Home Makala CCM INAWEZA KUOKOLEWA NA MBINU KUNGUNI

CCM INAWEZA KUOKOLEWA NA MBINU KUNGUNI

800
0
SHARE

NA GORDON KALULUNGA


NIMESHUHUDIA mabadiliko makubwa ndani ya Taifa ambayo yanalenga ama kua demokrasia au vyama vya siasa ili kuimarisha vyama hivyo ili viwe na mfumo wa kiserikali yaani mfumo dola.

Katika hali ya kawaida na mazoea, hakuna hata mtu mmoja ambaye huwa anaenda kuomba kazi katika ngazi yoyote mahala popote serikalini kwa vigelegele, nderemo na vifijo huku akiwa amewafungisha washangiliaji vibwebwe ambao wanakuwa na tambo za kila aina na madaha.

Iwe halmashauri, kwenye kampuni, mashirika ya Serikali ama mashirika Binafsi, hakuna anayekwenda kwa shangwe za aina yoyote hata yule mwenye uhakika wa kupata kazi huwa anaishia kutabasamu na kushangilia moyoni.

Ni kwenye mfumo wa vyama vya siasa pekee ndiko burudani na mambo yafananayo na burudani huwa yanajitokeza kwa nia ya kushamirisha vyama vya siasa na kuonekana ukubwa, ukomavu na uvumilivu wa wanaohitaji kuwemo katika mfumo huo wa siasa.

Tumeshuhudia miaka kadhaa ya chaguzi za uongozi ndani ya vyama vya Siasa, ambapo baadhi ya waliokuwa wakihitaji kuwa viongozi wakawa wanachambana kwa utani wa siasa na kukaa pamoja, huku bendera za vyama vyao zikipeperushwa kwa ustadi mkubwa.

Mwaka huu wa uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaendelea huku wajumbe waliochukua fomu za uchaguzi wakionywa vikali kwenda na wafuasi wao na kutoa pesa kwa viongozi wa chama hicho.

Nakipongeza sana chama hicho kwa uamuzi wa kupiga marufuku uchukuaji wa fomu kwa kuzinunua kwa makatibu wa jumuiya zake na ngazi ya chama wilaya, mkoa na hata Taifa.

Jambo hilo ni kubwa hasa kwa wanachama wasio na ukwasi wa fedha na jambo hilo limeleta nidhamu ya wanachama wa chama hicho kujiona wako sawa mbele ya chama na bila shaka chama hicho kinaweza kupata viongozi wazuri kwa chama chenyewe na jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Naamini hata wajumbe wa mikutano husika watachagua viongozi na wala hawatachagua wafadhili wa chama hicho kinachojipambanua kuwa ni chama cha ukombozi kusini mwa bara la Afrika katika njia au mfumo wa ujamaa na kujitegemea.

Shaka yangu inakuja katika suala la pili la kukataza wagombea kujishangilia wenyewe kabla ya kura yaani kwenda kuchukua fomu na kushangilia au kutangaza kuwa wamechukua fomu za kuomba nafasi za uongozi.

Chama cha siasa utamu wake ni pamoja na shamrashamra ili jamii ijue uwepo wa chama chenyewe na hali hiyo inaleta hamasa kubwa kwa wanachama wengine wasio wagombea na baadhi kujua kuwa kuna kitu kinaendelea.

Nina uhakika kwa utaratibu huu wa sasa wa iitwayo CCM Mpya, Tanzania Mpya ambayo mambo ni kimyakimya, umewanyima baadhi ya wanachama kujua hata kama kuna uchaguzi wa ndani ya chama unaendelea.

Naamini kuwa baadhi watahitaji kuwania nafasi hizo wakati utaratibu wa uchukuaji wa fomu umemalizika na yawezekana baadhi wataanza kushtuka wakisoma makala haya, hivyo hao wasubiri uchaguzi mwingine mwaka 2022.

Siamini kama chama hicho kinataka kujirudisha katika enzi za zidumu fikra za mwenyekiti ndani ya kizazi cha kuhoji.

Siamini kama tunaweza kuwaambia Watanzania wavae magome ya miti ndani ya utandawazi huu ingawa simaanishi kuwa haiwezekani, maana watatii na machozi yao kupotea kama samaki majini.

Lakini naamini chama hicho kinataka kufanya kazi zake mithili ya mdudu kunguni na mambo yake ya kushtukiza na kuumiza kisha akikuumiza huwezi kumtambua.

Kunguni akivamia mahala huwa anamng’ata mtu kisha anakimbia kwa kasi kwenda kujificha.

Kwa waliowahi kung’atwa na kunguni wanafahamu jinsi mdudu huyo alivyo mahiri wa mashambulizi kwa binadamu na bingwa wa mbio za kujificha bila kelele.

Lakini najiuliza kuwa je, mfumo huu utawapa fursa wanachama wote wa chama hicho wanaofaa na hata wasiofaa kuwa viongozi? Maana ushahidi upo kuwa ngazi nyingi uchaguzi hautangazwi na kuwafikia wanachama wengi.

Kwa maana hiyo wengi wa wagombea hasa ngazi za nafasi kubwa za wilaya, mikoa na Taifa wanaweza kuwa wanatoka katika makundi yasiyozidi matatu.

Makundi hayo ni pamoja na wanachama wenye fedha, wanachama wanaoishi katika miji na wanachama maarufu.

Najua hapa linaweza kutokea jibu kuwa chama hicho kina uwanja mpana wa mawasiliano kutoka ngazi ya Shina, Tawi, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa.

Jibu hilo ni zuri sana lakini kuna mwimbaji mmoja aliwahi kumwambia mjomba wake kuwa wachunguze watu uliosimama nao……

CCM inaweza kuokolewa na mbinu hii ya kunguni, pia inaweza kuipunguzia mwonekano kama chama cha siasa kwa baadhi ya wanachama na walio nje ya chama kwa kuonekana kama chama dola.