Home Makala Chadema na ujenzi wa ‘ukuta’ nyakati za kifuku

Chadema na ujenzi wa ‘ukuta’ nyakati za kifuku

1022
0
SHARE

NA TOBIAS NSUNGWE

KWA mara nyingine tena viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wametakiwa kuacha kuota ndoto za mchana kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana.

Rais John Magufuli amesema viongozi wa Ukawa wasitake kucheza na yeye kwani hakutakuwa na uchaguzi mwingine mkuu hadi mwaka 2020. Kwa sasa rais huyo anasisitiza kuwa Serikali yake na ile ya Mapinduzi Zanzibar ziachwe zifanye kazi ya kuwatumikia Wananchi.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika kisiwa cha Pemba wiki iliyopita Magufuli aliendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda amani na kuwataka Ukawa kuacha kucheza ‘ngoma wasiyoijua’.

Kauli za rais kisiwani Pemba zimekuja siku chache tu baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuahirisha maandamano kupitia wanachokiita Umoja wa Kuondoa Udikteta Tanzania (Ukuta).

Chama hicho kikuu cha Upinzani chenye wabunge wengi zaidi nchini kimekuwa kikiutuhumu uongozi wa awamu ya tano kwa kuminya ustawi wa demokrasia nchini na kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kinapendelewa.

Kwa kweli Chadema hawamwelewi kabisa Rais Magufuli anaposema mikutano yote ya vyama vya siasa isubiri hadi mwaka 2020 nchi itakapofanya tena uchaguzi mkuu. Karibu viongozi wote wa Ukawa wanadai Magufuli ni ‘dikteta’

Katika historia ya uongozi wa taifa letu marais wote waliopita walipewa majina mbalimbali kuonesha kupinga au kukubaliana na sera zao. Kwa mfano tunahadithiwa na wazee wetu kwamba rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliitwa ‘haambiliki’. Hii ilitokana na kile kilichodaiwa kwamba Mwalimu Nyerere akiamini au kulikataa jambo fulani ilikuwa si rahisi kumshauri vinginevyo.

Wapo pia waliomtuhumu kuwa na chembechembe za udikteta. Rais Nyerere hakulipenda jina hilo lakini alivumilia pale alipoitwa ‘mchonga’na baadhi ya wapinzani wake wakielezea mpangilio wa meno yake.

Rais wa awamu ya pili, Ali Hassani Mwinyi naye alipewa majina kadhaa. Jina lililopata umaarufu zaidi ni ‘Mzee ruksa’. Wapinzani wake walikuwa wakimlaumu kwa kuachia mianya ya rushwa na ufisadi.

Inadaiwa katika uongozi wake rushwa ilitamalaki sana nchini na mfumuko wa bei ulipanda sana. Hata hivyo historia inambeba Mzee Mwinyi kwa kufungua milango ya demokrasia. Chini ya uongozi wake Tanzania ilirejesha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Akaja Mzee wa Ukweli na uwazi katika awamu ya tatu, Rais Benjamin Mkapa. Anasifika kwa kurejesha nidhamu serikalini ingawa hakufanikiwa sana kupambana na rushwa.

Wapinzani walimtaja Mkapa kama rais ‘mbabe.’ Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete naye amepewa majina mengi ikiwemo kuitwa ‘rais dhaifu’na baadhi ya viongozi wa upinzani.

Hata baadhi ya makada CCM walimlaumu Kikwete kwamba ‘upole’ wake ulikuwa unaupa upinzani nguvu ya kuweza kusitawi na hivyo kuhatarisha uhai wa chama tawala.

Wapo waliodai kuwa utawala wake ulikuwa unaongea zaidi kuliko kutenda. Hata mwaka mmoja haujaisha tangu aondoke madarakani,  baadhi ya viongozi wa upinzani wamesikika ‘wakimkumbuka’ Kikwete na kukiri kwamba angalau aliachia demokrasia isitawi na uhuru wa habari kushamiri.

Waliomtukana Kikwete sasa wanatafakari na kujuta. Hata hivyo si busara kuishi kwa kufananisha namna marais wanavyofanya kazi zao. Kila mmoja ana staili yake, haiba yake, mapungufu yake na mchango wake. Hakuna sababu ya kuwafananisha Kikwete na Magufuli kwani hawa ni watu tofauti, wenye elimu tofauti na hata historia tofauti za maisha yao kabla hawajaijongea Ikulu.

Kuwa upinzani hasa barani Afrika si lelemama. Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alipomkaribisha Edward Lowassa mwaka jana alimtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani kuwa tayari kupata misukosuko ya polisi.

Tayari amekwisha onja joto ya polisi hii ni pamoja na kukataliwa kuingia mkoani Katavi na juzijuzi kukamatwa na polisi wakati wakiwa kwenye kile kinachoitwa mikutano ya ndani ya jinni ya kupanga mikakati ya Ukuta ambayo kimsingi ilikwishapigwa marufuku na Serikali.

Hakuna aliyefikiria siku moja Lowassa mwenye ushawishi mkubwa nchini angekamatwa na polisi japo kwa mahojianao tu.  Ni dhahiri safari yake ya ‘matumaini’ imekuwa na misukosuko mingi na imedhihirika sasa kwamba urais si rahisi kuukwaa.

“Jakaya aliwabatiza wapinzani kwa maji. Magufuli anakuja kuwabatiza kwa moto” hayo yalisemwa na kada machachari wa CCM Mzee Yusufu Makamba katika Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho uliomchagua Rais Magufuli kuwa mwenyekiti. Hii iliashiria kuwa rais na mwenyekiti mpya wa CCM hatokuwa na uvumilivu sana na wapinzani kama alivyokuwa Kikwete.

Chadema wanadai wameahirisha maandamano ya Ukuta hadi mwezi ujao kufuatia wito wa viongozi wa dini. Ni jambo jema pale viongozi wa dini wanapopaza sauti zao pale amani ya nchi inapojaribiwa. Inadaiwa viongozi wa makanisa ya Pentekoste, Lutherani, Jumuia ya Kikristo Tanzania (CCT),  na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na makanisa mengine yaliwasihi Chadema kusetisha maandamano.  Viongozi wa Kiislamu nchini nao walifanya hivyohivyo.

Hata hivyo, yawapasa makasisi na masheik kuwa makini wanaposhughulika na wanasiasa. Siasa ina mbwembwe na minyukano mingi ambayo haitapendeza mbele ya dini. Viongozi wetu wa kiroho waongozwe na maneno ya Bwana Yesu ( Nabii Issa) aliyesema : Ya Mungu mwachieni Mungu na ya Kaisari mwachieni Kaisari.Wasipendelee upande wowote.

Juhudi za kupanua wigo wa demokrasia nchini ni jambo endelevu. Hata hivyo itawabidi Chadema kubadili mbinu. Wananchi wetu hasa vijijini hawajengi ukuta nyakati za masika kwani wanajua utabomolewa na mvua. Kipindi cha kifuku wakulima hukitumia kwa ajili ya kilimo. Ujenzi wa nyumba hufanyika nyakati za kiangazi.

Chadema isijenge ‘ukuta’ nyakati hizi za kifuku. Kuna sehemu nimekutana na bango limeandikwa : Hapa Kazi tu Ukawa majungu. Nyakati hizi Wananchi wametakiwa na Serikali yao kufanya kazi kwa bidii.

Maandamano hayapewi nafasi tena. Huu si wakati wa kutumia nguvu kuidai demokrasia. Waache mazungumzo yachukue nafasi. Ukawa wamtambue na kumkubali Magufuli kwamba ndiye rais. Vilevile Magufuli akubali kukutana na viongozi wa Ukawa ili kwa pamoja washirikiane kuijenga nchi.

Haina haja kutunishiana misuli. Kwa faida ya nani? Chadema waache kuidai demokrasia barabarani. Tunataka kuwaona wakifanyia harakati bungeni ambako kwa sasa wana sauti kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Hiki ni kipindi cha kifuku hakifai kujenga ukuta.