Home Makala Kimataifa CARL GUGASIAN: MHALIFU WA BENKI MWENYE AKILI KULIKO WOTE

CARL GUGASIAN: MHALIFU WA BENKI MWENYE AKILI KULIKO WOTE

1299
0
SHARE

NA KOMBO KASSIM

MWAKA 2021 ulimwengu utashuhudia Mmarekani aliyefanikiwa zaidi kutekeleza matukio ya ujambazi akitoka gerezani, baada ya kutumikia kifungo cha miaka 17. Hiyo ni baada ya kufanikiwa kuishawishi serikali na mahakama kupunguza kifungo chake kutoka miaka 115 mpaka miaka hiyo 17.

Atakapotoka na kurudi uraiani atakuwa na miaka 69. Anaitwa Carl Gugasian, maarufu kama ‘The Friday Night bank robber’, mhalifu aliyeiumiza kichwa FBI kwa miaka 30 akitekeleza matukio 50 ya kuvamia na kuiba benki pasipo kukamatwa, kitendo kilichopelekea FBI na waendesha mashitaka wa Marekani ‘kumsifu’ kuwa ndiye mhalifu mwenye akili na aliyefanikiwa zaidi katika historia ya Marekani (the most prolific bank robber).

Kumekuwa na kelele nyingi kutoka kwa ‘mashabiki’ wakiitaka Hollywood watengeneze muvi kuhusu maisha ya ‘The Friday night bank robber’!

Jambo lililowashangaza wengi na ulimwengu wote ni jinsi gani binadamu mmoja aliweza kutekeleza matukio 50 ndani ya miaka 30 akiwa peke yake na FBI washindwe kujua identity yake wala kuwa na hata mbinu ya kuweza kumzuia au kumkamata.

Mbinu, weledi na nidhamu aliyokuwa nayo na kutumia kutekeleza matukio yake yalikuwa ni siri na kitendawili mpaka pale alipokamatwa na kuamua kuwasimulia FBI ili kujaribu kuwashawishi kumpunguzia adhabu ya kifungo. Na hii ni historia yake ‘kwa kifupi’ tu.

ALIWEKA DHAMIRA AWE “MHALIFU MWELEDI”

Akiwa na miaka 15, Carl alitekeleza tukio lake la kwanza la ujambazi ambapo alijaribu kuiba fedha katika candy store bila mafanikio na alipigwa risasi tumboni na kukamatwa. Baada ya kukamatwa alipelekwa katika jela ya watoto ya Camp Hill kwa miezi 18.

Baada ya kutoka jela, Carl alidhamiria sasa kuwa ni lazima awe mhalifu mwenye weledi wa hali ya juu kiasi kwamba atafanikiwa katika kila tukio na hataweza kukamatwa na akadhamiria kama anataka kufanikiwa aibe fedha nyingi kwa wakati mmoja, basi sehemu sahihi ya kuiba ni benki na kama anataka kweli awe mhalifu mweledi, anatakiwa ajue namna sehemu hizo (majengo na mifumo) zinavyofanya kazi, afahamu namna ya kutumia silaha, ajue namna ya kujihami na namna atakavyotoroka na fedha.

Baada ya kuweka dhamira hiyo, Carl akachukua hatua ya kwanza na alichofanya ilikuwa ni kujiunga na Chuo Kikuu cha Villanova, ambako alisomea uhandisi wa umeme. Akiwa chuoni alitumia mwanya huo kujiunga na programu maalumu ya jeshi la Marekani kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana walioko chuoni! Baada ya kumaliza chuo akaenda kutumikia jeshi kwa muda mfupi kituo cha Fort Bragg na akiwa huko akapata mafunzo maalumu ya kijeshi (Special Forces and tactical weapons training).

Baada ya kupata mafunzo ya kijeshi, Carl akarudi Chuo kusoma masters degree ya System Analysis na alipomaliza Shahada ya uzamivu akafanya mafunzo ya awali kwa ajili ya shahada ya uzamivu katika takwimu.

Pia mtaani alipokuwa anaishi alijiunga na kituo cha kufundisha mafunzo ya kujihami (karate na judo) ambapo alifanikiwa kupata mkanda mweusi (third degree black belt).

Baada ya kufanikiwa kufanya maandalizi yote hayo na kupata kila aina ya mafunzo na uzoefu aliyohitaji ili kuwa ‘mhalifu wa daraja la kwanza’, sasa ulikuwa ni wakati kwake kupita kila benki kukomba fedha na kuudhihirishia ulimwengu kuwa hakujapata kuwapo na itachukua miaka mingi kutokea mhalifu kama yeye Carl ‘the Friday night bank robber’.

MAANDALIZI KABLA YA TUKIO

Moja kati ya vitu vilivyomsaidia Carl kufanya matukio ya uhalifu kwa mafanikio ni uwezo wake wa kuweka mkakati wa utekelezaji jinsi gani atakavyofanikisha azma yake! Ni dhahiri kuwa, mafunzo ya kijeshi aliyoyapata yalimsaidia sana kuwa mwanamkakati mzuri wa kiufundi wa matukio! Carl alikuwa anatumia hadi miezi kadhaa katika kupanga utekelezaji wa tukio moja tu.

Kwanza kabisa Carl alichunguza benki zilizopo katika miji midogo. Baada ya kupata orodha ya benki katika miji kadhaa midogo Carl aliangalia kati ya benki hizo ni benki gani haziko katikati ya mji (kwa maana kwamba ziko pembezoni/nje ya mji). Kisha Carl aliichagua benki mojawapo kati ya hizo na benki ambayo inakuwa haiko karibu sana na makazi ya watu au iko karibu na msitu, basi benki hiyo anaipa kipaumbele katika orodha yake.

Baada ya kuamua ni benki gani atafanya tukio, Carl alianza tafiti juu ya tukio lenyewe atakavyolitekeleza… Kwanza kabisa Carl alianza kwa kusoma mandhari yanayozunguka benki na lengo lake kubwa inaelezwa kuwa alitafiti zaidi msitu ambao unakuwa karibu na benki. Inaelezwa kuwa, Carl angeutembelea msitu huo na kuukagua nukta baada ya nukta, haijalishi ni muda gani angetumia mpaka kumaliza kuukagua!
Inaelezwa kuwa, lengo lake lilikuwa ni kujua ni maeneo gani ya msitu ambapo watu huwa wana mazoea ya kupita au kutembelea, ni eneo gani la msitu limejificha zaidi, ni upande gani wa msitu unakuwa rahisi kuifikia barabara, ni eneo gani la msitu lina umajimaji na eneo gani ni kavu na kadhalika na kadhalika.. Inaelezwa kuwa, Carl angeutafiti huo msitu na kuufahamu kuliko hata wenyeji wa eneo hilo husika. Angeufahamu msitu nukta kwa nukta!

Baada ya kuufanyia tafiti msitu, inaelezwa kuwa Carl alikuwa anageukia kuitafiti benki yenyewe na wafanyakazi wake. Kuhusu benki, angetafiti je, hiyo benki inafungwa na kufunguliwa saa ngapi, ni siku zipi huwa wanachelewa kufunga, ni siku gani wanakuwa na kiasi kikubwa cha fedha n.k! Kisha akimaliza hapo anageukia kuwatafiti wafanyakazi wa benki husika… Hapa alitafiti kuhusu ‘shifti’ zao za kazini, nani teller, nani ni meneja na pia kitu kingine cha msingi alijitahidi kuwasoma wadhifa wao.

Baada ya kumaliza kufanya tafiti zake, Carl alikwenda hatua ya pili ya maandalizi, ambapo ilikuwa ni kuandaa ‘makazi na stoo’ yake ya muda katika msitu uliopo karibu na benki, ambapo alichimba handaki dogo kwa ustadi mkubwa na kulificha kabisa kwa juu mtu asiweze kujua kwa namna yoyote ile. Moja ya wapelelezi ambao walihusika kufanikisha kumkamata Carl anaeleza Carl anaeleza kuwa, siku ambayo walifanikiwa kugundua na kuliona handaki mojawapo ambalo lilichimbwa na Carl walistaajabu (kumbuka Carl alikuwa na zaidi ya mahandaki 30 sehemu tofauti tofauti za nchi ya Marekani)! Inaelezwa kuwa, kinachostaajabisha kuhusu mahandaki ya Carl ni jinsi yalivyochimbwa kiustadi na kujengewa kwa ndani kwa vitofali vidogo vidogo. Pia handaki lilikuwa lina mpangilio wa hali ya juu wa kiwango cha kijeshi (military precision). Ndani ya handaki kulikuwa na kila kitu ambacho angekihitaji, silaha, nyaraka za ‘research’, kifurushi cha kujikimu (survival kit), madawa ya dharura (first aid kit), vinyago vya kuficha sura (masks), fedha taslimu, majarida ya mazoezi ya kawaida na kijeshi na vitu vingine vingi..

Baada ya kumaliza maandalizi haya ya msingi, Carl alijichimbia katika maktaba ya umma ya Philadelphia ambako ndiko alipafanya kama ofisi yake, kwani inaelezwa kuwa, alikuwa na mazoea ya kutumia muda mwingi hapo akifanya tafiti na angekuwa hapo kwa wiki kadhaa ili kumalizia mpango wake na kufanya hitimisho la jinsi atakavyotekeleza tukio lenyewe. Itaendelea wiki ijayo.