Home Makala CCM YAREJEA UTAMADUNI ULIOUASI MIONGO MINGI

CCM YAREJEA UTAMADUNI ULIOUASI MIONGO MINGI

646
0
SHARE
Aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT, Sofia Simba.

NA HILAL K SUED


Wiki iliyopita Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilifanya vikao vyake vya juu, ukiwemo Mkutano Mkuu Maalumu kwa ajili ya kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya Katiba yake.

Aidha, katika vikao hivyo chama hicho kikongwe kilitoa maamuzi mazito ambayo hayajawahi kutolewa na chama hicho kwa miongo kadhaa ambapo kiliwafukuza chamani makada wake 11 kwa makosa ya usaliti kwa chama.

Inadaiwa makada hawa walikwenda kinyume na maagizo ya chama wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 wa kumuunga mkono aliyeweka nia kugombea urais Edward Lowassa ambaye jina lake lilikatwa na Kamati Kuu (CCM-CC), bila kufuata Katiba ya chama na kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi kwa wanachama.

Mmoja wa waliofukuzwa, Sophia Simba, alikuwa kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Wanawake (UWT), kitengo nyeti na chenye ushawishi mkubwa hasa katika ufuasi na upigaji kura.

Lakini haya yote yamejiri chini ya uongozi wa chama hicho wa mwenyekiti mpya, Rais John Magufuli ambaye hajaweka siri ya azma yake ya mabadiliko makubwa katika mfumo mzima wa chama na uendeshaji wake.

Kwa ujumla huu ni utamaduni mpya kabisa katika chama ambacho daima kimekuwa kikiwavumilia na kuwalea ‘wapinzani’ wake wa ndani pamoja na wale wanaobeba tuhuma nyingine zikiwemo za jinai. Lakini mabadiliko haya yameanza nyuma kidogo katika Awamu ya Jakaya Kikwete.

Miaka mitatu iliyopita baada ya sakata la vurugu zilizotokea Mtwara kuhusu mustakabali wa gesi asilia iliyogundulika mkoani humo kwa wingi, niliandika makala katika safu hii nikisema Serikali ya CCM ilikuwa imechukua uamuzi wa kihistoria wa kumpeleka mahakamani aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Hasnein Murji, kwa kosa la uchochezi.

Uamuzi ule haukufikiwa kwa uchangamfu mkubwa, nadiriki kusema ulifikiwa kwa shingo upande. Alifikishwa mahakamani zaidi ya miezi minne tangu tarehe ya kutendeka kosa. Kamwe haikuwa kawaida kwa mamlaka zetu zilizo chini ya utawala wa CCM hususan polisi kuchukua muda mrefu hivyo kwa makosa ya aina hii, yaani ya uchochezi.

Hakuna haja ya kubishana katika hili kwani tumeona namna viongozi/wafuasi wa chama kimoja cha upinzani ambao hukamatwa mara moja, hata saa nane ya usiku kwa makosa yanayodaiwa ni ya uchochezi.

Wakati wa enzi za utawala wa chama kimoja, haya mambo hayakuwapo. Vyombo vya sheria na usalama vilikuwa havibagui namna ya kuwashughulikia wahalifu hata waliokuwa viongozi wa chama pamoja na kwamba hakukuwapo vyama vya upinzani. Ilikuwa kitu cha kawaida kwa makada wa chama tawala (TANU/CCM) kukamatwa mara moja na kufikishwa mahakamani kila wanapotenda makosa ya jinai.

Mfano mkubwa ulitokea miaka ya mwanzoni baada ya uhuru kwa aliyekuwa Waziri wa Serikali, Abdallah Saidi Fundikira, kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kupokea rushwa ya Sh 50,000, ambazo ni fedha nyingi sana kwa enzi hizo.

Mfano mwingine ninaoukumbuka ni kukamatwa, kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa jela miaka 12 kwa aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini, Abdurabi Ali Yusuf, mwishoni mwa miaka ya 80 kwa kosa la kukutwa na pembe za ndovu.

Mbali na makosa ya jinai yaliyokuwa yakiwakumba makada wake, chama chenyewe kilikuwa hakiwaonei haya viongozi na makada wake kila wanapokiuka maadili ya uongozi na sheria za nchi.

Mwishoni mwa miaka ya 80 wabunge sita, wakiwemo T. Bakampenja (Ihangiro), S. Kabuga (Mufindi) Wilfrem Mwakitwange (Taifa), R. Choga (Kilolo) na wengineo, walitimuliwa uanachama na hivyo kupoteza ubunge kwa kwenda kinyume na maadili. Kikao kilichowafukuza cha Halmshauri Kuu ya TANU kiliketi Tanga, Oktoba 15, mwaka 1968.

Lakini baada ya ujio wa vyama vingi, chama hicho tawala kimekuwa na uvumilivu wa ajabu kuhusu yote yaliyo hasi katika uongozi wake hasa safu zake za juu. CCM imekuwa ikilea viongozi na makada wa kila aina; mafisadi wanaojulikana, wafanyabiashara ya mihadarati, wakwepaji  kodi, wachakachuaji wa madawa ya binadamu, majangili na wasafirishaji wa nyara za Serikali, waporaji ardhi za watu wengine na hata wasaliti dhidi ya chama chao.

Lakini hawa imekuwa nadra kuguswa na inapotokea dhahiri kwamba ni lazima sheria ichukuwe mkondo wake, basi hili hufanyika kwa shingo upande kwa mhusika kukamatwa lakini baadaye usanii na danadana hufuata na hatimaye hata mashtaka kufutwa bila ya sababu yoyote ya msingi.

Tumeona mwaka jana tu wabunge watatu wa chama hicho waliokamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kudai/kupokea hongo, waliachiwa baada ya kufutiwa mashtaka.

Lakini hakuna mahali ambapo tabia hii ya kuoneana haya ndani ya chama hicho imeonekana dhahiri kama kuhusu ile dhana yao ya miaka sita iliyopita ya ‘kujivua gamba’ kama msamiati walioubuni wao wenyewe ulivyokuja kujulikana.

Mchakato huu ulilenga kuwaondoa kwenye nyadhifa za chama viongozi waliokuwa wanabeba tuhuma za ufisadi ama wajiondoe wenyewe kwa hiari yao, au chama kiwaondoe kwa nguvu. Na si ubishi kwamba watuhumiwa hawa walikuwamo ndani ya uongozi wa chama hicho kwani haikuingia akilini kwa chama hicho kufukuzia kitu ambacho hakipo.

Lakini hadi leo hii hakuna lolote lililofanyika katika zoezi hilo mbali na kada mmoja kujivua nyadhifa zake zote za chama ikiwemo ubunge. Wengi walibakia chamani kama vile zoezi zima lilikuwa dhihaka kubwa.

Na waliolianzisha na kulisimamia na hata kulipangia muda, waliamua kukaa kimya sana sana walikuwa wanapenda suala lisiwe linatajwa tajwa tena.

Na labda kwa kuongezea tu hapa imekuwa nadra sana kwa viongozi wa upinzani kukamatwa na kushtakiwa kwa jinai za ufisadi kwa sababu moja kubwa; jinai hii huwaandama zaidi watumishi wa umma wa ngazi za juu waliopewa dhamana kubwa za nchi ambao ni nadra sana kuwemo wale wa upinzani.

Jinai inayowaandama zaidi wapinzani ni hii ya ‘uchochezi’ na kwa kipindi fulani huko nyuma iliongezwa ile ya ‘ugaidi.’ Na ndiyo maana tumeshuhudia wabunge wa CCM wakipandishwa kizimbani kwa jinai za ‘ufisadi’ au ‘kutumia madaraka vibaya” na si ‘uchochezi’ kwani kama nilivyotaja hapo mbele kwa CCM ‘uchochezi’ ni jinai mbaya zaidi kuliko ‘ufisadi’.