSNews’ katika taarifa yake ya Alhamisi ya Mei 16, 2002. (Rejea http://goo.gl/BFYHBE)

Hapo ilitumika mbinu ya kuanza kutamka lile lililokuwa limepangwa kutukia, wakidai kuwa ni Osama aliyekuwa amepanga, ili litakapotokea hatimaye, idaiwe kuwa ni Osama kwa sababu tayari lilikuwa limeshasemwa kabla halijatukia.

Tayari walimwengu walikuwa wameshaanza kuandaliwa bongo zao zikubali kuwa Osama alihusika. Kwa mujibu wa CBSNews, Rais Bush aliambiwa miezi kadhaa kabla ya mashambulizi ya Septemba 11 kwamba mtandao wa kigaidi wa Osama bin Laden “unaweza kuteka ndege za abiria za Marekani…”

Hayo ndiyo yale tuliyoambiwa na vyombo hivyo. Ukitazama sana vyanzo vya habari hizo utakuta ni FBI, CIA au Marekani yenyewe.

Aliyekuwa mwandishi wa habari wa Ikulu ya Marekani tangu Januari 2001 hadi Julai 2003, Ari Fleischer, alisema utawala wa Marekani “ulivitaarifu vitengo muhimu tu katika kiangazi cha mwaka 2001 kwamba utekaji ungeweza kufanyika.” Rejea http://goo.gl/eAbeYC. Kiungo hiki sasa kimeondolewa)

 

Tukutane toleo lijalo…