Home Uhondo wa Siasa ‘CCM NI CHAMA CHA WATU SI CHA MTU’

‘CCM NI CHAMA CHA WATU SI CHA MTU’

1884
0
SHARE

Na Victor Makinda

“Chama cha Mapinduzi (CCM),  kimejengwa katika misingi ya kujitegemeza kwa watu ambao ni wanachama wote na sio mtu mmoja au kikundi cha watu kwa maslahi binafsi. Hiki ni chama cha Watu na sio mtu. Tangia kuasisiwa kwake CCM kimekuwa na msingi imara wa kukubalika na kutenda kadiri ya watu watakavyo na sio mtu atakavyo. Hivi karibu CCM, ilitaka kugengeuka. Ilitaka kuacha misingi ya kuwepo kuasisiwa kwake,ilivamiwa na wachache waliolenga kukiyumbisha chama wakidhani kuwa wao wana nguvu kuliko chama ikiwa ni kinyume chake.

Kuna kundi la watu lilitaka kuteka chama na kukigeuza kutoka kuwa chama cha wanachama wote na kuwa chama cha wanachama  wa kundi fulani kwa maslahi yao. Chama kimeliona hilo. Tumepambana na tutazidi kupambana kuhakikisha tunaondoa na kuwaondoa wote wenye dhamira mbaya juu ya chama hiki adhimu.”  Anaanza kuzungumza katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro, Kulwa Omar Milonge  alipozungumza na Rai ofisini kwake mjini Morogoro kuhusu tathimini ya uchaguzi wa chama hicho kwa ngazi ya Mashina, Tawi, kata na Wilaya uliokamili siku chache zilizopita.

Milonge anasema kuwa katika uchaguzi huo wa viongozi wa chama kwa ngazi za mashina, tawi, kata na wilaya, chama  kilihakikisha kuwa kinaondoa malmuki wote ili kukisafisha chama na kubaki na viongozi ambao ni wanachama kweli na sio wanachama mapopo ambao hawajulikani mchana huwa CCM na usiku huwa upinzani.

“ Nakili kuwa uchaguzi mkuu  wa mwaka 2015 ulikiacha chama kikiwa na makovu makubwa. Chama kilikuwa na mamluki wengi waliosalia chamani. Kuna methali moja ya Kiswahili inasema, ukimfukuza mwendawazimu, mtupie na mizigo yake.  Kuna baadhi ya watu walikuwa kama wendawazimu chamani. Haiwezekani mtu uwe mwanachama wa CCM halafu upigie debe upinzani. Mkoani Morogoro, tulichokifanya hatukuwapa nafasi wasaliti hao. Tumewaengua wao na wapambe wao. Tumehakikisha tunapata viongozi ambao ni kweli wanachama wafia chama. Chama sasa kipo salama katika ngazi hizo ambazo tayari uchaguzi umefanyika.” Anasema Milonge.

Akizungumza kuhusu rushwa na malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye chaguzi za chama zilizopita kuhusu matumizi makubwa ya rushwa kwa mintaarafu ya kuwarubuni wapiga kura, Milonge anasema kuwa rushwa imethitibi wa kiwango kikubwa katika uchaguzi wa chama ndani ya mkoa wa Morogoro.

“ Mimi ndiye mkurugenzi wa uchaguzi wa mkoa wa Morogoro kwa ngazi ya Chama. Chama kimefanya uchaguzi wa kihistori ndani ya chama na katika jumuiya za kichama.  Hapa naiongelea UVCCM, UWT NA Jumuiya wa Wazazi CCM.Kama yapo malalamiko ni ya kawaida na ni kawaida  dosari ndogo ngodo kujitokeza baadhi ya maeneo. Ni hii ni kawaida. Hakuna kinachofanywa na kukamilika kwa asilimia mia. Lakini nachoweza kusema kuwa CCM, mkoa wa Maorogoro imefanya uchaguzi safi safi sana. Hakukuwa na hapatokuwa na Rushwa. Na kuthibitisha hili nimetoa vyeti vya pongezi kwa Makatibu wa CCM wilaya zote za mkoa wa Morogoro. Nimetoa vyeti hivyo kuwatambua, kuwashukuru na kuwapongeza kwa jinsi ambavyo wameweza kusimamia uchaguzi huu kwa kiwango kilichotukuka. Sisi CCM  mkoa wa Morogoro lengo letu kubwa katika uchaguzi huu ni kuhakikisha kwanza hatumpi malmuki kuwa kiongozi, na pili ni kuhakikisha kuwa kiongozi mtoa rushwa na asiye na sifa za uongozi hapati nafasi kukiongoza chama. Ni kweli tumethibiti haswa na tumefanikiwa hilo.

Wote waliodhani wanaweza kujipenyeza kwa njia za rushwa na umamluki, tumewatupa nje wote waliokuwa na dhamira chafu. Shukrani nyingine ziende kwa Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa  nmana walivyohakikisha kuwa wanazuia mazingira yoyote ya kutoa na kupokea rushwa. Unajua rushwa ni adua wa haki, Mwana CCM, anapaswa kuiimba ahadi hii ya TANU, mama wa CCM kuwa Rushwa ni adui wa haki, na akatae kutoa wala kupokea Rushwa. Ni kwa maslahi mapana ya Taifa na Tanzania.

CCM ndio chama kinachotekeleza ilani yake kwa sasa. Ni baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu uliopita. Sasa unapokuwa na viongozi ndani ya chama ambao ni watoa na wapoekea rushwa, chama kitayumba na serikali itayumba. Bla CCM imara hakuna serikali imara.CCM imara inatoka na chama kuwa na viongozi wasafi wasiotokana na rushwa ili waweze kuisimamia serikaliyao na kuishauri kikamilifu kutekeleza ilani ya chama.” Anaongeza kusema Katibu wa CCMmkoa wa Morogoro Kulwa Omar Milonge.

KUHUSU MAJIMBO YANAYOTAWALIWA NA UPINZANI

Milonge anasema kuwa kama kuna kitu kinachomnyima raha na usingizi basi ni kuona kuwa mkoa wa Maorogoro una majimbo matatu yanayotawaliwa na wabunge wa Chama pinzanii.

“Sipati usingizi. Nawaza namna tunavyoweza kuyakomboa majimbo ya Mlimba, Kilombero na Mikumi. Majimbo haya yapo mikononi mwa chama pinzani Chadema. Chama tumefanya tafiti na kubaini kwa nini Chadema walishinda katika majimbo haya. Zipo sababu nyingi zilizowafanya washinde. Kubwa ni usaliti wa wana CCM wenyewe. Tumedhibiti na tunaendelea kudhibiti wasaliti ili majimbo haya yawe rahisi kuyakomboa. Nakuhakikishia ndugu mwandishi tutayakomboa majimbo haya iwe isiwe kwani kama chama tumejipanga kikamilifu. Siwezi kuuza mbinu za vita ila Kilombero, Mikumi na Mlimba ni majimbo yatakayorejea CCM iwe isiwe, kwani naumia kuona katika mkoa wangu kunakuwa na majimbo yanaoongozwa na wapinzani. Na hii sio majimbo tu hata kata, vijiji na vitongoji vyote vilivyo upinzani tutavirejesha CCM. Tunachokifanya kwa sasa ni kutekeleza ilani ya chama kwa wananchi wa majimbo hayo na maeneo mengine ili kama imani yao iliondoka kwa CCM, irudi.” Anaongeza Milonge.

Kuhusu Rais Magufuli kuongezewa Muda wa kuongoza

Milonge anasema kitendo cha watu mbali mbali  kusema kuwa Rais Dr John Pombe Magufuli aongezewe muda wa utawala kabla hata kipindi chake cha miaka mitano kwisha na kipindi cha miaka mitano mingine kwisha, ni kumchanganya Rais wetu.

“Ni kweli Rais Dr John Pombe Maguli, uongozi wake unatenda miujiza mingi. Nasema miujiza kwa sababu hatujawahi  kuwa na awamu ya uongozi iliyo imara madhubuti kama hii. Kwa kipindi kirefu tulikuwa  na viongozi ambao hawakuwa wakali na wenye kusimamia rasilimali za Taifa kwa uchungu kama kipindi hiki cha awamu ya tano. Rais Magufuli, amejitoa muhanga, hamtazami mtu usoni, hana urafikia na yoyote wala hamlindi mtu pale penye maslahi ya Taifa. Ni nadra sana kumpata kiongozi wa Kiafrika mwenye moyo wa uzalendo kwa nchi yake na wananchi wake wanyonge mfano wa Rais Magufuli.  Watanzania tumepata bahati ya pekee kumpata Magufuli.

Lakini kujadili kumwongezea muda kabla ya muda wake kwisha ni kumchanganya Rais wetu. Tumwache afanye kazi yake. Matokeo ya kazi yake ndiyo yatakayoamua kuwa anafaa kuuendelea baada ya muda wake kwisha  au lah, kwani muda huwa unasema. Tuuache muda useme na tusijaribu kuchokonyoa na kunyofoa vifungu vya katiba kwa lengo la kumuongezea muda rais.Hii inaweza kuleta mgogoro wa kikatiba na hata machafuko. Tumwache rais wetu mpendwa, kipenzi cha watanzania atimize nadhiri yake.  Nikimwangalia usoni Rais Magufuli huo ninaiona Tanzania mpya. Nauona uso wa uzalendo wenye uchungu na uchu wa maendeleo ya wanyonge. Tusimchanganye, nasema tusimchanganye kwa kumtoa kwenye reli yake. Acha aendelee kutenda miujiza. Rais huyu atatuvusha na kutupeleka nchi ya Maziwa na asali. Dalili zote njema zinaonekana. Anasema Kulwa Omary Milonge, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro.

KUHUSU MATUKIO YA KIHALIFU

Milonge anaionya jamii ya Kitanzania kuwa makini sana na watu ambao wana malengo ya kutugombanisha. Anasema kuwa mwenenedo wa Taifa letu kwa sasa unatishia watu na mataifa yenye husuda na kasi yetu ya maendeleo. Amani yetu inaonewa tamaa. Vita ya kiuchumi tunayopigana chini ya Jemedari wetu, John Pombe Magufuli na kushinda inawafanya mabepari na watu wasiopenda maendeleo yetu kututazama kwa jicho la husuda. Anasema hawa wapo tayari kufanya lolote ili kutugombanisha na kutusambaratisha. Kama Taifa tunapaswa kuwa makini sana.

“ Mtu yoyote ambaye anaonesha dalili za uchochezi na uvunjifu wa amani, huyu ashughulikiwe kwa nguvu zote. Amani yetu ni tunu yetu kutoka kwa Mungu, tuitunze sana. Haya matukio ya watu kuvamiwa yanapaswa kuchunguzwa kwa kina na kuyapatia majibu yake. Tanzania tuna vyombo imara vya dola. Tuna imani navyo sana, bado nchi yetu ipo salama na matukio haya machache yasitufanye tufarakane. Nchi hii chini ya uongozi mahiri wa CCM ni salama sana. Anamaliza kusema Kulwa Omar Milonge.