Home Habari CCM: Wananchi wanatufuata wenyewe

CCM: Wananchi wanatufuata wenyewe

490
0
SHARE*Polepole aipa mbinu Chadema

GABRIEL MUSHI

CHAMA Cha Mapinduzi kimesema hakifanyi mikutano ya hadhara kama inavyodaiwa na upinzani bali wananchi huwafuata viongozi wa chama hicho pindi wanapofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. RAI linaripoti.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole wakati akijibu maswali ya baadhi ya watu kwenye moja ya mitandao ya kijamii, ambapo pamoja na mambo mengine amebainisha tafsiri tatu zinazowasababisha wapinzani kuhisi CCM inafanya mikutano ya hadhara.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ya wanachama wa kundi la mtandao wa kijamii wa Whatsap la ‘Kanda ya Kaskazini’, Polepole mbali na kusema wananchi huwafuata, pia alisema chama hicho hufanya mikutano ya ndani na si ya hadhara.

“Si la kweli, ni uongo, ningependa watu wote wapuuze uongo huu. Hii inaonesha udhaifu wa upinzani na sasa unatafuta huruma hata kwa mambo ambayo hayana tija, tumekubaliana kuwa baada ya uchaguzi uwe muda wa kufanya kazi”, alisema.

Alisema imekuwa ikizoeleka kuwa baada ya uchaguzi ni vurumai za uchaguzi mpaka uchaguzi mwingine unapowadia jambo ambalo anajiuliza wananchi watakula vurumai za uchaguzi bila kufanya kazi au lah!

Alisema Rais John Magufuli alieleza kimsingi hoja ya kuzuia mikutano ya hadhara na kuweka utaratibu mzuri, kwamba kila mwenye eneo lake ashirikiane na wananchi wake kuleta maendeleo.

“Tulipokuwa tumefikia ni kwamba mbunge fulani anakwenda kwenye jimbo la mbunge mwingine kumtukana. Ile ni vurumai… ndio maana tukasema Mbowe afanye mikutano kwenye jimbo lake la Hai, Mwaka 2017 Julai nimekwenda Hai kimyakimya maana hatuna jimbo kule, tangu achaguliwe 2015 hajawahi kufanya mkutano wa hadhara.

 “Niliwahi kumuuliza ana kwa ana akachenga, badala yake akaniambia ana namna nyingi za kuzungumza na watu wake. Nikamwambia kama una namna nyingi za kuzungumza na watu wa Hai, kwanini unalazimisha kufanyike mikutano ya hadhara?,” alihoji.

Alisema CCM haifanyi mikutano ya hadhara, inafanya mikutano ya ndani kama ambavyo Chadema inafanya mikutano ya ndani.

“Tunafuatilia kila kitu ndugu zetu wanachofanya. Sisi tuna ofisi na uwanja, wao hawana.Tumejenga na kuwekeza, Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Karatu, Ngorongoro kila mahala tumewekeza ofisi na uwanja, sasa tunajenga Longido  kwenye maeneo yetu.

“Juzi tulikuwa na mkutano mkubwa wa ndani pale Karatu lakini picha ikipigwa inaonekana mkutano wa hadhara. Lakini ukweli ni kwamba upo ndani ya eneo la CCM na geti lipo. Na huwezi kuja hivihivi lazima uje kwa mwaliko,” alisema.

Aliongeza kuwa yeye na viongozi wenzake  wamepewa dhamana ya kusimamia serikali, hivyo wanafuatilia miradi ya maendeleo inavyofanyika kwa sababu awamu zilizopita CCM iliwaachia viongozi wa serikali kufuatilia na kusimamia miradi hiyo ila wakaharibu.

“Tumeona sasa hivi tuende tukasimamie wenyewe. Kwa mfano mimi kiongozi wa kitaifa nikienda pale Longido kuna daraja linaitwa ‘korongo la wazee’, nimeenda kukagua mradi huu ili kujua mkandarasi anamaliza lini, je, muda tulioweka atamaliza? Kama hamalizi tutoe maelekezo gani kwa waziri husika. Sasa nikienda pale wananchi wanakuja darajani wanasema tuna kero za wafugaji na vitu kama hivyo. Sasa huwezi kuzuia.

“Nimetoka hapo nimeenda kwenye soko la kimataifa la mifugo, sisi tumeandika katika ibara ya 25, fungu la 25 la ilani ya CCM kifungu J, inazungumzia kuhusu masoko ya bidhaa za mifugo, nikifika hapo kusikiliza kero za wafugaji kwa sababu soko lile linatakiwa lifanye biashara litoe pesa nyingi na gawio kwa serikali… ukifika pale wafugaji wote wanakuja sokoni sehemu ulipo, huo unaita ni mkutano wa hadhara?

“Ule sio mkutano hadhara ni wananchi wanajua sehemu mbili ambazo wanaweza kupeleka kero zao, kwenye ofisi ya serikali na CCM. Ukipeleka ofisi ya serikali itafanyiwa kazi, isipofanyikwa kazi nenda CCM, ukipeleka CCM sisi ni wazee wa kuanua, lazima itafanyiwa kazi. Ndicho ambacho wananchi wanatufuata lakini si kwamba tumekwenda kuandaa mkutano wa hadhara hiyo si kweli,” alisema. Endelea kusoma mahojiano hayo maalumu…

SWALI: Polepole wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ‘Tume ya Warioba’ na huyu wa CCM ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, wamekuwa vitu viwili tofauti. Je, msimamo wako wa sasa kuhusu katiba mpya umebadilika?

POLEPOLE: Hapana Polepole huyu ni yuleyule hakuna tofauti… kilichobadilika ni dhamana tu, ila misingi na misimamo imebaki vilevile. Misimamo ya miaka 10 iliyopita nitabaki nayo pia. Unatakiwa kufahamu kuwa kipindi kile nilikuwa Kamishna wa tume ya katiba, mchakato kwa mujibu wa sheria umeahirishwa, utakapoanzishwa tena kwa kuwa ni sehemu ya viongozi wa CCM nitashirikiana na wenzangu kwa kuwa ninafahamu viongozi wa CCM wana dhamira njema  na wanafahamu umuhimu wa masuala haya kwa Taifa letu.

Ila kupanga ni kuchagua ni vizuri kufahamu kwanini tulikwama, bahati mbaya watu wengi hawatafakari kwanini tulikwama wanajikita katika mkwamo wenyewe. Anachofanya Rais Magufuli ni kurejesha nidhamu ya viongozi ambayo sio siri kipindi fulani ilitetereka, unapozungumzia tukio la Katiba mpya lazima uwe na viongozi ambao sio wabinafsi, weledi na wanyenyekevu kiasi kwamba tunapozungumza masuala ya kitaifa hawaweki mikono yao.

Neno kama ‘ananyoosha nchi’, ni mifano ya lugha inayoakisi uhalisi fulani, tunajaribu kuhakikisha tuna viongozi waaminifu, wanaochukizwa na rushwa, sio wabinafsi, hayo yote ninasimamia, nimepewa heshima kubwa na timu hii inayofanya kazi ya kuturejeshea misingi ambayo chama chetu kilianzishwa.

Misimamo yangu inafanana kabisa na misimamo ambayo  tangu awali imenasibishwa na uhai wa CCM.

SWALI: Maendeleo ni ya watu na vitu, tunajivuniaje vitu wakati maisha ya watu wa kawaida yanazidi kuwa duni?

POLEPOLE: Si kweli, katika shahada yangu nimesomea maendeleo, huwezi kutenganisha maendeleo ya vitu na maendeleo ya watu. Unatakiwa kufahamu kimantiki ni kama mfano wa kuku na yai, ila lazima utaanza na kuku kwanza… kwamba alitaga yai. Kwa hiyo lazima uamue kuwekeza kotekote katika kupiga hatua au kuanza uwekezaji mkubwa katika eneo moja.

Huwezi kupiga hatua ya maendeleo ya kijamii kama huna miundombinu ya vitu, madarasa ya shule, barabara za kufika vijijini, huna watalaam wa ugani, vyuo vya ufundi, treni, meli za kupeleka mizigo haraka na bei nafuu sana. Miundombinu ya mawasiliano, hayo yote ni maendeleo  ya vitu.

Ila huwa yanatafsiri katika maendeleo ya watu moja kwa moja, unapokuwa na vyuo utatengeneza walimu na wanafunzi, utapata wataalama wa afya na watu kupata tiba. Hivyo Rais amefanikiwa katika hilo.

Katika uchumi kuna kitu kinaitwa Macro level ecenomy, micro level economy, maendeleo ya vitu yapo kwenye macro level economy yaani uchumi mkubwa, hapa unazungumzia miundombinu mikubwa ya barabara au reli. Ila unaposema micro level economy ni uchumi mdogomdogo kama kuwezesha watu kupata fedha. Lakini watu watapata fedha kwa sababu wamepata ajira katika ujenzi, viwanda, umeme  wa uhakika. Huo ni uchumi jumuishi.

Hata kipindi hiki anayesema maisha yamekuwa magumu si kweli, mtu ambaye alikuwa mpiga dili, alikuwa akipata kipato cha kuungaunga katika njia zisizo halali pale bandarini hawezi kukubali maisha kuwa ni marahisi maana hapigi dili tena. Licha ya wapiga dili kuwa na watu wanaowategemea lakini ni haramu kuwa mnufaika chanya katika mapato haramu. Tunapofanya mageuzi katika nchi wapo watakaoumia katika mnyororo ni wale waliofanikiwa katika njia isiyo halali.

Lakini tukumbukwe kipindi hiki watu wanamaisha mazuri zaidi, watumishi wa serikali wanalipwa mishahara kwa wakati.

Wapinzani wengi wanatabia ya kupiga kelele ila hawafahamu utaratibu, sasa hivi serikali imekuwa ikilipa madeni ya walimu. Halmashauri zenye uwezo mkubwa zimewekewa utaratibu wa kulipa madeni ya ndani. Madai mengi yamekuwa hewa. Hivyo nitoe raia kwa watumishi wa umma kuwa waminifu katika kukokotoa madeni ya walimu.

Mfano mikopo ilikuwa inatolewa kwa asilimia 10, sasa wanapewa fedha za kuazima. Zipo taasisi nyingi za serikali zinatoa fedha kwa asilimia moja. Tanzania ya sasa ipo mifumo ya kuwazuia watu wasiangukie katika umaskini. CHF -bima ya jamii, Tiba kwa kadi na NHIF. 

Pia Rais Magufuli pia amesaidia kaya maskini kulipwa mishahara kila mwisho wa mwezi, miezi miwili miwili kama sehemu ya kuondoa umaskini. Tanzania ni nchi ya kwanza katika kuwasaidia wananchi wake kulipwa na kuondokana na umaskini.

SWALI: Katika Ilani ya CCM, imeahidi  kulinda Watanzania kiusalama. Hata hivyo, hali imekuwa tofauti kwani maiti zilizo kwenye viroba zinaokotwa ufukweni, watu wanapotea, mauaji ya wanasiasa yamekithiri na wengine kujeruhiwa kama vile Tundu Lissu. Je, CCM inajisikiaje kukithiri kwa matukio haya yanayoashiria kushindwa kulinda watu wake bila kujali itikadi?

POLEPOLE: Mambo ya ulinzi na usalama hayapaswi kuwekewa siasa ndani yake. Ulinzi na usalama ndio msingi wa haki kutamalaki na maendeleo kutolewa, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha tunasimama kama walinzi wa amani ya nchi yetu.

Ni bahati mbaya wenzetu hasa wa upinzani wamechukulia masuala ya usalama hasa yanapotetereka kama mtaji wa kisiasa. Ni kitendo kinachokosa uzalendo wa hali ya juu. Kuna vitendo vya kijinai vinavyofanyika duniani kote. Marekani ndio inaongoza kwa raia wake wao kwa wao kuuana kwa silaha.

Tanzania ni nchi ambayo kwa muda mrefu tumekuwa na amani, kumekuwa na matukio machache ya jinai na uhalifu. Haikuwahi kuwa desturi ila dunia inabadilika, hivyo ningeshauri viongozi wa kisiasa wakaketi wakazungumza na kuambiana ni wakati gani wa kufanya siasa na ni wakati gani si wa kufanya siasa, kama kuna watu wamekutwa kwenye viroba ufukweni ni jukumu letu wote kutafakari pamoja kama Taifa, ila kufanya hilo jambo la kisiasa na kuanza kuituhumu serikali ambayo imepewa dhama ya kulinda watu wake ni siasa ya kipumbavu sana.

Ningeshauri wakati mwingine ni vizuri kutizama mambo haya, ameshambuliwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, tayari limeshageuzwa ni jambo la kisiasa. Tena wapo viongozi wanachukulia kama mtaji wa kisiasa, hata yeye mwenyewe aliyeshambuliwa amejigeuza mtaji wa kisiasa na tukio lile ni mtaji wa kisiasa, ni bahati mbaya sana.

 Kwa mfano wamefariki ndugu zetu pale Mkuranga, Kibiti na Rufiji wako viongozi wengine wakuu wamekebehi jitihada za serikali kumaliza tatizo hilo ambalo wengi walipoteza maisha, walikuwa viongozi wa serikali na wa chama tawala. Wakati sikuona viongozi wa upinzani wakisema chochote.

Lakini wao waliweza kuona kuna watu wamepotea, sasa wadhibitishe! Ila wameshindwa kuonesha moyo wa huruma kwa familia zilizopoteza ndugu zao. Mtu aliyepona alikuwa kiongozi wetu kule Rujifi, alipigwa risasi, alijeruhiwa na alitobolewa macho.

Ukizungumza na watu wa Mkuranga wataeleza vizuri, navishukuru sana vyombo vya ulinzi na usalama, kwa kurudisha hali ya usalama. CCM ni chama kongwe na kikubwa kimekuwa na mifumo ya kitaasisi hadi ngazi ya chini ilibidi kusimamisha uchaguzi kwa wilaya tatu za mkoa wa Pwani kwani sisi ndio tulikuwa tunalengwa. Sasa tunatakiwa kutoa msaada wakijamii na kisiaikolojia na tusigeuze jambo hili kuwa la kisiasa.

Polisi wamezuia matukio mengi sana mabaya. Tumeminya baadhi ya watu kimyakimya na tumekata mabomba ya watu kupata msaada pengine. Tunapaswa kuwatia moyo wapiganaji wetu… jeshi  la polisi na vyombo vyote vya dola.

SWALI: Tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani, wapinzani wamekuwa wakilalamika hakuna demokrasia ya kuruhusu uhuru wa upinzani kukosoa, kutokuwapo kwa uhuru huo unaiona hatma ya CCM mbeleni?

POLEPOLE: Nataka kukuhakikishia kwamba hii ni bahati mbayakwa upinzani kipindi hiki kwa sababu ya wakati umebadilika. Ni kama vile wenzetu upinzani walikuwa wamekariri aina ya siasa waliyokuwa wanaifanya. Waliamini kwamba siasa waliyokuwa wakifanya kwamba serikali inakosea kisha unakosoa, sasa amekuja mtu ambaye anafanyia kazi ukosoaji wote uliotolewa hapo awali na kuimarisha nidhamu ya serikalini.

Upinzani wanapaswa wakae chini wajitafakari namna bora ya kuenenda na serikali ambayo inapambana na rushwa, inakuza uchumi, inawezesha watu wake, mbadhirifu anachukuliwa hatua. Serikali ambayo ipo karibu na watu wake.

Upinzani unatakiwa kutafakari kwamba ‘unadeal’ na serikali ambayo haijakubali kupiga magoti kwa wafadhili wakubwa ambao walikuwa wanatufadhili kwa ufedhuli, inatekeleza miradi mikubwa ya kihistoria. Kwa hiyo serikali hii inataka mbinu tofauti ya kushughulika nayo ukiwa sehemu ya upinzani, kwa sababu ukitaka kusema rushwa tumekamata watu kibao wapo ndani. 

Ndio maana upinzani sasa hivi umekosa hoja. Kuna watu fulani nawafahamu na hata watu wa upinzani wanawafahamu, watuhumiwa wa wezi, ufisadi na hawajawekwa ndani… ipo siku haki itatendeka. Watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Wapo waliokamatwa hivi karibuni cha ajabu wapinzani wanawatetea watu wale. Na wanajua walikuwa wakwepa kodi na mambo mengine.

Wapinzani sasa wamebadilika, walisema hatujawahi kujenga reli hata mita moja, leo Magufuli kaonesha jeuri ya kuwa ya kujenga reli ya kisasa, natamani siku moja niwapeleke viongozi wa vyama vya siasa watembelee mradi huu unaofanyika kwa fedha ya ndani.

Wapinzani sasa wana haya. Kwa sababu yale waliyotaka yatendekea yanatendeka sasa. Ndio maana nasema upinzani wa sasa unatakiwa kuwa na mbinu tofauti za kushughulika na CCM ambayo ina viongozi madhubuti.

 Mfano walisema shirika la ndege limekufa, sasa Rais Magufuli amelifufua kwa namna ya kimkakati… amenunua ndege ambazo zinamilikiwa na serikali.  Shirika limerudi mahala pake limezalisha zaidi  pato la jumla zaidi ya bilioni 25. Hatujawahi kuwa na ndege za abiria za kubeba watu zaidi ya 78 kama ilivyo Bombardia, Air bus na Dream Liner. Haya yote wapinzani walitarajia yangekuwa hoja ya kujenga dhidi ya serikali.

Waliwahi kumkosea heshima Rais Kikwete na kusema ni dhaifu, mtu wa kutabasamu tu, mimi nimewahi kufanya kazi chini ya yule mzee, ni mzee madhubuti kwelikweli, nimepata heshima alinipa dhamana ya kuhudumu katika serikali, lakini walimkosea heshima, CCM tukawapatia kitu ambacho watanzania wamekitaka wakati wote, mtu ambaye yupo serious, kutabasamu kuwe kwa timing, mtu asiyesafiri. Lakini nikamshangaa Mbunge wa Mbeya Mjini aliposema rais atoke nje ya nchi abadilishane mawazo na wenzake. Nikamshangaa kwa sababu awali walisema Rais anasafiri sana, amekuwa Vasco dagama.

Nimegundu kabisa upinzani una hali ngumu sana, tumefanya utafiti katika majimbo yote tumebaini una hali mbaya kwa sababu haukuwa umejijenga kitaasisi. Wala haukuwa umejiandaa kupata chama na serikali ambayo inafanya mambo yake kisayansi.

Inatakiwa kuwe na mfumo mpya, kinyume na hapo tutawasafisha na tutawafagia wote, ifikapo 2020 hatutaki kufanya siasa za ubabaishaji, tunataka watu wenye mawazo mbadala.  Niliwahi kuwaambia sera mbadala wakatengeneza sera mbadala, wala hawaelewi sera mbadala, kwa hiyo tumekuwa na upinzani lalamishi. Mtindo huu huwezi kusaidia watanzania.

SWALI: Kwa kuwa wapinzani waliohamia CCM wamedaiwa kuwa wamenunuliwa na chama hicho ikiwamo kupewa madarakani, Je, bado chama kinaendelea kuwapokea na tuhuma hizo unazizungumziaje?

POLEPOLE: Hili ni jambo la kusikitisha sana kwa upinzani kutoa kauli za uongo kwa kiwango hiki. Natoa tu mbinu labda wakitumia wanaweza kupiga hatua kwani bado hali ya upinzani ni mbaya sana, labda wanaweza kupata mtangamano wa kisiasa.

Hakuna anayenunuliwa hata mmoja. Juzi Karatu kuna mtu mmoja tajiri sana maarufu kama ‘Mkubwa’, amekuwa kiongozi wa Chadema, amekuwa kiongozi wa Halmashauri, tumekataa kumpokea, na mwingine kijana alikuwa mwenyekiti wa kijiji, maarufu sana Karatu, alikuwa amedhulumu hekta tatu, akaomba kuja CCM. Tukamkataa na kuwambia CCM sio chaka la kulinda wahalifu, nikamwambia rudisha heka za umma. Watu wameondoka upinzani ni kama Mungu amewapiga upofu, kwa sababu upinzani hakuna chama kuna watu.

Wapinzani waliopo huko, wapo tu kwa sababu ya ubunge na wameshakopa pesa ya ubunge na hawawezi kuondoka na tumewakataa CCM, wanajua jambo hilo. Ukisema wabunge wa upinzani wananunuliwa, watazame Paulina Gekuli, yule mama mchapakazi kwelikweli, Chadema walishamtenga kwa sababu anapenda ukweli. Wapo viongozi wa Chadema ambao masuala ya mashambulio ya aibu wamebobea. Sasa tabia hizi zinakwaza watu.  Hakuna mtu anayenuliwa, wameondoka kwa sababu ya kero za ndani ya vyama vyao.