Home Makala CCM NI LAZIMA KITETEE NGUVU ZAKE DHIDI YA SERIKALI

CCM NI LAZIMA KITETEE NGUVU ZAKE DHIDI YA SERIKALI

1046
0
SHARE

LUQMAN MALOTO,

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo chama kinachoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Msingi huo ni kuwa wanachama walioaminiwa na CCM ndiyo marais wa Serikali hizo.

Jamhuri ya Tanzania ni dola yenye mihimili mitatu, Serikali, Bunge na Mahakama. Serikali inaongozwa na CCM kupitia mwanachama wao ambaye walimpa tiketi ya kugombea urais na kushinda.

Bunge ambao ni mhimili wa dola wa utungaji wa sheria na wenye kuisimamia Serikali, kwa theluthi mbili wajumbe wake ni CCM ambao walichaguliwa kuwa wabunge katika majimbo yao, vilevile viti maalum na zile nafasi za uteuzi.

Mahakama ni mhimili wa dola ambao nafasi zake hujazwa kitaaluma. Hautakiwi kuonekana una sura ya u-CCM wala chama kingine chochote. Majukumu yote ya kutafsiri sheria na kutoa haki, yamekasimishwa kwa Mahakama.

Serikali ndiyo mhimili wa dola wenye kuhusika na utawala wa nchi (executive). Rais ndiye mkuu wa Serikali, anapochaguliwa hujaza nafasi nyingine zote kwa kuteua wasaidizi wake kwenye nafasi mbalimbali.

Baada ya Rais, ndani ya Serikali hakuna mwingine ambaye huchaguliwa na wananchi. Wote huteuliwa na Rais, hata watendaji wa Serikali kama makatibu wakuu wa wizara na wasaidizi wao, wakurugenzi, makatibu tawala wa mikoa na wilaya na kadhalika, Rais huteua.

Kwa mantiki hiyo Rais anapochaguliwa anakuwa na mamlaka yote ya kiutawala. Ndiyo maana likatungwa Bunge ili kuisimamia na kuidhibiti Serikali. Unapozungumzia kuisimamia na kuidhibiti Serikali, maana yake ni pamoja na kumsimamia na kumdhibiti Rais.

MAMLAKA YA CCM

CCM kama chama hakipaswi kuonekana kikichomoza serikalini na kutoa maagizo, huo siyo utaratibu. Rais anapochaguliwa anakuwa mali ya wananchi wote, CCM, vyama vingine na hata wale wasio na vyama.

Hata hivyo, Rais anapaswa kuwa mtiifu na mnyenyekevu kwa CCM kwa sababu ndicho chama ambacho kilimpa tiketi ya kugombea, kikamfanyia kampeni na kumwezesha kushinda.

CCM kinatakiwa kiwe chama chenye nguvu ya kumwita Rais kama kinaona anakwenda nje ya mstari na kumpa mwongozo. Kiwe na mamlaka yenye nguvu ya kumshinikiza Rais kupangua hata Baraza la Mawaziri kama chama kinaona kuna watu wanachelewesha matarajio ya wananchi.

CCM kinatakiwa kiwe na nguvu ya kumkalisha chini Rais na kumweleza kuwa anachokifanya kipo nje ya Ilani ambayo waliitumia kumuombea kura kwenye uchaguzi.

Vilevile kiwe na sauti ya kumshurutisha atekeleze Ilani. Naye ahofie, maana akicheza anaweza kunyimwa tiketi katika muhula wa pili.

CCM kama chama kina misingi yake na viongozi wa chama hasa wajumbe wa sekretarieti, wanapaswa kuwa viranja wenye kuifuatilia Serikali inayotokana na chama chao, kuona kama inaongoza nchi kwa misingi yake.

Ukisoma sehemu ya kwanza ya Katiba ya CCM, palipo na Jina, Imani na Madhumuni.

Mfano yale madhumumi ya 15, kwamba CCM inahitaji kuona kuwa Serikali na vyombo vyote vya umma, vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wanawake na wanaume, bila kujali rangi, kabila, dinia au hali ya mtu.

Katika eneo hilo, siku akitokea Rais ambaye atakuwa mbaguzi, anafanya uteuzi wa nafasi za Serikali pamoja na mashirika ya umma kwa kuzingatia ukabila, udini, ukanda, jinsia na kadhalika, je, CCM inaweza kumwita, kumweka chini na kumpa muongozo wa kufuata Katiba ya chama chao?

CCM INAPOJIONDOLEA MENO

Ukiisoma Katiba ya CCM, unaona kuwa chama kimejipa meno ya kuwa kiranja wa Serikali inayoongozwa kwa tiketi yake. Hata hivyo, meno hayo yanaondoka kutokana na muundo wake wa kiuongozi.

CCM ndiyo chama ambacho kinaongoza Serikali na Bunge kwa sasa. Hivi sasa, mbunge akitaka kukiona cha mtema kuni basi afanye mambo yenye kukipaka matope chama au awakosee adabu viongozi wa chama.

Ni rahisi mno mbunge wa CCM kufukuzwa uanachama kama ataonekana anafanya mambo ambayo kwa namna moja au nyingine hayawafurahishi viongozi wa chama chake.

CCM imeweka utaratibu mzuri wa vikao vyake. Mathalan, ndani ya Bunge kuna vikao vya kamati ya wabunge wa chama hicho (CCM caucus). Malengo yake ni kujenga sauti ya pamoja katika utetezi wa maslahi ya nchi, kulinda maslahi ya chama chao kwa misingi yake na Ilani, vilevile kuitetea Serikali ya CCM.

Utetezi wa Serikali yenye tiketi ya CCM ni jambo la mwisho baada ya maslahi ya nchi pamoja na yale ya chama chao. Utaona kuwa CCM kuwa na wabunge wengi, maana yake kinakuwa na nguvu kubwa dhidi ya utawala (Serikali).

Pamoja na ukweli kuwa CCM kama chama hakina uwezo wa kumwondoa madarakani Rais hata kama kitamvua uanachama, bado kina uwezo kupitia mtaji wake wa wabunge wengi.

Bunge kupitia Ibara ya 46A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limepewa mamlaka ya kumwondoa Rais madarakani kwa kumshitaki ndani ya Bunge kisha mashitaka hayo kupata uhalali wa kikatiba.

Kwa mantiki hiyo, CCM ni chama chenye nguvu kilicho na mamlaka ya kumtikisa Rais. Hata hivyo, muundo wake wa uongozi unafanya chama hicho kikose meno ambayo kinapaswa kuwa nayo.

KWA NINI CCM HAKINA MENO?

Sababu ni mfumo wake wa uongozi. Rais ndiye mkuu wa utawala (Serikali) kisha utaratibu wao ni kumfanya Rais anayetokana na CCM kuwa mwenyekiti wa chama.

Kwa msingi huo, kiongozi wa chama ambaye angepaswa kuwa wa kwanza kuhoji mwenendo wa Serikali ndiye mkuu wa chama. Inawezekana vipi mtu ajihoji mwenyewe kuhusu mwenendo wake wa kiuongozi?

Sekretarieti ambayo imekasimishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), majukumu ya utendaji wa shughuli za kila siku za chama, wajumbe wake wote wanateuliwa na mwenyekiti wa chama kisha kuthibitishwa na wajumbe wa Nec.

Mwenyekiti ambaye ndiye huteua watendaji wa chama ndiye huyo ambaye ni mkuu wa Serikali. Nani mwenye nguvu kuanza kuhoji utendaji wa Serikali?

Muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne, Katibu Mkuu wa CCM ambaye ndiye mwenyekiti wa sekretarieti, Abdulrahman Kinana, aliongoza timu yake kufanya mikutano wakitaja mawaziri ambao walikuwa mizigo.

Nguvu ya Kinana iliishia kuzungumza kwenye mikutano na kuwadhalilisha mawaziri husika lakini yeye kama mtendaji mkuu wa chama hakufanya chochote. Maana ndani ya chama anafanya kazi chini ya mtu ambaye ndiye bosi wa aliowalalamikia.

Rais Jakaya Kikwete ndiye alikuwa Mkuu wa Serikali, vilevile mwenyekiti wa chama. Kwa maana hiyo, alipoona mtu wa chama anamlaumu waziri wa Serikali, alitafsiri kuwa wasaidizi wake walikuwa wakishtumiana.

Profesa Jumanne Magembe aliitwa waziri mzigo alipokuwa anaongoza Wizara ya Maji, alimaliza salama na Rais Kikwete na sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii chini ya Rais John Magufuli. Kinana bado Katibu Mkuu CCM.

Wabunge wa CCM hawawezi kuiwajibisha Serikali wakati mwenyekiti wa kamati yao ni Waziri Mkuu ambaye ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za Serikali.

CCM KINAJIHARIBIA CHENYEWE

Mfumo wa kumfanya Rais wa nchi kuwa mwenyekiti wao ni mbaya. Unakiharibia zaidi chama kisha unamlinda Rais. Hii ni kwa sababu makosa yote ya Serikali yanaelekezwa moja kwa moja kwenye chama.

Kama chama kingeweza kutenganisha uongozi wake na ule wa Serikali, ingewezekana pale kinapoona mambo hayapo sawa, na chenyewe kinaisema Serikali au kutishia kumvua Rais uanachama.

Mwaka 2004, chama cha United Democratic Front (UDF) cha Malawi, kilipoona Rais Bingu wa Mutharika anakwenda nje ya misingi yao, walimbana mpaka ikabidi aanzishe chama chake cha Democratic Progressive (DPP), uchaguzi uliofuata aligombea kwa chama kingine.

UDF waliweza kwa sababu Bingu hakuwa kiongozi wa chama. Hata ANC Afrika Kusini, walimwondoa Thabo Mbeki madarakani baada ya kufanikiwa kumng’oa kwenye uongozi wa chama mwaka 2007, kisha Jacob Zuma akawa Rais wa ANC.

CCM ikijifanyia masahihisho kwa kutenganisha uongozi wa chama na Serikali, itaweza kutetea nguvu zake kama chama tawala. Kwa sasa kwa hali iliyopo ni chama tawala kwa sababu Serikali inaundwa na wanachama wake lakini hakina nguvu kama chama kufanya mageuzi serikalini hata kwa kupitia bungeni.